fonetiki na fonolojia ya kiswahili

65
FONETIKI AU UTAMKWAJI WA SAUTI- FONIMU ZA KISWAHILI SANIFU 3.2.1 Maana Ya Fonetiki Fonetiki ni taaluma inayojishughulisha na jinsi sauti yo yote inavyotolewa au inavyopatikana. Hii ni sayansi huru ambayo inatumia nadharia za sayansi halisi kama vile fizikia, uhandisi, baiolojia, nk. na kufaidi matokeo ya kiutafiti ya taaluma hizi. Mathalani, ili mwanafonetiki aelewe jinsi ala za sauti zinavyofanya kazi wakati wa utolewaji wa sauti, atafaidika na maelezo ya kibaiolojia kuhusu namna mfumo wa mwili wa mwanadamu unavyofanya kazi. Mgulu, (2001:48) anadai: ‘ ... fonetiki ni moja tu, lakini fonolojia zipo nyingi kama lugha zenyewe zilivyo nyingi. Kwa mfano, hatuna fonetiki ya Kiingereza au fonetiki ya Kiswhili. Fonetiki ni fonetiki tu. Kwa upande mwingine, tuna fonolojia za lugha mbalimbali ambazo hutofautiana. Tunazo, kwa mfano, fonolojia ya Kiswahili, fonolojia ya Kiingereza, fonolojia ya Kifaransa, fonolojia ya Kinyamwezi, fonolojia ya Kindendeule, nk. Tunapozungumzia upatikanaji wa sauti za lugha za binadamu, tunafafanua jinsi sauti za lugha husika zinavyotamkwa katika bomba la sauti la mwanadamu. (Tazama Jedwali 3.5). Tunazibainisha ala, hususani alasogezi na alapahala husika katika kuitamka sauti husika. Alasogezi ni ile ala ambayo inaweza kujimudu wakati wa utamkwaji wa sauti husika. Alapahala au Ala-tuli ni ile ala ambayo haiwezi kujimudu wakati wa utamkwaji wa sauti husika. (Tazama Kielelezo 3.1). Ni alasogezi ambayo hujisogeza kwenye alapahala husika wakati wa utamkwaji wa sauti husika (Nchimbi, 1979). 3.2.2 Utamkwaji wa Sauti-Fonimu za Kiswahili Ieleweke kwamba hewa itokayo kwenye chemba ya mapafu ambayo sisi sote twaitumia kwa kupumua ili tuishi, ndiyo hiyo hiyo itumikayo

Upload: msangi

Post on 22-Jun-2021

65 views

Category:

Art & Photos


18 download

DESCRIPTION

Kiswahili Linguistics

TRANSCRIPT

FONETIKI AU UTAMKWAJI WA SAUTI-FONIMU ZA KISWAHILI SANIFU

       3.2.1   Maana Ya Fonetiki 

Fonetiki ni taaluma inayojishughulisha na jinsi sauti yo yote inavyotolewa au inavyopatikana. Hii ni sayansi huru ambayo inatumia nadharia za sayansi halisi kama vile fizikia, uhandisi, baiolojia, nk. na kufaidi matokeo ya kiutafiti ya taaluma hizi. Mathalani, ili mwanafonetiki aelewe jinsi ala za sauti zinavyofanya kazi wakati wa utolewaji wa sauti, atafaidika na maelezo ya kibaiolojia kuhusu namna mfumo wa mwili wa mwanadamu unavyofanya kazi.

Mgulu, (2001:48) anadai: ‘ ... fonetiki ni moja tu, lakini fonolojia zipo nyingi kama lugha zenyewe zilivyo nyingi. Kwa mfano, hatuna fonetiki ya Kiingereza au fonetiki ya Kiswhili. Fonetiki ni fonetiki tu. Kwa upande mwingine, tuna fonolojia za lugha mbalimbali ambazo hutofautiana. Tunazo, kwa mfano,  fonolojia ya Kiswahili, fonolojia ya Kiingereza, fonolojia ya Kifaransa, fonolojia ya Kinyamwezi, fonolojia ya Kindendeule, nk.

Tunapozungumzia upatikanaji wa sauti za lugha za binadamu, tunafafanua jinsi sauti za lugha husika zinavyotamkwa katika bomba la sauti la mwanadamu. (Tazama Jedwali 3.5). Tunazibainisha ala, hususani alasogezi na alapahala husika katika kuitamka sauti husika. Alasogezi ni ile ala ambayo inaweza kujimudu wakati wa utamkwaji wa sauti husika. Alapahala au Ala-tuli ni ile ala ambayo haiwezi kujimudu wakati wa utamkwaji wa sauti husika. (Tazama Kielelezo 3.1). Ni alasogezi ambayo hujisogeza kwenye alapahala husika wakati wa utamkwaji wa sauti husika (Nchimbi, 1979).

3.2.2   Utamkwaji wa Sauti-Fonimu za Kiswahili

Ieleweke kwamba hewa itokayo kwenye chemba ya mapafu ambayo sisi sote twaitumia kwa kupumua ili tuishi, ndiyo hiyo hiyo itumikayo katika utamkwaji wa sauti za lugha za binadamu. Hewa hiyo itapitishwa kwenye chemba zilizomo katika bomba la sauti kwa mujibu wa sauti inayotarajiwa kutamkwa hadi nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo au chemba ya pua

Hewa hiyo ikipitia chemba ya pua tu au chemba ya pua na chemba ya midomo, basi hisia za sauti itakayotamkwa zitakuwa za sauti-ng’ong’o. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejishusha kutoka kwenye ukuta wa marakaraka (paroi pharangale) ili hewa hiyo ipate ku

Lakini hewa hiyo, isipopitia chemba ya pua, ikapitia chemba ya midomo tu hadi nje, basi hisia za sauti itakayotamkwa zitakuwa za sauti-sing’ong’o. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. (Tazama Kielelezo 3.4).

Tutaanza kufafanua utamkwaji wa sauti-fonimu-irabu za Kiswahili, ukifuatiwa na ufafanuzi wa utamkwaji wa sauti-fonimu-konsoni za Kiswahili. Ufafanuzi utafanywa kwa kuzingatia vigezo vin’ne, navyo ni:

(a)    utamkwaji ki-alapahala,        

(b)    utamkwaji ki-sampuli,

(c)    utamkwaji ki-ughuna,

(d)    utamkwaji ki-ung’ong’o na,  

(e)    msimamo wa midomo hususani kuhusu  utamkwaji wa fonimu-irabu.             

3.2.3   Utamkwaji wa Fonimu-Irabu-Mama za Lugha za Binadamu

Irabu-mama katika lugha zote za binadamu ni /i a u/ ambazo utamkwaji wake katika bomba la sauti unajitokeza kwenye alapahala ya burutio-gumu/kaakaa-gumu ikishirikiana na alasogezi ya ulimi-kati ki-alasogezi-pahala kama ilivyo kwenye Kielelezo 3.5.

Katika Kielelezo 3.5 alasogezi-pahala za irabu, irabu-mama /I/ inajidhihirisha kuwa ni ya juu-mbele wakati irabu-mama /U/ ni ya juu-nyuma. Irabu-mama /A/ ni ya chini-kati.

Vigezo vya kufafanulia matamshi ya irabu ni kama ifuwatavyo:

 (i)       Kwa Mujibu wa Alapahala:ni burutio-gumu; ama sehemu ya mbele, ama sehemu ya kati, ama sehemu ya nyuma ya burutio-gumu.

 (ii)      Kwa Mujibu wa Alasogezi: ni ulimi; ama sehemu ya mbele (ulimi-mbele), ama sehemu ya kati (ulimi-kati), ama sehemu ya nyuma ya ulimi (ulimi-nyuma).

(iii)     Kwa Mujibu wa Midomo: ni ama midomo-tandazi au midomo-futuzi.

(iv)      Kwa Mujibu wa Mpenyo: ni ama mpenyo-mwembamba, ama mpenyo-mwembamba-kiasi, ama mpenyo-mpana.

(v)       Kwa Mujibu wa Kidaka-Tonge: ni ama irabu-ng’ong’o ama irabu-sing’ong’o

(vi)      Kwa Mujibu wa Nyuzi za Sauti/Glota: ni ama irabu-ghuna ama irabu-sighuna.

3.2.4   Utamkwaji wa Fonimu-Irabu //i e a o u/

Fonimu-irabu za kiswahili sanifu ni /i e a o u/. Fonimu-irabu-mbele za kiswahili sanifu ni /a e i/ na fonimu-irabu-nyuma ni /a o u/. Fonimu-irabu na nusu-irabu-mbele /a e i j/.

           

Wakati wa utamkwaji wa fonimu-irabu-mbele / a e i /, alasogezi ya ulimi-kati hujikweza kuelekea kwenye alapahala ya burutio-gumu-mbele. Mpenyo unaofanyizwa kati ya alasogezi ya ulimi-kati na alapahala yake ya burutio-gumu-mbele ni mpana wakati wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [a], ni mpana kidogo wakati wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [e] na ni mwembamba wakati wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [i].

Mpenyo huu wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [i] unapofanyizwa kuwa mwembamba zaidi , basi matamshi ya sauti-endelezi ya nusu-irabu [j] hudhihirika, yaani [a e i j]. Aidha, midomo hubakia tandazi (Nchimbi,1979). Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o.

Utamkwaji wa Fonimu-Irabu na Nusu-Irabu-Nyuma /a o u w/:Wakati wa utamkwaji wa fonimu-irabu-nyuma / a o u /, alasogezi ya ulimi-kati hujikweza kuelekea kwenye alapahala ya burutio-gumu-nyuma. Mpenyo unaofanyizwa kati ya alasogezi ya ulimi-kati na alapahala yake ya burutio-gumu-mbele ni mpana wakati wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [a], ni mpana kidogo wakati wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [o] na ni mwembamba wakati wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [u].Aidha, alasogezi ya mdomo-chini na alapahala ya mdomo-juu hujifutua, na kwa hiyo, kufanyiza mpenyo aina ya mviringo.

Mpenyo huu wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [u] unapofanyizwa kuwa mwembamba zaidi, basi matamshi ya sauti-endelezi ya nusu-irabu [w] hudhihirika, yaani [a o u w], na midomo hubakia futuzi. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o.

Kielelezo 3.7:  Alasogezi-Pahala za Irabu na Nusu-Irabu za Burutio-Gumu-Nyuma na Midomo-Futuzi  [o u w]

Tija itokanayo na mfumo wa matamshi ya sauti-irabu za kiswahili sanifu: maelezo yanayotokana na (a) utamkwaji wa fonimu-irabu za burutio-gumu-mbele  [a  e i] na nusu-irabu [j] na (b) utamkwaji wa fonimu-irabu za burutio-gumu-nyuma  [ o u] na nusu-irabu [w], yanatuwezesha kufanyiza (i) Jedwali ya mfumo wa matamshi ya irabu za kiswahili sanifu [i e a o u], (ii) Tarapezi ya mfumo wa irabu za kiswahili sanifu [i e a o u], na (iii) Jedwali la mfumo wa matamshi ya nusu-irabu/konsoni za kiswahili sanifu [j w], kama ilivyo katika Jedwali 3.6.  

Jedwali 3.6:  Jedwali ya Mfumo wa Matamshi ya Irabu za Kiswahili Sanifu [i e a o u]

ALAPAHALA YA KITAMKWA

Burutio-gumu Mbele.

Burutio-Gumu Kati.

Burutio-Gumu Nyuma

MPENYO

I

u

UNG’ONG’O

Mwembamba

   (Juu)

Sing’ong’o

Mpana Kiasi

   (Kati)

E

o

Mpana

 (Chini)

a

Ulimi-kati mbele

Midomo-tandazi/sifutuzi

Ulimi-kati nyuma

Midomo-futuzi/sitandazi

ALASOGEZI YA KITAMKWA

Kielelezo 3.8: Tarapezi ya Mfumo wa Irabu za Kiswahili Sanifu [i e a o u]

Jedwali 3.7:  Jedwali ya Mfumo wa Matamshi ya Nusu-Irabu/Konsoni za Kiswahili Sanifu [j w]

MSIMAMO WA MIDOMO

ALAPAHALA YA KITAMKWA

UGHUNA

BURUTIO-GUMU

BURUTIO-LAINI

Midomo tandazi

J

Ghuna

Midomo futuzi

w

Ulimi-Kati                     Ulimi Nyuma

ALASOGEZI

  

ZOEZI

1.     Zitaje chemba (cavities) zinazolijenga bomba la sauti la mwanadamu.

2.     Zitaje alasogezi (articulators) zilizomo katika bomba la sauti la mwanadamu.

3.     Zitaje alapahala (places of articulation) zilizomo katika bomba la sauti la mwanadamu.

4.     (a)    Tofautisha matamshi ya irabu-mbele na irabu-nyuma.

