mdhihiriko wa utanzia katika ushairi wa kiswahili: mifano
TRANSCRIPT
The University of Dodoma
University of Dodoma Institutional Repository http://repository.udom.ac.tz
Humanities Master Dissertations
2020
Mdhihiriko wa utanzia katika ushairi wa
Kiswahili: Mifano kutoka Kichomi na Dhifa
Machimu, Josephine
Chuo Kikuu cha Dodoma
Machimu, J. (2020). Mdhihiriko wa utanzia katika ushairi wa Kiswahili: Mifano kutoka Kichomi
na Dhifa (Tasnifu). Chuo Kikuu cha Dodoma, Dodoma.
http://hdl.handle.net/20.500.12661/2858
Downloaded from UDOM Institutional Repository at The University of Dodoma, an open access institutional repository.
MDHIHIRIKO WA UTANZIA KATIKA USHAIRI WA
KISWAHILI: MIFANO KUTOKA KICHOMI NA DHIFA
JOSEPHINE MACHIMU
SHAHADA YA UMAHIRI KATIKA FASIHI YA
KISWAHILI
CHUO KIKUU CHA DODOMA
DISEMBA, 2020
MDHIHIRIKO WA UTANZIA KATIKA USHAIRI WA
KISWAHILI: MIFANO KUTOKA KICHOMI NA DHIFA
NA
JOSEPHINE MACHIMU
TASINIFU ILIYOWASILISHWA KWA AJILI YA KUTUNUKIWA
SHAHADA YA UMAHIRI KATIKA FASIHI YA KISWAHILI
CHUO KIKUU CHA DODOMA
DISEMBA, 2020
i
IKIRARI NA HAKIMILIKI
Mimi, Josephine Machimu, ninathibitisha kwamba tasinifu hii ni kazi yangu halisi;
na kwamba, haijawahi kuwasilishwa na wala haitawasilishwa katika Chuo Kikuu
kingine chochote kwa ajili ya kutunukiwa Shahada ya Umahiri au Shahada nyingine
yoyote.
Hairuhusiwi kuiga, kuchapisha, kutoa nakala, kutafsiri wala kusambaza sehemu
yoyote ya tasinifu hii kwa namna yoyote ile bila ya kibali cha maandishi kutoka kwa
mwandishi au Chuo Kikuu cha Dodoma.
ii
ITHIBATI YA MSIMAMIZI
Aliyesaini hapa chini anathibitisha kwamba, ameisoma tasinifu hii inayoitwa
“Mdhihiriko wa Utanzia katika Ushairi wa Kiswahili: Mifano Kutoka Kichomi
na Dhifa” na anapendekeza ikubaliwe kwa ajili ya kutunukiwa Shahada ya Umahiri
katika Fasihi ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dodoma.
-
iii
SHUKURANI
Awali ya yote, ninashukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema kipindi
chote cha masomo yangu mpaka kuniwezesha kukamilisha tasinifu hii kwa wakati.
Najua sio kwa nguvu zangu ila ni kwa baraka na neema zake alizonijalia nimefika
hapa.
Kwanza, ninapenda kumshukuru msimamizi wangu, Dkt. Aginiwe Nelson Sanga,
ambaye alijitoa sana katika kuniongoza kwa kipindi chote tangu naanza kazi hii.
Ijapokuwa alikuwa na majukumu mengi ya kikazi na kifamilia lakini alijitoa katika
kuniongoza na kunishauri kuanzia hatua ya pendekezo la utafiti mpaka kukamilika
kwa tasinifu hii. Ninakushukuru sana Dkt. Sanga, mwenyezi Mungu akujalie afya
njema ili uendelee kutimiza wajibu wako.
Pili, ninatoa shukurani zangu za dhati kwa walezi wangu, shemeji yangu, Bw.
Leonard Lwabuzala, na dada yangu mpendwa Bi. Jane Machimu, kwa moyo wao wa
ukarimu. Kwa sababu waliacha majukumu yao mengine na kuchukuwa jukumu la
kuwa wazazi kwangu kwa kunisomesha, kunilea, kuniongoza na kunishauri katika
hatua zangu zote za malezi na makuzi mpaka sasa. Sina cha kuwalipa ila nazidi
kuwaombea afya njema na miaka mingi zaidi, Mungu awabariki sana na pale
mlipopungukiwa Mungu awazidishie zaidi.
Tatu, shukurani zangu za dhati ziwafikie wahadhiri wote walionifundisha kozi
mbalimbali kwa kuniongoza na kunishauri katika kipindi chote cha masomo. Pia,
ninawashukuru wanafunzi wenzangu wa umahiri katika fasihi ya Kiswahili mwaka
2018/2020 kwa ushirikiano wao wa dhati kwa kipindi chote cha masomo.
Nne, shukurani za pekee ziende wa ndugu zangu Joachimu Machimu, Deogratias
Machimu, Salome Machimu, Janeth Machimu, Justa Machimu, Suzan Kafuje,
mtumishi Everson Rweramila pamoja na Paul Shayo kwa kunitia moyo pale
nilipokuwa na wakati mgumu na kuniombea.
iv
TABARUKU
Natabaruku kazi hii kwa marehemu wazazi wangu wapendwa baba yangu mzazi,
Henry Kassian Machimu, na mama yangu mzazi, Magreth Jeremiah Blackwell. Pia,
kwa pacha wangu Justina Henry Machimu pamoja na marehemu dada zangu Juliana
Henry Machimu na Judith Henry Machimu siku zote mpo moyoni mwangu,
inawakumbuka na kuwaombea daima. Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi,
Amina.
v
IKISIRI
Tasinifu hii ilijikita katika kujadili mdhihiriko wa utanzia katika ushairi wa
Kiswahili. Diwani zilizochunguzwa ni Kichomi na Dhifa. Dhana ya utanzia katika
tasinifu hii imetumika kama mbinu bunilizi inayotumia vipengele mbalimbali
vizuavyo huzuni, masikitiko, machungu, majonzi pamoja na maumivu ya mwili,
roho na akili kwa hadhira. Utafiti umeongozwa na malengo mahususi matatu ambayo
ni: kubainisha matukio ya utanzia yaliyodhihirika katika diwani teule, kufafanua
dhima za matumizi ya utanzia katika diwani teule na kufafanua athari za matumizi ya
mbinu ya utanzia kwa wasomaji kupitia diwani teule. Utafiti ulifanyika maktabani na
uwandani. Data ambazo zimetupatia majibu ya tasinifu hii zilikusanywa toka kwa
wataalamu wa fasihi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma na Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam kwa njia mbili, usaili na uchanganuzi matini. Matokeo yaliyopatikana ni:
kubainika kwa matukio ya utanzia katika diwani teule. Matukio hayo ni: hali ngumu
ya maisha, ulemavu wa viungo, vifungo, maradhi, ukatili, majanga na vifo. Vilevile,
tumebainisha dhima za matumizi ya utanzia katika kazi za fasihi. Dhima hizo ni:
hujenga hisia za woga, hufikirisha, hujenga uhalisia wa maisha na kuibusha majonzi
kwa hadhira lengwa. Utanzia kama mbinu ya utunzi huwa na athari hasi au chanya
katika matumizi yake katika fasihi ya Kiswahili. Athari chanya ni pamoja na:
kufikisha ujumbe, kuakisi uhalisia wa maisha, kuweka karibu msomaji na mwandishi
na kuitafakarisha hadhira. Athari hasi ni: kupunguza wasomaji, ugumu katika
kueleweka na huwapa wasomaji hali ya kukata tamaa kuhusu maisha. Kupitia
tasinifu hii, wasomaji na wahakiki wataweza kufahamu sababu za waandishi kutumia
utanzia katika kazi zao za kiutunzi. Halikadhalika, imeonesha namna mbinu hii
inavyoweza kutumika katika kujenga maudhui, hasa katika utanzu wa ushairi. Zaidi,
tasinifu imebainisha kwamba mbinu ya utanzia inaweza kutumiwa na washairi katika
kujenga maudhui yao, tofauti na hapo mwanzo ambapo utanzia ulizoeleka kuonekana
kwenye tamthiliya pekee.
vi
YALIYOMO
IKIRARI NA HAKIMILIKI ......................................................................................... i
ITHIBATI YA MSIMAMIZI ...................................................................................... ii
SHUKURANI ............................................................................................................. iii
TABARUKU .............................................................................................................. iv
IKISIRI ......................................................................................................................... v
ORODHA YA VIFUPISHO VILIVYOTUMIKA ...................................................... x
SURA YA KWANZA ................................................................................................. 1
UTANGULIZI ............................................................................................................ 1
1.1 Utangulizi ............................................................................................................... 1
1.2 Ufafanuzi wa Istilahi Muhimu ............................................................................... 1
1.2.1 Tanzia .................................................................................................................. 1
1.2.2 Utanzia ................................................................................................................ 2
1.2.3 Ushairi ................................................................................................................. 2
1.3 Usuli wa Tatizo la Utafiti ....................................................................................... 3
1.4 Tamko la Tatizo la Utafiti ...................................................................................... 5
1.5 Malengo ya Utafiti ................................................................................................. 6
1.5.1 Lengo la Jumla .................................................................................................... 6
1.5.2 Malengo Mahususi .............................................................................................. 6
1.6 Maswali ya Utafiti .................................................................................................. 6
1.7 Manufaa ya Utafiti ................................................................................................. 7
1.8 Mawanda ya Utafiti ................................................................................................ 7
1.9 Historia ya Euphrase Kezilahabi ............................................................................ 7
1.10 Muhtasari wa Sura ya Kwanza ........................................................................... 10
SURA YA PILI ......................................................................................................... 11
MAPITIO YA MAANDIKO NA KIUNZI CHA NADHARIA ........................... 11
2.1 Utangulizi ............................................................................................................. 11
2.2 Mapitio ya Maandiko ........................................................................................... 11
2.2.1 Maandiko kuhusu Utanzia................................................................................. 11
2.2.2 Maandiko kuhusu Ushairi wa Euphrase Kezilahabi ......................................... 15
vii
2.2.3 Mapengo Yaliyojitokeza Kutokana na Mapitio ya Maandiko .......................... 18
2.3 Kiunzi cha Nadharia ............................................................................................. 18
2.4 Muhtasari wa Sura ya Pili .................................................................................... 21
SURA YA TATU ...................................................................................................... 22
METHODOLOJIA YA UTAFITI .......................................................................... 22
3.1 Utangulizi ............................................................................................................. 22
3.2 Usanifu wa Utafiti ................................................................................................ 22
3.3 Mkabala wa Utafiti ............................................................................................... 22
3.4 Eneo la Utafiti ...................................................................................................... 23
3.5 Walengwa wa Utafiti............................................................................................ 23
3.5.1 Wango Tafitiwa ................................................................................................. 23
3.5.2 Usampulishaji na Sampuli ya Watafitiwa ......................................................... 24
3.5.2.1 Usampulishaji ................................................................................................. 24
3.5.2.2 Sampuli ya Watafitiwa ................................................................................... 24
3.6 Ukusanyaji wa Data ............................................................................................. 26
3.6.1 Njia na Zana za Kukusanyia Data ..................................................................... 26
3.6.1.1 Usaili .............................................................................................................. 26
3.6.1.2 Uchanganuzi Matini ....................................................................................... 26
3.6.2 Mchakato wa Ukusanyaji wa Data .................................................................... 27
3.7 Uchanganuzi wa Data .......................................................................................... 27
3.8 Itikeli ya Utafiti .................................................................................................... 28
3.9 Uhalali na Uthabiti wa Matokeo ya Utafiti .......................................................... 28
3.10 Changamoto za Utafiti na Utatuzi Wake ........................................................... 29
3.11 Muhtasari wa Sura ya Tatu ................................................................................ 29
SURA YA NNE ......................................................................................................... 31
UWASILISHAJI NA MJADALA WA MATOKEO YA UTAFITI .................... 31
4.1 Utangulizi ............................................................................................................. 31
4.2 Utanzia katika Ushairi wa Euphrase Kezilahabi .................................................. 31
4.2.1 Muhtasari wa Diwani Teule .............................................................................. 31
4.2.1.1 Muhtasari wa Diwani ya Kichomi ................................................................. 31
4.2.1.2 Muhtasari wa Diwani ya Dhifa ...................................................................... 33
viii
4.2.2 Utanzia katika Diwani Teule ............................................................................. 33
4.2.3 Hali Ngumu ya Maisha ..................................................................................... 33
4.2.4 Ulemavu wa Viungo ......................................................................................... 36
4.2.5 Kifungo ............................................................................................................. 37
4.2.6 Maradhi ............................................................................................................. 38
4.2.7 Ukatili ................................................................................................................ 39
4.2.8 Majanga ............................................................................................................. 42
4.2.9 Kifo ................................................................................................................... 44
4.2.10 Mateso ............................................................................................................. 46
4.3 Dhima za Matumizi ya Utanzia katika Diwani Teule .......................................... 47
4.3.1 Kujenga Hisia za Woga kwa Hadhira ............................................................... 47
4.3.2 Kufikirisha Hadhira ........................................................................................... 48
4.3.3 Kujenga Uhalisi wa Maisha .............................................................................. 50
4.3.4 Kuibua Majonzi kwa Hadhira ........................................................................... 53
4.3.5 Kujenga Upekee wa mtunzi .............................................................................. 54
4.3.6 Nyenzo ya Kuhuzunisha Hadhira...................................................................... 56
4.4 Athari za Matumizi ya Mbinu ya Utanzia ............................................................ 57
4.4.1 Athari Chanya za Matumizi ya Utanzia katika Diwani Teule .......................... 57
4.4.1.1 Nyenzo ya Kufikisha Ujumbe kwa Hadhira .................................................. 57
4.4.1.2 Huakisi Uhalisi wa Maisha ............................................................................ 58
4.4.1.3 Humweka Karibu Mwandishi na Msomaji .................................................... 59
4.4.1.4 Kuitafakarisha Hadhira .................................................................................. 60
4.4.1.5 Kumpambanua Mtunzi ................................................................................... 61
4.4.2 Athari Hasi za Matumizi ya Utanzia katika Diwani Teule ............................... 63
4.4.2.1 Kutopata Wasomaji ........................................................................................ 63
4.4.3 Ugumu katika Kueleweka kwa Kazi ya Fasihi ................................................. 64
4.4.4 Athari za Utumizi wa Mbinu za Kisanaa kwa Watunzi Wengine .................... 65
4.4.5 Kukata tamaa ..................................................................................................... 66
4.5 Muhtasari wa Sura ya Nne ................................................................................... 67
ix
SURA YA TANO ..................................................................................................... 69
MUHTASARI, HITIMISHO NA MAPENDEKEZO ........................................... 69
5.1 Utangulizi ............................................................................................................. 69
5.2 Muhtasari ............................................................................................................. 69
5.3 Hitimisho .............................................................................................................. 70
5.3.1 Utoshelevu wa Nadharia ................................................................................... 70
5.3.2 Mchango Mpya wa Tasinifu ............................................................................. 70
5.4 Mapendekezo kwa Tafiti Zijazo........................................................................... 71
MAREJELEO .......................................................................................................... 72
VIAMBATISHO ...................................................................................................... 77
x
ORODHA YA VIFUPISHO VILIVYOTUMIKA
BAKITA Baraza la Kiswahili la Taifa
BAKIZA Baraza la Kiswahili Zanzibar
Bi. Bibi
BK Baada ya Kristo
Bw. Bwana
Dkt Daktari (Ph.D)
Ht Hakuna tarehe
Khj Kama hapo juu
Ltd Limited
S. A. W Swalallahu Alaihi Wasalaam
TATAKI Taasisi ya Taaluma za Kiswahili
TUKI Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili
Uk. Ukurasa
UKIMWI Upungufu wa Kinga Mwilini
UWAKI Ukatili wa Kijinsia
1
SURA YA KWANZA
UTANGULIZI
1.1 Utangulizi
Utafiti wetu ulihusu Mdhihiriko wa Utanzia katika Ushairi wa Kiswahili: Mifano
Kutoka Kichomi na Dhifa. Sura hii ya kwanza inawasilisha taarifa za utangulizi
kuhusiana na mada iliyotafitiwa ili kumpa msomaji picha ya nini kilisukuma utafiti
huu na muundo wa jumla wa tasinifu yenyewe. Hivyo, sura hii ina sehemu tisa (9).
Sehemu hizo ni ufafanuzi wa istilahi muhimu zilizotumika, usuli wa tatizo la utafiti,
tamko la tatizo la utafiti na malengo ya utafiti. Sehemu nyingine ni maswali ya
utafiti, manufaa ya utafiti, mawanda ya utafiti, historia fupi ya mwandishi pamoja na
muhtasari wa sura ya kwanza.
1.2 Ufafanuzi wa Istilahi Muhimu
Tumefafanua istilahi ili kuweka msingi kwa wasomaji na kurahisisha uelewa. Istilahi
zilizofafanuliwa katika sehemu hii ni tanzia, utanzia na ushairi.
1.2.1 Tanzia
TUKI (2004) na BAKITA (2017) wanafasili tanzia kuwa ni habari ya kifo
inayotolewa kwa lengo la kuwafikia watu walio mbali. Katika fasihi, dhana ya tanzia
imekuwa ikihusishwa na utanzu wa tamthiliya ambayo inahusu kuanguka kwa nguli
au mhusika mkuu na kuishia kwa kifo (Wamitila, 2003). Kwa mujibu wa Semzaba
(1997), tanzia ni tamthiliya yenye huzuni kutokana na hatima ya mhusika mkuu
kuwa ya kupatikana na janga. Katika historia yake, tanzia hutokea kutokana na
udhaifu au dosari fulani ya shujaa ambayo inasababisha anguko lake.
Wamitila (2002) anasema, tanzia ni aina ya tamthiliya ambayo huwa na suala la
matendo ya malengo ya dhati. Utanzu wa tamthiliya kama mwigo au uigaji wa tendo
ambalo lina udhati, ukamilifu, ubora na ukuu fulani. Tendo hilo lazima liwe na
uwezo wa kuwaathiri watazamaji na kuwafanya waingiwe na huzuni au kihoro
pamoja na kuwa na uwezo wa kuzitakasa hisia za woga au huzuni. Hapa Wamitila
(khj) amebainisha kuwa tanzia ni yale matendo ya dhati katika tamthiliya. Matendo
hayo ya dhati ni halisi kwa sababu yanatendwa na wanadamu (wahusika). Matendo
hayo huibua hali ya huzuni, masikitiko machungu na woga ndani yake. Kutokana na
2
dhana ya tanzia ndipo tunaipata dhana ya utanzia ambayo itachunguzwa katika utafiti
huu.
1.2.2 Utanzia
Dhana ya utanzia imetokana na dhana ya tanzia, yaani mambo yanayoibua huzuni au
masikitiko katika tamthiliya. Utanzia ni mbinu ambayo mtunzi hutumia vipengele
mbalimbali vizuavyo majonzi, msawajiko, jitimai na mateso kwa hadhira yake.
Utanzia katika tasinifu hii inamaanisha hali ijengwayo na maneno, matukio au
mazingira yoyote yenye kuwafanya watu kuingiwa na simanzi, wasononeke na
kupata uchungu. Utafiti unaitofautisha dhana ya utanzia na tanzia kutokana na
ukweli kwamba, tanzia kwa kiasi kikubwa hujiegemeza katika utendaji, hususani
matendo ya jukwaani pamoja na kuonesha anguko la mhusika mkuu. Lakini, utanzia
siyo lazima ujitokeze katika matendo ya jukwaani pekee. Kwa mantiki hiyo, utanzia
huweza kujitokeza katika tanzu anuwai za fasihi (simulizi na andishi) na si katika
tamthiliya peke yake (Ponera, 2014; Mazongela, 2016).
1.2.3 Ushairi
Kwa mujibu wa Mulokozi na Kahigi (1982), ushairi ni sanaa inayopambanuliwa kwa
mpangilio maalumu wa maneno fasaha na yenye muwala, kwa lugha ya mkato,
picha, sitiari au ishara, katika usemi, maandishi au mahadhi ya wimbo ili kuleta wazo
au mawazo, kufunza au kueleza tukio au hisi fulani kuhusu maisha au mazingira ya
binadamu kwa njia inayogusa moyo. Kutokana na fasili hiyo, tunaweza kueleza
kuwa ushairi, tofauti na nathari, hauelezi tu, bali huonesha, husawiri na hutupa picha
ya hisi, wazo, hali, kitu au tukio fulani papo hapo huvuta au kuathiri hisia zetu.
Usawiri huo unaofafanuliwa na Mulokozi (2017) unaweza kufanywa kwa mpangilio
wa kijadi wa urari wa vina na mizani na beti, au kwa mpangilio tofauti usiozingatia
urari wa vina na mizani.
Ushairi wa Kiswahili umetokana na nyimbo mbalimbali za kazi. Kabla ya kuja kwa
wageni, hasa Waarabu, ushairi wa Kiswahili ulitolewa kama nyimbo katika matukio
mbalimbali kama vile wakati wa kuwinda, kulima, kuvua, harusi, vita, kubembeleza
watoto na matambiko. Ushairi huo haukuzingatia arudhi za vina na mizani (Senkoro,
1988; Mulokozi, 1996).
3
Ujio wa Waarabu na dini ya Kiislamu katika Pwani ya Afrika Mashariki katika karne
ya 7BK uliathiri kwa kiasi kikubwa utamaduni wa Waswahili. Waarabu
waliwafundisha Waswahili dini ya Kiislamu, nyimbo za kumsifu Mtume Muhammad
(SAW) na hati ya maandishi ya Kiarabu. Nyimbo hizo (kasda) zilitungwa kwa
kufuata arudhi za vina na mizani. Arudhi za vina na mizani ziliwezesha kasda
kuimbika kwa kufuata midundo maalum na kukaririwa kwa urahisi. Kutokana na
athari hiyo, taratibu Waswahili nao walianza kutunga nyimbo zao mbalimbali kwa
kuzingatia arudhi za vina na mizani. Baada ya muda mrefu, hiyo ikawa sehemu ya
kaida katika utunzi wa ushairi wao. Mashairi ya kale kama Fumo Liyongo, Utenzi wa
Hamziyya, Utenzi wa Siri La’sirari, Utendi wa Tambuka, Utenzi wa Shufaka yana
athari za ushairi wa Kiarabu (TUKI, 1983; Senkoro, 1988).
1.3 Usuli wa Tatizo la Utafiti
Kwa muda mrefu ulimwengu wa fasihi umekuwa ukihusishwa na matumizi ya mbinu
ya utanzia. Mbinu hii ambayo mtunzi hutumia vipengele vinavyozua huzuni
imekuwa maarufu katika tanzu mbalimbali za fasihi ulimwenguni (Soileau, 2006).
Utanzia ni mbinu kongwe na imechipuka kutokana na dhana ya tanzia, yaani matukio
yanayoibua huzuni au masikitiko katika tamthiliya (Wamitila, 2003; Mazongela,
2016). Kwa upande wa tanzia (kama dhana mama) ilianza kushughulikiwa na
Aristotle. Kwa mujibu wa Semzaba (1997), Aristotle alikuwa mtu wa kwanza
ambaye baada ya kuyatazama maandishi ya tamthiliya ya Kigiriki aliandika maana
ya tanzia katika kitabu chake cha Poetics. Kutokana na uchunguzi wake, Aristotle
aliiona tanzia kuwa tamthiliya yenye huzuni ambayo inagusa hisia za watazamaji
kiasi cha kuogopesha na kumwonea huruma mhusika mkuu ambaye hupata janga
(Semzaba, 1997; Wamitila, 2003; Mulokozi, 2017).
Kiusuli, dhana ya tanzia ambayo katika utafiti huu tunairejelea kama dhana mama
imekuwa ikihusishwa na utanzu wa tamthiliya pekee (Semzaba, 1997; Wamitila,
2003). Katika utanzu wa tamthiliya kwa mujibu wa Semzaba (khj), dhana ya tanzia
imegawika katika matapo makuu manne ambayo ni tanzia ya urasimi, tanzia ya
urasimi mpya, tanzia ya kisasa na tanzia ya uhalisia wa ujamaa. Kila tapo la tanzia
lina sifa na mwelekeo wake ambao unaitofautisha na tapo lingine.
4
Hata hivyo, dhana ya tanzia ni tofauti na utanzia. Utanzia ni mbinu ya ubunilizi
ambayo ni kinyume cha ufutuhi (Ponera, 2014). Mbinu hii hutumika kufafanua
ukosefu wa furaha ambayo mtu huuhisi maishani. Ukosefu huo wa furaha ndio
ambao husababisha hali ya huzuni na masikitiko kwa mtu. Kila mwanadamu
hukumbwa na hali ya huzuni kutokana na mambo mbalimbali anayokumbana nayo.
Mazongela (2016) anatanabahisha kuwa huzuni ni jambo la kawaida kwa
mwanadamu na hivyo ni vizuri na muhimu kutofautisha baina ya ukosefu wa furaha
ya maisha ya kawaida na dalili za hali ya huzuni.
Katika maisha, watu wengi hukumbwa na hali ya jitimai, mateso, sononeko, huzuni
na masikitiko kiasi cha kuwaathiri kisaikolojia na kimaisha. Muathirika wa hali hizo
hukosa hamu ya kuishi na hata kufanya mambo yake kwa makini na ari (Shahid,
1980). Watu hawa huwa na hali ya lawama, hukosa tumaini na kufikia hata hatua ya
kujiua. Hii ni kutokana na ukweli kuwa mawazo yanayoambatana na sononeko la
nafsi au huzuni huwakosesha raha kiasi cha kukata tamaa ya maisha.
Kwa upande wa jamii za ulimwengu, utanzia unaonekana kuchomoza katika nyanja
mbalimbali za maisha, yaani kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Mazongela (khj)
anatueleza kuwa katika siasa kuna matukio mengi yanayoibua utanzia kwa jamii.
Matukio haya tunaweza kuyaona katika kampeni za chaguzi mbalimbali za viongozi.
Kiuchumi, kuna matukio ya kitanzia yanayoibuka siku hadi siku na kusababisha
utanzia kwa jamii na taifa kwa jumla. Mfano mzuri, nchini Tanzania kumekuwa na
mapigano ya mara kwa mara baina ya wafugaji na wakulima katika mikoa
mbalimbali, kwa mfano Morogoro. Mapigano hayo husababisha vifo, huzuni na
kukosekana kwa utulivu katika eneo na nchi kwa jumla. Suala hili hurudisha nyuma
maendeleo ya shughuli za kiuchumi kwa wahusika ambazo ni kilimo na ufugaji.
Aidha, kiutamaduni matukio ya utanzia yameweza kusawiriwa kwa namna
mbalimbali. Hapa tunaweza kuona kupitia matukio kama vile unyanyasaji wa
wanawake na ndoa za utotoni. Matendo hayo kwa jumla huwafanya wenye
kutendewa kuwa mbali na furaha na kuwa na huzuni muda wote.