(b)    Eleza tofauti kati ya matamshi ya irabu [i] na nusu-irabu [j], au irabu [u] na nusu-irabu [w].

5.     Eleza tofauti kati ya alasogezi na alapahala.

3.2.5  Utamkwaji wa Sauti-Fonimu-Konsoni za Kiswahili Sanifu

Utamkaji wa fonimu-konsonanti za Kiswahili utafafanuliwa kwa mujibu wa vigezo vinne: utamkaji ki-alapahala, utamkaji ki-sampuli,     utamkaji ki-ughuna, na utamkaji ki-ung’ong’o.             

(i)     Utamkwaji wa Sauti-Fonimu-Konsoni za Kiswahili Ki-Alasogezi-Pahala

Fonimu-konsoni zote ishirini na tisa (29) za Kiswahili sanifu hudhihirishwa kimatamshi kwa kutumia alapahala saba (7) ambazo nazo huhusishwa moja kwa moja na alasogezi husika zilizomo katika bomba la sauti (Nchimbi, 1979), kama ifuatavyo:

           

Utamkwaji wa Vimidomo [p, b]: Wakati wa matamshi ya sauti za midomoni [p, b], alasogezi ya mdomo-chini hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya mdomo-juu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo.

Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka, kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o. (Tazama Kielelezo 3.8).

Utamkwaji wa Vimdomochini-Menojuu [f  v]: Wakati wa matamshi ya vimdomochini-menojuu [f] na [v], alasogezi husika ambayo ni mdomo-chini, hujikweza na, ama kujibandika kwenye alapahala ya meno-juu, au hujisogeza na kuacha nafasi finyu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni hujipenyeza kwa taabu kadiri unavyopitishwa katikati ya nafasi finyu inayofanyizwa kwa mdomo-chini na meno-juu, au kati ya jino na jino wakati mkondo huo unapoelekezwa n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomoni.

Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o.

Utamkwaji wa Viulimincha-Menojuu [θ  ð]: Wakati wa matamshi ya viulimincha-menojuu [θ] na [ð], alasogezi ya ulimi-ncha  hujisogeza kwenye alapahala ya meno-juu na kuacha nafasi finyu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni hujipenyeza kwa taabu kadiri unavyopitishwa katikati ya nafasi finyu inayofanyizwa kwa ulimi-ncha na meno-juu wakati mkondo huo unapoelekezwa nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomoni.

Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o.   

                       

Utamkwaji wa viulimincha-ufizijuu [t d s  z ]: Alasogezi ya ulimi-ncha  na alapahala ya ufizi-juu ndizo zinazotumika wakati wa matamshi ya viulimincha-ufizijuu. [t d s  z  r l].

Utamkwaji wa [t d]: Alasogezi ya ulimi-ncha inajikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ufizi-juu; mkondo wa hewa utokao mapafuni haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo.

Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika ndii... kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o. Kwa mantiki hii, viulimincha-ufizijuu vinavyotamkwa ni [t  d ].

Utamkwaji wa [s z]: Wakati alasogezi ya ulimi-ncha inapojisogeza kiasi cha kuacha nafasi finyu kati yake na alapahala ya ufizi-juu, mkondo wa hewa utokao mapafuni hupata nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo.

Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o [s z ].

Utamkwaji wa Viulimikati-Burutiogumu [c ɟ ʃ  j]: Utamkwaji wa [c ɟ]

Wakati wa matamshi ya viulimikati-burutiogumu [c ɟ], alasogezi ya ulimi-kati, hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya burutio-gumu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya Bomba la Sauti kwa kupitia chemba ya midomo.

Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o [c ɟ].

    

                  

Utamkwaji wa [ʃ  j]: Wakati wa matamshi ya viulimikati-burutiogumu [ʃ  j ]; alasogezi ya ulimi-kati hujisogeza kiasi cha kuacha nafasi finyu kati yake na alapahala ya burutiogumu.

Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o [ʃ  j].

Utamkwaji wa Viuliminyuma-Burutiolaini [k g  Ɣ]: Wakati wa matamshi ya viulimikati-burutiogumu [k  g], alasogezi ya ulimi-nyuma, hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya burutio-gumu-nyuma kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo.

Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o [k  g], Tazama Kielelezo 3.15.

Unapojitokeza wakati wa matamshi ya [Ɣ], alasogezi ya ulimi-nyuma hujisogeza kiasi cha kuacha nafasi finyu kati yake na alapahala ya ukuta wa marakaraka au ncha ya kidaka-tonge. Nafasi hii itaruhusu mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo. Midomo hubakia tandazi itamkwapo sauti [Ɣ]

Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o [Ɣ]

Utamkwaji wa Kiglota [h]: Wakati wa matamshi ya kiglota [h], alasogezi ya ulimi hubakia chini kiasi cha kuacha nafasi kubwa kati yake na alapahala ya burutio. Mkondo wa hewa kutoka mapafuni unapopita katika chemba ya koromeo, nyuzi sauti zilizomo katika chemba hiyo ama hurindima na ikapatikana sauti [ h ], au hazirindimi na kupatikana sauti [h]. Aidha , mkondo huu wa hewa kutoka mapafuni hupitishwa moja kwa moja katika chemba ya kinywa bila kizuizi mpaka n’nje ya kinywa. Kwa mantiki hii, nyuzi sauti zinaweza kueleweka kama alasogezi ya matamshi ya sauti [h] ya fonimu /h/.

Midomo hubakia tandazi itamkwapo sauti [h]. Na alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o [h]

(ii)    Utamkaji wa Sauti za Fonimu za Kiswahili  Ki-Sampuli

Utamkwaji wa sauti ki-sampuli unabainisha kati ya sauti-endelezi na sauti-sendelezi.Utamkaji wa sauti ki-sampuli ni ule unaosababishwa na alasogezi ya ulimi na mdomo-chini inaponyanyuka kuelekea kwenye alapahala husika. Ulimi au mdomo-chini unaponyanyuka kuelekea kwenye alapahala husika, husababisha matamshi ya sampuli za sauti zifuatazo:

           

Sauti-sendelezi-konsoni ambayo wakati wa utamkwaji wake, alasogezi husikahujikweza na kujibandika kwenye alapahala husika; ambayo kwa [p b ] ni mdomo-juu, kwa [t d] ni ufizi-juu, kwa [c ɟ ] ni burutio-gumu-mbele na kwa [k g N] ni burutio-gumu- nyuma kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti. Kuzuiliwa kwa mkondo huu wa hewa ni kwa muda mfupi sana. Kwa mantiki hii utamkaji wa sauti-konsonanti-katizi hauendelezeki. Mifano ya sauti-konsonanti-katizi katika Kiswahili ni [p b  t d  c ɟ k g ].

Sauti-endelezi-konsoni-madende ambayo wakati wa utamkaji wake, alasogezi ya ulimi-ncha hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ufizi-juu, kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti. Kuzuiliwa kwa mkondo huu wa hewa ni kwa muda mfupi sana. Kwa mantiki hii, alasogezi ya ulimi-ncha huonekana ikiyumbishwa kana kwamba inajigongagonga kwenye matuta ya alapahala ya ufizi-juu. Aidha, utamkaji wa sauti hii huwa katizi unaoendelezeka kwa vigongo, yaani, kimadende.

Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o. Mfano wa sauti-konsonanti-madende-endelezi ni [r].

Sauti-Endelezi-Konsoni-Kwama Kwamizi ambayo wakati wa utamkwaji wake, alasogezi husika hujikweza na kuunda mpenyo mwembamba sana kwenye alapahala husika, kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao kwenye           chemba ya koromeo hupita, lakini kwa hukwamizwa kwamizwa, unapoelekea n’nje ya Bomba la Sauti. Matokeo yake ni matamshi ya sauti-konsonanti-endelezi kwama kwamizi, kama vile: [f  v θ ð s ʃ [Ɣ] h] 

Sauti-endelezi-konsonanti-tambazi ambayo wakati wa utamkaji wake, alasogezi ya ulimi-ncha hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ufizi-juu, kiasi kwamba sehemu ya mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo haupati nafasi hapo kwenye alapahala ya ufizi-juu ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti, na sehemu iliyobakia ya mkondo huo wa hewa huchepukia pembezoni mwa ulimi na hatimaye kuelekea n’nje ya bomba la sauti.       

Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua.

Kwa mantiki hiyo, hisia za n’nje zinazosikika ni za aina ya sauti-endelezi sing’ong’o ambapo hewa yake inatambaa.  Mfano wa hii sauti-konsonanti-tambazi ni [l].

           

3.2.6   Utamkwaji wa Sauti za Fonimu za Kiswahili Ki-Ughuna

3.2.6.1  Utangulizi

Utamkwaji wa sauti ki-ughuna unabainisha kati ya sauti-ghuna ambayo husababishanyuzi za sauti/glota zilizomo kwenye chemba ya koromeo zitetemeke, yaani hisia ya kwenye chemba ya koromeo [KO] huwa ya mawimbi-mawimbi, yaani:

 [KO:  ], na  sauti-sighuna ambayo haisababishi nyuzi za sauti/glota zilizomo kwenye chemba ya koromeo zitetemeke, na kwa hivyo, hisia inayojitokeza si ya mawimbi-mawimbi,  yaani: [KO:___________]. Aidha, hisia za sauti-sighuna  hazijitokezi kwenye Chemba ya Pua [PU:____________], wala kwenye chemba ya kinywa [KI:__________] wala kwenye Hisi N’nje [NJE:________]. Tazama kwa mintarafu ya Kielelezo 3.19. 

Kielelezo 3.19:  Utamkwaji Wa Sauti-Ghuna Na Sauti-Sighuna, Kwa Mfano,  Katika  Neno “Sasa” Kwenye Mingogramu (Mingo)

Ufasili wa Mingo hii ya Neno “Sasa”:

(a)    Sauti [s]:

(i)     ni sauti sighuna kwa kuwa nyuzi sauti/glota hazioneshi ishara ya kutetemeka/mawimbi-mawimbi kwenye msitari wa chemba ya koromeo, yaani: [KO:  ___________]

(ii)    ni sauti sing’ong’o kwa kuwa nyuzi sauti/glota hazioneshi ishara ya kutetemeka/mawimbi-mawimbi kwenye msitari wa chemba ya pua, yaani: [PU:_______].

(b)    Sauti [a]:

ni sauti ghuna kwa kuwa nyuzi sauti/glota zinaonesha ishara ya kutetemeka/mawimbi- mawimbi kwenye msitari wa chemba ya koromeo, yaani: [KO: ]

Utamkwaji wa sauti-ghuna-sing’ong’o-endelezi za Kiswahili sanifu: Katika Kiswahili sanifu, sauti-ghuna-sing’ong’o-endelezi zinazojitokeza ni [a], [e],   [i], [o], [u], [v], [ð], [z], [r], [l], [j],  [Ɣ]. Sauti-ghuna hizi ndizo zinazosababisha nyuzi za sauti/glota zilizomo kwenye chemba ya koromeo zitetemeke, yaani hisia ya kwenye Chemba ya Koromeo [KO] huwa ya mawimbi-mawimbi, yaani:  [KO: ].

Kumbuka kwamba wakati wa utamkwaji wa sauti-ghuna,  alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka, kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua wakati wa utamkwaji wa sauti-ghuna-sing’ong’o-endelezi.

 (iv)     Utamkwaji wa Sauti za Fonimu za Kiswahili Ki-Ung’ong’o

Hewa hiyo inayotoka mapafuni, ikipitia chemba ya pua tu au chemba ya pua na chemba ya midomo, basi hisia za sauti itakayotamkwa zitakuwa za sauti-ng’ong’o. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejishusha kutoka kwenye ukuta wa marakaraka (paroi pharangale) ili hewa hiyo ipate kupita na kutoka n’nje ya bomba la sauti.

Utamkwaji wa Sauti-Konsoni-Ghuna-Ng’ong’o-Endelezi  [m]: Wakati wa matamshi ya sauti ya midomoni [m], alasogezi ya mdomo-chini hujikweza na kujibandika ndii... kwenye alapahala ya mdomo-juu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo. Lakini wakati huo, alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka  na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua; sauti-ghuna-ng’ong’o-endelezi [m] hudhihirishwa na ikadhihirika.

Utamkwaji wa Sauti-Konsoni-Ghuna-Ng’ong’o-Endelezi  [n]: Alasogezi ya ulimi-ncha na alapahala ya ufizi-juu ndizo ala zinazotumika wakati wa matamshi ya kiulimincha-ufizijuu [n] ambayo ni sauti-konsoni-ghuna-ng’ong’o-endelezi.

Wakati wa matamshi ya sauti ya kiulimincha-ufizijuu [n], alasogezi ya ulimi-ncha hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ufizi-juu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo. Lakini wakati huo huo, alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka  na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua; sauti-ghuna-ng’ong’o-endelezi [n] hudhihirishwa na ikadhihirika.