Katika ulimwengu wa fasihi, matumizi ya utanzia yana mizizi madhubuti. Hii ni
kutokana na watunzi mbalimbali kuitumia mbinu hii katika kusawiri hali halisi ya
maisha Soileau (2006). Mathalani, katika fasihi ya Kiarabu, Shahid (khj) anautaja
5
ushairi wa kasida wa Waarabu kama moja ya fani inayohusisha utanzia. Kupitia
kasida hizo, watunzi huelezea vita, hali ngumu ya maisha, vifo, maombolezo na
mateso aliyoyapata Mtume Muhammad katika kusimamisha dini ya Uislamu.
Katika fasihi ya Kiswahili, halikadhalika, utanzia unaonekana kujitokeza katika
tanzu zote simulizi na andishi (Senkoro, 2011). Kwa mfano, katika fasihi andishi ya
Kiswahili zimepatikana kazi ambazo zimetumia mbinu hii. Hapa tunaweza kuziona
kazi kama vile, Utenzi wa Fumo Liyongo (Muhammed Kijumwa), Utenzi wa Al -
Inkishafi (Seyyid Abdallah bin Ali bin Nassir), Utenzi wa Vita vya Wadachi
Kutamalaki Mrima (Hemed Abdallah El-Buhry), na Sauti ya Dhiki (Abdilatif
Abdalla). Kazi hizo kwa kiasi kikubwa zimebeba utanzia katika kujenga maudhui
yake. Kwa upande wa riwaya, tunaziona riwaya kama Uhuru wa Watumwa (James
Mbotela), Mzimu wa Watu wa Kale (Muhammed Said Abdulla), na Simu ya Kifo
(Faraji Katalambulah) nazo zikitumia utanzia kama kiunzi cha kujenga maudhui
yake.
Kwa yakini, utanzia umekuwa ukijitokeza kwa muda mrefu katika fasihi ya
Kiswahili. Haji (2015) na Moh’d (2016) wamechunguza matumizi ya utanzia katika
riwaya na kasida na kubainisha namna mbinu hii ilivyojitokeza katika kazi za hizo za
kifasihi. Hata hivyo, hadhira imekuwa ikiona ni jambo la kawaida kwa sababu
hakuna misingi imara iliyowekwa kuhusu mbinu hii. Jambo hili linaonesha na
kudhihirisha wazi kuwa mbinu ya utanzia haijashughulikiwa vya kutosha na
wataalamu wa fasihi, hasa katika utanzu wa ushairi. Hivyo basi, hali hii ilimchochea
mtafiti kuchunguza mdhihiriko wa utanzia katika diwani teule za Euphrase
Kezilahabi ikiwa ni kiwakilishi cha kazi anuwai za kishairi.
1.4 Tamko la Tatizo la Utafiti
Utanzia ni mbinu ambayo mtunzi hutumia vipengele mbalimbali vizuavyo huzuni,
masikitiko, jitimai na mateso kwa hadhira (Ponera, 2014). Utanzia ni suala
lisiloepukika katika maisha ya jamii yoyote ile. Kwa kuwa fasihi ni zao la jamii,
suala hili limekuwa likidhihirishwa kupitia kazi mbalimbali za fasihi. Katika fasihi
ya Kiswahili, mbinu ya utanzia imeweza kujitokeza zaidi katika kazi za tamthiliya na
riwaya tofauti na utanzu wa ushairi. Watunzi wa kazi za fasihi wamekuwa
wakiitumia mbinu hii katika kuwasilisha maudhui yao kwa jamii. Baadhi ya
6
wahakiki na watafiti wameweza kuchunguza mbinu ya utanzia katika kazi za fasihi
ambao ni Haji (2015), Mazongela (2016) na Moh’d (2016) wamechunguza kwa kiasi
kikubwa utanzia katika tamthiliya na riwaya ambapo pengo limejitokeza kwenye
utanzu wa ushairi. Hivyo, mbinu hii katika fasihi ya Kiswahili bado haijatafitiwa vya
kutosha katika utanzu wa ushairi; yumkini, hii ni kutokana na hali na sifa za utanzu
wenyewe kuonekana mgumu kwa wasomaji. Kwa kiasi kikubwa, kutochunguzwa
kwa mbinu hii kunawaathiri wasomaji wa kazi za fasihi. Hii ni kwa sababu,
wasomaji husoma kazi ya fasihi na kushindwa kufahamu hisia za mtunzi kuhusiana
na matukio ya kazi hiyo ya kifasihi. Pia, wanashindwa kufahamu utanzia katika kazi
husika na athari za utanzia kwani kutomakiniwa kwa dhana ya utanzia huweza kuwa
kizuizi cha kuelewa kazi ya fasihi (Soileau, 2006). Utafiti huu ulikusudia
kuchunguza mdhihiriko wa utanzia katika diwani teule za Euphrase Kezilahabi ili
kubainisha vipengele vya utanzia vilivyotumika katika diwani hizo. Aidha,
kubainisha dhima iliyomsukuma mtunzi kutumia utanzia katika diwani zake pamoja
na kuchambua athari za utanzia kwa jamii.
1.5 Malengo ya Utafiti
Utafiti huu ulikuwa na lengo la jumla moja na malengo mahususi matatu.
1.5.1 Lengo la Jumla
Lengo la jumla la utafiti huu ni kuchunguza mdhihiriko wa utanzia katika diwani za
Euphrase Kezilahabi.
1.5.2 Malengo Mahususi
Malengo mahususi ya utafiti huu ni:
a) Kubainisha utanzia katika diwani teule;
b) Kufafanua dhima za utanzia uliotumika katika diwani teule; na
c) Kufafanua athari za utanzia kwa wasomaji wa diwani teule.
1.6 Maswali ya Utafiti
Maswali yaliyouongoza utafiti huu ni:
a) Utanzia unajitokezaje katika diwani teule?
b) Je, utanzia unaotumika katika diwani teule una dhima gani?
7
c) Utanzia uliotumika katika diwani teule una athari gani kwa msomaji wa
diwani hizo?
1.7 Manufaa ya Utafiti
Utafiti huu unatarajiwa kuleta manufaa yafuatayo: Kwanza, kuwasaidia wahakiki na
wachambuzi wa fasihi, hususani wataalamu wa ushairi, kuelewa na kuitumia mbinu
ya utanzia katika kazi za kifasihi hasa ushairi. Pili, utafiti huu utasaidia kuikuza na
kuendeleza mbinu bunilizi ya utanzia katika kazi za fasihi. Tatu, matokeo ya utafiti
huu yataongeza marejeleo muhimu katika uwanja wa fasihi hususani utanzu wa
ushairi. Nne, utafiti huu utasaidia kukuza na kuendeleza ya fasihi Kiswahili hasa
katika matumizi ya nadharia ya upokezi kwa kufaa kwake katika uchambuzi wa kazi
za kifasihi.
1.8 Mawanda ya Utafiti
Utafiti huu ulijikita katika kuchunguza mdhihiriko wa utanzia katika diwani za
Euphrase Kezilahabi. Utafiti ulichunguza jumla ya diwani mbili zilizoandikwa na
Euphrase Kezilahabi ambazo ni Kichomi (1974) na Dhifa (2008). Uteuzi wa diwani
hizo ulitokana na uchunguzi wa awali kuonesha kuwa matumizi ya mbinu ya utanzia
imetumika kwa kiasi kikubwa katika diwani teule. Diwani nyingine za Euphrase
Kezilahabi kama vile Karibu Ndani (1988) na kazi zake nyinyine za kifasihi,
hazikuchunguzwa kwa namna ya kuzamiwa kwa kina bali zilisomwa na kutazamwa
kwa jicho la jumla katika kutafuta ushikamani kuhusiana na mbinu ya utanzia.
Vilevile, utafiti huu ulishughulikia utanzia katika diwani teule. Mbinu nyingine
mbali na dhana hiyo hazikushughulikiwa ingawa zimerejelewa hapa na pale ili
kujenga hoja na kuweka mkazo katika ufafanuzi.
1.9 Historia ya Euphrase Kezilahabi
Tumeona ni bora kuelezea historia fupi ya Euphrase Kezilahabi kwa sababu ni
muhimu kumwelewa mwandishi wa kazi za fasihi ili kuwa katika nafasi nzuri ya
kuzielewa kazi zake.
Euphrase Kezilahabi alizaliwa kijiji cha Namagondo wilaya ya Ukerewe, mkoani
Mwanza Tanzania tarehe 13/04/1944. Euphrase Kezilahabi ni mtoto wa nane kati ya
watoto tisa wa familia hiyo ya jamii ya Kikerewe. Alipata elimu ya msingi katika
8
shule ya Nakasahenge mwaka 1952 hadi 1956 na kujiunga na elimu ya sekondari
katika shule ya Seminari ya Mtakatifu Maria, Jijini Mwanza mwaka 1957. Mnamo
mwaka 1967 alijiunga na Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki, Dar es Salaam na
kupata shahada ya kwanza. Pia, alitunukiwa Shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu
cha Wisconcin - Madison huko Marekani mwaka 1985. Euphrase Kezilahabi
aliajiriwa katika ngazi ya Mkufunzi Msaidizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
mwaka 1971. Aliendelea na kuwa, Mhadhiri na kuendelea kupanda hadi kufikia
kuwa profesa mshiriki mwaka 1987. Pia, alikuwa mwanachama wa vyama
mbalimbali vya kitaaluma na mtafiti ambaye ameshughulikia nyanja mbalimbali za
fasihi na lugha ya Kiswahili. Kezilahabi amekuwa mhadhiri wa fasihi katika vyuo
mbalimbali ndani na nje ya nchi ya Tanzania. Miongini mwa vyuo hivyo ni Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo Kikuu cha
Botswana (Fuluge, 2013).
Kiimani, Euphrase Kezilahabi alikuwa na msingi wa mafundisho ya dini ya
Kikatoliki kutokana na kupata elimu katika shule ya Seminari. Kutokana na msingi
wa Kikatoliki aliweza kuwa na maadili bora ijapokuwa baadae aliachana na masuala
ya kiseminari. Malezi na makuzi aliyoyapata yamempelekea kuandika kazi za
kifasihi kutokana na mazingira halisi anayoyafahamu. Kwa mfano, katika diwani ya
Kichomi, Dhifa na Karibu Ndani kuna mashairi ya Namagondo I, II, III ambayo
yanaonesha namna mwandishi alivyokuwa akithamini na kuonesha rasilimali
zinazopatikana katika nchi ya Tanzania. Pia, kuonesha asili yake na namna kijiji cha
Namagondo kilivyobadilika kutokana na uhalibifu wa mazingira.
Katika fani ya utungaji, alianza kutunga bunilizi katika fasihi ya Kiswahili mwaka
1960. Kazi yake ya kwanza iliyomtambulisha ni Rosa Mistika (1971). Baada ya hapo
aliendelea kutunga kazi nyingine katika tanzu za riwaya, tamthiliya, ushairi na
hadithi fupi. Mwandishi Euphrase Kezilahabi ametunga kazi mbalimbali za kifasihi
kama riwaya, ushairi, tamthiliya na hadithi fupi kazi hizo ni:
i) Riwaya
a) Rose Mistika (1971) Gamba la Nyoka (1979)
b) Kichwa Maji (1974)
c) Dunia Uwanja wa Fujo (1975)
9
d) Gamba la Nyoka (1979)
e) Nagona (1990)
f) Mzingile (1991)
ii) Ushairi
a) Kichomi (1974)
b) Karibu Ndani (1988)
c) Dhifa (2008)
iii) Tamthiliya
a) Kaptula la Marx (1996)
Pia, alitunga hadithi fupi kama; Magwanda Kubilya na Vyama Vingi, Mayai Waziri
wa Maradhi, Utapiamlo, Balenzi, Ulingo wa Uchaguzi, Cha Mnyonge Utakitapika
Hadharani na Wasubiri Kifo.
Euphrase Kezilahabi amewahi kupata tuzo mbalimbali kuhusiana na uandishi wake.
Tuzo hizo ni pamoja na tuzo ya Kiitaliano iitwayo Edwardo Sanguinett Memorial
Prize mwaka 1990; tuzo ya Shaaban Robert Memorial Prize, iliyotolewa na Baraza la
Kiswahili la Taifa mwaka 1995, na tuzo ya Zeze ambayo hutolewa na Mfuko wa
Utamaduni kila mwaka kwa ajili ya kuwathamini watu mbalimbali waliotoa
mchango wao katika fasihi ya Kiswahili (Malugu, 2011; Faustine, 2012 na Ponera,
2014).
Kupitia uandishi wake, Euphrase Kezilahabi katika fasihi ya Kiswahili alisaidia
kuleta mapinduzi ya uandishi kwa mtindo mpya katika utanzu wa ushairi, hivyo
kupelekea kuongezeka kwa waandishi wapya ambao walitunga kazi za kishairi na
kuleta maendeleo makubwa katika ushairi wa Kiswahili (Malugu, 2011; na Ponera,
2014).Euphrase Kezilahabi aliaga dunia akiwa na umri wa miaka sabini na sita (76)
mnamo tarehe 09/01/2020. Katika Fasihi ya Kiswahili, atakumbukwa daima
kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa katika kuleta mapinduzi ya uandishi
wa kazi za fasihi.
10
1.10 Muhtasari wa Sura ya Kwanza
Sura hii imefafanua vipengele mbalimbali vya utangulizi. Vipengele hivyo ni usuli
wa tatizo la utafiti, tamko la tatizo la utafiti na malengo ya utafiti. Aidha, sura hii
imebainisha maswali ya utafiti, manufaa ya utafiti, mawanda ya utafiti na historia ya
mwandishi. Katika sura inayofuata tutachambua mapitio ya maandiko na kiunzi cha
nadharia.
11
SURA YA PILI
MAPITIO YA MAANDIKO NA KIUNZI CHA NADHARIA
2.1 Utangulizi
Utafiti huu ulihusu Mdhihiriko wa Utanzia katika Ushairi wa Kiswahili, ambapo
mifano imedondolewa kutoka katika diwani za Euphrase Kezilahabi za Kichomi na
Dhifa. Sura ya pili inaweka misingi ya kinadharia na kubainisha kilichokwisha
kufanywa na watafiti waliotangulia. Hivyo, sura hii imeshughulikia mapitio ya
maandiko na kiunzi cha nadharia. Pia, imebainisha mapengo yaliyojitokeza kutokana
na mapitio ya maandiko. Kutokana na hilo, sura hii imegawanyika katika sehemu
kuu tatu: Sehemu ya kwanza ni mapitio ya maandiko. Katika sehemu hiyo
tumefafanua maandiko mbalimbali yanayohusiana na mada iliyoshughulikiwa.
Sehemu ya pili ni mapengo ya utafiti. Katika sehemu hiyo tumebainisha mapengo ya
maarifa yaliyotokana na mapitio na maandiko na jinsi yatakavyoshughulikiwa.
Sehemu ya tatu ni kiunzi cha nadharia, ambapo tunafafanua nadharia iliyoongoza
utafiti wetu.
2.2 Mapitio ya Maandiko
Mapitio ya maandiko yamegawanywa katika makundi mawili. Kundi la kwanza
linajumuisha maandiko kuhusu dhana ya utanzia. Kundi la pili linajumuisha
maandiko kuhusu na ushairi wa Euphrase Kezilahabi. Pia, sehemu hii imeyabainisha
mapengo yaliyojitokeza kutokana na kupitia maandiko.
2.2.1 Maandiko kuhusu Utanzia
Mganga (2019) anafafanua matumizi ya ramsa na tanzia katika utenzi wa Al-
Inkishafi Katika utafiti wake, amebaini kuwa ramsa na tanzia kama dhana pacha
zinajitokeza katika utenzi huo. Utafiti huu wa Mganga umefungua njia kwa namna
ulivyoishughulia dhana ya tanzia ambayo ndiyo dhana mama ya utanzia. Utafiti huu
umetusukuma zaidi kuuchunguza utanzia katika mashairi ili kuonesha namna
unavyodhihirika kwa kuchunguza matukio ya utanzia, dhima na athari zake kwa
wasomaji.
Mwangi na wenzake (2017) anafafanua vigezo vya ki-Aristotle vya kitanzia katika
utendi wa Fumo Liyongo. Katika uhakiki wao wamebaini kuwa utendi wa Fumo
Liyongo umejengwa katika misingi ya kitanzia kutokana na mhusika Fumo Liyongo
12
kuchomwa sindano ya shaba kitovuni na mtoto wake, jambo lililosababisha anguko
lake. Uhakiki huu ulikuwa na nia ya kutaka kudhihirisha kuwa utanzia kama mbinu
ya kiutunzi haijitokezi katika tamthiliya pekee. Kwa hakika, andiko hili lilimsaidia
mtafiti kwa kuweza kufahamu vigezo vya kitanzia vya ki-Aristotle vilivyojitokeza
katika utendi wa Fumo Liyongo. Aidha, andiko hili limeweza kubainisha kuwa
utendi wa Fumo Liyongo umejengwa kitanzia jambo ambalo lilituchochea katika
kuzamia mashairi huru ya Kezilahabi ili kuweza kuchunguza utanzia uliomo ndani
yake.
Mazongela (2016) anafafanua matumizi ya utanzia katika riwaya pendwa ya
Kiswahili. Anabainisha kuwa utanzia upo katika kazi mbalimbali za fasihi (simulizi
na andishi). Aidha, amebainisha aina tatu za utanzia ambazo ni utanzia wa kimwili,
utanzia wa kisaikolojia na utanzia wa kimaumbile. Vilevile, andiko hili limechambua
matukio mbalimbali ya utanzia yanayopatikana katika riwaya teule
zilizoshughulikiwa pamoja na ulinganisho wa riwaya hizo. Andiko hili lilimpa
mwanga mtafiti na kumchochea kuutafiti utanzia katika ushairi wa Kiswahili kama
utanzu mmojawapo wa fasihi ili kuonesha jinsi unavyodhihirika kupitia mashairi ya
Euphrase Kezilahabi. Hivyo, utafiti huu ulisaidia kubainisha matukio ya utanzia
kupitia mashairi teule au vitabu teule pamoja na athari zinazojitokeza na namna
mbinu hii ilivyotumika.
Ponera (2014) anajadili kuhusiana na fasihi na ubunilizi. Katika mjadala wake
anatueleza kuwa ubunilizi huweza kufanywa kwa kutumia mbinu mbalimbali.
Miongoni mwa mbinu hizo ni utanzia. Anaendelea kufafanua kuwa, utanzia ni
kinyume cha ufutuhi. Mbinu hii ya utanzia imekuwa ikitumia vipengele mbalimbali
vizuavyo huzuni, masikitiko, jitimai na mateso kwa hadhira. Andiko hili ni la
muhimu katika utafiti huu kwani lilitupa hamasa ya kuchunguza dhana ya utanzia
jinsi inavyodhihirika katika ushairi wa Kiswahili. Katika andiko hilo, Ponera (khj)
amebainisha tu mambo yanayopelekea utanzia lakini hajaelezea dhima na athari
zinazotokana na mbinu ya utanzia katika kazi za kifasihi.
Haji (2015) anajadili kuhusiana na matumizi ya utanzia katika riwaya teule za Said
Ahamed Mohamed. Katika uchunguzi wake anabainisha kuwa utanzia unapatikana
katika kazi za kifasihi (riwaya, tamthiliya na ushairi). Aidha, uchunguzi wake
13
unaelezea dhana ya utanzia kwa ujumla na vipengele vya utanzia kama vile, vifo,
ajali, vifungo, mabalaa, ulemavu, vilio, maradhi njaa na mateso kama vilivyotumika
katika riwaya teule. Andiko hili limetupa mwanga katika kuutafiti utanzia katika
ushairi wa Euphrase Kezilahabi kwani limedhihirisha wazi kuwa utanzia
haujajitokeza tu kwenye tamthiliya bali hata katika riwaya na ushairi. Hivyo, kuna
haja ya kubainisha matukio, kufafanua dhima na kufafanua athari za utanzia katika
diwani teaule za Euphrase Kezilahabi.
Chiraka (2011) anahakiki riwaya ya Takadini na kusema kuwa miongoni mwa mbinu
aliyoitumia mwandishi katika kuunda riwaya yake ni mbinu ya utanzia. Mhakiki
anaeleza kuwa riwaya hii ni ya mwendo wa taratibu kutokana na kujaa maudhui
yaliyojaa utanzia mwingi. Ameonesha matukio anuwai yaliyozua utanzia katika
riwaya hii kama vile ugumba wa Sekai kwa muda wa miaka tisa, ulemavu wa
Takadini, vita, upweke wa Sekai na kuuawa kwa walemavu na mapacha katika jamii
ya Sekai. Tahakiki hii ni muhimu katika utafiti huu kwa sababu ilionesha baadhi ya
matukio yaliyoibua utanzia kwa jamii. Zaidi, andiko hili lilitusaidia kuchunguza
utanzia katika ushairi wa Kiswahili ili kubainisha vipengele vya utanzia na athari
zake kwa wasomaji.
Soileau (2006) anatafiti kuhusiana na tanzia katika riwaya za karne ya kumi na tisa.
Katika utafiti wake, ametuonesha tofauti baina ya tanzia na utanzia katika fasihi.
Akitoa tofauti hiyo anasema kuwa tanzia ni kazi ya fasihi hasa katika tamthiliya
ambayo kwa sasa inajitokeza hata katika riwaya, ambayo inatoa maana halisi ya
maisha ya mwanadamu au mateso (anguko) pamoja na kuibua hisia fulani. Wakati
“utanzia” ni mbinu ya kisanaa inayoonesha tabia ya kiutamaduni inayoenea katika
dunia ya fasihi inayojulikana na kuhusiana na taratibu za maisha. Andiko hili
lilitusaidia, kwani limeweza kutoa tofauti ya dhana ya tanzia na utanzia katika fasihi.
Hivyo, andiko hili lilitupa hamasa ya kuangalia mbinu ya utanzia ili kuweza
kuthibitisha kuwa mbinu hii inapatikana hata katika utanzu wa ushairi.
Sengo (1992) anaandika kuhusiana na utamaduni wa Kiswahili wilaya ya Kusini
Unguja. Katika maelezo yake anavitaja vipengele anuwai vya kitamaduni kwa
Waswahili wa Kusini Unguja. Kipengele kimojawapo kinachotajwa ni mazishi.
Anaeleza kuwa, mazishi ni taasisi ya kuwarejesha waja walikotoka, ama
14
kuwakumbusha walio hai juu ya marejeo hayo kwa Mola. Msiba wa kufiwa huwa ni
faradhi-kifaya kwa Waislamu wote ujiranini. Anaendelea kutueleza kuwa, huzuni za
kufiwa huwa ni za wote na kazi kubwa ya majirani na marafiki ni kuwafariji
wanandugu waliofiwa. Katika andiko hili, Sengo ametuelezea kuhusiana na suala la
kifo na mazishi kama kipengele cha kitamaduni. Kupitia vipengele hivyo, tunaona
jinsi jamii inavyoingia simanzi na masikitiko kutokana na kuondokewa na mwenza
wao. Hivyo basi, tunaona umuhimu wa kubainisha matukio hayo ya utanzia na
namna yanavyodhihirika katika jamii, dhima na athari zake kwa jamii.
Mackeon (1974) anasema kuwa tanzia ni aina ya tamthiliya yenye uzito
unaodhihirika kihisia au kifikra. Tanzia huwa na suala, matendo na malengo ya dhati.
Aristotle alikuwa mtu wa kwanza ambaye baada ya kuyatazama maandishi ya
tamthiliya za Kigiriki aliandika maana ya tanzia katika kitabu chake cha Poetics.
Kutokana na uchunguzi wake aliona tanzia kuwa ni tamthiliya yenye huzuni ambayo
inagusia hisia za watazamaji kiasi cha kuogopesha na kumwonea huruma mhusika
mkuu ambaye hupata janga. Andiko hili lilitupatia dira kuwa hali ya huzuni kwa
mtazamaji au msomaji haipo katika tamthiliya peke yake, bali hata kwenye riwaya na
ushairi. Hivyo, mtaalamu Mackeon ametupa mwongozo juu ya utanzia katika
tamthiliya na kuchunguza matumizi ya mbinu ya utanzia katika ushairi wa Kiswahili.
Moh’d (2016) anashughulikia utanzia katika Kasida za Kiswahili kwa kutumia
mifano kutoka Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja. Anabainisha kuwa utanzia
umedhihirika katika Kasida za Kiswahili. Pia amebainisha maana ya utanzia na
kusema kuwa ni maneno au mazingira yanayozua huzuni, jitimai, majonzi,
masikitiko, majuto na maumivu ya mwili, roho au akili kwa hadhira. Anabainisha
dhima na kuchambua sifa za utanzia zilizojitokeza katika Kasida za Kiswahili.
Andiko hili limeweza kuleta hamasa tulitumie kutokana na kwamba limeelezea
utanzia kwa kina kwa sababu ameelezea dhima na vipengele vya utanzia. Hivyo,
kumchochea mtafiti kuutafiti utanzia katika diwani teule za Euphrase Kezilahabi.
Vilevile, andiko hili limesaidia katika kubainisha dhima za utanzia kupitia diwani
teule na athari zinazojitokeza katika kutumia mbinu ya utanzia.
15
2.2.2 Maandiko kuhusu Ushairi wa Euphrase Kezilahabi
Wamitila (2016) anaandika kuhusiana na jazanda katika mashairi ya Kiswahili.
Katika maelezo yake, anahakiki mashairi ya Kezilahabi yaliyomo katika diwani ya
Kichomi na Karibu Ndani. Wamitila anatueleza kuwa Kezilahabi ni stadi katika
kutumia jazanda ndani ya tungo zake. Kwa kutumia njia hii, mshairi ameweza
kujenga taswira ya picha kutokana na maelezo yake. Miongoni mwa shairi
lililohakikiwa na Wamitila ni “Chai ya Jioni”. Kupitia shairi hili, msomaji anajiwa na
picha au taswira ya mtu na mwenzake ambao wameketi wakielekea jua linakozama
huku wakinywa chai. Andiko hili lina umuhimu katika utafiti huu kwa kuwa
limeweza kutoa picha ya jumla kuhusiana na mashairi ya Euphrase Kezilahabi
kuhusiana na matumizi ya jazanda. Hata hivyo, halikushughulikia suala la utanzia,
jambo ambalo limetupa hamasa kuchunguza mdhihiriko wake katika diwani teule za
Euphrase Kezilahabi.
Senkoro (1988) anahakiki diwani ya Kichomi ya Euphrase Kezilahabi. Mhakiki huyu
ameonesha dhamira anuwai zilizojitokeza katika diwani hii ikiwa ni pamoja na
harakati za ujenzi wa jamii mpya, ukoloni mamboleo, falsafa ya maisha na ndoa na
mapenzi. Aidha, amehakiki matumizi ya vipengele vya kifani kama matumizi ya
taswira, muundo, mtindo na matumzi ya lugha. Uhakiki wa Senkoro ulikuwa na tija
katika utafiti huu, kwani umeweza kutufungulia njia ya kuyaelewa maudhui ya
diwani ya Kichomi pamoja na mbinu zake za kifani zilizotumika katika diwani hiyo.