Utamkwaji wa Sauti-Konsoni-Ghuna-Ng’ong’o-Endelezi  [ɲ]: Alasogezi ya ulimi-kati  na alapahala ya burutio-gumu(kaakaa-gumu) ndizo ala zinazotumika wakati wa matamshi ya kiulimi-kati [ɲ] ambayo ni sauti-konsoni-ghuna-ng’ong’o-endelezi.

Wakati wa matamshi ya sauti ya kiulimi-kati [ɲ], alasogezi ya ulimi-kati hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya  burutio-gumu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo. Lakini wakati huo huo, alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka  na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua; sauti-ghuna-ng’ong’o-endelezi [ɲ], hudhihirishwa na ikadhihirika.

Utamkwaji wa Sauti-Konsoni-Ghuna-Ng’ong’o-Endelezi [ŋ]: Alasogezi ya ulimi-kati  na alapahala ya burutio-laini(kaakaa-laini) ndizo ala zinazotumika wakati wa matamshi ya kiulimi-kati [ŋ] ambayo ni sauti-konsoni-ghuna-ng’ong’o-endelezi.

Wakati wa matamshi ya sauti ya kiulimi-kati [ŋ], alasogezi ya ulimi-kati hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya  burutio-gumu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo. Lakini wakati huo huo, alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka  na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua; sauti-ghuna-ng’ong’o-endelezi [ŋ], hudhihirishwa na ikadhihirika.

Katika mfumo wa sauti-irabu za Kiswahili Sanifu [a e i o u ], tunagundua kwambaapana sauti-irabu-ng’ong’o hata moja baina yao, zote ni sauti-irabu-sing’ong’o. Lakini katika mazungumzo ya kimtindo, aghalabu hizi sauti-irabu-sing’ong’o huweza kung’ong’oishwa na msikilizaji akapata hisia ya sauti-irabu-ng’ong’o, kama hivi: [a e i o u ], yaani wakati wa utamkwaji wa kila irabu kivyake, hewa itokayo mapafuni lazima itoke n’nje sambamba kwa kupitia chemba ya midomo na tundu za pua, kama Kielelezo 3.25 kinavyoushereheshea.

Hewa hiyo inayotoka mapafuni, ikipitia chemba ya pua tu au chemba ya pua na chemba ya midomo bila kusitishwa, basi hisia za sauti itakayotamkwa zitakuwa za sauti-ng’ong’o-endelezi [a], [e], [o], [m], [ŋ], nk., yaani, sauti za ming’ung’uto. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejishusha kutoka kwenye ukuta wa marakaraka (paroi pharangale) ili hewa hiyo ipate kupita na kutoka nje ya bomba la sauti, bila kusitishwa!

                       

(v)    Utamkwaji wa Sauti za Fonimu za Kiswahili Ki-Mang’ong’o

Utamkwaji wa Mang’ong’o ya Kiswahili Sanifu  [mb] au [], [nd] au [], [nj] au [], [ng]  au [] 

Utamkwaji wa sauti za fonimu za Kiswahili ki-mang’ong’o, ni utamkwaji wa sauti-fonimu-mang’ong’o  [mb] au [], [nd] au [], [nj] au [], [ng]  au [].  Huu niutamkwaji wa sauti-ng’ong’o-sendelezi, yaani utamkwaji wa MANG’ONG’O kama kielelezo3.26 kinavyotushereheshea:

Kila sauti-fonimu-mang’ong’o ni sauti-ghuna, ughuna ambao hujidhihirisha kwenye msitari wa chemba ya koromeo [KO:  ] na hususani kwenye msitari wa chemba ya pua [PU:  ] kama ilivyo katika utamkaji wa sauti-fonimu-ng’ong’o za kawaida [m n ɲŋ],

Kivyake, kila sauti-fonimu-mang’ong’o hutamkwa kama ifuatavyo:

(a)       Utamkwaji wa Sauti-Ng’ong’o-Sendelezi [mb] au [] 

Utamkaji wa sauti-ng’ong’o-sendelezi [mb] au []   hudhihirishwa katika hatua zifuatazo:

             

·        alasogezi ya mdomo-chini inapojikweza na kujibandika kwenye alapahala ya mdomo-juu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo haupati nafasi ya kutoka n’nje ya Bomba la Sauti. Wakati kitendo cha hapo juu kinatendeka, kitendo kifuatacho hufanyika:

·        alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka  na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua.

·        mrindimo-ng’ong’o unapoanza kujidhihirisha kwenye nyufa za chemba ya pua, alasogezi ya mdomo-chini hujibandua kutoka kwenye alapahala ya mdomo-juu na alasogezi ya kidaka-tonge hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka; vitendo vyote hivi vitatu hutendeka wakati mmoja.  

(b)       Utamkwaji wa Sauti-Ng’ong’o-Sendelezi [nd] au []

Utamkaji wa sauti-ng’ong’o-sendelezi [nd]  hudhihirishwa katika hatua zifuatazo:

·        alasogezi ya ulimi-ncha inapojikweza na kujibandika ndii kwnye alapahala ya  ufizi-juu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo haupati nafasi ya kutoka n’nje ya Bomba la Sauti. Wakati kitendo cha hapo juu kinatendeka, kitendo kifuatacho hufanyika:

·        alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka  na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua.

·        mrindimo-ng’ong’o unapoanza kujidhihirisha kwenye nyufa za chemba ya pua, alasogezi ya ulimi-ncha hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ufizi-juu na alasogezi ya kidaka-tonge hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka; vitendo vyote hivi vitatu hutendeka wakati mmoja. 

           

 (c)      Utamkwaji wa Sauti-Ng’ong’o-Sendelezi  [nj] au []

Utamkaji wa sauti-ng’ong’o-sendelezi [nj] hudhihirishwa katika hatua zifuatazo:

·        alasogezi ya ulimi-kati inapojikweza na kujibandika kwenye alapahala ya burutiogumu-mbele kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo haupati nafasi ya kutoka n’nje ya bomba la sauti. Wakati kitendo cha hapo juu kinatendeka, kitendo kifuatacho hufanyika:

·        alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka  na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua.

·        mrindimo-ng’ong’o unapoanza kujidhihirisha kwenye nyufa za chemba ya pua, alasogezi ya ulimi-kati hujibandua kutoka kwenye alapahala ya burutiogumu-mbele na alasogezi ya kidaka-tonge hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka; vitendo vyote hivi vitatu hutendeka wakati mmoja.        

           

(d)       Utamkwaji wa Sauti-Ng’ong’o-Sendelezi , [ng]  au []

Utamkaji wa sauti-ng’ong’o-sendelezi []  hudhihirishwa katika hatua zifuatazo:

·        alasogezi ya ulimi-nyuma inapojikweza na kujibandika kwenye alapahala ya burutiogumu-nyuma kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo haupati nafasi ya kutoka n’nje ya bomba la sauti, (angalia Kielelezo 3.27). Wakati kitendo cha hapo juu kinatendeka, kitendo kifuatacho hufanyika:

·        alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka  na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua.

·        mrindimo-ng’ong’o unapoanza kujidhihirisha kwenye nyufa za chemba ya pua, alasogezi ya ulimi-nyuma hujibandua kutoka kwenye alapahala ya burutiogumu-nyuma na alasogezi ya kidaka-tonge hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka; vitendo vyote hivi vitatu hutendeka wakati mmoja.        

Jedwali 3.7 (a): Mfumo wa Matamshi ya Konsoni za Kiswahili Sanifu

Alasogezi

Alapahala

Alasogezi-Pahala

Kitamkwa/Sauti

Mdomo-chini

mdomo-juu

Midomo

[p], [], [b], [m], [w]

Mdomo-chini

meno-juu

mdomochini-menojuu

[f], [v]

Ulimi-ncha

meno-juu

ulimincha-menojuu

[θ], [ð]

Ulimi-ncha

Fizi-juu

ulimincha- fizijuu

[t], [], [d], [n], [s], [z], [r], [l]

Ulimi-kati

Burutio-gumu(kaakaa-gumu)

ulimikati-burutiogumu

[c], [], [ ɟ], [ɲ], [ʃ], [j].

Ulimi-nyuma

Burutio-laini(kaakaa-laini)

uliminyuma- burutiolaini

[k], [], [g], [ŋ], [Ɣ], [w]

nyuzi-sauti (nyuzi-glota)

Glota

Glota

[h].

3.2.7   Uhusiano Baina ya Fonetiki na Fonolojia

Sauti-fonimu-irabu na konsoni zilivyojipanga katika mfumo wa kifonetiki/matamshi ambao unasababisha kuwako tofauti ya maana katika jozi milinganuo finyu za lugha ya Kiswahili ndio unaotuonesha uhusiano baina ya fonetiki na fonolojia.

Upo uhusiano wa karibu sana kati ya taaluma ya fonetiki na taaluma ya fonolojia. Sifa-bainifu za kifonolojia asili yake iko kwenye sifa-bainifu za kifonetiki. Kwa mfano, (a) sauti [p] inatofautiana na sauti [b] kwa sifa ya kifonetiki ya u-ghuna; kwamba [p] ni [ - ghuna] wakati sauti [b] ni [+ ghuna]; (b) sauti [b] inatofautiana na sauti [k] kwa sifa mbili za kifonetiki: (i) sifa ya ki-ghuna, kwamba sauti [k] ni [ - ghuna] wakati sauti [b] ni [+ ghuna];  (ii)  sifa ya ki-alasogezipahala, kwamba sauti [b] ni ki-midomo wakati sauti [k] ni ki-uliminyuma-burutiolaini.

Sifa hizi za kifonetiki/matamshi ndizo zinasababisha maana ya neno ibadilike, kwani badala ya neno kutamkwa [paka] linatamkwa [baka]; au [bata] linatamkwa [kata]; nk.

Kwa mantiki hii, sifa-bainifu za kifonetiki ndizo zinazosababisha kuwako kwa sifa-bainifu za kifonolojia. Na tunazibaini fonimu (ambacho ndicho kipashio cha fonolojia)kwazo. Kwa mfano:  

(a)       pata ~ peta ~ pita ~ pota ~ puta;

Kwa mbinu ya nitoe-nikutoe (commutation), tunadiriki kudai kwamba sauti [a], [e], [i], [o], na [u] ni fonimu /a/, /e/, /i/, /o/, /u/ katika Kiswahili.

(b)       yeye ~ wewe;  yote ~ wote

Kwa mbinu ya nitowe-nikutowe, tunadiriki kudai kwamba sauti nusu-irabu [j] na [w] ni fonimu /j/ na /w/ katika             Kiswahili.

           

(c)       pawa ~ bawa ~ tawa ~ dawa ~ chawa ~ jawa ~ kawa ~ gawa.

Kwa mbinu ya nitoe-nikutoe, tunadiriki kudai kwamba sauti sauti  [p], [b], [t], [d], [c], [ɟ], [k], [g] ni fonimu /p/, /b/, /t/, /d/, /c/, /ɟ/, /k/, /g/ katika Kiswahili.

Hii ndiyo mbinu kongwe ya kiisimu ambayo inatumiwa na wanaisimu katika utafiti wa fonimu za lugha yo yote ya binadamu. Na ndiyo mbinu iliyotumiwa kuzigundua fonimu za lugha, kama vile fonimu za Kiingereza, Kifaransa, Kiswahili, nk. ambazo tunajifunza katika vyuo vyetu. 

MAREJELEO

Maganga (1997), OSW 102: Historia ya Kiswahili. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Masebo, J. A. Nyengwine, N. (2002), Nadharia ya Lugha ya Kiswahili, Kidato cha 5 na 6. Aroplus Industries Ltd: Dar es Salaam.