Kutokana na uhakiki huu kuwa ni wa jumla mno, tulihamasika kuishughulikia mbinu
ya utanzia na kuona jinsi inavyodhihirika katika diwani teule za Euphrase
Kezilahabi.
Wamitila (2008) anaandika kuhusu mbinu ya ucheshi katika fasihi. Katika andiko
lake ameeleza kuwa ucheshi ni mbinu pana ambayo huweza kuelezwa katika namna
mbalimbali. Kwa kutumia diwani ya Dhifa, Wamitila (khj) anabainisha kuwa
mashairi mengi yaliyomo ndani ya diwani hii yametumia mbinu hii ya ucheshi.
Miongoni mwa ucheshi unaodhihirika humu ni ucheshi wa kibwege ambao
unapatikana katika shairi la ‘Mahojiano na Kifo’ (uk.42). Maelezo haya ya Wamitila
yamekuwa na umuhimu mkubwa katika utafiti huu. Hii ni kutokana na Wamitila
kujikita kuuchambua ucheshi katika mashairi ya Kezilahabi jambo ambalo limeacha
kinyume chake huzuni (utanzia) ambao umeshughulikiwa katika utafiti huu.
16
Wafula na Njogu (2007) wanasema kuwa kazi za ushairi za Kezilahabi zimetawaliwa
na mawazo ya kidhanaishi hasa kwenye diwani za Karibu Ndani (1988) na Kichomi
(1974). Katika mashairi hayo wameweza kubainisha msimamo wa mwandishi juu ya
maisha, ambapo anaona kuwa maisha hayana maana na hapa dunia tunapita tu.
Wametumia shairi la “Kisu Mkononi” (Kichomi uk. 13) ambalo wameliona
linasawiri ukosefu wa haki, na hatimaye, kujiamulia kwa mwanadamu kutenda
anavyotaka kabla ya kunaswa na mauti. Hivyo, andiko hili lilitusaidia katika kutafiti
zaidi kuhusiana na mbinu ya utanzia katika ushairi wa Kiswahili.
Senkoro (2011) anahakiki taswira katika baadhi ya mashairi ya Euphrase Kezilahabi.
Katika uhakiki wake, Senkoro anatueleza kuwa Kezilahabi amefaulu sana katika
kutumia taswira kwenye mashairi yake. Pia, mhakiki huyu ametushauri kuwa ili
kuweza kuyaelewa mashairi ya Kezilahabi basi hapana budi kwanza kuifahamu
falsafa yake. Akihakiki shairi la “Nimechoka” ambalo linapatikana katika diwani ya
Kichomi, anasema kuwa limezungumzia falsafa ya mwandishi kuhusu maisha.
Mshairi ameonesha ubaya wa maisha na vile ambavyo mtu hachagui wala hajiamulii
mwenyewe kuzaliwa. Tahakiki hii imemjulisha mtafiti kuhusiana na mambo
yanayopaswa kuzingatiwa katika uchunguzi wa mashairi ya Kezilahabi na
kumhamasisha kuichunguza zaidi diwani ya Kichomi ili kuweza kubaini matukio ya
utanzia, dhima za utanzia na athari zake kwa jamii vitu ambavyo
havikushughulikiwa katika tahakiki ya Senkoro.
Gaudioso (2018) anaandika kuhusiana na mikondo ya mtiririko wa ushairi wa
Kezilahabi na Mulokozi. Kwa upande wa Kezilahabi, mwandishi ametumia diwani
ya Kichomi katika kuthibitisha data zake. Gaudioso amebainisha kuwa kupitia diwani
ya Kichomi, Kezilahabi ana mchango mkubwa katika ushairi wa Kiswahili. Hii ni
kwa sababu ushairi wa Kiswahili uliweza kupata mkondo au mwelekeo mpya kupitia
tungo za mtiririko zilizomo ndani ya diwani teule. Makala hii ni muhimu katika
utafiti huu kwani imejadili mikondo mbalimbali ya ushairi wa Euphrase Kezilahabi
na mbinu mbalimbali za kibunilizi zilizotumika. Kwa kuwa Gaudioso
hakushughulikia utanzia, utafiti huu ulijikita kushughulikia utanzia kwa kubainisha
matukio ya utanzia na athari zake kwa jamii.
17
Mwakibete (2014) alichunguza kejeli na dhihaka katika mashairi ya Euphrase
Kezilahabi. Anabainisha sababu za kutumia kejeli na dhihaka katika mashairi yake
pamoja na kufafanua athari zinazotokana na mbinu hizo za kibunilizi. Pia, amebaini
kwamba kuna taswira, sitiari, ishara na picha zinazojenga mbinu ya kejeli na dhihaka
katika ushairi wa Euphrase Kezilahabi. Andiko hili ni muhimu kwa utafiti huu
kutokana na kuchunguza ushairi wa Euphrase Kezilahabi na kutoa uelekeo kwa
mtafiti kutumia katika utafiti wake. Mwakibete (khj) hakuchunguza utanzia bali
anachunguza kejeli na dhihaka katika mashairi ya Euphrase Kezilahabi ambazo
zimetoa mchango katika kueleweka kwa mashairi yanadhihirisha utanzia. Hivyo,
andiko hili limetupa hamasa ya kuangalia mbinu ya utanzia katika diwani teule za
Euphrase Kezilahabi.
Acquaviva (2004) anaandika kuhusiana na jazanda za njozi katika mashairi ya
Euphrase Kezilahabi. Anabainisha sitiari na mafumbo yanayojitokeza katika diwani
ya Kichomi (1974) na Karibu Ndani (1988). Anaendelea kuelezea namna njozi za
ulimwengu zinavyotokeza katika ushairi wa Kezilahabi zinafanana sana na zile za
mtu anayeweweseka akiwa usingizini. Jazanda za njozi hizo zinadhihirika katika
diwani ya Kichomi kwenye shairi la “Wimbo wa Mlevi” (uk.64). Makala hii imetupa
mwanga kwa sababu inajadili juu ya sitiari na mafumbo yalivyojitokeza katika
mashairi ya Euphrase Kezilahabi. Acquaviva hajazungumzia utanzia ila anatoa picha
ya jumla ya ushairi wa Euphrase Kezilahabi, hivyo utafiti utajikita katika kubainisha
matukio, dhima na athari ya utanzia katika diwani teule.
Gaudioso (2014) anajadili kuhusiana na kuwako na wakati, mipaka ya lugha kama
hatua za falsafa katika mashairi ya Euphrase Kezilahabi. Vilevile, anashughulikia
namna lugha ilinavyotumika katika mashairi ya Kezilahabi na namna yanavyoendana
na wakati husika. Anaelezea umuhimu wa lugha katika mashairi ya Kezilahabi
pamoja na mgogoro katika lugha ya kishairi. Pia, anafafanua falsafa ya mtunzi na
kulinganisha na wanafalsafa wa Magharibi kama Martin Heidegger na Friederich
Nietzsche. Makala hii ina umuhimu katika utafiti huu kwa sababu imeonyesha
falsafa ya mwandishi ambayo imetusaidia kufahamu mbinu ya kitanzia ilivyojitokeza
kwa mwandishi Euphrase Kezilahabi. Hivyo, andiko hili limetupa mwanga katika
kuchunguza zaidi juu ya utanzia katika diwani teule.
18
2.2.3 Mapengo Yaliyojitokeza Kutokana na Mapitio ya Maandiko
Kwa jumla, maandiko tuliyoyapitia hapo juu yamejikita katika kushughulikia mambo
mbalimbali yanayohusiana na dhana ya utanzia pamoja na ushairi wa Euphrase
Kezilahabi. Hata hivyo, kutokana na mapitio ya maandiko hayo tumebaini kuwa
utanzia katika fasihi ya Kiswahili si toshelevu kwa sababu imejitokeza katika utanzu
wa tamthiliya na riwaya licha ya mbinu hii kuwaathiri sana watunzi wa kazi za
fasihi. Pia, kwa utanzu wa ushairi imekuwa shida sana kwa wasomaji na wahakiki
kuielewa mbinu ya utanzia katika kazi kwa urahisi na kuonekana kuwa ni ngumu.
Kutokana na maandiko tuliyoyapitia tulibaini mapengo yafuatayo: Mosi,
kutobainishwa kwa matukio ya utanzia katika ushairi wa Kiswahili. Pili,
kutofafanuliwa kwa kina dhima za matumizi ya utanzia katika ushairi wa Kiswahili.
Tatu, kutochunguzwa kwa athari za utanzia katika ushairi wa Kiswahili. Hivyo,
kutokana na mapengo hayo, tasinifu hii imekusudia kuyaziba kwa kubainisha
matukio ya utanzia yanavyodhihirika katika diwani teule. Pia, utafiti umebainisha
dhima za utanzia katika diwani teule. Na mwisho, tumefafanua athari za utanzia kwa
wasomaji kupitia diwani teule.
2.3 Kiunzi cha Nadharia
Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya Upokezi. Uteuzi wa nadharia hii ulitokana na
ukweli kwamba, mihimili yake inaumana na malengo ya utafiti wetu. Hivyo,
ukusanyaji wa data, uchambuzi na uwasilishaji wake ulifanywa kwa kuzingatia
mihimili ya nadharia ya upokezi.
Kwa mujibu wa Wafula na Njogu (2007), upokezi ni nadharia inayoshughulikia
upokeaji wa matini za fasihi zinayohusiana na ulimbwende na mitazamo ya
kisaokolojia. Kimapokeo, msomaji huwa na mawazo juu ya matini anayoipitia.
Kutokana na tajriba ya usomaji, msomaji hupata hisi maalumu. Utunzi na upokeaji
wa sanaa hushirikishwa sana na hisi kwa mujibu wa imani na nadharia za
kilibwende. Hisi ndizo humpa mwanasanaa msukumo wa kutunga. Vilevile, msomaji
anatazama kuipokea kazi ya fasihi kwa kuzingatia mielekeo yake binafsi.
Nadharia hii imeanza kupata mashiko zaidi kuanzia miaka ya sabini ya karne ya
ishirini. Waasisi wake wakuu ni Wolfgang Iser (1974, 1978), Stanley Fish (1980),
James Tompkins (1980), na Haus Robert Jauss (1982). Nadharia hii inayohusisha
19
upokeaji wa sanaa na inanuia kubainisha na kufafanua kadhia zinazomkutanisha
msomaji na kazi ya fasihi. Wanafasihi wa nadharia hii hujishughulisha na maswali
manne ya msingi ambayo ni;
(i) Kuna uwiano wowote kati ya maana ya kazi inayosomwa na jinsi
msomaji anavyohakiki?
(ii) Je, kila kazi ya fasihi ina maana kufuatana na msomaji binafsi na jinsi
msomaji anavyoichukulia?
(iii) Kuna wasomaji ambao husoma na kufasiri kazi ya fasihi vizuri zaidi
kuliko wasomaji wengine?
(iv) Msomaji hutumia vigezo gani kujijulisha iwapo mawazo yake juu ya kazi
fulani yanafaa au hayafai?
Baada ya msomaji kujiuliza maswali ya muhimu katika nadharia ya upokezi katika
kazi ya sanaa, hufuata hatua tatu ili kuelewa kazi ya fasihi. Hatua hizo ni:
(a) Kurejelea kazi hiyo inayosomwa kwa tafsiri ili ithibitishwe kwamba kazi
hiyo inaafikiana na yale yanayokumbukwa na msomaji.
(b) Kubainisha jinsi miktadha ya matini isiyohusika moja kwa moja na
maandishi inavyoweza kuhusishwa na kutenganishwa na msomaji.
(c) Kudhihirika kwa maoni ya msomaji yanayofungamana na mada muhimu za
hadithi.
Adena Rosmarin (katika Murfin, 1991) anasema, kazi ya fasihi ni kama kinyago
ambacho hakijakamilika. Mchongaji wa kinyango hiki kisichokuwa kamili hujaribu
kukikamilisha. Hata katika kazi ya fasihi, msomaji huikamilisha kazi ya sanaa kwa
kuijaliza kwa usomaji makini au huidhalilisha kazi hiyo kwa usomaji wa kiholela.
Nadharia inasisitiza athari za kazi ya kifasihi juu ya akili na maarifa ya mwandishi.
Athari zinaweza kufasiriwa na wasomaji mbalimbali kwa namna tofauti tofauti. Fish
anasema, sanaa ya maneno haichanganuliwi kwa kutumia mikakati ya jambo la
kisayansi katika maabara. Jaribio la kisayansi laweza kuonyesha ujuzi uliofanikiwa
au ambao haujafanikiwa. Anayefanya jaribio la kisayansi ameweka mpaka wa kihisia
na kimawazo kati ya nafsi yake na jambo linalomshughulisha. Tofauti na hayo
20
mhakiki wa kazi ya fasihi hawezi kujitenga na riwaya, tamthiliya au ushairi
aliousoma.
Iser na Fish wanadai kwamba kazi ya fasihi mara kwa mara ina mapengo mengi,
msomaji anapaswa kuyaziba mapengo hayo. Kutokana na kujiuliza, msomaji
ulazimika, kutunga matini mpya ambazo zimechochewa na kuzalika kutokana na
matini asili zilizopo kwenye kurasa. Maneno na sentensi zilizomo kwenye matini
asilia humsukuma msomaji kuandika maneno mengine mapya na sentensi nyingine
mpya. Hivyo, msomaji anajukumu kubwa na gumu la kuandika kazi mpya
iliyotokana na matini asilia. Jukumu hili ni kujizatiti kufahamu kazi ya fasihi kadiri
ya uwezo wake. Kwa mujibu wa Ponera (2014), mihimili ya nadharia ya upokezi
kama ifuatavyo:
Mosi, nadharia hii inamlenga moja kwa moja msomaji wa matini ya kifasihi,
msomaji anapaswa kuijenga upya kazi ya fasihi kulingana na kile alichokielewa
kutoka kwenye hiyo matini asilia. Pili, nadharia hii hushughulikia uhusiano uliopo
kati ya fanani wa kazi ya fasihi, msomaji wa kazi, mchakato wa usomaji pamoja na
maana ya matini.
Hivyo basi, mihimili hiyo ndiyo iliyotumika katika ukusanyaji wa data, uchambuzi
na uwasilishaji wa matokeo ya utafiti. Vipengele vya kitanzia vilichunguzwa kwa
kuhusishwa na vipengele vingine vya maisha ya mtunzi kama vile, matukio ya
kihistoria yaliyojiri kabla au wakati wa utunzi, tabia na mwenendo halisi, hali halisi
ya maisha tangu kipindi cha baada ya kazi husika kutungwa hadi sasa na jografia ya
alipokuwa mtunzi (kurejelea maana ya kazi iliyosomwa). Aidha, uchunguzi
ulihusisha mabunio na fikra binafsi za mtafiti kuhusiana na lugha na mawazo
mbalimbali yaliyojitokeza katika diwani teule (hapa tuliweza kubainisha miktadha ya
matini inayohusiana na maandishi). Vilevile, uchambuzi wa data ulizingatia mtindo
mahususi wa lugha ambao mtunzi aliutumia katika kuwasilisha mawazo yake kwa
kutumia mbinu ya utanzia (hapa kudhihirisha maoni ya msomaji yanavyofungamana
na mada husika).
21
2.4 Muhtasari wa Sura ya Pili
Sura hii imebainisha maandiko mbalimbali yanayohusiana na mada ya utafiti.
Maandiko hayo yamegawanywa katika makundi mawili. Kundi la kwanza
limejumuisha maandiko kuhusu dhana ya utanzia; kundi la pili limejumuisha
maandiko kuhusiana na ushairi wa Euphrase Kezilahabi. Pia, sura hii imeyabainisha
mapengo yaliyojitokeza kutokana na kupitia maandiko. Aidha, katika sura hii
tumefafanua nadharia ya upokezi ambayo ndiyo ilituongoza katika utafiti wetu. Sura
inayofuata inafafanua methodolojia ya utafiti, ambapo vipengele anuwai vya
kimethodolojia vimejadiliwa kwa kina.
22
SURA YA TATU
METHODOLOJIA YA UTAFITI
3.1 Utangulizi
Sura hii ya tatu katika utafiti uliohusu Mdhihiriko wa Utanzia katika Ushairi wa
Kiswahili: Mifano Kutoka Kichomi na Dhifa inawasilisha namna utafiti
ulivyofanyika ili kupata data stahiki. Hivyo, katika sura hii tumefafanua
methodolojia1 ya utafiti.Katika sura hii tumevifafanua vipengele vya methodolojia ya
utafiti ambavyo ni: usanifu wa utafiti, mkabala wa utafiti, eneo la utafiti, walengwa
wa utafiti, ukusanyaji wa data, njia na zana za kukusanyia data na mchakato wa
ukusanyaji wa data. Vipengele vingine ni uchanganuzi wa data, itikeli za utafiti,
uhalali na uthabiti wa matokeo ya utafiti na changamoto za utafiti na utatuzi wake.
3.2 Usanifu wa Utafiti
Kwa mujibu wa Kothari (2004), usanifu wa utafiti ni mpango wa kazi wa jumla wa
namna ya kufanya utafiti. Hii ni hoja ya kifikra kabla ya mtafiti hajaanza kufanya
utafiti wake. Utafiti huu ulihusisha usanifu wa kifenomolojia. Usanifu huu
hujihusisha na kusaka data za uyakini wa fenomena husika kwa kujigeza sana katika
uelewa, mtazamo na tajiriba za watafitiwa. Hii humaanisha kuwa, mtafiti hutakiwa
kutengeneza mazingira ya kuwa na muda unaomwezesha kuonana ana kwa ana na
watafitiwa wake ili kupata data sahihi na za kina kuhusu jambo analolitafiti (Ponera,
2019).
3.3 Mkabala wa Utafiti
Utafiti huu ulitumia mkabala wa kitaamuli. Ponera (2016) anasema kuwa, katika
mkabala wa kitaamuli, utafiti hutumia zaidi tafakuri katika kuhusisha taarifa
mbalimbali za kitafiti, kisha kutoa ufafanuzi kwa kuzingatia misingi ya nadharia
husika pamoja na ithibati bayana zipatikanazo uwandani.
Utafiti huu ulikuwa wa maktabani na uwandani ambapo data zake zilikusanywa kwa
kufuata mkabala wa kitaamuli. Enon (1998) anabainisha kuwa mkabala wa kitaamuli
ni njia ya ukusanyaji wa data zinazolenga kupata data kwa njia ya maelezo. Naye
Kothari (2004) anatueleza kuwa, mkabala wa kitaamuli unaleta matokeo yasiyoweza
1 Methodolojia ni jumla ya seti na taratibu zinazofuatwa katika ufanyaji wa jambo fulani. Hivyo,
methodolojia huangazia sayansi nzima ya kuteua, kutumia na kuhusisha mbinu na hatua mbalimbali
zinazotumika kuendesha utafiti (Ponera, 2019).
23
kupimwa na yasiyoonesha idadi au kiasi na unalenga kutoa maelezo zaidi. Hivyo
basi, katika utafiti huu data hazikuwasilishwa kitakwimu. Hii ni kwa sababu mkabala
huu unahusika na ukusanyaji wa data kwa njia ya maelezo bila ya kuhusisha
takwimu. Mkabala huu unafaa zaidi kutumika katika tafiti zinazohusu masuala ya
sayansi ya jamii kama vile fasihi. Aidha, haufungwi na kanuni na huweza kutumika
pamoja na njia zingine kama vile mahojiano na udurusu wa maandiko ambazo
zimetumika katika utafiti huu. Data zipatikanazo kwa kutumia mkabala huu
hupambanuliwa kiimani, kiitikadi au kimtazamo. Hivyo, zinaweza kuwa na tafsiri
nyingi (Enon, 1998; White, 2002) Kwa mantiki hiyo, ukusanyaji wa data,
uchanganuzi wa data na utoaji wa matokeo ya utafiti vilifanywa kwa kutumia
mkabala wa kitaamuli.
3.4 Eneo la Utafiti
Utafiti huu ulifanyika katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma. Sababu ya
kuuchagua mkoa wa Dar es Salaam ni kwa kuwa kuna maandiko ya kimaktaba
kutoka makavazi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na ukongwe wa chuo
hicho. Makavazi hayo yalimsaidia mtafiti kudurusu machapisho mbalimbali kama
vile vitabu, majarida na tasnifu zilizohusiana na mada yetu ya utafiti. Pia,
walipatikana wataalamu waliojishughulisha na uhakiki au utafiti kuhusiana na diwani
za Euphrase Kezilahabi. Mkoa wa Dodoma tuliuchagua kwa sababu ya kuwapo kwa
matini yanayohusiana na fasihi ya Kiswahili pamoja na wataalamu wa fasihi ya
Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma ambao walisailiwa na mtafiti ili kupata
data zinazoendana na utafiti wetu.
3.5 Walengwa wa Utafiti
Walengwa wa utafiti ni wale wote watakaohusika katika utafiti husika (Ponera,
2014). Katika utafiti huu, walengwa wa utafiti waligawanyika katika makundi
mawili ambayo ni wango tafitiwa na sampuli ya watafitiwa.
3.5.1 Wango Tafitiwa
Kwa mujibu wa Ponera (2014), wango tafitiwa ni vitu vyote ambavyo mtafiti
anaweza kuvitumia kwa ajili ya kupata data za utafiti wake. Jamii ya watafitiwa
huweza kuwa kundi la watu, eneo fulani la kijografia, aina ya miti au aina fulani ya
24
maandiko. Hivyo, taarifa za utafiti huu zilipatikana kutoka katika makundi
yafuatayo:
i. Vitabu anuwai vya ushairi vilivyoandikwa na Euphrase Kezilahabi: Kupitia
diwani hizi tuliweza kuona utanzia jinsi ulivyodhihirika;
ii. Wataalamu wa fasihi ya Kiswahili waliozisoma au kuzihakiki diwani za
Euphrase Kezilahabi;
iii. Wasomaji wa diwani teule za Euphrase Kezilahabi ambao ni wanafunzi wa
shahada ya umahiri na uzamivu na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma
na Dar es Salaam. Hawa walisaidia katika kutuelezea namna
wanavyoathirika na utanzia uliomo katika diwani teule za Eupharse
Kezilahabi.
3.5.2 Usampulishaji na Sampuli ya Watafitiwa
Usampulishaji na sampuli ni istilahi muhimu katika mchakato wa utafiti kutokana na
mada ya utafiti. Maelezo kuhusu istilahi hizi ni kama ifuatavyo:
3.5.2.1 Usampulishaji
Usampulishaji ni mchakato wa kuteua sehemu ndogo ya kundi kubwa la watafitiwa
kwa lengo kumpatia mtafiti taarifa ambazo anazitumia kutoa majumuhisho
yanayowakilisha kundi la watafitiwa (Trochim, 2006). Pia, Sanga (2018) anasema
usampulishaji ni mbinu ya kuteua sehemu ndogo ya wanajamii katika jamii kubwa ili
watumike kama kiwakilishi cha sifa, mienendo, mawazo, hisia na mitazamo ya jamii
nzima. Sanga (khj) anaendelea kusema kwamba, idadi ya watafitiwa inaweza
kupatikana kwa kuzingatia malengo ya utafiti, data zinazokusanywa na sifa za
watafitiwa. Mara kwa mara katika utafiti wa kitaamuli watafitiwa huwa wachache
tofauti na utafiti wa kitakwimu ambao huhitaji majibu kutoka kwa watafitiwa. Utafiti
wa kitaamuli uhitaji mtafiti kutumia muda mwingi kuwahoji watafitiwa ili kuweza
kupata maelezo yao kwa kina.
3.5.2.2 Sampuli ya Watafitiwa
Sampuli ni sehemu ya jamii ya watu iliyochaguliwa ili kutoa taarifa zitakazokuwa
kiwakilishi cha jamii nzima. Katika utafiti huu, mtafiti alitumia sampuli lengwa.
Kwa mujibu wa Kombo na Tromp (2006), usampulishaji lengwa ni mbinu ambayo
mtafiti hulenga kundi fulani la watu, vitu au dhana zinazoaminika na kuwa na
25
uhakika juu ya utafiti husika. Sababu ya kuchagua mbinu hii ni kwamba, inampa
uhuru mtafiti wa kuteua watafitiwa kwa mujibu wa kusudio na malengo ya utafiti
wake. Prewitt (1985) anasema kuwa idadi ya sampuli haihitaji kuwa sawa na watu
waliolengwa katika utafiti lakini sifa ya sampuli itakiwayo katika idadi ni muhimu
kufikiwa. Vilevile, mbinu ya sampuli lengwa husaidia kupata data zenye ukubalifu
na utoshelevu na husaidia katika kuokoa muda pamoja na kupunguza gharama.
Aidha, mbinu hii hufaa zaidi katika utafiti wa kitaamuli kama huu, yaani usiotumia
takwimu.
Watafitiwa walichaguliwa kutokana na ufahamu wao na jinsi walivyotosheleza
matakwa na malengo ya utafiti huu. Sampuli hiyo ilichaguliwa kutoka katika
makundi yote yaundayo wango la watafitiwa ili kutoa fursa sawa kwa kila mlengwa
kutafitiwa. Katika kufanikisha hili, vigezo vilivyotumika kuwapata ni viwili
ambavyo ni asili ya utafiti ambao ni wa kitaamuli na miongozo ya kinadharia kuhusu
tafiti za kitaamuli kutoka kwa wataalamu wa utafiti kama vile Kothari (2004) na
Ponera (2019) Hivyo, sampuli yetu katika utafiti huu ilikuwa kama ifuatavyo:
i) Diwani mbili za ushairi zilizotungwa na Euphrase Kezilahabi ambazo ni
Kichomi na Dhifa. Uteuzi wa diwani hizi ulitokana na ukweli kwamba
zimetumia mbinu ya utanzia kwa kiasi kikubwa;
ii) Wataalamu wanne waliosoma au kuzihakiki diwani teule. Hawa walisaidia
katika kueleza maana ya mashairi ya Kezilahabi na mbinu zake; na
iii) Wasomaji wanane wa diwani teule za Euphrase Kezilahabi ambao ni
wahadhiri pamoja na wanafunzi wa shahada ya uzamivu. Hawa walisaidia
katika kutuelezea namna wanavyoathirika na utanzia uliomo katika diwani
teule.