Nkwera, Fr. F. V. (2003), Sarufi, Fasihi na Uandishi wa Vitabu, Sekondari na Vyuo. Creative Prints Ltd: Dar es Salaam

FONOLOJIA YA KISWAHILI UTANGULIZI NA USULI WA TAALUMA YA FONOLOJIA

Neno fonolojia linatokana na maneno mawili ya Kigiriki phone-sauti za kusemwa na logos- taaluma/mtalaa. Masimulizi yanadai kuwa taaluma hii ilianza zamani sana kati ya mwaka 460 kabla ya Masia huko India ya kale, ambapo mtu aliyeitwa Panini, na ambaye huaminika kuwa ni baba wa isimu aliandika kuhusu fonolojia yaKisansikriti katika matini aliyoiita Shiva Sutras. Ni katika andiko hili ndipo alipobainisha kuwepo kwa dhanna ambazo leo hii hujulikana kama fonimu, mofimu namzizi. Baada ya andiko hilo, habari za taaluma ya fonolojia ni kama zilipotea kabisa katika uwanja wa isimu hadi ilipofika karne ya 19 ambapo wanaisimu wengine waliibuka na kuzungumzia upya masuala ya fonolojia. Miongoni mwa wanaisimu wa mwanzo wanaotajwa kujihusisha na fonolojia ni Mpolandi "Jan Baudouin de Courtenay",(pamoja na mwanafunzi wake wa zamani "Mikołaj Kruszewski" alipobuni neno fonimu mnamo mwaka 1876, na kazi yake, ijapokuwa hairejelewi sana, inachukuliwa kuwa ni mwanzo wa fonolojia mamboleo. Mwanaisimu huyu si tu alishughulikia nadharia ya fonimu, bali pia vighairi vya kifonetiki (ambavyo leo huitwa alofoni na mofofonolojia). Maandishi ya Panini (Sarufi ya Kisanskriti) pamoja na Jan Baudouin de Courtenay yalikuja kuwa na athari kubwa kwa anayeaminika kuwa baba wa nadharia ya Umuundo Mamboleo, Ferdinand de Saussure, ambaye pia alikuwa ni profesa wa Sansikriti. Wanaisimu wote hawa walikuwa wanajaribu kulinganisha sauti za lugha za Asia Mashariki na za Ulaya, lengo lao likiwa ni kujua mizizi ya lugha zilizoitwa India-Ulaya. Kutokana na mkabala huo, katika kipindi hicho isimu ilikuwa Isimu-linganishi tu. Kutokana na tafiti zao hizo waliweza kupata maneno yenye sauti na maana zilizolingana, kufanana au kukaribiana. Utafiti huo uliweza kugundua jamii mbili za lugha ambazo ni jamii ya lugha za Kirumi na jamii ya lugha za Kijerumani. Baadhi ya wanaisimu mahususi kabisa wanaokumbukwa kuchangia katika maendeleo ya fonolojia ni pamoja na:

(i)          Jan Baudouin de Courtenay (1845-1929) Kama ilivyoelezwa hapo awali, huyu ni mwanaisimu aliyebuni dhanna za foni na fonimu. Katika nadharia yake, alidai kuwa sauti za mwanadamu ni za aina mbili—foni na fonimu.  Alisema kuwa foni ni sauti za kutamkwa tu lakini fonimu ni sauti za lugha. Hata hivyo, de Courtenay hakutumia istilahi za foni na fonimu (kama zinavyotajwa sasa) bali alitumia istilahi za anthrophonics—foni na psychophonics—fonimu. Yeye alidai kuwa foni zipo karibu sana na taaluma ya kumuelewa binadamu pamoja na alasauti zake ambazo kwa hakika hutofautiana sana na za wanyama wengine. Na kuhusu fonimu, alidai kuwa zinahusu kumwelewa binadamu pamoja na akili zake na namna anavyofikiri katika akili yake. Alidai kuwa, mara nyingi, binadamu hupokea kinachotamkwa na kufasiliwa.

(ii)        Ferdinand de Saussure (1887-1913): Ni mwanaisimu wa Kiswisi anayejulikana kama baba wa isimu kutokana na mchango wake alioutoa katika taaluma hii. Yeye anakumbukwa zaidi kutokana na uwezo wake wa kutofautisha dhanna alizoziita langue-mfumo wa lugha mahsusi,parole-matamshi ya mzungumzaji wa lugha husika na Langage ambayo hufafanuliwa kuwa ni uwezo alionao mzungumzaji wa lugha mahususi wa kuzungumza na kuelewa matamshi ya mzungumzaji mwingine wa lugha hiyohiyo. Ni sehemu ya lugha inayowakilisha maarifa kati ya sauti na alama. Ni mfumo wa alama kwa maana ya kiufundi tu. Dai lake la msingi ni kuwa alama inategemea vitu viwili-kitaja na kitajwa-hivyo ili mawasiliano yafanyike, mfumo wa ishara lazima ufahamike na ukubaliwe na wanajamii wote. Kwa upande wa parole, anadai kuwa ni matendo uneni.

 Ni namna lugha inavyotamkwa katika hali halisi na mtu mmoja mmoja. Dhanna ya parole inalingana na dhanna ya performance (utendi) yaNoam Chomsky. Katika lugha, parole ni matamshi tofauti ya sauti moja-alofoni. Wanaisimu wanaonekana kukubaliana na madai yaSaussure kwa kuwa inaelekea kuthibitika kuwa hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kitaja na kitajwa [alama (lugha) na kinachowakilishwa (masilugha)], bali makubaliano baina ya wazungumzaji wa lugha moja husika ndiyo hutawala.

(iii)       Nikolai Trubetzkoy (1890-1939) Ni miongoni mwa waanzilishi wa taaluma ya fonolojia akichota mizizi ya taaluma ya isimu kutoka katika Skuli ya Prague. Mwanaisimu huyu aliandika misingi ya fonolojia kwa kutumia maarifa yaliyoibuliwa na Ferdinand de Saussure. Ni mtaalamu wa kwanza kufasili dhanna ya fonimu. Aliandika vitabu vingi kwa lugha ya Kijerumani, miongoni mwake ni Grundzüge der Phonologie (Principles of Phonology, 1939), ambapo ni katika kitabu hicho ndimo alimotoa fasili ya fonimu pamoja na kubainisha tofauti baina ya fonetiki na fonolojia.

(iv)        Noam Chomsky (1928-) Huyu ni mwanaisimu wa Kimarekani anayevuma sana kwa mchango wake katika taaluma ya isimu kwa ujumla. Dhanna zacompetence (umilisi/umahiri) na perfomance (utendi) zimemfanya awe maarufu ulimwenguni. Dhanna hizi zinaelezea tofauti baina ya maarifa na udhihirishaji wa maarifa hayo ya mtumiaji wa lugha. Katika fonolojia, Chomsky anakumbukwa kwa ufafanuzi wake wa dhana ya fonimu kwa mtazamo wa kisaikolojia. Anapochunguza dhanna hii, hudai kuwa fonimu ni tukio la kisaikolojia, hivyo fonimu zimo kichwani mwa mzungumzaji wa lugha.

Daniel Jones (1881-1967) Ni mwanafonetiki kinara na maarufu kabisa katika nusu ya kwanza ya karne ya ishirini. Ni Mwingereza msomi ambaye alikuwa na shahada ya kwanza ya hisabati na shahada ya umahiri wa sheria, shahada ambazo hata hivyo, hakuwahi kuzitumia. Baadaye, alisomea lugha na kuhitimu shahada ya uzamivu. Daniel Jones alifunzwa fonetiki na maprofesa mbalimbali, japokuwa aliathiriwa zaidi naPaul Passy na Henry Sweet. Hamu yake kuu ilikuwa kwenye nadharia ya fonetiki. Anafahamika zaidi kwa ufafanuzi wa dhanna ya fonimu kwa mtazamo wa kifonetiki (ufafanuzi wake tutauchunguza katika sehemu ya mitazamo ya dhana ya fonimu).

FONETIKI NA FONOLOJIA

Fasili ya taaluma ya fonolojia haiwezi kukamilika, na pengine kueleweka, iwapo hakuna linalosemwa kuhusiana na taaluma ya fonetiki. Hali hii inatokana na ukweli kuwa kuna uhusiano wa kinasaba kati ya fonolojia na fonetiki. Massamba na wenzake (2004:5) wanaeleza ukweli huu kwamba: .... fonetiki na fonolojia ni matawi mawili tofauti ya isimu lakini yenye kuhusiana sana. Uhusiano wa matawi haya unatokana na ukweli kwamba yote mawili yanajihusisha na uchunguzi na uchambuzi unaohusu sauti za lugha za binadamu. Kutokana na ukweli huu, jitihada za kufasili dhanna ya fonolojia inaelekea kuwa nyepesi, dhanna hizi mbili zinapofasiliwa kwa mlinganyo. Tuanze na fonetiki:

FONETIKI NI NINI?

Fonetiki ni tawi la isimu linalochunguza sauti za kutamkwa na binadamu ambazo huweza kutumika katika lugha asilia. Massamba na wenzake (kama hapo juu) wanafasili fonetiki kuwa ni tawi la isimu linalohusika na uchunguzi na uchambuzi wa taratibu za utoaji, utamkaji, usafirishaji, usikiaji, na ufasili wa sauti za lugha za binadamu kwa ujumla. Wanasisitiza kwamba, kinachochunguzwa katika fonetiki ni [maumbo] mbalimbali ya sauti zinazoweza kutolewa na alasauti za binadamu (yaani sauti za binadamu zinazotamkwa tu). Kipashio cha msingi cha uchambuzi wa kifonetiki ni foni. Foni ni sauti yoyote inayotamkwa na binadamu na inayoweza kutumika katika lugha fulani. Hivyo basi, foni ni nyingi sana na hazina maana yoyote. Wanafonetiki hudai kuwa foni zimo katika bohari la sauti (dhanna dhahania) ambalo kila lugha huchota sauti chache tu ambazo hutumika katika lugha mahususi. Sauti chache zinazoteuliwa na lugha mahususi kutoka katika bohari la sauti huitwa fonimu.

 Matawi ya Fonetiki:

Kuna mitazamo miwili tofauti kuhusiana na matawi  ya fonetiki. Mtazamo wa kwanza ni unaodai kuwepo matawi matatu; na mtazamo wa pili ni unaodai kuwepo matawi manne. Mtazamo wa kuwepo matawi matatu unataja fonetiki matamshi, fonetiki akustika (safirishi), nafonetiki masikizi. Mtazamo wa kuwepo matawi manne (kama Massamba na wenzake (kama hapo juu), pamoja na matawi tuliyokwisha yataja, wanongezea tawi la fonetiki tibamatamshi.

(a)     Fonetiki matamshi huchunguza jinsi sauti za lugha zinavyotamkwa kwa kutumia alasauti. Hususani, huchunguza namna na mahali pa kutamkia sauti husika mfano: [p] Ni kipasuo sighuna cha midomo.

(b)     Fonetiki akustika huchunguza jinsi mawimbi ya sauti yanavyosafiri kutoka katika kinywa cha mtamkaji hadi kufika katika sikio la msikilizaji.

(c)     Fonetiki masikizi hujihusisha na mchakato wa ufasili wa sauti za lugha, hususani uhusiano uliopo baina ya neva za sikio na za ubongo.

(d)     Fonetiki tibamatamshi ni tawi jipya lililozuka mwanzoni mwa karne hii, ambalo huchunguza matatizo ya utamkaji ambayo binadamu huweza kuzaliwa nayo au kuyapata baada ya kuzaliwa. Ni tawi linalojaribu kutumia mbinu za kitabibu kuchunguza matatizo na kutafuta namna ya kuyatatua mfano: Kuna tatizo la mtu kuzaliwa na paa la kinywa au kaakaa lililogawanyika ambalo huathiri matamshi katika usemaji.

FONOLOJIA NI NINI?

Fonolojia ni taaluma ya isimu inayochunguza mifumo ya sauti za kutamkwa zinazotumika katika lugha asilia mahususi za binadamu. Inapolinganishwa na fonetiki, inasisitizwa kuwa fonolojia ni tawi la isimu linalochunguza mifumo ya sauti za lugha mahususi tu, kama vile sauti za Kiswahili, Kiingereza, Kigogo, n.k. Hata hivyo, wapo wanaisimu wanaoelekea kukubaliana kuwa kuna fonetiki ya lugha mahususi pia, na kuna fonolojia ya jumla, na fonetiki ya lugha mahususi. Mathalani,Massamba (1996) licha ya kufasili fonolojia kuwa ni taaluma ya isimu inayochunguza mfumo wa sauti za lugha mahususi, anaenda mbele zaidi na kudai kuwa fonolojia inaweza kuchunguza sauti kwa ujumla wake bila kuzihusisha na lugha mahususi. Akmajian na wenzake (2001), nao wanadokeza msimamo kama wa Massamba wanapodai kwamba fonolojia inaweza kuchunguzwa kwa mitazamo miwili tofauti. Kwanza, fonolojia kama tawi dogo la isimu linalochunguza mfumo na ruwaza za sauti za lugha mahususi ya binadamu; na pili, fonolojia kama sehemu ya nadharia ya jumla ya lugha ya binadamu inayohusika na tabia za jumla za mfumo wa sauti za lugha asilia za binadamu. Katika mhadhara huu, hata hivyo, tutakuwa wafuasi wa mtazamo unaoona kuwa fonolojia ni tawi la isimu linaloshughulikia mfumo wa sauti za lugha mahususi tu, hivyo, tunapata fonolojia ya Kiswahili, fonolojia ya Kiingereza, fonolojia ya Kiha, fonolojia ya Kihehe, na fonolojia ya Kibena, n.k. Kipashio cha msingi cha fonolojia ni fonimu.

FONIMU: Ni kipashio kidogo kabisa cha kifonolojia kinachoweza kubadili maana ya neno. Hivyo basi, fonimu ina maana, kwa kuwa inaweza kubadili maana ya neno inapobadilishwa nafasi katika neno husika. Foni chache zilizoteuliwa kutoka katika bohari la sauti ili zitumike kwenye mfumo wa sauti za lugha mahususi ndiyo fonimu. Hivyo, fonimu ni chache ikilinganishwa na foni. Idadi ya fonimu za lugha hutofautiana kati ya lugha moja na nyingine. Mathalani, Kiarabu kina fonimu ishirini na nane (28), Kiswahili kina fonimu thelathini (30), Kifaransa kina fonimu thelathini na tatu (33), na Kiingereza kina fonimu arobaini na nne (44). Sauti ambayo huweza kubadilishwa nafasi yake katika neno lakini maana ikabaki ileile huitwa alofoni.

Alofoni ni kipashio cha kifonolojia kinachotaja hali ambapo fonimu moja hutamkwa na kuandikwa tofautitofauti bila kubadili maana ya neno. Mfano: Fedha na feza Sasa na thatha, Heri na kheri. Kwa kifupi, alofoni ni matamshi tofautitofauti ya fonimu (sauti) moja.

 MITAZAMO YA DHANNA YA FONIMU

Juhudi za kufasili dhana ya fonimu zilizofanywa na wanaisimu mbalimbali zimezua mitazamo mbalimbali ya namna ya kuchambua dhana hii. Hadi sasa, mitazamo mitatu ifuatayo ndiyo hujulikana zaidi.

(i)          Fonimu kama tukio la Kisaikolojia; Huu ni mtazamo uliokuzwa na kutetewa na wanasarufi geuzi-zalishi, mwanzilishi wake akiwa ni Noam Chomksy. Kwa mujibu wa mtazamo huu, fonimu ni dhanna iliyo katika akili ya mzungumzaji wa lugha. Mtazamo huu unadai kuwa kila mzungumzaji wa lugha ana maarifa bubu ya idadi na jinsi ya kutamka fonimu za lugha yake. Chomsky anayaita maarifa haya kuwa ni umilisi (competence). Anadai kuwa maarifa haya ya fonimu hufanana kwa kiasi kikubwa miongoni mwa wazungumzaji wa lugha moja husika. Kinachotofautiana ni jinsi ya kudhihirisha (kutamka)  fonimu hizo, yaani utendi (perfomance). Chomsky anabainisha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuhitilafiana baina ya umilisi na utendi kutokana na matatizo mbalimbali ambayo mzungumzaji hukabiliana nayo. Matatizo hayo ni kama vile uchovu, ulemavu wa viungo vya matamshi (alasauti za lugha), athari za mazingira, ulevi, na maradhi. Hivyo, kutokana na hali hii, fonimu hubaki kuwa tukio la kiakili, yaani kisaikolojia tu.

(ii)        Fonimu kama tukio la Kifonetiki; Wafuasi wa mtazamo huu wanaongozwa na Daniel Jones. Daniel Jones anaiona fonimu kuwa ni [umbo] halisi.

(iii)       Fonimu kama tukio la kifonolojia; Huu ni mtazamo wa kidhanifu, ambapo huaminika kuwa fonimu ni kipashio cha kimfumo, yaani fonimu huwa na maana pale tu inapokuwa katika mfumo mahususi. Mwanzilishi wa mtazamo huu ni Nikolas Trubetzkoy. Yeye huamini kuwa fonimu ni dhanna ya kiuamilifu na uamilifu huu hujitokeza tu fonimu husika inapokuwa katika mfumo wa sauti wa lugha husika. Kwa mujibu wa mtazamo huu, fonimu ni kipashio kinachobainisha maana ya neno. Mtazamo huu hutumia jozi sahihi kudhihirisha dai lake. Mathalani, maneno kama:

-     baba na bata yana maana tofauti kwa sababu ya tofauti ya fonimu /b/ na /t/. Mtazamo huu hujulikana kuwa ni wa kifonolojia. Na kwa hakika, mawazo haya ndiyo yaliyoshika mzizi zaidi katika taaluma ya fonolojia na ndiyo inayofunzwa hivi sasa katika sehemu nyingi ulimwenguni.

  Tofauti kati ya Fonetiki na Fonolojia

FONETIKI

FONOLOJIA

Huchunguza sauti za lugha ya mwanadamu kwa ujumla.

Huchunguza sauti za lugha mahususi.

Ni pana{huchunguza sauti nyingi}

Ni finyu {huchunguza sauti chache}

Huchunguza sauti zinavyozalishwa

Hushughulika na sauti zinavyotumika

Ni moja tu duniani kote

Ni nyingi kwani kila lugha ina fonolojia yake duniani.

Uwasilisho wa suti hutumia mabano mraba mf. []

Sauti huwasilishwa na mabano mshazari. mfano //

Inahusisha sayansi huru katika uchunguzi wake

Haitumii sayansi huru katika uchunguzi wake

DHANNA YA FONOLOJIA VIPANDE NA FONOLOJIA ARUDHI  

Fonolojia imegawanywa katika aina kuu mbili ambazo ni Fonolojia arudhi na Fonolojia vipande sauti.

(a)     Fonolojia vipande sauti; ni aina ya Fonolojia ambayo hushughulikia uchunguzi wa vipande sauti vyenyewe. Wanaisimu katika aina hii hubainisha vipande sauti bainifu katika lugha kama vile alofoni na fonimu pia hueleza fonimu hizo jinsi zinavyoweza kuathiriana katika maeneo mbalimbali. (Mgullu, 2010).

(b)     Fonolojia arudhi; tawi hili hushughulikia masuala mengine ya sauti ambayo hayaathiri vipashio vikubwa zaidi kuliko fonimu moja. Pia aina hii huchunguza mfumo wa kuweka mkazo katika maneno na tungo katika lugha fulani kama vile kiimbo na muundo wa silabi. (Mgullu, 2010). Fonolojia ya Kiswahili hujishughulisha na vipengele mbalimbali ambavyo vinahusiana na sauti pamoja na mpangilio wake wa uundaji maneno katika lugha mbalimbali. Vipengele hivi ni kama vile; matamshi, kiimbo, mkazo, na mfuatano wa sauti katika kuunda mofimu na maneno.

(i)          Matamshi; ni utaratibu utumikao katika utoaji wa sauti za maneno ya lugha ya binadamu. Utaratibu wa matamshi ya sauti za lugha huzingatia mahali pa matamshi na jinsi ya utamkaji. Mfumo huu ni maalumu kwa sababu binadamu hutumia ala za sauti na upumuaji katika utamkaji.

(ii)        Lafudhi; ni sifa ya kimasikizi inayomtambulisha msemaji anatoka eneo gani kijiografia. Lafudhi hutokana na athari ya lugha ya kwanza au mazingira. Mfano:

   Usiniretee maswara ya ubaguzi wa kikabira hapa (Wakuriya)

    Amemupiga mutoto ya watu juu amemuibia mafaranga makumi mawili (Wakongo)

    Ukikaa nchale, ukichimama nchale (Wamakonde)

    Wewe unakamuaga mang’ombe tu moja

  kwa moja (Wasukuma)

    Mbona unakuwa kinganganizi,

 nilishakwambia sikupendi rakini

 wewe bado unaningangania tu!

 (Wahaya)

(iii)       Silabi; ni kipashio cha utamkaji ambacho kwa kawaida ni kikubwa kuliko fonimu na kidogo kuliko neno. Silabi ni kipashio cha kifonolojia kinachohusu matamshi ya sauti za lugha zinapotamkwa kwa pamoja kama fungu moja linalojitegemea kimatamshi. Fungu hilo laweza kujumuisha sauti moja pekee au sauti mbili kutegemea muundo wa lugha husika. (Massamba na wenzake, 2004). Mpaka wa silabi hutenganishwa na alama ifuatayo; $ mfano: $ma$,$ma$, $a$,$na$,$ku$,$la$.

(iv)         Kiimbo; ni utaratibu maalumu wa upandaji na ushukaji wa mawimbi ya sauti katika usemaji wa lugha au kiimbo ni kipengele cha kifonolojia chenye maana ya kupanda na kushuka kwa mawimbi ya sauti za lugha. Vilvile kiimbo ndicho kinafanya sentensi iwe ya swali, mshangao au maelezo. Mfano.

o   John ameondoka?

o   John ameondoka!

o   John ameondoka.

(v)          Mkazo/shadda; Katika lugha ya Kiswahili kuna namna ya kutamka maneno ili kuleta maana mbali mbali, kwa mfano neno “barabara” litaleta maana husika kulingana na jinsi lilivyotamkwa. Hivyo, mkazo ni pale silabi inapotamkwa kwa kukazwa. Maneno ya Kiswahili huwa na silabi moja ambayo hutamkwa kwa nguvu zaidi kuliko silabi nyingine. Unapotamka silabi iliyotiwa mkazo, sauti hupandishwa juu kiasi.

Maneno mengi ya Kiswahili, hasa yale yenye asili ya Kibantu hutia mkazo katika silabi ya pili kutoka mwisho.

Kwa mfano: ba’bu, maya’i, rama’ni (mimi nilikuwa nikitamka ra’mani), baraba'ra (njia).

Baadhi ya maneno yenye asili ya kigeni, huwa na mkazo katika silabi nyingine. Kwa mfano: bara'bara (sawa sawa), Alha’misi. Zipo baadhi ya lugha zenye uwezo wa kuhamisha mkazo na maana ya neno ikabadilika.

Mfano: Kiingereza

     A                  B

         Produ’ce          Pro’duce

  (zalisha)          (mazao)

         Pro’ject          Proje’ct

(mradi)        (panga mradi)

         Per’mit            Permi’t

(ruhusu)          (ruhusa)

Katika lugha kama kiingereza mkazo unaweza kuhama na kubadili maana lakini katika Kiswahili mkazo huwa hauwezi kuhama.

(vi)        Kidatu, Massamba, Kihore, na Msajila (2004), wanakitazama kidatu kwa maana ya sauti isikikayo wakati wa utamkaji ama kuwa juu, kuwa katikati, au kuwa chini. Hii humaanisha kwamba katika usemaji, mtu anaweza kupandisha kiwango cha sauti (yaani akaiweka katika kidatu cha juu), kukishusha kidogo kiwango hicho na kuiweka sauti katika kidatu cha kati, au kukishusha zaidi na kuiweka sauti katika kidatu cha chini. Ni muhimu kuelewa kwamba kupanda au kushuka kwa mawimbisauti na kupanda au kushuka kwa kiwango cha kidatu ni vitu viwili tofauti. Kupanda au kushuka kwa mawimbisauti si lazima kuathiri kidatu; wala kidatu si lazima kuathiri kupanda au kushuka kwa mawimbisauti. Hii ni kwa sababu mzungumzaji anaweza kusema kwa kidatu cha juu (sauti ya juu), kidatu cha kati (sauti ya kati) au kidatu cha chini (sauti ya chini) na bado akaweza kubadilisha mawimbisauti akiwa katika kidatu hicho hicho kimoja. Lakini pia mzungumzaji anaweza kubadili kidatu. Kwa mfano, anaweza kuanza kuzungumza kwa sauti ya juu (kidatu cha juu) akamalizia kwa sauti ya kati (kidatu cha kati) au sauti ya chini (kidatu cha chini).

Othografia; Kila lugha ina mfumo tofauti wa usemaji na hutumia mfumo tofauti wa sauti. Kila lugha inakuwa haina budi kubuni mfumo wake wa kuziwakilisha sauti zake katika maandishi. Mfumo huo wa maandishi ndio ujulikanao kama othografia. Mfumo huu huwa unawasilisha herufi maalumu zinazobuniwa ili kuwakilisha sauti za lugha inayohusika kimaandishi. Neno uthografia lina asili ya kigiriki na maana yake ni utaratibu wa kutumia alama au michoro ya maandishi kuwakilisha sauti zisikikazo katika lugha.

(vii)       Toni; Kwa mujibu wa Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha (2009:87). Toni ni sifa inayowakilisha kiwango pambanuzi cha kidatu cha silabi katika neno au sentensi na ambayo huweza kubadilisha maana ya neno katika sentensi kisemantiki au kisarufi. Hivyo basi, Toni ni sifa katika lugha ambapo maana ya neno huathiriwa na jinsi linavyotamkwa. Au. Toni ni kiwango cha kidatu pamoja na mabadiliko yake ambayo hutokea wakati mtu anapotamka silabi au neno. Katika lugha mabadiliko ya toni hubadili maana za yale yanayosemwa na sifa za toni hubainika katika kiwango cha neno na silabi zake mbalimbali. Lugha nyingi za kibantu kama vile kikuyu na kikamba zina sifa ya toni lakini lugha ya Kiswahili haina sifa hii. Kuna aina tatu za toni ambazo ni, Kwanza, toni juu ni toni ambayo hudhihirishwa na kidatu cha juu. Pili, toni kati ni toni ambayo hudhihirishwa na kidatu cha kati. Tatu, toni chini ni toni ambayo hudhihirishwa na kidatu cha chini.