Sampuli hii ilipatikana kwa kutumia usampulishaji sinasibu ambapo mchakato wa
kuwateua watafitiwa ulifanywa na mtafiti kwa kuelekeza fikra kwa baadhi ya
watafitiwa kulingana na wanavyoweza kukidhi data za utafiti. Mara nyingi, aina hii
ya usampulishaji inahusu tafiti zinazihitaji sampuli ndogo na hutumika hasa kwa
tafiti za kitaamuli. Usampulishaji huo umefanywa kwa kutumia mbinu ya uchaguzi
lengwa. Uchaguzi lengwa unahusiana na kuchagua watafitiwa kwa kujiegemeza
katika kuwapo kwa sifa za kipekee zinazofanya ufaafu na uhusika wao katika utafiti
26
husika kuwa wa upekee. Mtafiti ameweza kuwateua watafitiwa kutokana na ufahamu
maarifa waliyonayo kuhusiana na mada ya utafiti pamoja ubobevu wao katika kazi
za Euphrase Kezilahabi.
3.6 Ukusanyaji wa Data
Sehemu hii inafafanua njia na zana mbalimbali zilizotumika katika ukusanyaji wa
data pamoja na mchakato wa kukusanya data.
3.6.1 Njia na Zana za Kukusanyia Data
Ukusanyaji wa data ulifanyika kwa kutumia zana mbalimbali kama vile kompyuta
pakatwa, simu kwa ajili ya kurekodi, kamera ndogo ya picha za mgando, mwongozo
wa usaili, mwongozo wa uchanganuzi wa matini, kalamu na daftari dogo. Njia
zilizotumika kukusanyia data ni usaili na uchanganuzi wa matini. Mtafiti alitumia
njia zaidi ya moja kwa sababu ya kuleta uhalali na uthabiti wa matokeo ya utafiti
wake. Pia, kutokana na ukweli kuwa hakuna njia moja ya ukusanyaji wa data
inayojitosheleza (Cohen na wenzake, 2007).
3.6.1.1 Usaili
Kombo na Tromp (2006) wanafafanua usaili kuwa ni njia ya kukusanya data kwa
kuhusisha mazungumzo baina ya mtafiti na mtafitiwa kuhusu jambo ambalo mtafiti
anakusudia kulipata. Hii ni njia inayotumika sana katika tafiti zinazotumia mkabala
wa kitaamuli (Kothari, 2004). Kwa mujibu wa King’ei na Kisovi (2005), usaili
unaweza kuwa wa ana kwa ana au kwa nyenzo za kielektroniki kama vile simu kwa
ajili ya kuendesha mazungumzo. Njia hii ni muhimu sana kwani ilimwezesha mtafiti
kupata data za awali na za kina. Pia, mtafiti aliweza kuuliza maswali ya ziada iwapo
kuna haja ya kufanya hivyo (Kothari, 2004; Hays na Sigh, 2012; Maxwell, 2013).
Mtafiti aliuliza maswali kwa wataalamu mbalimbali wa taaluma ya Fasihi kwa
kutumia mwongozo wa maswali ya usaili ulioandaliwa.
3.6.1.2 Uchanganuzi Matini
Uchanganuzi wa matini ni njia ya kukusanya data ambapo taarifa hukusanywa
kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya maandishi (Maxwell, 2013). Hivyo, humpa
mtafiti undani wa suala linalotafitiwa kwa kulinganisha na kupatanisha ushahidi
uliopatikana katika vyanzo vya awali. Vilevile, taarifa za njia hii ya uchanganuzi
27
matini huwa hazibadiliki na zinaweza kupitiwa na wengine. Uchanganuzi wa matini
unahusisha vitabu teule. Kwa kutumia mwongozo wa uchanganuzi wa matini, mtafiti
alidurusu na kuchanganua matini zinazohusiana na mada ya utafiti ili kupata data na
kushadidia hoja na data za msingi. Katika kufanikisha hili, mtafiti alitumia maktaba
ya Chuo Kikuu cha Dodoma na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili kusoma
machapisho yaliyohusiana na mada ya utafiti ili kupata data za upili.
3.6.2 Mchakato wa Ukusanyaji wa Data
Ukusanyaji wa data za utafiti ulizingatia taratibu zinazoongoza mchakato wa kufanya
utafiti. Mosi, tuliomba rihusa ya kufanya utafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma.
Pili, tuliomba ridhaa ya kufanya utafiti katika mamlaka husika kabla ya kuanza
shughuli ya ukusanyajiwa data za uwandani na maktabani. Tatu tuliomba ridhaa kwa
watafitiwa na kuwaeleza malengo na makusudio ya utafiti huu, muda tutakaotumia
katika utafiti pamoja faidi na athari zitakazojitokeza tusipopata ushirikiano wao.
Data zilikusanywa kutoka maktabani na uwandani. Data za maktabani zilikusanywa
kutoka katika tasinifu, majarida vitabu, makala na data za mtandaoni. Mchakato wa
ukusanyaji data uliongozwa na mwongozo wa uchanganuzi matini na ulitumia
mwezi mmoja katika kukusanya data. Mwongozo wa usaili ulitumika kukusanyia
data za uwandani. Data zilikusanywa kutoka kwa wataalamu wa fasihi kwa njia ya
mahojiano. Ukusanyaji wa data za uwandani ulifanyika kwa majuma matatu katika
mikoa ya Dar es Salaam tulitumia jumamoja na Dodoma majuma mawili.
3.7 Uchanganuzi wa Data
Uchanganuzi wa data ni mchakato wa kuzishughulikia data zitakazopatikana katika
mchakato wa ukusanyaji ili ziweze kueleweka zaidi (Kothari, 2004). Data za utafiti
huu zilichanganuliwa kwa kutumia mbinu ya kusimbisha maudhui. Kwa mujibu wa
Ponera (2019), mbinu hii ni maarufu katika kufafanua ujuzi, tajriba, maana na uhalisi
wa watafitiwa. Data zilichanganuliwa kwa kutathmini jinsi matukio yalivyotokea
pamoja na maingiliano ya vilongo na vionjo vya kijamii. Aidha, data za utafiti huu
zimewasilishwa kwa njia ya maelezo. Mbinu hii hutumika kuchanganua data bila ya
kutumia mahesabu (Kombo na Tromp, 2006). Katika hatua hii, mtafiti alifafanua na
kuchanganua maelezo ya msingi yaliyotolewa na watafitiwa kulingana na
yanavyohusiana na mada kwa kuzingatia mahitaji ya malengo ya utafiti. Mtafiti
28
alizipanga data zake kulingana na malengo ya utafiti na kuzitolea maelezo. Data
ziliwasilishwa kwa njia ya maelezo ambayo yalihusiana na lengo mahususi husika na
kisha kutoka katika dondoo hilo ambapo maelezo ya kiuchambuzi yalitolewa. Kwa
kufanya hivyo, aliweza kukamilisha malengo ya utafiti kwa namna ambayo
inatakiwa.
3.8 Itikeli ya Utafiti
Utafiti huu uliendeshwa kwa mujibu wa maadili yaongozayo mchakato mzima wa
utafiti. Katika hatua hii, mtafiti alizingatia mambo muhimu kama vile kuomba ridhaa
kutoka katika mamlaka zinazohusika ili zimruhusu kukusanya data za kimaktaba
katika maeneo au taasisi zao; kuomba ridhaa ya watafitiwa ili wakubali kutafitiwa,
utunzaji wa siri za taarifa na uhifadhi wa majina ya watoa taarifa kadiri ya matakwa
ya watafitiwa. Itikeli ya utafiti ni dhana inayorejelea mazingatio ya haki ya mtafitiwa
na kuzuia madhara dhidi yake (Hays na Sigh, 2012).
Katika kuhakikisha itikeli ya utafiti inazingatiwa, kabla ya kuanza mchakato wa
kukusanya data, mtafiti aliomba kibali kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma na mamlaka
zinazohusika katika utafiti huu, pia kuomba idhini ya kufanya utafiti katika Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam. Vilevile, mtafiti alijitambulisha kwa watafitiwa na
kuomba utayari wao ili kuweza kushirikiana nao katika mchakato wa ukusanyaji
data. Baada ya hapo, mtafiti alijenga mahusiano mazuri na watafitiwa uwandani
ikiwa ni pamoja na kuwaeleza lengo la utafiti huu kuwa ni la kitaaluma tu na si
vinginevyo. Pia, mtafiti aliomba ridhaa ya kurekodi na kupiga picha za mnato,
vielelezo vilivyokuwa na uhusiano na utafiti huu ili kusaidia katika kuhifadhi
kumbukumbu katika uchanganuzi wa data. Vilevile, mtafiti alitunza siri za
watafitiwa.
3.9 Uhalali na Uthabiti wa Matokeo ya Utafiti
Sanga (2018) anasema utafiti uliosanifiwa vizuri huweza kuyafikia malengo ya
utafiti kwa namna iliyo wazi na inayoeleweka, ubora wa utafiti hutokana na sifa ya
uhalali na uthabiti wake katika matokeo ya utafiti. Maxwell (1996) na Dey (2005)
wanafafanua kuwa uhalali wa matokeo katika mkabala wa kitaamuli huhusisha hali
ya kuaminika kwa maelezo, hitimisho, ufafanuzi, ufasili na aina yoyote ya maelezo
yaliyotolewa. Uhalali wa matokeo hudhihirika wakati mbinu, vifaa na njia za utafiti
29
zinaleta matokeo yasiyo badilikabadilika katika muktadha au mazingira husika.
Uthabiti wa utafiti ni uhalisi wa matokeo ya utafiti na hupatikana ikiwa taarifa za
utafiti zitatokana na vyanzo sahihi vya tatizo la utafiti (Patton & Michael 2002).
Uhalali wa matokeo ya utafiti huu ulifikiwa kwa mtafiti kuweka bayana mipaka ya
utafiti kwa watafitiwa. Pia, mtafiti alitumia lugha nyepesi na ya moja kwa moja
katika kukusanya data ili sampuli isipate tabu kuelewa kinachotafitiwa. Vilevile,
mtafiti alitumia njia zaidi ya moja katika kukusanya data za utafiti. Hivyo,
utekelezaji huu, ulipelekea matokeo ya utafiti kuwa ni halali na thabiti.
3.10 Changamoto za Utafiti na Utatuzi Wake
Ijapokuwa kumekuwa na mafanikio katika utafiti huu, lakini mtafiti amekumbana na
changamoto mbalimbali katika ukusanyaji wa data za uwandani na maktabani.
Kwanza, ni mlipuko wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona 2019 (UVIKO-19) na
kupelekea mtafiti kuchelewa kukusanya data kwa wakati aliopanga. Hii ilitokana na
kuwa, kwa muda wa miezi mitatu vyuo vilifungwa nchi nzima kutokana na ugonjwa
wa virusi vya korona. Changamoto hii ilitatuliwa kwa kuwatafuta watafitiwa
wachache waliopatikana na kuweza kukidhi malengo ya utafiti. Pili, kutofahamika
kwa urahisi kwa dhana ya utafiti huu kwa watafitiwa na kusababisha ugumu katika
upatikanaji wa data. Kutofahamika kwa mbinu ya utanzia kutokana na kutotafitiwa
vya kutosha na kufahamika kwa wataalamu wengi hasa katika utanzu wa ushairi.
Changamoto hii ilitatuliwa kwa mtafiti kuwaelewesha kuhusuiana na dhana ya
utanzia na utumikaji wake katika ushairi. Tatu, kutosomwa kwa kina kazi za ushairi.
Watafitiwa wengi walishindwa kukidhi malengo ya utafiti huu kwa kuwa
waliposoma diwani teule hawakusoma kwa kina zaidi, hivyo kushindwa kukidhi
malengo husika. Changamoto hii, ilitatuliwa kwa mtafiti kujikita kwenye mawazo ya
wataalumu wachache na kuyahusisha na yale yaliyopatikana kutoka kwenye matini
mbalumbali.
3.11 Muhtasari wa Sura ya Tatu
Katika sura hii tumevifafanua vipengele vya methodolojia ya utafiti. Vipengele hivyo
ni usanifu wa utafiti katika kipengele hicho tunapata mchakato mzima wa namna ya
ukusanyaji data na namna ya kuzichanganua data. Eneo la utafiti katika kipengele
hiki mtafiti anapaswa kuelezea eneo la kijografia ambapo anakwenda kufanyia utafiti
na kuelezea sababu ya kuchagua eneo hilo kwa kuzingatia vigezo vya upatikanaji wa
30
watafitiwa na eneo la kupata nyaraka za kusoma. Walengwa wa utafiti, ukusanyaji
wa data, njia na zana za kukusanyia data na mchakato wa ukusanyaji wa data.
Vipengele vingine ni uchanganuzi wa data, itikeli za utafiti, uhalali na uthabiti wa
matokeo ya utafiti na changamoto za utafiti na utatuzi wake. Sura inayofuata
inawasilisha na kujadili matokeo ya utafiti.
31
SURA YA NNE
UWASILISHAJI NA MJADALA WA MATOKEO YA UTAFITI
4.1 Utangulizi
Sura hii inawasilisha na kujadili matokeo ya utafiti uliohusu Mdhihiriko wa Utanzia
katika Ushairi wa Kiswahili: Mifano Kutoka Kichomi na Dhifa. Utafiti huu
ulifanyika kutokana na kuchunguza mdhihiriko wa utanzia katika diwani teule na
ulikusudiwa kutimiza malengo matatu mahususi kama ifuatavyo: kubainisha utanzia
katika diwani teule, kufafanua dhima za utanzia uliotumika katika diwani teule na
kufafanua athari za utanzia kwa wasomaji wa diwani teule. Ili kupata data
zilizohitajika, mtafiti alitumia mbinu zifuatazo kukusanya data ambazo ni usaili na
uchaganuzi matini. Data hizo zilichanganuliwa kwa kutumia mbinu ya maelezo na
mkabala wa kitaamuli, ambapo nadhari ya upokezi iliongoza ukusanyaji, uchambuzi
na ufasiri wa data. Hivyo, ili kuwasilisha mjadala wa matokeo ya utafiti, sura
imegawanyika katika sehemu tano. Sehemu ya kwanza imeelezea muhtasari wa
diwani teule za Kichomi na Dhifa. Sehemu ya pili inabainisha matukio ya utanzia
katika diwani teule ambalo ni lengo la kwanza la utafiti. Sehemu ya tatu inafafanua
kuhusu dhima za utanzia katika diwani teule ambalo ni lengo la pili la utafiti.
Sehemu ya nne inafafanua athari za utanzia kwa wasomaji ambalo ni lengo la tatu la
utafiti. Sehemu ya tano inatoa muhtasari wa sura ya nne.
4.2 Utanzia katika Ushairi wa Euphrase Kezilahabi
Sehemu hii inawasilisha mjadala wa matokeo ya utafiti kwa kulichambua lengo letu
la kwanza la utafiti wetu ambalo ni kubainisha matukio ya utanzia yaliyodhihirika
katika diwani teule. Sehemu hii itaundwa na vijisehemu vinne ambavyo ni muhtasari
wa diwani ya Kichomi, muhtasari wa diwani ya Dhifa na matukio ya utanzia katika
diwani teule.
4.2.1 Muhtasari wa Diwani Teule
Sehemu hii inatoa muhtasari wa diwani teule zilizotumika katika utafiti huu. Diwani
hizo ni Kichomi na Dhifa.
4.2.1.1 Muhtasari wa Diwani ya Kichomi
Diwani ya Kichomi imetungwa mnamo mwaka 1974 na kuchapishwa na Heinemann
Educational Books (E.A) L.t.d Nairobi, Kenya. Katika diwani hii kuna jumla ya
32
mashairi arobaini na mbili (42) yaliyo katika sehemu mbili. Mashairi tisa ya mwanzo
yameandikwa kwa lugha ya Kiingereza na baadaye kutafsiriwa kwa lugha ya
Kiswahili, na sehemu ya pili yaliandikwa kwa lugha ya Kiswahili. Katika diwani ya
Kichomi kumejadiliwa mambo mbalimbali yanayoikumba jamii kwa njia ya ushairi.
Kichomi ndio diwani ya kwanza ya mwandishi Euphrase Kezilahabi ambayo imeleta
mapinduzi makubwa katika uga wa ushairi wa Kiswahili kwa kutunga bila kuzingatia
arudhi za vina na mizani. Mashairi katika diwani ya Kichomi si guni kwa kuwa
hayajafuata kanuni za kutunga mashairi za Amri Abedi. Euphrase Kezilahabi
ametunga mashairi yake kwa kufuata mtindo mpya wa kuandika mashairi ya
Kiswahili na kusaidia kukuza fasihi ya Kiswahili kwa kuiletea mtindo mpya wa
kutunga mashairi.
Topan (1973), katika dibaji ya diwani ya Kichomi, anasema:
Muundo alioutumia Kezilahabi haukufungika upande wa mistari: si
lazima kila ubeti wa shairi uwe na idadi maalumu ya mistari;
haikufungika upande wa vina; si lazima mistari yenyewe iwe na vina
haikufungika upande wa mizani: si kila mstari uwe na idadi sawa ya
mizani. Mashairi yale (yaani ya kimapokeo) yaimbwa, haya hayaimbwi
Maudhui yaliyomo katika mashairi ya Euphrase Kezilahabi ni mawazo ya kisasa,
aliyoandika kijana aliyezungukwa na mazingira ya kisasa, kielimu, kijamii na kidini.
Diwani ya Kichomi ilileta mapinduzi katika umbo, miundo na mitindo ya utunzi wa
ushairi kulikuwa na lengo la kupanua uhuru wa kisanaa na kirahisisha uelewa wa
ushairi kutokana na matumizi ya lugha ya kawaida. Mtindo mpya wa utunzi
unaotumia lugha ya watu wa kawaida ulijibu changamoto iliyotokana na
kutoeleweka kwa mashairi ya wanamapokeo ambayo yalitumia lugha ngumu ya
kimafumbo, methali na taswira ambazo hazikuwa rahisi kutafirika.
Diwani hii imeelezea mambo mbalimbali yanayoikabili jamii kwa ujumla. Mfano ni:
matabaka, uongozi mbaya, mgawanyo wa matabaka, ukombozi wa kifikra usaliti,
masuala ya dini, ndoa na mapenzi. Hivyo, kutokana na mawazo na fikra zilizoelezwa
katika diwani hii vimetumika ili kuonyesha mdhihiriko wa utanzia katika diwani ya
Kichomi.
33
4.2.1.2 Muhtasari wa Diwani ya Dhifa
Hii ni diwani ya tatu kutungwa na Euphrase Kezilahabi mnamo mwaka 2005 na
kuchapishwa na Vide-Muwa Publishers Nairobi, Kenya. Diwani ya Dhifa imejikita
katika kuelezea masuala ya kisiasa na ujenzi wa jamii mpya. Katika diwani ya Dhifa
kuna mashairi hamsini na mawili (52) yaliyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili. Dhifa
ina maana ya sherehe rasmi ya chakula iliyoandaliwa kwa watu maalumu, hasa
viongozi. Katika diwani hii mwandishi ameonesha namna viongozi wanavyoweza
kutumia rasilimali za nchi kwa matakwa yao binafsi na kuwasahau wananchi
waliowapa dhamana hiyo. Hali hiyo inawafanya wananchi kuwa katika hali duni ya
kimaisha na kupelekea kukosa huduma muhimu za kijamii kama vile elimu, haki ya
kisheria, huduma za afya na maji. Amefichua uchafu unaofanywa na viongozi
walioaminiwa na wananchi kwa ajili ya kuleta maendeleo. Mwandishi ametumia
sauti ya ukali ili kuibua hisia kwa wasomaji wake katika kutazama maisha ya jamii
kwa ujumla na kukemea uovu unafanywa na viongozi dhidi ya wananchi. Wamitila
(2008), katika utangulizi wa diwani hii, anasema kuwa dhamira zinazojadiliwa katika
diwani “zinawataka wasomaji wake wadadisi, wahoji, wachunguze na kujichokonoa
nafsi zao, mazingira yao, siasa yao, nchi yao, utambulisho wao, ulimwengu wao na
maisha yao wenyewe.”
4.2.2 Utanzia katika Diwani Teule
Kabla ya kuelezea matukio ya utanzia yaliyojitokeza katika diwani teule za Euphrase
Kezilahabi, tunaweza kuyagawa matukio ya utanzia kwa kuzingatia makundi matatu
ya utanzia. Mazongela (khj) anabainisha makundi matatu ya utanzia kama ifuatavyo:
utanzia wa kisaikolojia ambao unahusisha zaidi ufahamu na utendaji wa akili, hapa
tunapata matukio ya kifo na kifungo. Utanzia wa kimwili ni ule unaosababishwa na
magonjwa pamoja na maumivu ya mwili, hapa tunapata matukio kama; hali ngumu
ya maisha, magonjwa na mateso. Utanzia wa kimaumbile unahusisha upungufu wa
viungo katika mwili wa mwanadamu hapa tunapata matukio ya ulemavu wa viungo,
majanga, ukatili na ugumba au utasa. Utafiti umebaini kuwa katika diwani teule kuna
matukio mbalimbali yanayoonesha utanzia. Matukio hayo ni haya yafuatayo:
4.2.3 Hali Ngumu ya Maisha
Said (2016) anabainisha kuwa hali ngumu ya maisha inaweza kusawiriwa sana katika
kazi za kifasihi ijapokuwa uhalisia huo huambatana na ubunifu. Hivyo, tunaona hali
34
ngumu ya maisha ni moja ya tukio la kitanzia. Kwa kawaida, mtu mwenye hali
ngumu ya maisha huandamwa na simanzi na masikitiko ya mara kwa mara. Hii
inatokana na ukweli kwamba mtu huyo hushindwa kuyamudu maisha yake kwa
kushindwa kujikimu kimaisha. Utafiti umebaini tukio hili la huzuni likijitokeza
katika mashairi ya Euphrase Kezilahabi. Mathalani, katika diwani ya Dhifa, kuna
shairi liitwalo “Kwa Walimu Wote” (uk. 1). Katika shairi hili, Euphrase Kezilahabi
ameonesha hali ngumu ya maisha inayomkabili mwalimu katika mazingira yake ya
kazi mpaka atakapostaafu. Kupitia shairi hili, tunaona utanzia ukijitokeza kwa namna
ya mwalimu alivyosawiriwa na kuchimuza utanzia. Mwandishi anasema:
Huu utakuwa wimbo wako
Utakapostaafu urudipo nyumbani
Umelewa kangara na nyayo zako
Zikishindwa kulenga njia nyembamba vijijini
Utakuwa kichekesho cha watoto
Watakaokuita, Ticha! popote upitapo
Kumbuka mwalimu utakapostaafu
Mijusi watataga mayai ndani ya viatu
Vyako vilivyokwisha visigino
Na ndani ya sidiria chakavu
Zilizoshikizwa kamba kwa pini
Mende watazaliana ndani ya chupa tupu
Za marashi na bia.
Mwandishi anaonesha hali ya maisha ya walimu na watumishi wengine wa serikali
yalivyo sasa na hatima yake baaada ya kustaafu. Walimu ambao ndio walezi wa taifa
wanaishi maisha duni na ya kusikitisha. Katika beti hizo tunaona hali ngumu ya
maisha ikisawiriwa kupitia maisha ya mwalimu atakapostaafu. Kwa hakika, shairi
hili linaibua hisia ya huzuni, machungu na masitikito makubwa kwa walimu, kwa
sababu mwalimu amekuwa kama kichekesho kwa jamii baada ya kustaafu. Hii
inatokana na maisha yao kuwa duni huku wakifanya kazi muhimu ya kufuta ujinga
kwa vijana wa taifa lao. Ujira wao ni mdogo ukilinganishwa na kazi kubwa na
muhimu wanayoifanya. Hali hii inaibua masikitiko makubwa anayoyapata mwalimu
kutokana na kupata ujira mdogo hata kushindwa kuweka akiba kwa ajili ya maisha
ya baadaye. Atwood (1982) anashadidia hoja kwa kusema kuwa, usomaji ni
mfanyiko unaombadilisha mtu. Hatuwezi kuwa wale wale tuliokuwa kabla na baada
ya kuisoma kazi fulani ya fasihi. Katika kazi hiyo kuna maarifa anayobakia nayo
35
msomaji ambayo yanaweza kubadili maisha yake kwa kupata funzo juu ya hali
ngumu ya maisha na kupelekea kuondokana na hali ya huzuni, masikitiko, machungu
na hata simanzi zilizomkumba kutokana na utanzia.
Pia, katika diwani ya Kichomi mwandishi anaendelea kuelezea hali ngumu ya maisha
anayoyapitia mwanadamu katika maisha yake ya kila siku. Changamoto za kimaisha
zinazowakabili wanajamii husababisha hali ya huzuni na masikitiko ambayo
huchochea ugomvi au vifo kwa wanajamii. Haya yanadhihirika katika shairi la
“Nimechoka” (uk. 34) mwandishi anasema:
Mikono inaniuma na waya imekwishanikata vidole
Damu imetiririka hadi kwapani kujipanguza siwezi
Nimechoka. Kadiri niendeleavyo kuning’inia, ndivyo
Sura yangu ionyeshavyo vizuri alama za uchovu
Ninatazama huku na huko kuwatafuta wenye huruma
Lakini wanadamu wote wazima wanainamisha vichwa
Chini kama kwamba hawajui hata jamaa zangu!
Ninaendelea kuning’inia kama picha iliyotundikwa
Katika shamba la mawele, na mwenye shamba
Huvuta waya kutoka nyumbani, itingishike kuwatisha ndege
Machozi yananitoka, kuyapangusa siwezi
Ninajitahidi kutoa sauti kwa nguvu
Jamani e! Nisaidie Ng’oeni hivyo vitimbo!
Lakini wanadamu wameinama. Wanaanza sasa kusali.
Katika shairi hili mwandishi anaelezea falsafa ya maisha na kuonesha kuwa maisha
ni adhabu na tanzia anayokumbana nayo mtu, kwani maisha yanaonesha upweke
mkubwa aliona mwanadamu. Hali hiyo ya upweke inampelekea mwanadamu kukata
tamaa ya kuendelea kuishi. Beti hizi zinadhihirisha hali ngumu ya maisha
anayoyapitia mwanadamu kutokana na mfumo wa maisha ya jamii yake. Katika
shairi hili, tunaona maumivu, uchungu na huzuni aliyonayo mtu ambaye yupo katika
hali ngumu ya maisha anayehitaji msaada kwa ndugu na marafiki lakini anaona
hakuna msaada wowote. Kutokana na maumivu anayoyapitia, anaona ni bora
apumzike kwa sababu amechoka kupambana na misukosuko katika maisha.
Changamoto anazozipitia zinamfanya aone kuwa yupo peke yake lakini ni wazi
kuwa changamoto hizo, zinazoikabili jamii kwa ujumla na kuona kuwa zitamalizwa
kwa kumwomba mwenyezi Mungu.
36
4.2.4 Ulemavu wa Viungo
Ali (2015) anasema kuwa, ulemavu ni sehemu ya mwili yenye kuonesha kasoro
fulani katika maumbile ya kiumbe hai. Kutokana na maelezo hayo tunaona kuwa,
ulemavu wa viungo ni hali ya mwanadamu kuwa na dosari katika viungo vyake.
Ulemavu upo wa aina mbalimbali kama vile: ulemavu wa ngozi, ulemavu wa macho
(upofu), ububu, ulemavu wa miguu na ulemavu wa mikono. Aina zote hizi za
ulemavu huibua hali ya majonzi na huzuni kwa wahusika na hata jamii
inayowazunguka kwa jumla. Mwandishi Eupharase Kezilahabi ameionesha hali hii
katika shairi lake liitwalo “Ukucha wa Mbwa” (uk.25) ndani ya diwani ya Kichomi.
Shairi hili la kihadithi linasimulia kuhusu kisa cha mama aliyekuwa kipofu na
matatizo yaliyomkumba. Katika ubeti wa kwanza, mshairi anatudokeza hali ya upofu
wa mama huyo kwa kusema:
Palikuwa na mama mmoja
Mama mjane kipofu na masikini
Aliishi shamba karibu na kilima
Haoni mvua haoni chakula
Akawa masikini wa kijiji
Majirani kumsaidia.
Akitembea fimbo yake
Yenye vijikengele hulia
Umasikini na kuomba msaada
Watoto humkimbilia fimbo
Kuchukua na kumwongoza
Miji mbali mbali kuongea.
Katika shairi hili mwandishi anazungumzia changamoto zinazowapata watu wenye
tatizo la ulemavu kutokana na madhila wanayofanyiwa katika jamii, maradhi pamoja
na umasikini. Nukuu hii inaonesha hali ya mama mwenye upofu inayomfanya
atembee kwa tabu. Alikuwa anatumia fimbo anapotembea (ubeti wa 3). Kutokana na
hali yake ya ulemavu wa macho, mama huyu alijikuta akitendewa maovu kama vile:
kubakwa na kunajisiwa (ubeti 4). Hali hii inamfanya mtu awe katika hali ya
masononeko na masitiko makubwa yanayopelekea kuwa na huzuni. Kutokana na
kushindwa kufanya vitu vyake mwenyewe kwa sababu ya ulemavu ulipelekea kuishi
maisha ya shida yenye machungu na masikitiko yaliyosababishwa na vitendo
alivyofanyiwa na baadhi ya wanajamii.
37
4.2.5 Kifungo
TUKI (1981) wanaeleza kifungo ni adhabu ya mtu kuwekwa mahabusu au rumande
au katika kizuizi. Kifungo pia huleta utanzia kwa wafungwa. Mtu anapofungwa
huwa anakosa uhuru wa kujiamulia na kutenda matendo yake kama ilivyo kawaida.
Kipengele hiki cha kifungo nacho kinajitokeza kama tukio linaloonyesha mbinu ya
utanzia. Maisha ya kufungwa gerezani yanazua huzuni na majonzi kwa mfungwa na
watu waliyokaribu yake. Mwandishi Euphrase Kezilahabi ameonesha hali ya kifungo
katika shairi lake la “Fungueni Mlango” katika diwani ya Kichomi (uk.23).
Mwandishi anasema:
Hewa kuikosa
Na jasho kunitoka ndani ya chumba
Kwa upweke
Ninajiona nimefungiwa
Sioni madirisha lakini
Mlango wa karatasi uko mbele yangu
Ninaugonga kwa mkono
Kichwa na mabega
Mlango unatoa mlio kilio
Lakini mwanadamu hatanifungulia
Damu
Damu puani, damu mdomoni
Damu kichwani itumikayo kama wino
Mikono, kichwa, mabega uchovu
Kwa kichwa kama cha mbuni
Mchangani, tena ninaugonga
Lakini mwanadamu hatanifungulia
Ninaona kizunguzungu
Ninapiga kelele kama
Ng’ombe machinjioni
Fungueni mlango
Mlango fungueni
Lakini mwanadamu hatanifungulia
Katika shairi hili, mwandishi anaelezea hali inayompata mhusika ambaye yupo
katika hali ya kutoeleweka, upweke na kifungo, huku akiomba msaada lakini hakuna
anayemsaidia. Kupitia beti hizi, tunaona jinsi majonzi na masikitiko yakijengwa
kupitia kifungo. Shairi linaelezea kilio cha mtu aliyefungwa na kusababishwa akose
hewa na jasho kumtiririka kwa sababu amewekwa kwenye chumba chenye dirisha
moja dogo linaloingiza hewa kidogo. Mtu huyu ingawa anaomba msaada wa
kufunguliwa mlango ili atoke ndani lakini hakuna anayemsaidia. Tunasoma shairi
hili tunaona hisia za kitanzia zikiibuliwa kutokana na tukio hilo la kifungo. Kwa
38
sababu ya kukosa uhuru anaoutaka mwanadamu kutokana na kifungo kunampelekea
kuwa na masikitiko, majonzi na simanzi kubwa.
4.2.6 Maradhi
Maradhi ni ile hali inayosababisha mtu kuwa katika hali ambayo hushindwa kufanya
kazi au kuishi katika hali asiyoizoea na kupungukiwa nguvu za utendaji wa kazi za
kila siku. TUKI (2013) wanasema maradhi ni kitu kinachosababisha mtu, mmea, au
mnyama kuwa katika afya mbaya. Maradhi hayo yanapelekea mtu au watu kuwa na
hali ya kuingiwa na huzuni kubwa kutokana na kukosa raha na furaha kwa sababu ya
kusumbuliwa na maradhi. Hali hii inapelekea hata ndugu kushindwa kuwahudumia
wagonjwa kutokana na maradhi yanayowasumbua. Hivyo, hufikia hatua kwa
mgonjwa kutengwa na jamii yake na kukosa mtu au watu wa kumfariji. Hapa
inapelekea kuwa na simanzi, huzuni na masitikiko makubwa, kama alivyodhihirisha
na mwandishi Euphrase Kezilahabi katika diwani ya Kichomi katika shairi la
“Ukucha wa Mbwa” (uk. 28-29) mwandishi anasema:
Kidonda kikawa kidonda
Maumivu yakawa maumivu
Siku tatu kupita
Naye kama mbwa akajifia
Wanawake kutaka mali
Uchumi wakamzika
Watoto, wanawake, wapishi
Wote wakachomwa na ukucha
Nao wasiuvumbue
Wakafa wameashama kwa kulia
Mali ya bure kuacha
Wakazikwa shimo moja kama taka
Kupitia shairi hili mwandishi anaelezea hali ya umasikini na maradhi yanayoleta
madhara makubwa katika jamii kama vile kifo. Katika ubeti huu tunaona namna
mwandishi alivyoonesha maradhi yanavyotesa na kumsumbua mtu mpaka kupelekea
kifo chake. Maradhi hayo yanaacha mafarakano makubwa baina ya wale wanaobakia
hasa kutokana na kuondokewa na ndugu yao waliyompenda. Hali ya kusumbuliwa
na magonjwa mbalimbali kunapelekea mtu kuwa katika majonzi, machungu na
wakati mwingine kukata tamaa ya kuishi kutokana na kuchoka kuvumilia maumivu
makali anayoyapitia.
39
Vilevile, katika diwani ya Dhifa mwandishi ameweza kuonesha namna maradhi au
magonjwa yanavyofupisha maisha ya wanajamii. Katika shairi la “Wazo Nje ya
Wakati” (uk. 23) anasema:
Umezoea watoto kuwavizia
Au wazee wanojikongoja
Uonapo mwenye kansa
Wanyatia kummalizia
Na kisha wajitapa
Uonapo watu wanalia.
Wachukia penye dawa
Waambaa penye chakula bora
Wasubiri kosa la dereva
Na magari yagonganapo
Wanong’oneza waloku
Wamekufa!
Hapa mwandishi anatoa mtazamo wake juu ya maradhi yanayowakumba watoto na
wazee ambao wapo kwenye hatari kubwa ya kupoteza maisha yao kutoka na
magonjwa mbalimbali. Ijapokuwa watu wanatumia dawa kupunguza makali ya
maumivu lakini wanakuwa katika huzuni, uchungu na masitiko makubwa kwa
sababu maradhi yanaingia kwa haraka lakini huchukua muda kutoka. Kushindwa
kupata lishe bora kutokana na hali ngumu ya maisha husababisha wagonjwa kukata
tamaa ya kupona. Hivyo, kuwa katika hali ya masikitiko na simanzi zinazopelekea
kukosa matumaini ya kuendelea kuishi mwisho wake huwa ni kifo.
4.2.7 Ukatili
Ni hali ya kuleta hofu, kitisho kwa mtu au mnyama kwa lengo la kumkandamiza kwa
maslahi ya mtu binafsi au kikundi fulani cha watu. UWAKI (2013) wanasema,
ukatili ni matumizi ya nguvu yanayompa mtu fursa ya kumtumia au kumkandamiza
mtu mwingine, ikiwamo kumsababishia kifo, woga au hofu, madhara ya mwili,
kifikra na kisaikolojia. Baadhi ya wafuasi wa nadharia ya upokezi wanaamini kuwa
kazi ya sanaa humwaathiri msomaji, msomaji hurushwa katika ulimwengu mpya na
mgeni na kukengeushwa katika maisha yake. Zaidi ya hayo, msomaji hufinyangwa
upya na akachukuana ipasavyo na matini anayoipitia. Ukatili unaweza kuwa na
madhara makubwa sana katika jamii kwa sababu huweza kumuathiri mtu kiakili,
kimwili hata kihisia kutokana na matendo aliyofanyiwa. Athari ambazo anaweza
kuzipata mtu aliyefanyiwa ukatili ni kama kukosa furaha, kuwa na masikitiko na
40
jitimai. Hali hii ya ukatili inaweza ikapelekea kifo na hata mtu kukata tamaa ya
kuishi kabisa. Vitendo vya ukatili vinaweza kuanzia katika ngazi ya familia hadi
katika jamii kwa ujumla. Ukatili unaweza kudhihirika katika makundi mbalimbali:
ukatili katika mapenzi, mauaji, ubakaji, uhalifu, dhuluma na ukatili wa kijinsia.
Endapo mtu atafanyiwa ukatili anapata madhara ya kudumu kwa sababu anakuwa
ameathirika kisaikolojia, hivyo, kupelekea hata kushindwa kumuamini mtu kutokana
na athari alizozipata baada ya kufanyiwa ukatili.
Katika diwani ya Kichomi, mwandishi Euphrase Kezilahabi amedhihirisha hali ya
ukatili katika mapenzi kama inavyooneshwa katika shairi la “Hutonihadaa” (uk.21)
mwandishi anasema:
Barua ameandika anasema hampendi tena
Naye kitandani anaisoma akicheka
Maringo ya bure nimemuweza mjinga
Jina lake nimeharibu hana la kujivunia
Kesho yake njiani kwa raha anatembea
Mara nyuma chapuchapu hatua anasikia.
Nani huyo anyatiaye nyuma yangu?
Sauti inasema ni mimi
Unafuata nini nami yote nimeona?
Barua umepata na yote umesoma
Sauti inasema lazima nikuage
Nimesema sikupendi tena yote nimeona
Sauti inasema mpenzi njoo tuagane.
Katika shairi hili, mwandishi anaelezea mapenzi yaliyochujuka baina ya watu wawili
waliokuwa wanapendana. Anatunaonesha namna wapenzi wawili waliokuwa na
mahusiano walivyoachana na mmoja wao kubaki na majonzi makubwa baada ya
kufanyiwa ukatili wa kimapenzi. Mapenzi hayo yaliyochujuka yalisababisha
mgogoro mkubwa baina ya wapenzi hao na kupelekea kuachana ijapokuwa mmoja
kati yao hakuridhika na maamuzi hayo. Hali hiyo ilipelekea simanzi, machungu na
majonzi makubwa kwa yule aliyeachwa na kuingiwa na woga wa kuona hatoweza
kuishi mwenyewe. Hapa, mwandishi ameonyesha hali halisi ya namna mtu
alivyofanyiwa ukatili katika mapenzi na kuachwa bila ya kuelewa hatima yake.
Ukatili huwa unaweza kusababisha madhara kama vile kuchanganyikiwa, kukosa
furaha, kukata tamaa ya kupenda tena na kuchukia mahusiano ya kimapenzi hasa
kwa yule aliachwa kutokana na mazoea aliyokuwa nayo katika mahusiano yake.
41
Vilevile, katika shairi la “Hadija” (uk.22) hali hii ya ukatili katika mapenzi
imedhihirika. Mwandishi anasema:
Hadija
Umekata mti mtima
Umeanguka nyumba yako
Uziba mto hasira
Nyumba yako sasa mafurikoni
Na utahama
Watoto kuwakimbia.
Hapa mwandishi anaonesha mwanamke aliyemuua mumewe kwa kumpa sumu ili
apate uhuru. Hii ilitokana na mapenzi aliyokuwa nayo mume kwa mkewe. Baada ya
kufariki mume, mke anapata uhuru ila anaingiwa na simanzi kubwa mpaka anafikia
hatua ya kukata tamaa ya maisha kutokana na ukatili alioufanya. Nukuu hii
inadhihirisha hali ya ukatili alioufanya mwanamke dhidi ya mwanaume bila kujali
kilichotokea. Ukatili alioufanya dhidi ya familia yake umeibua hali ya majonzi,
simanzi na machungu makubwa kwa watoto kukosa watu wa kuwafariji na kukosa
baba, mlezi na hata mshauri katika makuzi yao. Kwa sababu mama sio mfano wa
kuigwa tena kutokana na ukatili alioufanya dhidi ya baba yao.
Katika diwani ya Dhifa mwandishi anaendelea kuonesha ukatili wa kijinsia
wanaofanyiwa baadhi ya watoto wa kike katika jamii. Kwenye shairi la “Hoja”
(uk.59) mwandishi anasema:
Lakini
Ninakumbuka habari nilizosoma
Nikiwa ndani ya daladala
Jana jioni kijana mmoja
Jinale limehifadhiwa
Alimbaka msichana
Wa miaka kumi na sita
Dhuluma ya ubabe huweza kuharibu
Haiba hulka ya utu kwa muda mfupi
Na adhabu, laini
Ni hoja
Ni bado asubuhi.
Katika shairi hili, mwandishi anaelezea falsafa kuhusu maisha. Anadhihirisha ya
kwamba unyanyasaji umekithiri katika jamii. Anaonesha namna watu wasivyojali
hisia za wanyonge. Ubeti huu unaonesha maumivu anayoyapata mtoto wa kike
ambaye amefanyiwa ukatili wa kijinsia ambao unaleta madhara ya kudumu katika
maisha yake. Mawazo ya nadharia ya upokezi yanaumana na mbinu ya utanzia kwa
42
sababu msomaji ufinyangwa na kubadilishwa fikra kutokana na matini anayoipitia.
Hivyo, kubadilika kifkira baada ya kuisoma kazi fulani ya kifasihi. Kutokana na
maumivu, uchungu na misukosuko aliyoipitia anakosa furaha katika maisha yake,
kwa sababu ya kitendo cha kikatili aliyofanyiwa na jamii kushindwa kumsaidia.
Ukatili huo unaweza kumsababishia kukata tamaa ya kuwa na mahusiano, kuathirika
kisaikolojia, kuwa na ukatili kwa wengine na kushindwa kuanziasha familia
kutokana na athari za kitendo alichofanyiwa
4.2.8 Majanga
Mazongela (khj) anafafanua kuwa, majanga ni matukio makubwa yanayoleta hasara
kwa jamii husika. Matukio hayo ni kama vile, mafuriko, tetemeko la ardhi na
vimbunga. Majanga hupelekea jamii kuingiwa na huzuni, hofu na masikitiko
yanayoleta watu kushindwa kupambana na kuleta maendeleo katika jamii. Hivyo,
mwandishi Euphrase Kezilahabi ameweza kuitumia kalamu yake katika kuonesha
hali halisi inayojitokeza katika jamii kutokana na majanga yanayoikabili jamii
husika. Katika diwani ya Dhifa kuna shairi la “Mafuriko Msumbiji 2000”
linalosema:
Nimekuja kugonga
Lango lenu la wakati
Kwa nyundo ya huruma
Amkeni! Enyi Wahenga!
Kwani huko Msumbiji
Mafuriko ya damu
Ya miaka iliyopita
Mafuriko ya mvua ya sasa
Yamekokota wanenu
Na mifupa yenu sasa
Tupu yaelea
Matundu ya macho yakitazama
Ukanda wa fedha upeoni
Mwa maji mengi.
Wanenu waponea
Vikombe vya machozi
Yaliyochotwa kutoka visiwa
Vya uoni wa ndugu wazamao.
Nge wenye mikia isokunjika
Na pembe zizungukazo, waruka
Lakini washindwa kung’ata
Na kuua vyanzo vya umaskini
Sikilizeni mgong’oto wa mshairi
Bubu asemaje na kuomba kwa moyowe.
43
Katika shairi hili mwandishi amedhihirisha namna majanga yanavyoathiri jamii kwa
kiasi kikubwa na kuleta athari ambazo zimedumu kwa kipindi kirefu katika jamii.
Hali hii inarudisha nyuma maendeleo ya jamii kutokana na madhara ya majanga
yaliyotokea. Mawazo ya nadharia yanaumana na mbinu ya utanzia kwa sababu
umchochea msomaji kujitafutia na kujigundulia mengi kwa kufumbua ujumbe
uliomo katika kazi inayosomwa. Majanga kama ya kimbunga, mafuriko na tetemeko
la ardhi yamekuwa tishio kwa ulimwengu mzima kwa sababu yameweza kuacha
watu bila makazi ya kudumu, yamepelekea vifo na kurudisha nyuma maendeleo kwa
ujumla.
Mwandishi Euphrase Kezilahabi anaendelea kudhihirisha kuwa maisha ya
mwanadamu yamegubikwa na majanga ambayo yanaleta madhara makubwa. Katika
diwani ya Kichomi katika shairi la “Mto Nili” (uk.7) mwandishi anasema:
Ninawaona wakimwagilia mashamba yao kwa damu
Ile damu ya watu waliozama zamani ziwani
Kwa sababu ya pepo za Julai
Ziwa, mto, bahari-maisha.
Mwandishi anaelezea madhila yaliyofanywa na ukoloni dhidi ya Afrika na
kusababisha madhara mbalimbali yaliyoacha kumbukumbu kubwa kwa wananchi.
Katika ubeti huo mwandishi anaonesha namna watu walivyopoteza maisha yao
kutokana na pepo zivumazo wakati wa kipupwe mwezi Juni na Julai kila mwaka.
Pepo hizo zilisababisha vyombo vya kusafiria majini kukosa uelekeo na kupelekea
watu kupoteza maisha. Madhara hayo yaliwakumba wanaotumia vyombo vya usafiri
kuvuka ziwani, mtoni na hata baharini. Kutokana na vifo vya watu waliopoteza
maisha yao katika maji imepelekea mwandishi kuona ni wazi maji yamejaa damu za
watu waliofariki kutokana na wingi wao. Kwa mfano, ajali ya meli ya Mv. Bukoba
ilipozama katika ziwa Victoria na kupoteza maisha ya watu wengi. Ajali hiyo
imekuwa ikikumbukwa kila mwaka katika nchi ya Tanzania kwa tarehe iliyotokea.
Hivyo, kufanyika maombolezo ya kuwakumbuka waliopoteza maisha yao kutokana
na ajali. Hali hiyo upelekea uwezekano kwa jamii kupatwa na hali ya utanzia kwa
kuingiwa na huzuni, majonzi pamoja masikitiko kwa sababu ya kuwapoteza
wapendwa wao.
44
4.2.9 Kifo
Mazongela (2016) anafafanua kuwa kifo ni tukio ambalo mtu au mnyama kukosa
uhai, umauti unaosababishwa na mambo mbalimbali. Pia, Ali (2015) anasema kifo ni
tukio la kufa au mwisho wa uhai. Anaendelea kusema kuwa athari za kifo hicho
huwaweka jamaa wa karibu kuwa na jitimai na huzuni kubwa kwa kuondokewa na
yule wanayempenda. Kifo kinaweza kutokea kutokana na maradhi au ghafla bila ya
kujali umri, pesa, madaraka wala uwezo wa watu. Hali ya kumpoteza mtu au watu
tunaowapenda kunapelekea huzuni na simanzi kwa wale wanaobaki na kusababisha
majonzi makubwa. Hivyo basi, tukio la kifo linaonyesha utanzia kwa wanajamii kwa
ujumla kutokana na kumkosa au kuwakosa wapendwa wao waliowapoteza. Matukio
ya vifo yamedhihirika kupitia mashairi mbalimbali ya mwandishi Euphrase
Kezilahabi katika diwani yake ya Kichomi kwenye shairi la “Kumbukumbu 1” (uk.
39). Mwandishi anasema:
Katika ushairi licha ya hekima kumwanga
Ulitafuta kiaminifu ukweli wa maisha
Kwa picha na maneno yenye mizani kilio,
Na ukatuonyesha utamu wa titi la mama.
Vizuu vianja vilivyokuja kwa bu vikifikiri
Sisi waama tusoweza kuelewana kichini
Havikutambua kilichokuwa nguoni mwao.
Kwa hiyo basi Shaaban, nitakuzika kaburi
Moja na Muyaka na juu ya lenu kaburi
Nitaandika “Malenga wa Kiswahili.”
Shairi hili linaelezea harakati za ujenzi wa jamii mpya ambao ulianzishwa na waasisi
wa ushairi wa Kiswahili, Shaaban Robert na Muyaka bin Haji, waliokuwa washairi
wa mwanzo. Mwandishi anatoa rai ya kuyaenzi yale waliyoyafanya kwenye taifa letu
huku akionesha huzuni aliyonayo baada ya kuwapoteza. Ubeti huu umedhihirisha
uwezekano wa hadhira kutokewa au kupatwa na hali ya utanzia kwa sababu ya
kuwapoteza washairi nguli Shaaban Robert na Muyaka bin Haji. Kutokana na
ubunifu wao katika kazi mbalimbali za fasihi kumeweza kusaidia waandishi wengi
kuchipukia kupitia kazi zao. Majonzi na simanzi yaliikumba jamii kutokana na
kuondokewa na waandishi nguli ambao walikuwa na mchango mkubwa katika fasihi
ya Kiswahili.
Pia, katika shairi la “Kumbukumbu 2” (uk.40-41) anaendelea kuelezea jambo hilo la
kifo kwa kumpoteza tena mshairi Mathias Mnyampala. Mwandishi anasema:
45
Na basi nitakupa? Kitu gani wataka kutoka
Kwangu? Machozi yangu hayana gharama:
Yanatoka hata kwa moshi. Inafaa tuonane
Nikuvike taji la ucheshi halafu nikutume
Kwa hiyo basi, nitamtuma maiti anayesema akuite,
Nami, kwa nguvu za uchawi wa kishairi
Nitakufufua ukae juu ya kaburi lako
Tuzungumze macho kwa macho
“Habari gani Mnyampala? Mbukwa! Mimi
Ni K. bin T. Unayafurahishiaje maisha baada ya
Kufa. Wanasemaje malenga wetu. Mwambie Robati
Na kwamba siku hizi Waafrika wenyewe
Wameanza kupalilia bustani yake. Mwambie
Kaluta kwamba ule mzozo sasa unajulikana
Na kwamba watu wengi siku hizi hutunga mashairi.
Katika shairi hili, mwandishi anaelezea harakati za ujenzi wa jamii mpya na kutoa
wasifu wa waandishi nguli walioaga dunia vipindi vya nyuma na kutambua mchango
wao katika fasihi ya Kiswahili. Hapa mwandishi ameonesha huzuni na masononeko
yake makubwa ya kuwapoteza watunzi wakongwe wa kipindi cha nyuma ambao ni
Shaaban Robert, Mathias Mnyampala, Kaluta Amri Abeid pamoja na Muyaka bin
Haji. Hawa walikuwa mashujaa na wenye mchango mkubwa sana katika ushairi wa
Kiswahili. Kutokana na hali ya kuwapoteza waandishi hao, mwandishi ameingiwa na
huzuni, simanzi na masikitiko makubwa yaliyopelekea utanzia katika kipindi kirefu
mpaka kuandika ushairi ili kuwaenzi daima.
Hata katika diwani ya Dhifa suala la kifo limeweza kuonekana kupitia shairi la
“Wazo Nje ya Wakati” (uk.23). Mwandishi anasema:
Wasubiri hitilafu za mitambo
Ndege ziangukapo na kuungua
Keshoye magazetini watangaza
Wavizia walio usingizini
Na wanawake wanaojifungua
Huwezi kujiwindia
Mbu aumapo mtu
Pembeni wazengeazengea
Usikiapo vita moyoni wafurahia
Radi ipigapo nyuma wanguruma
Kujitangazia ushindi
Mieleka hatujaianza.
Ubeti huu unaonyesha namna maisha ya mwanadamu yalivyozungukwa na umauti
na kifo. Hapa mwandishi anaonyesha hofu na mashaka aliyonayo mwanadamu, hasa
46
anapokuwa katika vyombo vya usafiri juu ya usalama wa maisha yake. Kifo
kimekuwa sababu ya kumfanya mwanadamu kukosa furaha kwa sababu hajui siku
wala saa. Hivyo kupelekea kuwa na huzuni, masikitiko, masononeko na simanzi
zinazopelekea utanzia.
4.2.10 Mateso
TUKI (2004) wanafasili mateso kuwa ni mambo yanayompa taabu mtu, uonevu,
madhila. Hivyo, mateso ni ile hali ya mtu kuwa katika maumivu ya mwili au akili
yanayosababishwa na mtu mwingine kwa kukusudia au bila ya kukusudia. Mateso
yanatokana na shida mbalimbali anazoweza kuzipitia mtu katika maisha yake
ambazo zinaweza kumsababishia maumivu ya kudumu. Hivyo basi, mateso
hupelekea mtu kukosa furaha, kuwa katika hali ya masikitiko, majonzi ya mwili au
akili na hata kufikia hatua ya kukata tamaa ya kuendelea kuishi. Katika diwani ya
Kichomi mwandishi Euphrase Kezilahabi amedhihirisha hilo katika shairi lake la
“Kuchambua Mchele” (uk. 63). Anasema:
Tukaanza kutoa chenga, moja moja
Vidole vikafanya kazi kama cherehani
Usiku na mchana macho yakauma
Tufanya kichuguu kidogo cheupe
Chenga na mchanga vikawa vingi sana
Tukapika baada ya muda mrefu wa kazi
Tukaanza kula,
Tukakuta bado mchanga na chenga!
Lini tutaula bila mchanga, bila chenga?
Katika shairi hili mwandishi anazungumzia harakati za ujenzi wa wa jamii mpya ya
Tanzania kipindi cha Azimio la Arusha. Hapa tunaziona juhudi za wananchi katika
kujenga ujamaa na kuondoa unyonyaji. Mwandishi anaonesha mchele kama mfumo
wa ujamaa unaoleta usawa katika jamii kati ya mtu na mtu ila chenga ni vikwazo
vilivyojitokeza katika harakati za kujikomboa zilizowakuta wananchi wa Tanzania.