MUHADHARA WA II:

VITAMKWA VYA LUGHA KWA UJUMLA:

SAUTI ZA LUGHA ASILIA

Wanaisimu wengi wanakubaliana kwamba lugha ya binadamu ni mfumo wa sauti nasibu zenye kubeba maana na ambazo hutumiwa na jamii fulani ya watu kwa madhumuni ya mawasiliano ya kimazoea tu ya watumiaji wa lugha inayosikika kati yao. Sauti nasibu ni sauti ambazo uteuzi wake haukufanywa kwa kufuata mantiki au vigezo fulani maalumu bali umetokana na makubaliano ya kimazoea tu ya watumiaji wa lugha husika. Hii ndiyo maana sauti za lugha mbalimbali  zinaweza kufanana sana au kwa kiasi fulani tu. Na pia zinaweza kusigana sana au kiasi fulani tu.

Mhimili muhimu wa lugha asilia ni sauti zitumikazo kuunda silabi au mofimu. Uunganishaji wa mofimu huunda maneno, maneno huunda virai, virai huunda vishazi na vishazi huunda sentensi. Utaratibu wa kuunganisha sauti kuunda maneno ni wa nasibu kama ambavyo sauti zenyewe ni za nasibu.

ALASAUTI ZA LUGHA ASILIA

Alasauti ni viungo vya mwili vinavyotumika katika utamkaji wa sauti mbalimbali za lugha. Utamkaji wa sauti zitumiwazo katika lugha ya mwanadamu hufanyika kwa kutumia sehemu au viungo mbalimbali maalumu vya mwili wa mwanadamu. Katika taaluma ya Isimu sehemu ya maneno yatumikayo katika utamkaji wa sauti za lugha hujulikana kama ala za sauti.

Ala hizo za sauti za lugha ni:

-    Mapafu

-    Umio

-    Kaakaa gumu na laini

-    Ulimi

-    Ufizi

-    Meno

-    Midomo

-    Pua, n.k

Kwa kutumia ala hizo mwanadamu anaweza kuzalisha sauti mbalimbali.

FONOLOJIA NA MOFOLOJIA

Fonolojia ni tawi la isimu linalojishughulisha na sauti za lugha mahususi jinsi zinavyotamkwa na mahali zinapotamkiwa.

Mofolojia ni taaluma ya kiisimu inayojishughulisha na maumbo ya lugha jinsi yanavyoundwa na kazi za maumbo hayo katika lugha.

Fonolojia na mofolojia hutegemeana kwa misingi kwamba mofolojia hutegemea sauti za fonolojia katika kuunda maumbo mbalimbali. Sauti hizo huunda silabi,mofimu na maneno. Bila fonolojia mofolojia haiwezi kufanya kazi wala uchambuzi wa haukamiliki.

Mfano: “baba” umbo hilo limeundwa na :

Fonimu -------4: b+a+b+a       

Silabi------- 2: ba + ba

Katika mfano huo utabaini kuwa umbo “baba” ni umbo tu la kimofolojia lakini uchanganuzi wake hutegemea fonolojia.

MUHADHARA WA III:

VITAMKWA VYA MSINGI VYA KISWAHILI SANIFU

Kitamkwa ni sauti dhahiri inayosikika wakati wa utamkaji wa maneno. Vitamkwa huwakilishwa kimaandhishi kwa kutumia alama zijulikanazo kama herufi za alfabeti. Mfano: p,the,dh, n.k

Kitamkwa hujitokeza kama kipande sauti kinachojibainisha kwa dhati yake kwa mfano: p,b, kila kimoja kina ubainifu uliowazi kwa kuzingatia vitamkwa hivyo vinavyosikika masikioni, ni dhahiri kwamba /p/ hutamkwa tofauti na /b/.

Vitamkwa vya kifonetiki

Tunapochunguza vitamkwa vya kifonetiki tunazingatia sauti za lugha jumla. Kifonetiki kitamkwa huzingatiwa jinsi kinavyotamkwa, kusafirishwa, usikikaji wake na ufasili wa vitamkwa hivyo bila kuvihusisha na lugha fulani maalumu.

Uchambuzi wa vitamkwa vya kifonetiki huzingatia sifa za jumla za vitamkwa kama vile kipasuo kutamkiwa kwenye midomo, kuviringa midomo, n.k

Hizo ni sifa za kitamkwa [p], sifa hizo huweza kujitokeza pia kwenye umbo [b]. katika kiwango hiki huwa haijalishi kama sauti zinazochunguzwa zinatumika kuundaa maneno tofauti katika lugha au la.

Vitamkwa vya kifonolojia

Hapa vitamkwa huchunguzwa katika lugha maalumu jinsi vinavyotamkwa, vinapotamkiwa na jinsi vinavyohusiana na kuathiriana kimatumizi katika kuunda maneno. Mfano: pumba,bumba,taka,daka

Katika mifano hiyo vitamkwa [p,b,t,d] vinaleta utofauti wa kimaana vinapotumika katika maneno.

Fonimu kwa ujumla

Fonimu – ni kitamkwa cha msingi katika lugha kituwacho kuunda maneno ya lugha fulani maalumu mfano: /p/,/b/,/u/,/m/,/t/,/d/,/a/,/k/,/n/ huweza kuunda maneno kama[ pumba,tunda,bumba,daka,] n.k. vilevile fonimu huweza kubadili maana ya neno.

Mfano:

-    Pumba – bumba

-    Funda – dunda

-    Damu – daku

-    Taka – daka

Fonimu huweza kubatilisha maneno yaani kuyafanya maneno yawe batili kwa jinsi yalivyoundwa.

Mfano:

-    Kaka – gaka

-    Sasa – thasa

-    Shoga – shosha

Dhanna ya alofoni

Alofoni ni nini?

Mgullu (1999) akimnukuu Hartman (1972) anasema kuwa alofoni ni sauti mojawapo miongoni mwa sauti kadhaa zinazowakilisha fonimu moja.  Alofoni hutokea katika mazingira mahsusi (mazingira ya kiutoano).

Aidha, Mgullu (1999) akimnukuu Ladefoged (1962) anasema kuwa alofoni ni matamshi tofauti tofauti ya fonimu moja.  Pia anasema alofoni za fonimu moja huunda kundi moja la sauti ambazo;

1.      Hazibadili maana ya neno,

2.      Hutokea katika mazingira tofauti ya kifonetiki, na

3.      Alofoni zote hufanana sana kifonetiki.

Kutokana na fasili hizo, tunaweza kusema alofoni ni maumbo tofauti tofauti ya fonimu moja, ingawa maumbo hayo huwa na tofauti ndogo ndogo za kifonetiki lakini hayaleti tofauti yoyote katika maana za maneno.

Tuchukue mifano ya maneno kutoka katika lugha ya Kiingereza;

                   tea; eat; writer;    

               /thi:/  /i:t/ /raita/         

Katika maneno yetu hapo juu sauti [th] inayotokea mwanzoni mwa neno, na sauti [t] inayotokea popote ni alofoni za fonimu /t/. Sauti hizi hazibadili maana ya maneno, zinatokea katika mazingira tofauti na zinafanana sana kifonetiki.

Katamba (1996) anasema alofoni zinaweza kujitokeza pia katika maneno:

                tea;  two; eighth;

               /ti:/  /twu/ /eitɵ/

[t] katika /ti:/  hutamkwa wakati midomo ikiwa imesambaa, [tw] katika /twu/  hutamkwa wakati midomo ikiwa mviringo na [t] katika /eitɵ/ ni sauti ya meno. Hivyo [t], [tw] na [t] ni alofoni za fonimu /t/

Katamba, anasema si kila sauti zenye kubadilishana mazingira basi zaweza kuwa alofoni katika lugha ya Kiingereza. Kwa mfano sauti /h/ na /ŋ/ hubadilishana mazingira ya utokeaji (sauti  /h/ hutokea mwanzoni mwa silabi ikifuatiwa na irabu mfano;  hat, head, n.k wakati sauti /ŋ/ hutokea mwishoni mwa silabi katika konsonanti zilizoungana, mfano; longer, long, bung n.k),   lakini hazifanani kifonetiki hivyo haziwezi kuwa alofoni za sauti moja.

Aghalabu alofoni hutumiwa katika muktadha au mazingira ya kifonetiki yaliyo tofauti, ambapo alofoni moja ikitumika katika mazingira fulani basi nyingine haiwezi kutumika  katika mazingira hayo  hayo.

  Mbinu za kuzitambua fonimu na alofoni.

Kuna mbinu mbalimbali za kuzibainisha fonimu na alofoni za lugha fulani. Mbinu au njia hizo ni kama; kufanana kifonetiki, jozi za mlinganuo finyu, mgawanyo wa kiutoano na mpishano huru.

(i)          Mbinu ya kufanana  kifonetiki.

Mbinu hii huelezea kwamba sauti ambazo huwa na sifa za kifonetiki zinazofanana basi huchukuliwa kuwa ni sauti za fonimu moja (alofoni). Kama sauti hazina sifa za kifonetiki zinazofanana basi huchukuliwa kama ni fonimu mbili tofauti. Kwa mfano tuchunguze sifa za kifonetiki za sauti /i/ na /u/ katika lugha ya Kiswahili;

       /i/                       /u/

     +irabu                    +irabu

    +mbele                     +nyuma

    +juu                       +juu

   -mviringo                   +mviringo

Kwa mujibu wa kigezo hiki, sauti /i/ na /u/ ni fonimu mbili tofauti katika lugha ya Kiswahili kwa sababu zina sifa tofauti za kifonetiki.

(ii)        Mbinu ya Jozi za Mlinganuo finyu.

Kama anavyoeleza Fischer (1975), mlinganuo finyu ni tofauti ndogo kabisa ya kifonolojia iliyopo baina ya maneno fulani: aghalabu maneno hayo huwa na;

         Idadi sawa ya fonimu

          Fonimu zinazofanana isipokuwa moja katika mazingira sawa ya kifonetiki

          Mpangilio wa fonimu uliosawa

         Maana tofauti

Tuchunguze seti ya maneno yafuatayo;

Pia      -       lia

Paka    -     taka

Wali    -      hali

Katika seti ya maneno hapo juu tunaona kwamba maneno /pia/ na /lia/ yapo katika jozi mlinganuo finyu kwa sababu yana idadi sawa ya fonimu, yaani fonimu tatu kila neno, fonimu zinazofanana isipokuwa moja, na mpangilio wa fonimu ulio sawa na maana zikiwa tofauti. Halikadhalika katika seti ya maneno /paka/ na /taka/ kwa sababu nayo yana idadi sawa ya fonimu yaani, fonimu nne zinazofanana isipokuwa moja na mpangilio wa fonimu ulio sawa. Pia katika seti ya maneno /wali/ na /hali/ tunaona kuwa yapo katika jozi mlinganuo finyu kwa sababu yana idadi sawa ya fonimu yaani fonimu nne zinazofanana isipokuwa moja na mpangilio wa fonimu ulio sawa. Njia hii hutusaidia kuzitambua fonimu za lugha kwa sababu tofauti ya fonimu moja yatosha kubadili maana za maneno hayo.

(iii)        Mbinu ya mgawanyo wa kiutoano.

Hyman (1975) anasema katika fonolojia, utoano ni dhanna ambayo hutumika kuelezea uhusiano uliopo baina ya sauti mbili (au zaidi) za fonimu moja ambazo haziwezi kutokea katika mazingira sawa katika neno. Hii ina maana kwamba sauti huwa ina mahali/mazingira yake maalum ambayo hayawezi kukaliwa na sauti nyingine ya kundi moja.

Tuchunguze mifano kutoka katika lugha ya Kiingereza; kuhusu sauti /ph/ yenye mpumuo na sauti /p/ isiyo na mpumuo. Sauti /ph/ yenye mpumuo hutokea mwanzoni mwa maneno tu, kwa mfano katika maneno /phin/, /phen/, /phut/ n.k . Kwa upande mwingine /p/ isiyo na mpumuo hutokea sehemu yoyote ya neno isipokuwa mwanzoni; mfano katika maneno kama /top/, /cup/, /span/, /spare/ n.k

Sauti ambazo ziko katika mgawanyo wa kiutoano huwa hazitofautishi maana za maneno, isipokuwa sauti hizo hugawana tu mahala pa kutokea au kutumika. Hivyo sauti hizo huwa ni alofoni za fonimu moja.

Tuchunguze sifa bainifu za sauti /ph/ yenye mpumuo  na  sauti /p/ isiyo na mpumuo;

       /ph/                      /p/

      +kons                    +kons

     +mpumuo                   -mpumuo

    -ghuna                     -ghuna

    +midomo                    +midomo

    +kipasuo                   +kipasuo

[ph] yenye mpumuo  na  sauti [p] isiyo na mpumuo ni alofoni za fonimu /p/. Sifa zote za sauti hizi zinafanana isipokuwa moja tu (sifa ya mpumuo).