Vikwazo hivyo vilipelekea hali ya masikitiko iliyowakumba wananchi wa Tanzania
katika kipindi cha Azimio la Arusha. Kutokana na hali ngumu ya maisha, watu
waliokuwa wakipitia ya kula mchele wa chenga wenye mchanga kwa muda mrefu
badala ya kula mchele ambao hauna mchanga. Baada ya kujenga Azimio la Arusha,
walijua kutakuwa na mabadiliko katika maisha yao kutokana na ujamaa lakini
waliendelea kupata mateso yaleyale mpaka waliamua kukata tamaa. Hapa mwandishi
47
amefananisha maisha duni kama chenga za mchele ambazo hazipaswi kuliwa na
mwanadamu.
Pia, katika shairi la “Fungueni Mlango” (uk.23) mwandishi ameelezea hali ya mateso
anayoyapitia mtu au watu katika jamii. Anasema:
Hewa kunikosa
Na jasho kunitoka ndani ya chumba
Kwa upweke
Ninajiona nimefungiwa.
Sioni madirisha lakini
Mlango wa karatasi uko mbele yangu
Ninaugonga kwa mkono
Kichwa na mabega
Mlango unatoa mlio kilio.
Lakini mwanadamu hatanifungulia.
Damu
Damu puani, damu mdomoni.
Katika shairi hili mwandishi anazungumzia mateso anayoyapitia mhusika kutokana
na kifungo kinachomkabili (hali ya kuwa kizuizini). Ubeti huu unaonyesha mhusika
yupo katika hali ya kutoelewa hatima ya maisha yake, upweke na kifungo; anaanza
kupiga kelele za kufunguliwa mlango uliofungwa katika maisha yake. Hali hiyo
inadhihirisha kuwa yuko katika misukosuko, machungu na majonzi ambapo
inaonyesha namna mioyo ya watu inavyotoka damu kutokana na mateso
waliyoyapitia na kukosa uhuru. Kutokana na mateso anayoyapitia mwanadamu kuna
wakati anakosa kabisa tumaini la kuendelea kuishi kwa sababu ya maumivu na
huzuni inayoibua utanzia katika maisha yake.
4.3 Dhima za Matumizi ya Utanzia katika Diwani Teule
Utafiti umebaini kuwa matumizi ya mbinu ya utanzia huwa na dhima mbalimbali.
Dhima hizo ni kama ifuatavyo: kujenga hisia za woga kwa hadhira, kufikisha ujumbe
kwa jamii, kujenga uhalisi wa maisha, kuibusha majonzi kwa hadhira, upekee wa
mtunzi na nyenzo ya kuhuzunisha hadhira. Sehemu hii inazifafanua dhima hizo.
4.3.1 Kujenga Hisia za Woga kwa Hadhira
Utanzia, kama mojawapo ya mbinu ya kibunilizi, imekuwa ikitumiwa na waandishi
wa kazi za fasihi kwa lengo la kujenga hisia za woga kwa wasomaji wao. Hii ni
kutokana na sehemu kubwa ya utanzia kutawaliwa na visa na mikasa yenye kuleta
48
hisia za huzuni. Katika visa au mikasa hiyo, aghalabu huwa na matukio yenye
kuogopesha kama vile ukatili anaofanyiwa mhusika kutokana na mfumo wa maisha
anamoishi, mateso anayoyapitia mhusika na namna anavyojikomboa na majanga
yanayoikumba jamii. Fish (1980) anadai kuwa, msomaji au mhakiki wa kazi ya
sanaa hawezi kutengwa na mawazo ya shairi analolisoma. Hii ni kwa sababu kazi ya
fasihi inaweza kumuathiri msomaji au mhakiki hata akiwemo katika harakati za
kuifafanua na kuifahamu kazi hiyo. Katika kazi ya fasihi maudhui ambayo
mwandishi anayajenga kupitia maandishi yake yanapelekea uwezekano wa hadhira
kupatwa au kuingiwa na hisia za woga. Mfano, tukirejelea shairi la “Mto Nili” (uk.7)
katika diwani ya Kichomi tunaziona hisia hizi za woga zikiibushwa kupitia huzuni
inayopatikana katika shairi. Katika ubeti wa pili, mwandishi anasema:
Ninawaona wakimwagilia mashamba yao kwa damu
Ile damu ya watu waliozama zamani ziwani
Kwa sababu ya pepo za Julai
Ziwa, mto, bahari- maisha.
Maelfu walifanywa watumwa na maelfu
Waliuawa kwa sababu zisijulikana
Halikuwa kosa lenu. Damu yetu
Iliwalewesha mlipotenda hivyo.
Shairi hili linaonesha madhara yaliyoikumba jamii kutokana na majira ya mwaka
pamoja na athari za utumwa katika bara la Afrika. Beti hizi zinasawiri tukio la
kuzama kwa watu katika maji. Hili ni tukio la kitanzia ambalo kwa hali ya kawaida
msomaji anapata kusisimka mwili na akili yake pamoja na kuingia woga kutokana na
mashamba kumwagiliwa kwa damu. Kutokana na kuwa kwa hali ya kawaida sio
rahisi kwa mashamba kumwagiliwa damu badala ya maji. Hali hii inaleta masikitiko
na majonzi zaidi kwa msomaji wa kazi ya fasihi kwa kupata picha halisi ya ziwa
lilojaa maji yenye damu.
4.3.2 Kufikirisha Hadhira
Kwa kiasi kikubwa, mbinu ya utanzia hufikirisha hadhira kutokana na matukio yake.
Matukio yanayoibua utanzia kama vile mateso, majanga, vifo, ugumba au utasa, hali
ngumu ya maisha na ukatili huwa yana kawaida ya kuifikirisha akili. Mtu anawaza
mara kwa mara kutokana na tukio lililomkumbuka ambalo lina utanzia ndani yake.
Mawazo ya nadharia yanaumana na mbinu ya utanzia kwa kuwa wanadharia wa
upokezi wanaamini kuwa, kazi ya fasihi ina mapengo mengi msomaji analazimika
49
kuyajaliza mapengo hayo. Kutokana na kuyajaliza, msomaji hushurutishwa kutunga
matini mpya ambazo zimechochewa kuzalika kutokana na matini asili. Hivyo,
mwandishi wa kazi ya fasihi, kama vile, Euphrase Kezilahabi hutumia mbinu ya
utanzia kuifikirisha hadhira yake. Katika diwani za Kichomi na Dhifa baadhi ya
mashairi yamejenga ukuta imara wa kufikiri kwa wasomaji na kuibuliwa kwa hali ya
jitimai na huzuni. Katika diwani ya Kichomi kuna shairi liitwalo “Kisu Mkononi”
(uk.13) ambalo mwandishi anasema:
Wakati miaka inaibwa mmoja mmoja
Kurudi nyuma, kusimama, kupunguza mwendo
Siwezi, kama gurudumu nitajiviringisha
Mtelemko mkali huu
Lini na wapi mwisho sijui
Mbele chui mweusi, nyuma mwanga
Nionako kwa huzuni vifurushi maelfu ya dhambi
Kisu maisha kafiri haya
Kama kutazama nyuma au mbele
Ni kufa moyo mzima.
Kupitia shairi hili, mwandishi amezungumzia mtazamo wa falsafa ya maisha.
Anaona kuwa, maisha ni adhabu na tanzia anayokumbana nayo mtu mpaka anafikia
hatua ya kujiua. Beti hizo zenye kuibusha hisia za kitanzia zinamtafakarisha
msomaji. Msomaji wa beti hizo anatafakari hatma ya maisha yake na misukosuko
anayokumbana nayo huku akizidi kuwa mnyonge na kutawaliwa na huzuni.
Misukosuko anayoipitia mhusika katika shairi hili kunapelekea msomaji kutafakari
kwa kina namna ya kujikwamua katika hali ngumu anayoipitia mhusika na kufikia
hatua ya kuonesha ni kwa namna gani afanye ili kuepukana na mateso anayoyapitia
mhusika huyo.
Hata katika diwani ya Dhifa mwandishi amemchochea au kuamsha msomaji; hivyo,
anapaswa kufikiria kwa kina ili aweze kubaini ni kitu gani amekusudia kuzungumza.
Katika shairi la “Madomo Mapana” (uk. 7), mwandishi anasema:
Nitafukuzwa mbinguni
Kwa ushairi wangu mbaya
Lakini hata motoni nitaimba
Wanasema
Wanasiasa ni kama jizi
Lililosukumwa mtoto pembeni
Na kunyonya ziwa la mama
Wakati amelala usingizi usiku.
50
Wanasema
Wanasiasa afapo
Tumejikimboa na domo
Moja pana lizibwalo na mchanga
Na kilima cha simenti ngumu
Lisisikike tena hadharani
Wanasema pia
Kusema haki
Kwa kawaida
Wanasiasa hatuwapendi
Kupiga kura ni hasira ya mkizi
Ni basi tu. Ni Ah!
Ah! Wanamalizia
Nchi mmeifilisi waacheni walimu
Wakajenge taifa jipya
Kama hamwezi kuona mbali
Bure kuweka mkono usoni
Bure kukuna kichwa
Kama hamwezi kufikiri.
Kupitia shairi hili, mwandishi anaelezea hali ya kusikitisha ya wanyonge kutokana
na kuwapo kwa viongozi ambao wanajifikiria wao wenyewe bila kujali maslahi ya
wananchi wanaowatawala. Katika ubeti huu mwandishi anaonesha namna wananchi
wanavyoteseka kutokana na madhila mbalimbali ya viongozi wa mfumo wa kibepari.
Mfumo huo ulioibua hisia za masononeko, majonzi na machungu anayoyapata
mwananchi kutokana ukandamizaji unaofanywa na viongozi. Hapa mwandishi
anamfananisha kiongozi kama jizi linalomsukuma mtoto pembeni ili lipate nafsi ya
kunyonya titi la mama na kumuacha mtoto bila maziwa ya mama yake. Mwananchi
anapompigia kura kiongozi anakuwa na matumaini mapya ya kutatuliwa changamoto
anazozipitia katika mfumo wa utawala lakini inakuwa kinyume na matarajio yake.
Mwananchi anaelezea majonzi na masikitiko aliyonayo baada ya kujikomboa kutoka
kwa wakoloni walionyonya nchi yake. Matarajio makubwa aliyokuwa nayo baada ya
uhuru yalikuwa kuijenga nchi na viongozi kutawala kwa usawa. Mwandishi
ametumia ubunifu mkubwa katika kusana ushairi wake na kupelekea msomaji
kufikiri kwa kina ili kuweza kugundua ni kitu gani alikuwa anakusudia kukisema.
4.3.3 Kujenga Uhalisi wa Maisha
Katika maisha ya mwanadamu kuna furaha na huzuni. Hali hizi mbili ni maarufu
kwa kila mtu hapa ulimwenguni. Ulimwengu umeumbwa na dhana ya uwili, yaani
kila kitu kina cha pili yake. Kwa mfano, kuna usiku na mchana, uhai na kifo, uzima
51
na ugonjwa, mke na mume, na mrefu na mfupi. Mwendo huo wa maisha umekuwa
ukijitokeza hata katika kazi za fasihi. Utafiti umebaini kuwa kwa kuwa furaha
mwenzake ni huzuni basi si ajabu upande huu wa pili, yaani huzuni, kujitokeza
katika kazi za fasihi. Hii ni kwa sababu fasihi ni zao la jamii na mwanafasihi
anatokana na jamii (Senkoro, 1987). Mwandishi wa fasihi anapoisana kazi yake na
kuweka vionjo vya kitanzia anakusudia kuujenga uhalisi wa maisha yetu ya kila siku.
Hii ni kwa sabababu hapana mtu mwenye furaha au huzuni daima. Hivyo, kupitia
mashairi ya Euphrase Kezilahabi yaliyomo katika diwani zake teule tunaona kuwa
ametumia utanzia ili kuujenga uhalisi wa mwendo wa maisha ya mwanadamu.
Mwandishi ameweza kuonesha dhahiri suala hilo katika diwani ya Dhifa kupitia
shairi la “Kwa Walimu Wote”. Anasema:
Huu utakuwa wimbo wako
Utakapostaafu urudipo nyumbani
Umelewa kangara na nyayo zako
Zikishindwa kulenga njia nyembmba vijijini
Utakuwa kichekesho cha watoto
Watakaokuita, Ticha! Popote upitapo
Kumbuka mwalimu utakapostaafu
Mijusi watataga mayai ndani ya viatu
Vyako vilivyokwisha visigino
Na ndani ya sidiria chakavu
Zilizoshikizwa kamba kwa pini
Mende watazaliana ndani ya chupa tupu
Za marashi na za bia.
Shairi hili linaelezea hali duni ya watumishi wa umma kutokana na ujira mdogo
wanaoupata na changamoto zinazowakabili baada ya kustaafu. Katika ubeti huu
mwandishi ameonyesha hali ya unyonge, huzuni, masononeko na masikitiko
yanayodhihirisha utanzia. Baada ya kustaafu mtumishi anapaswa kupumzika na
kuishi maisha mazuri ya kustaafu; hata hivyo, imekuwa kinyume kwa watumishi
wengi wa umma. Hii inasababishwa na kushindwa kuweka akiba kwa sababu ya
mshahara mdogo anaopokea akiwa kazini. Ugumu wa maisha baada ya kustaafu
unapelekea baadhi ya walimu kuwa walevi ili kupunguza mawazo na changamoto za
maisha wanayoyapitia. Shairi hili limedhihirisha kuwa watumishi wanatumia muda
wao mwingi katika kufanya kazi lakini baada ya kustaafu wanakuwa katika hali
ngumu kimaisha. Hali hiyo ya kushindwa kuyamudu maisha baada ya kustaafu
52
yanawafanya wawe katika masikitiko, majonzi, machungu hata huzuni kubwa na
kuona kama wamesahaulika.
Hata katika diwani ya Kichomi mwandishi amejenga uhalisia wa maisha aliyoishi
alipokuwa amezaliwa katika kijiji cha Namagondo kwa kuonesha huzuni yake
kutokana na kukosekana kwa mambo yaliyokuwepo hapo zamani. Katika shairi la
“Namagondo” (uk.67), mwandishi anasema:
Nakumbuka Namagondo mahali nilipozaliwa
Ya wapi tena mawele, mawele tuliyopiga
Leo hapa, kesho pale, kesho kutwa kwa jirani?
Viko wapi viazi vitamu vilivyowashinda walaji
Shambani vikajiozea kwa kutokuwa na bei?
Nalilia Namagondo kijiji nilipozaliwa.
Iko wapi tena pamba tuliyovuna kwa wingi
Vyumba vikajaa, watu tukavihama!
Nawakumbuka wanawake wenye nyingi shanga,
Karibu na barabara wakikoga kisimani
Na pembeni, watu wanavuna mpunga
Uko wapi tena mpunga uliokitajirisha watu?
Hapa kwa mzee Mbura, pale kwa mzee Mfunzi
Jiraniye ni Kahunda, pale mzee Magoma
Karibu yake, mzee Nabange, pale mzee Lugina
Sasa wote wamekwenda waliokiongoza kijiji
Miji mingine imevunjika, watoto wajihamia
Wameanza kufarakana kwa kujijengea miji.
Kupitia shairi hili, mwandishi anazungumzia mabadiliko ya mazingira na maisha.
Hali hii inatokana na uharibifu mkubwa uliofanywa wa mazingira uliopelekea
kupungua kwa shughuli za uzalishaji mali kama vile kilimo, uvuvi na biashara.
Katika beti hizo mwandishi ameonyesha hali halisi ya maisha waliyokuwa wanaishi
watu wa Namagondo ambayo kwa sasa hayapo tena. Anaelezea masikitiko, majonzi
na simanzi aliyonayo baada ya kuona vitenga uchumi kama vile kilimo, ufugaji na
uvuvi vilivyokuwa vinawapatia wananchi riziki ya kila siku havipo tena hii ni
kutokana na mifumo mipya ya maisha.
Mawazo ya nadharia ya upokezi yanaumana na mbinu ya utanzia iliyodhihirika
katika diwani teule. Hali hii imetokana na kuwa nadharia hii inahusisha historia na
ujumi au umbuji unaohusiana kwa kiasi kikubwa na dhana ya mkondo wa matarajio,
kwani msomaji huwa na matarajio fulani anapoisoma kazi fulani. Matarajio ya
53
mhusika katika shairi la “Namagondo” yalikuwa kuona kijiji chake kinapiga hatua za
mbele zaidi na sio kurudi nyuma kimaendeleo. Mwandishi anasononeka
anapowakosa wazee wake kama vile: Mbura, Mfunzi, Magoma, Nabange na Lugina.
Wazee hao walikuwa msaada mkubwa kwa vijana, hasa katika ushauri mbalimbali,
kwa sasa hawapo tena. Hivyo, ni huzuni kubwa kwa waliobaki kwa sababu
wanazikosa hekima na busara zao. Anaonyesha kuwa, kilichokuwepo hapo mwanzo,
kama vile kilimo na uvuvi walivyokuwa wanavitegemea katika kujipatia kipato
havipo tena; bali yamebaki makaburi ya wazee wao tu.
4.3.4 Kuibua Majonzi kwa Hadhira
Utanzia unapotumiwa katika kazi ya fasihi huwa na lengo la kuibua majonzi kwa
wasomaji. Utafiti umebaini kuwa mashairi mengi ya Euphrase Kezilahabi
yaliyotumia mbinu hii ya utanzia yanaibua hisia za majonzi na huzuni kwa wasomaji.
Wafuasi wa nadharia ya upokezi wanaamini kuwa maana ya kazi yoyote ya kifasihi
humtegemea kwa kiasi kikubwa msomaji wa kazi hiyo. Jambo hili linamfanya
msomaji kusawiriwa kama mwenye mchango mkubwa katika kuijaza na kuibua
maana ya kazi inayohusika. Hali hiyo imeweza kudhihirika zaidi katika matukio
yaliyojitokeza katika diwani teule kama vile, ukatili katika mapenzi, ukatili wa
kijinsia, mateso, hali ngumu ya maisha na vifo. Mfano mzuri tunaweza kuuona
katika shairi la “Kwa Walimu Wote” (uk.2) katika diwani ya Dhifa. Shairi hili
limetumia lugha ya moja kwa moja katika kueleza hali halisi ya maisha ya mwalimu.
Limewakumbusha walimu pindi watakapostaafu na namna watakavyokabiliwa na
changamoto za kimaisha kutokana na kutokuwa na uwezo wa kujikimu. Mwandishi
ameibua majonzi na masikitiko kwa walimu kupitia shairi hili na kuwafanya walimu
wawaze maisha yao ya baadaye yatakuwaje. Anasema:
Tazama hilo rundo la madaftari mezani
Utalimaliza kwa mshahara mkia wa mbuzi?
Tuzungumze. Ninyi na mimi
Acha mioyo yenu izungumze
Mkiwa waoga na kujikunja kama jongoo
Mtawekwa kwenye vijiti na kutupwa
Nje ya ua, na ndani mtawaacha
Wacheza ngoma wakitunga nyimbo mpya.
Sikilizeni kwa makini
Umoja hatuna
Twasambaratika kama nyumbu
Tulichonacho ni woga
54
Na kinachotuangusha ni unafiki
Lakini tusikate tamaa kama mbuni
Tukiupata umoja bado tunayo silaha
Kura.
Hapa, mwandishi ameonesha dhahiri hali duni ya maisha na mazingira magumu ya
kufanyia kazi wanayoipitia walimu kutokana na unyonge pamoja na uoga wao katika
kutekeleza majukumu yao ya kila siku. Mateso, misukosuko, machungu na tabu
wanazopitia za kupata ujira mdogo kwa kufanya kazi ngumu ya kuelimisha jamii
huishia kuishi maisha ya tabu na dhiki. Halikadhalika, baaada ya kustaafu wanaishia
kuwa na maisha duni kwa kuwa wamekata tamaa na wamekosa mtetezi wa
kuwatetea ili kupata haki zao za msingi. Hali ya kukosa umoja na mshikamano ndio
imekuwa chanzo kikubwa cha kushindwa kujikwamua katika changamoto
zinazowakabili.
4.3.5 Kujenga Upekee wa mtunzi
Utumikaji wa mbinu ya utanzia umeweza kuonyesha namna mwandishi anavyoweza
kuwa na mtindo wa kipekee katika kazi yake tofauti na ya mwandishi mwingine.
Upekee huo umeonekana pindi mwandishi anapoelezea jambo lilelile katika namna
tofauti na mwandishi mwingine. Topan (1973) anasema kuwa, mwandishi Euphrase
Kezilahabi hutumia hisi za ndani kueleza maisha na fikra zilizomjaa kichwani kwa
mtungo mpya. Katika kazi za ushairi, hutumia mpangilio wa maneno katika tungo
unaoambatana na mtiririko wa mawazo toka mwanzo hadi mwisho. Hudhihirisha
upekee mkubwa, kutokana na matumizi ya lugha ya picha, mafumbo kejeli na
dhihaka katika tungo zake kwa namna anavyolielezea jambo.
Mwandishi Euphrase Kezilahabi ametumia mbinu ya utanzia katika kazi zake za
ushairi kwa namna ya kuleta taharuki kwa msomaji na kufanya kazi yake kuwa na
upekee, tofauti na waandishi wengine. Mawazo ya nadharia ya upokezi yanaumana
na mbinu ya utanzia kwa sababu humchochea msomaji kujitafutia na kujigundulia
mengi kwa kufumbua ujumbe uliomo katika kazi inayosomwa. Hii ni kutokana
ufundi stadi wa mwandishi katika kutunga kazi yake ya kifasihi. Katika diwani zake
za Kichomi na Dhifa mwandishi ameelezea masuala mbalimbali yanayoonyesha
utanzia na kuleta simanzi, masitikito na kuhuzunisha hadhira yake. Masuala hayo
yameonyesha matukio ya kitanzia kama vile, ukatili, ajali, ugumba au utasa, majanga
au mabaa, magonjwa na vifo vinavyoikumba jamii na kuibua utanzia miongoni mwa
55
wanajamii. Katika diwani ya Kichomi shairi la “Nimechoka” (uk.34) mwandishi
anasema:
Kati ya vitimbo, vichwa vinazuka ardhini
Ukweli wa masiha unakuwa kama ndoto ya uwongo
Kichwa kimoja kinasema kwa sauti “Mnaliona Hilo!”
Halafu vichwa vyote vyeupe vinacheka. Ninashangaa
Ninashangaa zaidi kusikia sauti ya baba
Ikicheka miongoni mwa vichwa hivyo vyeupe
Siyaamini macho, siyaamini masikio, sikiamini kichwa.
Wanadamu wameinama. Wanasali kwa haraka sasa
Utafikiri wanahesabu mchanga utakaojaza kaburi langu
Vichwa vyeupe vinacheka. Kingine kinasema tena
“Mnaliona Hilo! Joga! Vichwa vinacheka. Wanasali
“Nyinyi nyote hamna akili! Mnaniudhi!
Hamwoni hali yangu! Napiga kelele. Lakini vichwa
Havitishiki, na wanadamu hawatingishiki.
Katika beti hizo tunaona mwandishi ametumia ufundi wa hali ya juu katika kuelezea
falsafa ya maisha inayomkabili mwanadamu na namna anavyoweza kujikwamua.
Shairi hili lina taswira ambazo hujenga falsafa ya mwandishi kuhusu maisha tangu
mwanzo tumwonapo akiwa kafungwa na waya mgumu wa maisha usio na mwanzo
wala mwisho. Vilevile, akining’inia kama ndege aliyenaswa na mtego wa mtoto
mdogo. Picha ya ndege aliyenaswa inadhihirisha wazi falsafa ya maisha yaliyo na
woga na mashaka ambayo chanzo wala mwishowe haujulikani. Mambo yanakuwa
mabaya zaidi, wakati tumwonapo mshairi akishindwa kudondoka kutoka kwenye
waya ngumu kwani chini yake ipo miti iliyochongoka iliyo tayari kumchoma kama
mshikaki. Hali hii inamfanya aamue kuendelea kushikilia waya angali anapata
maumivu makali huku mwili umetapakaa damu na jasho. Hali ngumu ya maisha
imemfanya mtu kuchoka kabisa na kumrudia Mungu ili aweze kumsadia katika
matatizo yake maana wanadamu wenzake hawana msaada tena kwake. Hali hiyo
inapelekea uwezekano wa hadhira kupatwa na hali ya utanzia na kusababisha
masikitiko, machungu na majonzi makubwa.
Vilevile, katika kuonesha upekee katika kazi ya fasihi, mwandishi ametumia ufundi
wa kisanaa kwa kusana kazi ya ushairi. Euphrase Kezilahabi ameonesha umahiri
mkubwa katika kutumia mafumbo, lugha ya picha pamoja na sitiari katika diwani ya
Kichomi kwenye shairi la “Kisu Mkononi” (uk. 13) kwa kuelezea falsafa ya maisha
na kufafanua changamoto zinazomkabili mwanadamu mwandishi anasema:
56
Mbele chui mweusi, nyuma mwanga
Nionako kwa huzuni vifurushi maelfu vya dhambi
Kisu, maisha kafiri haya
Kama kutazama nyuma au mbele
Ni kufa moyo mzima!
Kupitia shairi hili, mwandishi anafafanua falsafa ya maisha ya mwanadamu pamoja
na changamoto zinazomkabili. Mambo aliyoyaona na kumpata maishani na fikira
zilizomjia kichwani zaelezwa katika shairi hili. Hisi za nadani zimeelezwa katika
mtungo mpya. Mpangilio wa maneno katika tungo unaambatana na kufautana na
mtiririko wa mawazo ya mshairi toka mwanzo hadi mwisho. Nukuu hii inaonesha
namna mwandishi alivyoitumia mbinu ya utanzia katika kuelezea maisha ya
mwanadamu pamoja na changamoto anazozipitia zinazopelekea kutaka kuondoa uhai
wake. Mwandishi anaelezea hisi na mawazo yake hatua kwa hatua kwa kuyaonesha
mawazo ya unyonge ya mwanadamu kwa kutokujua la kufanya wakati maisha
yanamtatiza na kuishia kukata shauri la kujiua na kukumbwa na huzuni, majonzi,
msawajiko na masikitiko makubwa kutokana na kukata tamaa ya kuishi.
4.3.6 Nyenzo ya Kuhuzunisha Hadhira
Utanzia, kama mbinu ya kibunilizi, umetumika katika kazi za mwandishi Euphrase
Kezilahabi ili kuleta taharuki ya majonzi kwa wasomaji wake. Ali (khj) anaeleza
kuwa utumiaji wa mbinu bunilizi ni sehemu mojawapo ya kuteka hisia za wasomaji.