(iv)        Mbinu ya Mpishano Huru.

Huu ni uhusiano wa fonimu mbili tofauti kubadilishana nafasi moja katika maneno maalum bila kubadili maana za maneno hayo. Hapa mpishano unatumika kwa ile maana ya “wewe ondoka, mimi niingie.” Kwa kuwa fonimu moja inatolewa katika neno fulani na fonimu nyingine inakaa mahali pake bila kubadili maana ya neno hilo. Mpishano huru unahusisha fonimu mbili kubadilishana nafasi moja katika neno moja.  Fonimu hizo huwa ni tofauti kabisa kifonetiki hivyo hatuwezi kuziita alofoni.

     Tuchunguze mifano ifuatayo;

         /buibui/ na /baibui/ sauti /u/ na /a/ zimepishana nafasi bila kubadili maana ya neno.

         /Wasia/ na /wosia/ sauti /a/ na /o/ zimepishana bila kubadili maana ya maneno.

         /kheri/ na /heri/ sauti /kh/ na /h/ zimepishana bila kubadili maana ya maneno.

Tuchunguze sifa bainifu za kifonetiki za sauti /a/ na /u/ katika maneno /baibui/ na /buibui

       /a/                        /u/

     +irabu                      +irabu

     +mbele                      +nyuma

    +chini                       +juu

    -mviringo                    +mviringo

Tuchunguze pia sifa bainifu za kifonetiki za sauti /a/ na /o/ katika maneno /wasia/ na /wosia/              

        /a/                            /o/

      +irabu                          +irabu

      +mbele                          +nyuma

      +chini                          +nusujuu

     -mviringo                        +mviringo

Sauti hizi haziwezi kuwa alofoni kwa sababu zinatofautiana sana kifonetiki. Pia sauti hizi haziachiani mazingira ya utokeaji wake hivyo ni ngumu sana kuyaelezea mazingira ya utokeaji wake.

Njia hizi zitumikapo, aghalabu kwa pamoja, kwa kusaidiana huweza kutusaidia kutambua fonimu na alofoni za lugha inayofanyiwa uchunguzi.

Alofoni katika lugha ya Kiswahili.

Sasa tuchunguze dhana ya alofoni kama inavyojadiliwa na wataalamu mbalimbali wa Isimu ya Kiswahili. Hapa tutaonesha fasili pamoja na mifano ya alofoni katika lugha ya Kiswahili kwa mujibu wa wataalamu hao.

Massamba na wenzake (2013) wanasema alofoni ni sura au maumbo mbalimbali ya fonimu moja.  Fonimu za lugha huweza kupata sura tofauti tofauti kulingana na mazingira katika neno ambamo hutokea. Hii ina maana kwamba fonimu inaweza kubadilika ikachukua umbo moja kutokana na kutokea kwake katika mazingira fulani na inaweza pia kubadilika ikachukua umbo jingine kutokana na kutokea kwake katika mazingira mengine tofauti katika neno. Wanatoa mifano ya alofoni kutoka katika lugha ya Kiswahili kama ifuatavyo:

 Mofimu za neno                                  Matamshi yake

(a) ki+ti   ki+refu                              [kiti kirɛfu]

(b) ki+ti   ki+eusi                              [kiti ʧeusi]

(c) u+limi m+refu                                [ulimi mrɛfu]

(d) n+limi n+refu                                [ndimi ndɛfu]

(e) n+buzi                                       [mbuzi]

(f) n+dama                                       [ndama]

(g) n+gombe                                      [ŋɔmbɛ]

Katika mifano ya Kiswahili hapo juu, tunaona mabadiliko ya kifonimu yakijitokeza.  Katika mfano wa (b) fonimu /k/ inapofuatiwa na irabu  /i/  halafu kukawa na mpaka wa mofimu, kisha  ikafuatiwa na irabu /e/ hubadilika na kuwa /ch/  ki+eusi = [ʧeusi] na katika  (d)  tunaona  wazi  kuwa  fonimu /l/ inapotanguliwa na nazali /n/ hubadilika na kuwa /d/  [n+limi = ndimi]. Halikadhalika katika mifano ya (e) na (g) tunaona kwamba nazali /n/ inapofuatiwa na kitamkwa  /b/ hubadilika na kuwa /m/, inapofuatiwa na kitamkwa /d/ hubakia /n/, na inapoafuatiwa na  kitamkwa /g/ hubadilika na kuwa /ŋ/. Hii  ina  maana  kwamba  katika  mazingira  haya  sauti  [ʧ]  ni  alofoni  yafonimu  /k/,  [d]  ni  alofoni  ya  fonimu /l/  na  [m],  [n]  na  [ŋ]  ni  alofani  za  fonimu  /n/(katika  fonolijia  herufi  hii  kubwa  hutumika  kuwakilisha dhanna  ya  nazali) na alama /N/ ikiwa kama kiwakilishi cha fonimu kuu.

Alofoni hizo hapo juu zimetokana na michakato ya kimofofonolojia (taaluma ya isimu inayoshughulikia uchunguzi na uainishaji wa vipengele vya kifonolojia vinavyoathiri maumbo ya mofimu au vipegele vya kisarufi vinavyoathiri maumbo ya fonimu). Pamoja na kwamba mabadiliko haya yameitwa mabadiliko ya kifonimu lakini tukichunguza vizuri tutaona kwamba kwa kiasi kikubwa ni maumbo yaliyobadilika na kwa kiasi fulani ni fonimu.

Kwa mfano, mofimu ya ngeli ya tisa {-n-} katika majina kama vile nyumba, mbuzi, ng’ombe, n.k (inabadilika katika mazingira tabirifu) kuwa mofimu {m}, {ŋ} na wakati mwingine hubaki vilevile {n}. Mchakato huu huitwa mchakato wa au kanuni ya konsonanti kuathiri nazali. Hivi kwamba mofimu {n} hubadilika na kuwa mofimu {m} pale inapokuwa imeitangulia sauti ya midomo. Halikadhalika fonimu {n} hubadilika na kuwa mofimu {ŋ} pale inapokuwa imeitangulia sauti ya kaakaa laini.

Kwa mantiki hii basi maumbo haya yote yatakuwa yanaiwakilisha mofimu moja yaani ngeli ya tisa {-n-}. Kama hivi ndivyo basi maumbo hayo yatakuwa ni alomofu na si alofoni.

Alomofu ni mojawapo ya viwakilishi viwili au zaidi vya mofimu moja ambavyo hujitokeza katika mazingira tofauti ya mtoano. Massamba na wenzake (2012)

Katika data ambayo imetolewa na Massamba na wenzake kuna baadhi ya sauti ambazo zinatokana na michakato ya kifonolojia au badiliko la kifonolojia ambapo nazali huiathiri konsonanti inayoambatana nayo ili kurahisisha matamshi. Sauti zinazoathirika hapa ni sauti za likwidi (kimadende /r/ na kitambaza /l/).

(a) u+limi m+refu                 [ulimi mrɛfu]

(b) n+limi n+refu                 [ndimi ndɛfu]

Sauti /l/ hubadilika na kuwa kipasuo /d/ katika mazingira ya kutanguliwa na nazali /n/, vilevile sauti /r/ hubadilika na kuwa kipasuo /d/ katika mazingira ya kutanguliwa na nazali /n/.

Sauti hizi zinatokea katika mazingira ya kiutoano na zinafanana sana kifonetiki hivyo twaweza kuziita alofoni.

Tuchunguze sifa za kifonetiki za sauti /r/ na /d/, na /l/ na /d/

  /r/        /d/                 /l/            /d/

+kons      +kons                +kons           +kons +ufizi     +ufizi               +ufizi          +ufizi

+kimadende +kipasuo          +ktambaza       +kipasuo

Mdee (1986), anadai kuwa sauti [x] na [h] ni alofani za fonimu /h/ kama inavyodhihirika katika  maneno /kheri/ na /heri/.

Tukichunguza sauti hizi, ni kweli kwamba  hazileti  tofauti za maana katika lugha ya  Kiswahili  isipokuwa  sauti hizi  ni  tofauti  mno  kifonetiki. Wakati sauti /x/ ni ya kaakaa  laini,  sauti /h/ ni ya glota.

Je, sauti moja inaweza kutamkiwa katika sehemu mbili tofauti?

Matinde (2012) anasema alofoni ni maumbo mawili au zaidi ambayo huwakilisha fonimu moja. Anaendelea kwa kusema kuwa alofoni ni matamshi tofauti tofauti ya fonimu moja ambayo hujitokeza kutegemea mazingira ya utokeaji wa sauti hiyo.

Matinde, yeye anatofautiana na wanaisimu kama Mdee ambao wanasema lugha ya Kiswahili ina alofoni kwa kutumia jozi za maneno /kheri/ na /heri/ wakisema /x/ na /h/ ni alofoni za fonimu /h/. Anasema tukizingatia vigezo vya kutambulisha alofoni, hizi ni sauti ambazo ni tofauti kabisa kwa misingi ya sifa bainifu za kifonetiki, hususan jinsi ya kutamkwa na mahali pa kutamkiwa.

Matinde, anasema alofoni katika lugha ya Kiswahili sawa na lugha ya Kiingereza, hudhihirika na vipasuo hafifu, hivi kwamba kipasuo hafifu kinapokuwa mwanzoni mwa neno kutamkwa kikiwa na mpumuo, ilhali kipasuo hicho kinapotanguliwa na fonimu tofauti hutamkwa bila mpumuo.

 Kwa mfano  neno /pale/ kipasuo (p) hutamkwa kikiwa na mpumuo (ph) lakini kipasuo hicho kinapotanguliwa na fonimu tofauti kwa mfano katika neno /alipo/ kipasuo /p/ hutamkwa bila mpumuo. Anaendelea kueleza kuwa hali hii hudhihirishwa pia katika maneno;

Neno                                       Utamkaji

Katika                                     /khatika/

Palipo                                      /phalipo/

Panda                                      /phanda/

Kaa                                        /khaa/

Kwa hivyo, maumbo yote mawili yaani  [p] na [ph] ni alofoni za fonimu /p/. Aidha, maumbo [k] na [kh] ni alofoni za fonimu /k/.

Sauti alizozionesha Matinde  kama alofoni ni vibadala tu katika lugha ambavyo hutokana na tofauti za kilahaja. Lakini pia mtindo wa uzungumzaji waweza kusababisha vibadala hivi. Ndio maana si ajabu kukutana na binti wa kimjini akitamka kwa madaa “palipo uzia penyeza mapenzi”.

Matamshi yake ni kama;  /phalipho uzia phenyeza maphenzi/

Mpumuo sio sifa bainifu ya sauti za Kiswahili sanifu. Sifa bainifu za sauti za Kiswahili ni kama vile; sifa ya ukonsonanti, namna ya kutamka, mahali pa kutamkia, mkao wa glota na unazali.

MUHADHARA WA IV:

SIFA PAMBANUZI (BAINIFU) ZA VITAMKWA VYA KISWAHILI

SIFA KUU ZA KONSONANTI

Katika taaluma ya fonolojia konsonanti zina sifa nyingi, hata hivyo sifa kuu za jumla ndizo hushughulikiwa zaidi. Sifa hizo za jumla ni jinsi konsonanti zinavyotamkwa,mahali zinapotamkiwa na kundi asilia la sauti husika.

Sifa ya jinsi ya matamshi hutusaidia kupata makundi asilia ya konsonanti kama vile vipasuo,vikwamizi,nazali,vilainisho,viyeyusho na irabu.

    AINA ZA SAUTI KONSONANTI

1.  Vipasuo ni sauti ambazo hutamkwa kwa mkondo hewa toka mapafuni kuzuiwa na kisha kuachiwa ghafla.

Mfano:

         Aina

Ghuna

sighuna

mifano

Vipasuo vya midomo

b

p

Papai,baba

Vipasuo vya ufizi

d

t

doa, toa

Vipasuo vya vya kaakaa gumu

 ɟ

 c

Juma, chama

Vipasuo vya vya kaakaa laini

g

k

gunia, kabati

2.  Vikwamizi ni sauti ambazo hutamkwa kwa mkondo wa hewa kuzuiliwa nusu hivyo kusababisha hewa kukwamakwama wakati wa utamkaji hewa hupenya na kupitia katika nafasi iliyowazi.

Aina

ghuna

sighuna

mifano

Vikwamizi vya mdomo meno

v

f

Vema, fata

Vikwamizi vya meno

ð

θ

Dhanna, thumni

Vikwamizi vya ufizi

z

S

Zee, saa

Vikwamizi vya kaakaa gumu

-

ʃ

- shamba

Vikwamizi vya kaakaa laini

ɣ

x

ghala, kheri

3.  Vizuio kwamizi ni sauti zenye kutamkwa kwa mkondo wa hewa kuzuiwa na kuachiwa taratibu kwa kukwama kwama hivyo kuzalisha vizuio kwamizi.

Mfano:

   Aina

ghuna

sighuna

  Mifano

Vizuio kwamizi vya ufizi

 ɟ

c

Juma, chuma

Katika lugha ya Kiswahili vizuio kwamizi ni vichache mno ila vipo katika ya Ibo, Yoruba, n.k

[PΦ],[bβ],[tθ],[dð],[gz]

4.  Nazali/Ving’ong’o

Sauti hizi hutamkwa kwa hewa kupitia chemba ya pua. Wakati wa kuzitamka sauti nazali kaakaa laini hushuka chini na kuzuia mkondo hewa unaopitia kinywani na kupitia puani.

Sauti nazali pia zipo ghuna na sighuna ingawa katika Kiswahili nazali zote ni ghuna kwa sababu hutamkwa kwa msogeano mpana.

Mfano:

Aina

ghuna

sighuna

mifano

Nazali ya midomo

m

  -

Mama,mtoto

Nazali ya mdomo meno

ɱ

  -

Mvi

Nazali ya ufizi

n

  -

Nani

Nazali ya kaakaa gumu

  -

Nyau

Nazali ya kaakaa laini

ŋ

  -

Ng’ambo

5.  Vilainisho (Ligwidi)

Kundi hili linahusisha aina mbili za sauti ambazo ni vimadende na vitambaza.

(i)          Vimadende- ni sauti inayotamkwa wakati ala fulani inachezacheza kwenye mkondo wa hewa.

Mfano: /r/ kama katika ramani

(ii)        Vitambaza- ni sauti zinazotamkwa kwa msogeano wa kubana katikati ya chemba ya kinywa. Hewa hubanwa na kupita kwenye pembe ya ulimi. Mfano: /l/ kama katika lala

6.  Viyeyusho

Ni sauti za kawaida katika lugha ya Kiswahili na huitwa hivyo kwa sababu vinatokea baada ya maathiriano ya irabu kuzalisha sauti mpya ambayo hushiriki sifa za irabu na wakati si irabu kwa asili. Katika Kiswahili viyeyusho ni viwili tu navyo ni /w/ na /y/.

7.  Irabu/Vokali/Vokoidi

Irabu ni sauti zinazotamkwa kwa msogeano mpana n azote ni ghuna isipokuwa kwa baadhi ya lugha za nchi fulani kama kichina na kijapani.

Uainishaji wa irabu

Katika kuainisha irabu mambo yanayozingatiwa ni:

(a)     Mwinuko wa ulimi

Hapa tunazingatia kama ulimi umeinuka juu kabisa,juu kiasi,chini kiasi au chini kabisa.

-    Irabu za juu kabisa (i,u)

-    Irabu za juu kiasi (e,o)

-    Irabu za chini kiasi (ɛ, ɔ)

-    Irabu za chini kabisa (a,ɑ)

(b)     Sehemu ya ulimi iliyoinuka

Hapa tunaangalia ulimi kama umeinuka sehemu ya mbele au ya nyuma,hii hutupatia irabu za mbele na irabu za nyuma.

-    Irabu za mbele ni (i, e, ɛ, a)

-    Irabu za nyuma ni (u, o, ɔ, ɑ)

(c)     Umbo la midomo

Utamkaji wa sauti irabu huwa wa umbo la mdomo mviringo au mtandazwa.

-    Irabu za umbo mviringo ni (u, o, ɔ)

-    Irabu za umbo mtandazwa ni (i, e, ɛ, a, ɑ)

                     Trapeza ya irabu za Kiswahili

i                             u (Juu kabisa)

                                                            irabu

     irabu      e                           O (Juu kiasi)    za                                 za

     mbele           ɛ                                            ɔ   (Chini kiasi)         nyuma

                                              

                                                 a                                    ɑ   (Chini kabisa)         

NAMNA YA KUBAINISHA VITAMKWA

1.  KONSONANTI

Uainishaji wa sauti konsonanti huzingatia vigezo vifuatavyo.

(i)          Kuanza na kundi asilia la sauti mf. Kipasuo,kikwamizo, n.k

(ii)        Kutaja endapo ni ghuna au si ghuna mf. Kipasuo ghuna.....

(iii)       Kutaja mahali pa matamshi mf. /p/ ni kipasuo sighuna cha midomo

NB: Vitamkwa ambavyo viko katika makundi yanayojibainisha hayahitajiki kutajwa sifa zake za kimatamshi (ghuna/sighuna) mf.

-    Irabu zote

-    Nazali zote

-    Vilainisho

-    Ving’ong’o

-    Viyeyusho

2.  IRABU

Uinishaji wa irabu huzingatia mwinuko wa ulimi,sehemu ya ulimi iliyoinuka na umbo la midomo (kama ilivyoelezwa hapo juu).

UNUKUZI WA KIFONETIKI

Unukuzi wa kifonetiki ni namna ya kuziandika sauti za lugha kwa kutumia misimbo ya kifonetiki kulingana na ALFABETI ZA KISWAHILI ZA KIMATAIFA (AKIKI). Mambo ya kuzingatia unaponukuu sauti kifonetiki.

(i)          Zingatia misimbo ya sauti mf. Ch-C

(ii)        Zingatia ubora wa sauti inayonukuliwa mf. ɛ # e

IRABU ZA KUREFUSHA

Irabu za kurefusha huandikwa kwa kutumia nukta pacha ambazo huwekwa mbele ya irabu ndefu. Mfano: dagaa huandikwa /dagɑ:/

KWA KUTUMIA SAUTI ZA KIFONETIKI HAPO JUU NUKUU MANENO YAFUATAYO KIFONETIKI

(i)          Chagudoa =      [Caŋgudɔa]

(ii)        King’ongo =      [kiŋɔŋgɔ]

(iii)       Maembe =         [maƐmbƐ]

(iv)        Malighafi =      [maliɣafi]

(v)          Utambulisho =    [utambuliʃɔ]

(vi)        Maandalizi =     [mɑ:ndalizi]

(vii)       Unyonyaji =      [uɲɔɲaɟi]

(viii)     Kinyang’anyiro = [kiɲaŋaɲirɔ]

(ix)        Kichongeo =     [kitʃɔŋgƐɔ]

(x)          Ubabaishaji =   [ubabaiʃaɟi]

MATAMSHI NA MOFIMU

Ilivyo ni kwamba katika baadhi ya mazingira mofimu zinapokubaliana hutokea mabadiliko mbalimbali ya sauti. Utokeaji huo wa mabadiliko hufuata taratibu maalumu za lugha inayohusika. Taratibu hizo hujulikana kiisimu kama kanuni au sheria. Kuna kanuni nyingi za kifonolojia zinazohusu lugha, kila kanuni ni matokeo ya mchakato fulani.

Michakato na kanuni za kifonolojia

Sauti zote za lugha ziko katika mpangilio ambao ukikiukwa sauti huathiriana. Kila kanuni hutokana na mchakato fulani.

Uundaji wa kanuni

Kanuni huanza kuelezea muundo ndani wa sauti inayohusika kisha huelezea muundo nje wa sauti hiyo. Muundo ndani ni muundo halisi wa sauti fulani ikiwa katika lugha yake ya asili na muundo nje ni ule unaojidhihirisha kama sauti hiyo ilivyo katika lugha ingine mfano: kibantu – Kiswahili.

Ufafanuzi wa kanuni

/x/                                [y]/N-

/x/                                [y]/-N

/x/ = sauti fulani x

                          = inajitokeza kama

[y] = sauti fulani y

/ = katika mazingira ya

N- = kutanguliwa na sauti fulani

-N = kufuatiwa na sauti fulani

Michakato

Kuna michakato anuwai inayotawala maathiriano ya sauti katika maneno,michakato hiyo ni:

  Michakato asilia ya kiusilimisho

  Michakato asilia isiyo ya kiusilimisho

1.  Michakato asilia ya kiusilimisho

Michakato asilia ya kiusilimisho ni taratibu zinazoonesha maathiriano ya sauti katika lugha nyingi duniani.

Usimilisho wa nazali; ni aina ya usilimisho ambao  nazali huathiriwa na konsonanti inayofuatana nayo hivyo nazali inasimilishwa yaani hutamkiwa mahali pale ambapo konsonanti inatamkiwa.

Kwa hiyo, / n /          [ m ]/ K-

          

Hivyo basi, fonimu nazali / n / inapofuatwa na konsonanti ya midomo inaathiriwa na kuwa nazali ya midomo ili iendane na konsonanti inayoiathiri.

 Mfano

umbo  ndani           umbo  nje

/n+buzi/                [mbuzi]

/n+bwa/                 [mbwa]

/n+papai/               [mpapai]

Usilimisho wa Konsonanti; ni aina ya usilimisho ambao  konsonanti huathiriwa na nazali inayofuatana nayo hivyo konsonanti inasimilishwa yaani hutamkiwa mahali pale ambapo nazali inatamkiwa. kuna baadhi ya sauti ambazo huathiriwa na nazali “n” inapokuwa inaandamia yaani kuna sauti ambazo huathiriwa zinapokaribiana kiasi au moja kwa moja na nazali “n”. Mara nyingi hutokea katika maumbo ya umoja na uwingi katika maumbo ya maneno

Mfano:-

  Umbo ndani                  Umbo nje

  /n+limi/                    [ndimi]

  /n+refu/                    [ndefu]

Hapa tunaona kwamba sauti [ l ] na [ r ] zinapokaribiana na irabu na irabu haziathiriki lakini zinapokaribiana na nazali “n” hubadilika na kuwa “d”

 

       /l/                  [d]/N-

      /r/                   [d]/N-

2.  Michakato asilia isiyo ya kiusilimisho

(a)     Udondoshaji; mchakato huu unahusu kuachwa kwa sauti fulani katika matamshi wakati mofimu mbili zinapokaribiana yaani katika mazingira hayo hayo ya sauti ambayo ilikuwepo hapo awali hutoweka. Kwa mfano irabu /u/ ikifuatiwa na konsonanti inayofanana nayo kwa sifa za matamshi kama nazali irabu hiyo hudondoshwa, kama inavyooneshwa hapa chini.

Umbo ndani              umbo nje

/mutu/                  [mtu]

/mwalimu/               [mwalim]

/muzito/                [mzito]

/u/                      [θ]/M-

                                                     

(b)     Uyeyushaji; wataalamu wengine huita irabu kuwa nusu irabu. Mgullu (1999), anasema huu ni mchakato ambao irabu za juu /u/ na /i/ hubadlika na kuwa /w/ au /y/ katika mazingira ya kufuatiwa na irabu zisizofana nazo. Kwa kifupi ni kwamba /u/ inapofuatiwa na irabu yoyote isiyofanana nayo hubadilika kuwa [w] na /i/ ikifuatiwa na irabu yoyote isiyofanana nayo hubadilika na kuwa [y].

Hivyo uyeyushaji ni kanuni inayoelezea mabadiliko ya sauti (irabu) na kuwa kiyeyusho kama [w] au [y], hii ni kwa irabu zote za juu zinapofuatana na sauti zingine zisizofanana nazo. Na sauti hizo hubadilika katika mazingira ya /u/ hubadilika kuwa [w] inapofuatana na irabu nyingine isiyofanana nayo na /i/ inabadilika na kuwa [y] pia inapofuatana na irabu isiyofanana nayo.

Mfano:

Umbo ndani                    Umbo nje

/mu+ezi/                      [mwezi]

/mu+alimu/                    [mwalimu]

/mu+izi/                      [mwizi]

/mi+aka/                      [myaka]

/Vi+angu/                     [vyangu]

    /u/                       [w]/-I; I # u

   /i/                        [y]/-I; I # i

           

(c)     Muungano/mvutano wa irabu; kanuni hii hutokea pale ambapo irabu ya mofimu moja inapokabiliana na irabu ya mofimu nyingine katika mpaka wa mofimu irabu hizo huungana na kuzaa irabu moja, na irabu hizo sharti moja iwe ya chini  na nyingine ya juu.

Mfano:

 Umbo ndani             umbo nje

 /Wa + enye/            [wenye]

/Wa + ingi/             [wengi]

/Ma + ino/              [meno]

/Wa + izi/              [wezi]

/a,i/                         [e]/k-k

(d)     Tangamano la irabu; Huu ni mchakato ambao irabu fulani hukubali kuandamana katika mazingira maalumu. Kwa mfano mofu [i] na [e] katika lugha ya Kiswahili huonekana kama alomofu au maumbo mbalimbali ya mofu moja ya kutendea na kutendesha, lakini utokeaji wake hutegemeana na mofu itakayojitokeza katika mzizi. Kama irabu ya mzizi  ni /a/, /i/ au /u/  basi irabu ya kiambishi cha utendea lazima iwe ni [i] , wakati irabu ya mzizi ikiwa ni /e/ au /o/  katika kauli ya utendea kiambishi chake kitakuwa ni [e].