Anaongeza kusema kuwa, kupitia hali ya majonzi, masikitiko na kuwafanya wawe na
huzuni hali hii huchimbuka kutokana na ustadi wa kuyajenga matukio ya utanzia
katika kazi ya fasihi. Nadharia ya upokezi huhusishwa na jinsi kazi au matini fulani
zianavyopokelewa na jamii moja katika vipindi tofauti. Matumizi ya mbinu hii
hamasa yanatoa ya kuelewa baadhi ya mambo mbalimbali yaliyotokea katika jamii
ya Kitanzania, hususani katika fasihi ya Kiswahili. Kuna matukio mbalimbali ya
kuhuzunisha yaliyotokea katika jamii yetu kama vile vifo, njaa, ajali, ulemavu wa
viungo, ukatili, mafuriko na maradhi ambayo imelifanya taifa lipate pengo kubwa
sana lisilozibika. Katika diwani ya Kichomi kuna shairi la “Kumbukumbu 1” na
“Kumbukumbu 2” ambapo mwandishi ameeleza huzuni aliyonayo pindi
alipowapoteza washairi nguli wa fasihi ya Kiswahili ambao waliweka misingi imara
katika uandishi wa kazi za fasihi. Mwandishi anasema:
Nini basi nitakupa? Kitu gani wataka kutoka
Kwangu? Machozi yangu hayana gharama
57
Yanatoka hata kwa moshi. Inafaa tuonane
Nikuvike taji la ucheshi halafu ikutume
Kwa hiyo basi, nitamtuma maiti anayesema akuite
Nami, kwa nguvu za uchawi wa kishairi
Nitakufufua ukae juu ya kaburi lako
Tuzungumze macho kwa macho
Habari gani Mnyampala? Mbukwa! Mimi
Ni K. bin T. Unayafurahiaje maisha baada ya
Kufa. Wanasemaje malenga wetu. Mwambie Robati
Kwamba yule mzungu amefanya kazi nzuri
Na kwamba siku hizi Waafrika wenyewe
Wameanza kupalilia bustani yake. Mwambie
Kaluta kwamba ule mzozo sasa unajulikana
Na kwamba watu wengi siku hizi hutunga mashairi.
Kupitia shairi hili, mwandishi anaelezea mambo mbalimbali yaliyofanywa na
mashujaa katika kazi za kifasihi. Nukuu hii inaonyesha simanzi, machungu na
masikitiko makubwa aliyonayo mwandishi katika kuelezea hisia zake baada ya
kuondokewa na waandishi wenzie. Mwandishi ametumia kalamu yake katika
kuwakumbuka watunzi mashuhuri waliofanya kazi kubwa katika fasihi ya Kiswahili
na sasa hawapo tena. Kutokana na majonzi aliyokuwa nayo, mtunzi angetamani
kupata nafasi nyingine ya kuwaeleza marehemu Shaaban Robert pamoja na Mathias
Mnyampala kile alichokuwa anafikiria. Hivyo, anaishia kutoa hisia zake kwa
kuandika mashairi kwa ajili ya kuwaenzi na kuonyesha umuhimu wao pamoja na
mawazo yao kuwa bado yanahitajika katika fasihi ya Kiswahili.
4.4 Athari za Matumizi ya Mbinu ya Utanzia
Utafiti umebaini kuwa matumizi ya utanzia katika mashairi ya Euphrase Kezilahabi
yana athari chanya na hasi kama ifuatavyo:
4.4.1 Athari Chanya za Matumizi ya Utanzia katika Diwani Teule
Utafiti umebaini athari chanya zifuatazo za utanzia: nyenzo ya kufikisha ujumbe kwa
hadhira, huakisi uhalisi wa maisha, humweka karibu mwandishi na msomaji,
kuitafakarisha hadhira na kumpambanua mtunzi.
4.4.1.1 Nyenzo ya Kufikisha Ujumbe kwa Hadhira
Utanzia ikiwa ni mbinu ya kibunilizi kama mbinu zingine za kisanaa hutumika
kufikisha ujumbe kwa hadhira. Mtunzi wa kazi ya fasihinapoyajenga maudhui yake
ya kitanzia huwa na kusudi la kufikisha ujumbe. Hii ni kwa sababu utanzia
58
umetumika kama suala la kiujumi ili kurahisisha uelewekaji wa ujumbe kwa jamii.
Langer (1977) anasema kuwa ujumi ni uzuri wa kisanaa au hali ya kutumia ufundi
stadi kwa lengo la kuwavutia wasomaji. Hivyo, mtunzi huweza kutumia mbinu hii
katika kuasa au kuonya jamii. Katika kuthibitisha hilo Mahenge (2020)2 anasema:
Mtunzi Euphrase Kezilahabi ametumia mbinu ya utanzia katika kazi
zake za Dhifa na Kichomi kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa
hadhira aliyoikusudia. Kupitia dhamira na migogoro iliyoibuka
katika mashairi yake kumeweza kuleta huzuni na masikitiko kwa
hadhira yake. Lakini lengo la mbinu hizo zilizotumika katika kazi ya
fasihi ni kufika ujumbe uliokusudiwa kwa hadhira.
Maelezo yaliyotolewa yanathibitisha kuwa pamoja na mbinu mbalimbali
zinazotumika katika kusana kazi za kifasihi, mtunzi huwa na lengo kuu la kufikisha
ujumbe kwa jamii husika. Fish (1980) anadai kuwa msomaji anapaswa kusoma kwa
kina kirefu ili kuweza kupata ujumbe ambao mtunzi amekusudia kwa hadhira yake.
Hii ni kwa sababu kusoma kwake kwa kina kunaweza kumfanya agundue maudhui
ya matini hiyo. Katika mashairi ya “Madomo Mapana” na “Ukucha wa Mbwa”,
mwandishi ametoa ujumbe kwa hadhira yake ijapokuwa humuhitaji msomaji kusoma
kwa kina ili kuwaweza kugundua ujumbe aliokusudia mwandishi.
4.4.1.2 Huakisi Uhalisi wa Maisha
Suala la binadamu kukumbwa na huzuni ni la kawaida katika maisha. Mtunzi
anapotumia mbinu ya utanzia huwa na azma ya kuiakisi hali halisi ya maisha. Watu
hufurahi na kuingiwa na majonzi kutokana na mambo tofauti tofauti. Hadhira huiona
mbinu ya utanzia kama nyenzo muhimu ya kuwathibitishia kuwa matatizo na
misukosuko ndio hali ya maisha. Hivyo, kuiandaa jamii kukabiliana nayo. Kama
asemavyo Msigala (2020)3:
Udhihirikaji wa uhalisi wa maisha uliopo katika mbinu ya utanzia
umejitokeza katika kazi za fasihi kupitia wahusika. Kutokana na
matukio ya huzuni, kilio, majonzi na masikitiko yanayoweza
kusababishwa na vifo, vita, ajali, ugumba, ulemavu na majanga
anayoyapitia mhusika, ndivyo vitu vinavyoweza kubeba dhamira
zinazoakisi maisha ya jamii kwa ujumla.
2 Maelezo haya ni ya Dkt. Elizabeth Mahenge, mahojiano haya yalifanyika ofisini kwake tarehe
11/06/2020. Dkt. Mahenge ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu Dar es Salaam. 3 Maelezo haya ni ya Bwana Selestin Msigala, mahojiano haya yalifanyika ofisini kwake 9/06/2020.
Bw. Msigala ni Mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
59
Maelezo hayo yanadhibitisha kuwa, mtunzi anapotumia mbinu bunilizi kama utanzia
katika kazi ya fasihi ni wazi kuwa kile anachokiandika kinaakisi jamii fulani. Hivyo,
wafuasi wa nadharia ya upokezi wanaona kwamba kazi ya fasihi ikiakisi uhalisi
huifanya kazi hiyo kuwa na uwazi mkubwa ambao utawezesha kutolewa maana
tofauti tofauti za matini ya kifasihi. Kama inavyodhihirika katika diwani ya Kichomi
kupitia shairi la “Namagondo” (uk. 67) ambapo mwandishi anaelezea huzuni, kilio
na masikitiko aliyonayo mhusika kutokana na mabadiliko yalipo katika kijiji cha
Namagondo. Namagondo ndiyo sehemu ambayo amezaliwa, amekulia na kuishi kwa
muda imebadilika tofauti na awali, hali hiyo ya mabadiliko imemfanya kuona uhalisi
wa eneo hilo haupo tena. Hii imetoka na uharibifu wa mazingira ambao umeleta
mfumo mpya wa maisha na kuondoa uoto wa asili uliokuwepo. Vilevile, katika
diwani ya Dhifa kupitia shairi la “Jibwa” (uk.5) anaakisi maisha halisi ya
ukandamizaji na unyonyaji kwa tabaka la chini. Kutokana mfumo mbaya wa utawala
kumechangia kutokea kwa matabaka mawili katika jamii (walionacho na
wasionacho). Hivyo kupelekea tabaka la chini kuona tabaka la juu kama jibwa lenye
tamaa ya fisi.
4.4.1.3 Humweka Karibu Mwandishi na Msomaji
Mbinu ya utanzia humweka karibu msomaji na mwandishi wa kazi husika. Hii ni
kutokana na uwazi kwamba, masuala yanayojenga utanzia ambayo yanajadiliwa
katika kazi husika huwa ni mambo ya kiulimwengu. Mambo haya kwa namna moja
au nyingine yanahitaji huruma ya watu. Watu husikitika na kusononeka kutokana na
matukio kama ajali, ugumba, majanga, mateso na hata maradhi. Mwandishi
anaposana mambo haya katika kazi yake hujikuta akiiweka karibu hadhira yake, hii
ni kutokana na msomaji kuingiwa na huruma, majonzi na humsikitikia mwandishi au
wahusika waliokumbwa na mikasa yenye utanzia. Kufanya hivyo, husaidia katika
kumfanya msomaji awe karibu naye kila hatua. Kyamba (2020)4 anathibitisha kwa
kusema:
Fasihi ya Kiswahili si ombwe bali inatoka katika jamii. Mwandishi
wa kazi za kifasihi anatunga kazi yake kutokana na yale
yanayoikumba jamii fulani kiuchumi, kisiasa na hata kiutamaduni.
Hivyo, yale anayoandika mtunzi yanatokea katika maisha ya kila
siku na kumfanya kuwa karibu sana na uhalisi uliopo kwenye jamii.
4 Maelezo haya ni ya Dkt. Anna Kyamba, mahojiano haya yalifanyika ofisini kwake tarehe
11/06/2020. Dkt. Kyamba ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
60
Maelezo hayo yanaonyesha namna mtunzi wa kazi za kifasihi anavyoweza kutumia
kalamu yake kuandika kile ambacho kinaikumba jamii na kumfanya kuwa karibu
zaidi na hadhira. Baadhi ya wafuasi wa nadharia ya upokezi wanaamini kuwa, maana
ya kazi yoyote ya kifasihi inamtegemea kwa kiasi kikubwa msomaji wa kazi hiyo.
Jambo hili linamfanya msomaji kusawiriwa kama mwenye mchango mkubwa katika
kuijaza na kuibuni maana ya kazi inayohusika. Hali unamfanya msomaji wa kazi ya
fasihi kuwa karibu zaidi na mwandishi kimawazo kutokana na kuingiwa na huzuni,
machungu hata kupata msawajiko kutokana na kile anachokipitia mhusika katika
kazi hiyo.
Katika diwani ya Kichomi na Dhifa kuna baadhi ya mashairi yanayoonyesha ukaribu
uliopo baina ya mwandishi na hadhira yake. Hii ni kutokana na kuwa masuala
anayoyazungumzia yameweza kuleta chachu kwa wasomaji kufananisha na uhalisi
uliopo katika jamii. Kwa mfano, katika diwani ya Dhifa kwenye shairi la “Kwa
Walimu Wote” (uk. 1) limedhihirisha wazi hali anayoipitia mwalimu baada ya
kustaafu. Mwandishi ametumia ubunifu katika kuelezea jambo hilo ambalo
linawakabili watumishi wengi baada ya kustaafu na kuleta hamasa katika kujiandaa
kabla ya kustaafu.
4.4.1.4 Kuitafakarisha Hadhira
Kwa kawaida utanzia humtafakarisha msomaji. Hii ni kutokana na matukio
yanayosababisha utanzia huwa yanaambatana na ufikiriaji wa hali ya juu. Hadhira ya
kazi ya fasihi huzama katika kufikiri kutokana na matendo yanayozua utanzia.
Katika utafakarishaji huo hadhira huweza kujiepusha au kuchukua tahadhari
kutokana na mambo yanayoleta utanzia kama vile ajali, majanga, kifo, kilio, mateso
n.k. Kimsingi, mbinu hii ni nyenzo muhimu ya kukuza uwezo wa kufikiri kwa
wasomaji wa diwani teule. Suala hili linatokana na ukweli kuwa kufikiri ndio afya ya
akili. Na watu hufikiri kutokana na matendo yanayowakumba katika maisha ya kila
siku. Hivyo, hata utanzia uliomo katika diwani teule hufikirisha hadhira. Thomas
(2020)5 anathibitisha hoja hiyo ya kuifanya hadhira kutafakari anasema:
Mtunzi huwa hatungi kazi ya fasihi kwa kupanga kile anachotunga,
ila msomaji au mhakiki ndio anaweza kupambanua kutokana na
mtazamo wake kulingana na kazi husika. Mwandishi anaweza akawa
5 Maelezo haya ni ya Dkt. Ramadhani Thomas, mahojiano haya yalifanyika ofisini kwake tarehe
9/06/2020. Dkt. Thomas ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
61
amemuathiri msomaji kiuchumi, kimwili hata kisaikolojia bila ya
mtunzi kufahamu hilo. Huenda mtunzi na msomaji au mhakiki wa
kazi ya kifasihi wanaweza kutofautiana kutokana na tafakari ya
msomaji.
Maelezo yaliyotolewa yanadhibitisha kuwa msomaji wa kazi za fasihi ana nafasi
kubwa katika kutafakari na kufafanua kazi ya mtunzi. Iser (1974) na Fish (1980)
wanadai kwamba kazi ya fasihi mara kwa mara ina mapengo mengi. Msomaji au
mhakiki anapaswa kuyaziba mapengo hayo. Kutokana na kuitafakari kazi ya fasihi
msomaji hulazimika kutunga matini mpya ambazo inatokana na matini aliyoipitia
(matini ya asili). Hivyo, msomaji wa kazi ya kifasihi ana jukumu kubwa la kufahamu
kwa kina kazi ya kifasihi. Kila msomaji au mhakiki wa kazi za Euphrase Kezilahabi
anaweza kuchambua kazi hiyo kwa namna alivyoelewa na mtazamo uliomwongoza.
Kama inavyoonekana katika shairi la “Mgomba” (uk. 8) anasema:
Hivyo ndivyo ufalme wa mitara ulivyo
Mti wa mji umelala chini hauna faida tena
Baada ya kukatwa na wafanya kazi
Wa bustani kwa kusita
Chumbani hakuna kitu
Isipokuwa upepo fulani wenye huzuni utingishao
Wenye hila waliokizunguka kitanda na kulia
Machozi yenye matumini yapiga
Mbiu ya hatari ya magomvi nyumbani.
Katika shairi mwandishi anaelezea harakati za ujenzi wa jamii mpya na fikira mpya
juu ya maisha na kuachana na zama za kizamani. Kupitia ubeti huu tunaona
mwandishi anaibua hisia za huzuni, masikitiko na mateso anayoyapata msomaji.
Tunaambiwa kuwa, kuna sauti ya kilio baada ya mhusika kushindwa kutimiza haja
zake za kimwili katika ndoa kwa wake zake, kama anavyosema “hivyo ndivyo
ufalme wa mitara ulivyo”. Hali inaonyesha majuto na masikitiko makubwa aliyonayo
mhusika baada ya kukosa nguvu za kushiriki tendo la ndoa kutokana na umri
mkubwa. Hivyo msomaji wa shairi hili anaweza kutafakari na kuweza kubaini maana
kulingana na uelewa wake binafsi pamoja na mtazamo uliomwongoza.
4.4.1.5 Kumpambanua Mtunzi
Utanzia pia huweza kumpambanua mtunzi kwa kuweza kumtofautisha na waandishi
wengine. Mbinu hii ya kiutunzi huwa ni kipambanuzi kizuri cha mtunzi. Mathalani,
wapo watunzi wamejiegemeza katika maandishi yao kutunga kutokana na hisia
62
walizonazo na mitazamo yao ambayo huwatofautisha na wengine. Senkoro (1982)
anashadidia hoja hii kwa kusema kuwa mtindo ni upangaji wa fani na maudhui
katika kazi ya fasihi kwa njia ambayo hutokeza nafsi na labda upekee wa mtungaji
wa kazi hiyo. Anaendelea kusema kwamba mtindo hubainishwa kwa vipengele vitatu
ambavyo ni mbinu bunilizi, uteuzi wa maneno na uhusika na wahusika. Fuluge
(2020)6 anafafanua suala la kujipambanua kwa mtunzi kwa kusema kuwa Euphrase
Kezilahabi ametunga kazi zake za ushairi kwa kuteua matukio ya kitanzia kwa
namna ya kipekee tofauti na watunzi wengine. Kutokana na ufundi stadi wake wa
kazi za kifasihi zimedhihirisha msimamo wake kuhusu falasafa ya maisha. Hivyo
msomaji anaweza kumtambua mwandishi kutokana na uelekeo fulani hasa katika
matumizi ya mbinu bunilizi kama utanzia katika kazi husika. Kwa mfano, mwandishi
Euphrase Kezilahabi ameweza kujipambanua kutokana na mtindo wake wa uandishi
wake wa kazi zake zinazoonyesha anguko la mhusika mkuu. Katika kuthibitisha hilo
Topan (1973) katika dibaji aliyoandika kwenye diwani ya Kichomi anaelezea kuwa:
Kezilahabi alifuata mtindo mpya wa kuandika mashairi ya
Kiswahili, na kuleta mtindo mpya wa kutunga mashairi. Shairi la
kwanza lililotumia mtindo huo ni “Kisu Mkononi” (uk.14). Shairi
hili halina vina vya nje na kati, mistari haina mizani zilizopangwa
sare katika kila mstari, wala ubeti hauna mistari sare. Mwandishi
anasema:
Wakati miaka inaibwa mmoja mmoja
Kurudi nyuma, kusimama, kupunguza mwendo
Siwezi, kama gurudumu nitajiviringisha
Mtelemko mkali huu
Lini na wapi mwisho sijui.
Mbele chui mweusi, nyuma mwanga
Nionako kwa huzuni vifurushi maelfu vya dhambi
Kisu maisha kafiri haya
Kama kutazama nyuma au mbele
Ni kufa moyo mzima!
Maelezo yaliyotolewa na Topan yanadhihirisha utofauti mkubwa aliokuwa nao
mwandishi Euphrase Kezilahabi na watunzi wengine wa zama zake. Hali hii
imeonyesha kwa namna ambayo mtunzi aliweza kujipambanua katika kazi zake za
kifasihi. Hapa mwandishi anaelezea hisia alizonazo mtu ambaye amepata
misukosuko katika maisha ambapo tunamuona mhusika ameshika kisu mkononi
6 Maelezo haya ni ya Bwana Adria Fuluge, mahojiano haya yalifanyika jijini Dodoma tarehe
13/03/2020. Bw. Fuluge ni Mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Mzumbe. Pia ni mwanafunzi wa
Shahada ya Uzamivu katika fasihi ya Kiswahili Chuo Kikuu cha Dodoma.
63
tayari kwa kujiua. Tukio hilo la kukata tamaa kwa mhusika limeoneshwa na
mwandishi katika namna tofauti ukilinganisha na watunzi wengine. Falsafa ya
maisha anayoonesha mwandishi Euphrase Kezilahabi katika kazi zake inamfanya
ajipambanue na kutambulika kwa wasomaji wake.
4.4.2 Athari Hasi za Matumizi ya Utanzia katika Diwani Teule
Utanzia huweza kuleta athari hasi. Utafiti umebaini athari hasi zifuatazo:
4.4.2.1 Kutopata Wasomaji
Ingawa utanzia ni mbinu ya kibunilizi yenye tija, hata hivyo inapokithiri katika kazi
ya fasihi husababisha kupunguza idadi ya wasomaji. Hii inatokana na ukweli kuwa
katika jamii si watu wote wanaopenda kusoma kazi zenye maudhui ya kusikitisha
kiasi cha kumtoa mtu machozi. Hii ni kwa sababu wasomaji wengi wanapenda
kusoma kazi zinazowaletea furaha, kuwachekesha na kuwaburudisha. Wanapokutana
na kazi zinazowafanya wawe na huzuni, simanzi na masikitiko makubwa, hujikuta
wanakata tamaa. Hali hii inampelekea msomaji wa kazi ya fasihi kulia na kukata
shauri. Badala ya kupambana na tatizo linalomkabili katika maisha yake, huingiwa
na huzuni na kukata tamaa katika changamoto inayomkabili. Mawazo haya
yanafafanuliwa zaidi na Fuluge (2020)7 kwa kusema:
Matumizi ya mbinu ya utanzia katika kazi za kifasihi yanapelekea
uwezekano wa hadhira kupatwa au kutokewa na hisia za kusikitisha
na kuhuzunisha. Hisia hizo zinaweza kumfanya mtu kupata
maumivu, uchungu, majonzi, hofu, jitimai na masikitiko
yatakayopelekea kushindwa kuendelea kusoma kazi hiyo.
Kwa maelezo hayo, tunaona namna kazi ya fasihi inaweza kumuathiri msomaji wa
kazi hiyo na kupelekea kushindwa kuendelea kusoma kazi zenye maudhui ya namna
hiyo. Wamitila (2002) anasisitiza kuwa kuna aina nyingi za wasomaji ikiwemo aina
ya msomaji lengwa na msomaji mwashiriwa. Msomaji anapatikana kutokana na sifa
za ndani au za nje za kazi ya kifasihi. Anaona kuwa ni kawaida kuwasikia waandishi
wa kazi fasihi wakidai kuwa kazi zao zinalenga wasomaji fulani, ingawa kazi
zenyewe zinaashiria wasomaji tofauti kutokana na wasifu wake wa kiumbuji na
kimuundo. Ndipo baadhi ya wasomaji na wahakiki huona kuwa kazi hizo ni kwa ajili
ya kundi fulani na sio wao.
7 Maelezo haya ni ya Bwana Adria Fuluge, mahojiano haya yalifanyika jijini Dodoma tarehe
13/03/2020. Pia Bw. Fuluge ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu Dodoma.
64
4.4.3 Ugumu katika Kueleweka kwa Kazi ya Fasihi
Matumizi ya mbinu ya utanzia katika ushairi yanapelekea kusababisha kazi
kutokueleweka kwa wasomaji kwa urahisi. Mbinu hii ya utanzia inachukua muda
kwa msomaji kutafakari kwa kina ili kuweza kuelewa namna mwandishi
alivyoitumia. Hata hivyo, Mohamed (2011) anaunga hoja hiyo kwa kusema kwamba
uelewekaji wa ushairi wa Euphrase Kezilahabi unategemea umahiri wa wasomaji
katika kutambua ishara mbalimbali zinazojengwa kupitia mbinu mbalimbali za
usimulizi. Msomaji wa kazi za ushairi wa Euphrase Kezilahabi kushindwa kuelewa
kazi zake kutokana na kupata maana zaidi ya moja katika mashairi yake. Matumizi
ya mbinu ya utanzia yamepelekea hali ya huzuni, majonzi na simanzi kwa hadhira
pindi wanapofasiri kazi ya mwandishi. Hali hiyo inawafanya hadhira kushindwa
kubainisha kwa urahisi lengo alilokusudia mtunzi katika kazi yake.
Vilevile, Ponera (2014) anasema kazi za Euphrase Kezilahabi husababisha utata
katika kueleweka kwa maudhui na fani aliyoitumia katika kuelezea mambo ya
kusikitisha, kuhuzunisha, kuogopesha na hata kukatisha tamaa. Kutokueleweka kwa
urahisi kwa kazi ya mwandishi kunawafanya wasomaji wa kazi zake kujenga maana
kulingana na upeo wao pamoja na kuhusisha na mazingira yanayowazunguka. Hata
baadhi ya wanafasihi wameshindwa kuzichambua kazi za mtunzi huyu kwa sababu
ya kasumba kuwa kazi zake ni ngumu kueleweka kwa urahisi. Katika kuthibitisha
hoja hii Feruzi (2020)8 anafafanua kwa kusema:
Mwandishi Euphrase Kezilahabi ameweza kuzisana kazi zake katika
ustadi wa juu sana hivyo, msomaji au mhakiki anapaswa kusoma
kwa makini na kwa kina ili kuweza kutafakari yale ambayo
mwandishi ameyaandika. Ndipo ataweza kuelewa kusudi la utunzi
wa kazi hiyo ya fasihi.
Maelezo hayo yanathibitisha kuwa mwandishi Euphrase Kezilahabi ni mtunzi
kwenye kutumia ubunifu wa hali ya juu katika kutunga kazi za kifasihi. Wafuasi wa
nadharia ya upokezi wanaamini kwamba wasomaji wachache wa kawaida ndiyo
ambao wanaweza kuzielewa kazi hizo kwa wepesi. Muumano wa mawazo haya ya
nadharia ya upokezi na mbinu ya utanzia yanadhihirisha kuwa msomaji wa kazi ya
kifasihi anapata ugumu kuielewa kazi hiyo, kutokana na namna ya uwasilishaji wa
dhamira zake kwa njia ya huzuni, majonzi au masikitiko. Hivyo, inahitaji mhakiki au 8 Maelezo haya ni ya Dkt. Abdul Malick Feruzi, mahojiano haya yalifanyika ofisini kwake tarehe
09/03/2020. Dkt. Feruzi ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dodoma.
65
msomaji wa kazi ya fasihi kusoma kwa kina kazi za kifasihi zilizotumia mbinu ya
utanzia ili kuweza kuelewa alichokusudia mwandishi.
4.4.4 Athari za Utumizi wa Mbinu za Kisanaa kwa Watunzi Wengine
Matumizi ya mbinu za kisanaa kama ufutuhi, kejeli na dhihaka yanaweza kudhihirika
katika kazi za watunzi wakongwe na watunzi chipukizi katika kazi zao. Hivyo,
kuathiri uumbaji wa vipengele vya fani na maudhui za kazi za kifasihi. Euphrase
Kezilahabi, kama waandishi wengine, ameweza kuathiriwa na mbinu hizo
mbalimbali za kibunilizi. Mwakibete (2014) anaeleza kuwa, Euphrase Kezilahabi
amewaathiri watunzi wengine katika mbinu za kisanaa. Baadhi ya watunzi hao ni
Kulikoyela Kahigi; Mugyabuso Mulokozi na Mohamed Said Abdulla katika uumbaji
wa kifani na kimaudhui. Hivyo, kupelekea mfanano mkubwa wa kazi zao na
kufifisha kazi za kifasihi kwa kushindwa kuibua mambo mapya hasa katika mbinu za
kisanaa. Kwa mfano, diwani za Euphrase Kezilahabi zimerandana kwa kiasi kikubwa
na diwani ya “Malenga wa Bara” ya Mulokozi M. M na Kahigi K. K hasa katika
vipengele vya uumbaji wa taswira, lugha ya picha na ishara. Katika kutumia mbinu
hii ya utanzia, hasa katika diwani zake za Kichomi na Dhifa, mwandishi ameonesha
ufundi mkubwa katika kuibua vipengele vya huzuni, masikitiko na jitimai. Katika
diwani ya Dhifa kupitia shairi la “Harusi”, mwandishi anasema:
Waogopao kufa
Hapa
Kuna wimbo:
Yawezekana kinyonga
Na konokono hajawahi
Harusi hata moja na labda hata mazishi
Lakini ingawa wasikia wakinung’unika
Yawezekana pia hakuna binadamu
Anayetaka kuwahi kufa
Hali ikiwa hii
Mwendo wa kinyonga na konokono
Ndio mwendo wa maisha
Haya basi
Tufe tufapo
Tufapo tumekufa.
Katika ubeti wa shairi hili mwandishi ametumia mbinu ya utanzia huku lugha ya
kificho ikitumika kuonyesha mwisho wa maisha ya mwanadamu. Badala ya
kuonyesha shughuli ya kuoa au kuolewa kitu ambacho hufurahisha na sio
kuhuzunisha. Mwandishi ameibua simanzi, kilio na majonzi kwa sababu ameonesha
66
mwisho wa maisha ya mwanadamu hutokea bila mtu kujua siku wala saa. Culler na
Iser (1976) wanasema kutokana ubunifu wa kutumia mbinu za kisanaa, kaida na
kanuni wanazotumia watunzi katika kazi za kifasihi inapaswa wasomaji wa kazi
hizo, kuwa na umilisi au ujuzi fulani wa kuzitumia kaida hizo. Kwa sababu kaida
hizo zitawezesha wasomaji kuimarisha uzoefu wao katika kupitia kazi za kifasihi
kikamilifu au kutozielewa kabisa kazi hizo. Katika kuunga mkono hoja hiyo
Mapunda9 anathibitisha kwa kusema:
Matumizi ya mbinu ya utanzia kama mbinu zingine bunilizi katika
fasihi ya Kiswahili imesaidia katika kukuza fasihi. Hivyo kuna
maendeleo makubwa katika fasihi ya Kiswahili hasa tunapoona
zikitumika katika tanzu mbalimbali hasa ushairi. Inaonekana
utanzia umejadili zaidi katika tanzu nyingine za fasihi, lakini kwa
sasa tunaona unajitokeza hata katika ushairi.
Maelezo hayo yanadhihirisha wazi matumizi ya mbinu za kibunilizi kama utanzia,
ufutuhi, dhihaka, kejeli na ucheshi sio tu zinatumika katika riwaya na tamthiliya bali
hata katika ushairi wa Kiswahili.
4.4.5 Kukata tamaa
Kukata tamaa ni hali ya kupoteza matumaini juu ya jambo fulani (TUKI, 2013).
Katika kutumia mbinu hii ya utanzia kuna masuala ambayo mwandishi anayaelezea
kwa wahusika wake yanayopelekea kukatisha tamaa. Masuala hayo yanaweza kuwa
kifo, maradhi, mateso, majanga na hata ulemavu yanayowafanya wasomaji wa kazi
za kifasihi kuona maisha hayana maana. Hii inatokana na ukweli kuwa, kazi za
kitanzia mhusika mkuu kufikwa na misukosuko, matatizo au dhiki; wakati mwingine
huishia katika kifo (Wamitila, 2003). Kutokana na kazi za kitanzia kudhihirisha
anguko la mhusika mkuu, ni rahisi kumfanya msomaji kukosa matumaini kabisa.
Hali hii upelekea utanzia unaomvaa msomaji wa kazi ya fasihi kupata funzo
kutokana na anguko la mhusika mkuu. Hivyo kunamfanya aone kuwa hapa duniani
maisha yamejaa misukosuko, pamoja na kukosa tumaini la kuendelea kupambana na
changamoto zinazomkabili.
9 Maelezo haya ni ya Bwana Henry Mapunda, mahojiano haya yalifanyika ofisini kwake tarehe
17/07/2020. Bw. Mapunda ni Mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Dodoma.
67
Senkoro (1987) anasema, Aristotle katika andiko lake la Poetics aliwagawa watu
katika pande kuu mbili. Sehemu ya kwanza ni tabaka la juu yenye uwezo wa
kuchanganua mambo ambao wanafaa kusoma kazi za kitanzia. Sehemu ya pili ni
tabaka la chini ambao wana uwezo mdogo wa kufikiri wanafaa kusoma kazi za
vichekesho. Hivyo, tungo za kitanzia zinatoa funzo kwa msomaji wa kazi ya kifasihi
kulingana na namna alivyoweza kuitafakari na kuielewa. Katika kufafanua mawazo
hayo Malugu10 anasema:
Katika shairi la “Kisu Mkononi” linaonesha mateso na misukosuko
anayopitia mtu na kufikia hatua ya kukata tamaa ya maisha. Hali
hiyo inaweza kumpelekea mhusika kukata tamaa mpaka anafikia
hatua ya kuona ni bora kifo kuliko kuishi. Kama inavyodhirika
katika ubeti wa pili (2) mwandishi anasema:
Mbele chui mweusi, nyuma mwanga
Nionako kwa huzuni vifurushi maelfu ya dhambi
Kisu maisha kafiri haya
Kama kutazama nyuma au mbele
Ni kufa moyo.
Maelezo haya yanadhihirisha uwezekano wa hadhira kupatwa na hali ya utanzia
ambayo inaweza kuleta majonzi, masikitiko na huzuni kubwa kwa wasomaji. Katika
kazi za kifasihi mbinu ya utanzia hutumika kuonesha matukio mbalimbali kama vile,
ukatili, kifo, hali ngumu ya maisha, mateso na yanayoelezwa na mwandishi ili
kuibua hisia za woga kwa wasomaji. Atwood (1982) anadai kuwa usomaji ni
mfanyiko na unakubadilisha. Huwezi kuwa mtu yule yule uliyekuwa kabla na baada
ya kuisoma kazi ya kifasihi. Hivyo msomaji wa kazi ya kifasihi anapoisoma kazi
iliyotumia mbinu ya kitanzia anaweza kuathirika kwa kuingiwa na simanzi, majonzi,
masikitiko, kilio na huzuni. Hali hiyo inampelekea kukata tamaa kutokana na
matukio ya kitanzia yaliyodhihirika katika kazi husika ya fasihi.
4.5 Muhtasari wa Sura ya Nne
Sura hii imehusu uwasilishaji na mjadala wa matokeo ya utafiti. Mjadala umehusisha
diwani mbili za Euphrase Kezilahabi ambazo ni Kichomi na Dhifa kwa kuangalia
mdhihiriko wa utanzia, huku ikijielekeza katika kutimiza malengo matatu ya utafiti.
Sura hii imegawanyika katika sehemu tano. Sehemu ya kwanza imeelezea muhtasari
10 Maelezo haya ni ya Bwana Alfred Malugu, mahojiani haya yalifanyika jijini Dodoma tarehe
26/06/2020. Bw. Alfred Malugu ni Mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine
Mwanza.
68
wa diwani teulu. Sehemu ya pili imebainisha matukio ya utanzia ndani ya diwani
teule. Matukio hayo ni hali ngumu ya maisha, kifo, maradhi, majanga, ukatili na
mateso. Sehemu ya tatu imefafanua lengo la pili la utafiti. Katika sehemu hii dhima
anuwai za utanzia zimebainishwa. Dhima hizo ni pamoja na kufikirisha hadhira,
kujenga uhalisi wa maisha, kuhuzunisha hadhira na kujenga hisia za woga kwa
hadhira. Sehemu ya nne imechambua athari chanya na hasi za utanzia kwa wasomaji
kwa kuzingatia misingi ya nadharia ya upokezi katika diwani teule. Tasnifu hii
imebainisha kwamba, wasomaji wa kazi za ushairi za Euphrase Kezilahabi
wameathiriwa waziwazi na uandishi wake kifani na kimaudhui. Athari hizo ni kukata
tamaa, kuibusha majonzi kwa hadhira, ugumu katika kueleweka kwa kazi ya fasihi,
athari za utumizi wa mbinu za kisanaa kwa watunzi wengine na kuitafakarisha
hadhira. Sehemu ya tano imeelezea muhtasari wa sura nne. Sura inayofuata
inafafanua muhtasari, hitimisho na mapendekezo.
69
SURA YA TANO
MUHTASARI, HITIMISHO NA MAPENDEKEZO
5.1 Utangulizi
Utafiti wetu ulihusu Mdhihiriko wa Utanzia katika Ushairi wa Kiswahili, ambapo
mifano imetolewa katika riwaya mbili za Euphrase Kezilahabi za Kichomi na Dhifa.
Katika sura hii ya mwisho, tumewasilisha muhtasari wa tasinifu, hitimisho na
mapendekezo. Sura imegawanyika katika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza inatoa
muhtasari wa tasnifu. Sehemu ya pili ni hitimisho la tasinifu na sehemu ya tatu ni
mapendekezo kwa tafiti zijazo.
5.2 Muhtasari
Tasinifu hii imechunguza matumizi ya utanzia katika mashairi ya Euphrase
Kezilahabi. Utafiti uliongozwa na malengo matatu ambayo ni kubainisha matukio ya
utanzia katika diwani teule, kufafanua dhima za matumizi ya utanzia katika diwani
teule na kuchambua athari za utanzia katika diwani teule. Nadharia ya upokezi
ilitumika katika ukusanyaji na uchambuzi wa data.
Tasinifu hii ina jumla ya sura tano. Sura ya Kwanza ni ya utangulizi wa jumla.
Katika sura hii vimejadiliwa vipengele mbalimbali vya utangulizi. Vipengele hivyo
ni usuli wa tatizo la utafiti, tamko la tatizo la utafiti na malengo ya utafiti. Aidha,
sura hii imebainisha maswali ya utafiti, manufaa ya utafiti na mawanda ya utafiti
pamoja na kuelezea historia fupi ya mwandishi.
Sura ya Pili imebainisha maandiko mbalimbali yanayohusiana na mada ya utafiti.
Maandiko hayo yamegawanywa katika makundi mawili. Kundi la kwanza
limejumuisha maandiko kuhusu dhana ya utanzia, kundi la pili limejumuisha
maandiko kuhusiana na ushairi wa Euphrase Kezilahabi. Pia, sura hii imebainisha
mapengo yaliyojitokeza kutokana na kupitia maandiko. Aidha, katika sura hii
tumefafanua nadharia ya upokezi ambayo ndiyo ilituongoza katika utafiti wetu.
Sura ya Tatu imevifafanua vipengele vya methodolojia ya utafiti. Vipengele hivyo ni
usanifu wa utafiti, eneo la utafiti, walengwa wa utafiti, ukusanyaji wa data, njia na
zana za kukusanyia data na mchakato wa ukusanyaji wa data. Vipengele vingine ni
uchanganuzi wa data, itikeli za utafiti, uhalali na uthabiti wa matokeo ya utafiti na
changamoto za utafiti na utatuzi wake.
70
Sura ya Nne imehusu uwasilishaji na mjadala wa matokeo ya utafiti. Sura
imegawanyika katika sehemu nne. Sehemu ya kwanza imechambua lengo la kwanza
la utafiti. Sehemu ya pili imechambua lengo la pili la utafiti. Sehemu ya tatu
imechambua lengo la tatu la utafiti wetu na kufuatiwa na muhtasari wa sura ya nne.
Sura ya Tano ina sehemu kuu tatu. Sehemu ya kwanza ni ya muhtasari. Sehemu ya
pili ni hitimisho ambapo tumeeleza kuhusu utoshelevu wa nadharia ya upokezi na
mchango mpya wa tasinifu hii. Sehemu ya tatu inatoa mapendekezo kwa ajili ya
tafiti zijazo.
5.3 Hitimisho
Katika sehemu hii tumejadili utoshelevu wa nadharia iliyotumika pamoja na
mchango mpya wa tasinifu.
5.3.1 Utoshelevu wa Nadharia
Utafiti uliongozwa na nadharia ya upokezi. Kupitia mihimili yake tumeweza
kukusanya na kuchambua data za utafiti wetu. Kwa kiasi kikubwa nadharia ya
upokezi imeweza kutusaidia katika malengo yote matatu ya utafiti huu. Kutumika
kwa nadharia hii katika utafiti huu kumetoa mwanga kwa mtafiti kubaini kuwa ili
msomaji wa kazi ya kifasihi aweze kuzielewa mbinu bunilizi hana budi kuzihusisha
na historia, siasa, uchumi na utamaduni. Euphrase Kezilahabi anajipambanua kwa
kuwatetea wanyonge kupitia ushairi wa Kiswahili kwa kutumia mbinu ya utanzia ili
kukwepa mkono wa dola. Matumizi ya mbinu ya utanzia yalimwezesha mwandishi
kufichua mambo mbalimbali yanayoikabili jamii kwa ujumla.
5.3.2 Mchango Mpya wa Tasinifu
Matokeo ya utafiti huu yameleta upya katika taaluma ya fasihi. Hii ni kwa sababu
tasinifu imeweza kuyabainisha matukio yaletayo utanzia. Pia, tasinifu imeweza
kufafanua sababu za utumiaji wa utanzia pamoja na kuchambua dhima za utanzia
katika diwani teule. Tasinifu hii imebainisha kuwa utanzia ni mbinu inayotumiwa na
washairi katika kujenga maudhui yao tofauti na hapo mwanzo utanzia uliweza
kuonekana kwenye tamthiliya pekee. Pia tasinifu hii imeweza kuonyesha tofauti kati
ya tanzia na utanzia katika kazi za fasihi.
71
5.4 Mapendekezo kwa Tafiti Zijazo
Kutokana na mipaka ya utafiti wetu kujikita katika malengo matatu na vitabu viwili
vya ushairi vya Euphrase Kezilahabi, tunapendekeza tafiti zijazo zishughulikie
utanzia kwa jicho la kilinganishi baina ya mtunzi mmoja na mwingine ili kuona
kufanana na kutofautiana kwao. Pia, utanzia unaweza kuchunguzwa katika tanzu
zingine za fasihi andishi kama riwaya na tamthilia. Aidha, katika fasihi simulizi ya
Kiswahili watafiti wanaweza kuchunguza na kubaini mbinu hii inavyofanya kazi
hasa katika tanzu za fasihi simulizi kama vile hadithi na semi. Vilevile, pamoja na
wataalamu wengi wa fasihi kujihusisha na utanzia katika tanzu mbalimbali za fasihi,
tunapendekeza tafiti zijazo zishughulikie suala la utanzia katika fasihi ya watoto.
72
MAREJELEO
Atwood, M. (1982). Second Words: Selected Critical Prose. Canada: House of
Anansi Press.
Acquaviva, G. (2004). “Jazanda ya Njozi katika Baadhi ya Mashairi ya Euphrase
Kezilahabi”. Katika Kiswahili Forum Juzuu 11 uk: 69-73.
BAKITA, (2017). Kamusi Kuu ya Kiswahili. Nairobi: Longhorn.
Chiraka, C. (2011). Tahakiki ya Vitabu Teule: Dar es Salaam: Afro-Plus Publishers.
Cohen, L. na Wenzake (2007). Research Methods in Educational6th Edition. London:
Routledge.
Enon, J. C. (1998). Educational Research, Statistics and Measurements. Kampala:
Makerere University.
Fuluge, A. (2013) “Dhana ya Kujiua katika Kazi za Euphrase Kezilahabi.” Tasnifu
ya Shahada ya Umahiri katika Fasihi ya Kiswahili.Chuo Kikuu cha Dodoma
(Haijachapishwa).
Gaudioso, R. (2018). “Mikondo ya Mtiririko wa Kishairi: Mabadiliko ya Ushairi wa
Kiswahili wa Kezilahabi na Mulokozi.” Fasihi, Lugha na Utamaduni wa
Kiswahili na Kiafrika: Kwa Heshima ya Profesa M.M Mulokozi. Dar es
Salaam: TUKI.
___________. (2014). “Kuwako na Wakati: Mipaka ya Lugha kama Hatua za Falsafa
katika Mashairi ya Euphrase Kezilahabi.” Katika Kiswahili Forum Juzuu 21.
Uk: 76-103.
Haji, A. K. (2015). “Matumizi ya Utanzia katika Riwaya teule za Said Ahmed
Mohamed”.Tasnifu ya Shahada ya Umahiri katika Fasihi ya Kiswahili.Chuo
Kikuu cha Dodoma (Haijachapishwa).
Hays, D. G.na Sigh, A. A. (2012). Qualitative Inquiry in Clinical and Educational
Settings. New York: The Guilford Press.
73
Kaishozi, L. (2012). “Kulinganisha Mitizamo ya maisha kati ya Euphrase Kezilahabi
na Sayyid Abdallah Bin Ali Bin Nassir. Tasnifu ya Shahada ya Umahiri
katika Fasihi ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dodoma (Haijachapishwa).
Kezilahabi, E. (1974). Kichomi: Nairobi: Heinemann Education Books (EA) Ltd.
________. (1988). Karibu Ndani: Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press.
________. (2008). Dhifa. Dar es Salaam: Vide-Muwa Publishers Ltd.
King’ei, G. K. na Kisovi, A. (2005). Misingi ya Fasihi Simulizi. Nairobi: Kenya
Literature Bureau.
Kombo, D. K na Tromp, D. L. A. (2006). Proposal and Thesis Writing: An
Introduction. Nairobi: Pauline Publication Africa.
Kothari, C. R. (2004). Research Methodology: Methods and Techniques 2nd Edition.
New Delhi: New Age International Publishers Limited.
Khatib, M. S. (1987). “Washairi wa Kiswahili Wanavyoliona Azimio la Arusha”
katika Mulika Na. 19. Dar es Salaam: TUKI. Kur. 69-73.
Mackeon, R. (1947). Introduction of Aristotle. New York: Randon House.
Malugu, A. (2011). “Suala la Itikadi Katika Riwaya za Euphrase Kezilahabi” Tasnifu
ya Shahada ya Umahiri katika Fasihi ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dodoma
(Haijachapishwa).
Maxwell, J. A. (2013). Qualitative Research Design: An Interactive Approach.
Calfonia: Sage Publication Inc.
Mazongela, K. S. (2016). “Matumizi ya Utanzia katika Riwaya Pendwa ya
Kiswahili: Ulinganisho wa Riwaya za Ben Mtobwa na Hussein Tuwa”.
Tasnifu ya Shahada ya Umahiri katika Fasihi ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha
Dodoma (Haijachapishwa).
74
Mganga, N. A. (2019). “Matumizi ya Ramsa na Tanzia katika Ushairi wa Kiswahili:
Mifano kutoka katika Utenzi wa Al-Inkishafi. Tasnifu ya Shahada ya
Uzamivu katika Fasihi ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dodoma
(Haijachapishwa).
Moh’d, H. K. (2016). “Utanzia katika Kasida za Kiswahili: Mifano kutoka Mkoa wa
Mjini Magharibi Unguja.” Tasnifu ya Shahada ya Umahiri katika Fasihi ya
Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dodoma (Haijachapishwa).
Mulokozi, M. (1983). “Uhakiki wa Dunia Uwanja wa Fujo” katika Kiswahili 50/1:1-
12Dar- es- Salaam: TUKI.
_______. (1996). Fasihi ya Kiswahili (OSW 105). Dar es Salaam: Chuo Kikuu Huria
cha Tanzania.
_______. (2017). Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam: KAUTTU
Limited.
Mulokozi, M. na Kahigi, K. (1982). Kunga za Ushairi na Diwani Yetu. Dar es
Salaam: Tanzania Publishing House.
Mwakibete, H. (2014). “Kejeli na Dhihaka katika Mashairi ya Euphrase Kezilahabi:
Sababu za Kutumika na Athari zake kwa Wasomaji”. Tasnifu ya Shahada ya
Umahiri katika Fasihi ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dodoma
(Haijachapishwa).
Ponera, A. S. (2019). Misingi ya Utafiti wa Kitaamuli na Uandishi wa Tasinifu.
Dodoma: Central Tanganyika Press.
_________. (2014). “Ufutuhi katika Nathari ya Kiswahili: Ulinganisho wa Nathari za
Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi”. Tasnifu ya Shahada ya Uzamivu
katika Fasihi ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dodoma (Haijachapishwa).
__________. (2010). “Ufutuhi katika Riwaya za Shaaban Robert: Dhima, Sababu na
Athari Zake kwa Jamii”. Tasnifu ya Shahada ya Umahiri katika Fasihi ya
Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dodoma (Haijachapishwa).
75
_________. (2016). Suala la Matumizi ya Nadharia kama Kiunzi cha Tafiti za
Kitaamuli: Mfano wa Matumizi ya Nadharia ya Ukanivali. Journal of
Humanities, School of Humanities, The University of Dodoma, 3(1), 116–
129.
Prewitt, C. R. (1995). Introductory Research Methodology. African Publication.
Ocassional Paper No. 10. Institute of Development Studies: University of
Nairobi.
Said, Z. (2016). “Usawiri wa Ufungwa katika Riwaya za Kiswahili: Mifano kutoka
katika riwaya za Umleavyo na Haini. Tasinifu ya Shahada ya Umahiri katika
Fasihi ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dodoma.
Sanga, A.N. (2018). “Mkengeuko wa Ujumi wa Kiafrika katika Hadithi fupi Andishi
za Kiswahili Kipindi cha Utandawazi: Mifano kutoka Magazeti ya Habari leo
na Nipashe na Mwananchi”. Tasnifu ya Shahada ya Uzamivu katika Fasihi ya
Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dodoma (Haijachapishwa).
Semzaba, E. (1997). Tamthiliya ya Kiswahili. Dar es Salaam: Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania.
Sengo, T. S. Y. (1992). “Utamaduni wa Kiswahili: Wilaya ya Kusini Unguja” katika
African Studies, Juz. Na. 1, uk 53-79.
Senkoro, F. E. M. K. (2011). Fasihi. Dar es Salaam: KAUTTU Ltd.
_______________. (1988). Ushairi: Nadharia na Tahakiki. Dar es Salaam: Dar es
Salaam Press.
________________. (1987). Fasihi na Jamii. Dar es Salaam: Press and Publicity
Centre.
________________. (1982). Fasihi. Dar es Salaam: Press and Publicity Centre.
Shahid, I. (1980). “Arabic Literature” katika Cambridge History of Islam.Tol.Na.
2B.uk. 657-671. Cambridge: Cambridge University Press.
76
Soileau, C. (2006). “Money and Tragedy in the Nineteeth- Century Novel”.Tasnifu
ya Shahada ya Uzamivu katika Fasihi Linganishi, Chuo Kikuu cha Lousiana
(Haijachapishwa).
Topan, F. (1974). “Utangulizi” katika Kezilahabi, E. Kichomi. Nairobi: Heinemann
TUKI. (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi: Oxford University Press.
UWAKI, (2013). “Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii: Mwongozo wa Kisera wa
Sekta ya Afya ya Kuzuia na Kupambana na Ukatili wa Jinsia”. Iliyosomwa
16/07/2020 katika w.w.w.healthpolicyinitiative.com.
Wafula, R.M. na Njogu, K. (2007), Nadharia za Uhakiki wa Fasihi, Sai Industries
Limited, Nairobi.
Wamitila, K. W. (2003). Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus
Books.
______. (2002). Uhakiki wa Fasihi: Misingi na Vipengele Vyake. Nairobi: Phoenix
Publishing Ltd.
______. (2016). Kichocheo cha Ushairi: Mwongozo wa Uchambuzi wa Mashairi.
Nairobi: Vide-Muwa.
White, B. (2002). Skills for Bussiness Management. London: Penguin Books Ltd.
77
VIAMBATISHO
A. Miongozo ya Mahojiano na Uchanganuzi Matini
A.1 Mwongozo wa mahojiano kwa Wataalamu wa Fasihi ya Kiswahili
Maswali:
1. Kwa maoni yako, unaielewaje dhana ya utanzia?
2. Je, utanzia huweza kudhihirishwa kupitia vipengele gani?
3. Kuna uhusiano wowote wa utanzia unaojitokeza katika kazi ya fasihi na matukio
ya maisha ya mtunzi? Kama upo, ni matukio gani husawiriwa na utanzia
4. Ni mashairi yapi katika diwani teule za Euphrase Kezilahabi yamedhihirisha
utanzia?
5. Je, mbinu ya utanzia itumikapo katika kazi ya fasihi huweza kuiathiri jamii
katika vipengele gani na kwa vipi?
6. Nini maoni yako kuhusiana na utumiaji wa mbinu ya utanzia katika ushairi wa
Kiswahili?
A.2 Mwongozo wa Uchanganuzi Matini
Uchanganuzi wa matini utashughulika na usomaji wa maandiko mbalimbali
yanayohusiana na mada ya utafiti. Maandiko yatakayodurusiwa ni yale ya maktabani
na kwenye vyanzo vya kielektroniki. Uchanganuzi wa matini katika vyanzo vya
kielektroniki utazingatia vyanzo vinavyohusisha taasisi zinazojulikana na kuaminika.
Mwongozo wa uchanganuzi wa matini unafafanuliwa katika jedwali lifuatalo:
Vyanzo vya Maarifa Vipengele
Vitakavyochanganuliwa
Lengo
Diwani ya Kichomi na
Diwani ya Dhifa
Mashairi, maana, dhana ya
utanzia inayojitokeza
Kuchanganua
matukio ya utanzia,
dhima na athari
zake kwa jamii.
78
B: BARUA ZA ITHIBATI YA KUFANYIA UTAFITI
79
80
C: PICHA MBALIMBALI ZINAZOHUSIANA NA UTAFITI
Picha Na. 1: Mtafiti (kulia) akifanya mahojiano na Dkt. Elizabeth Mahenge wa
Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam. Mahojiano haya yalifanyika tarehe 11/06/2020 ofisini kwake
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
81
Picha Na. 2: Picha ya Dkt. Abdul Malick Feruzi akiwa na mtafiti (kulia) akifanya
mahojiano ofisini kwake tarehe 09/03/2020, Chuo Kikuu cha
Dodoma.
82
D: TAARIFA ZA WATAFITIWA
Na JINA TAREHE
ZA USAILI
MAHALI PAUSAILI
1. Dkt. Elizabeth Mahenge 11/06/2020 Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam
2. Dkt. Anna Kyamba 11/06/2020 Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam
3. Dkt. Ramadhani Thomas 09/06/2020 Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam
4. Dkt. Abdul Malick Feruzi 09/03/2020 Chuo Kikuu cha Dodoma
5. Bw. Adria Fuluge 13/03/2020 Jijini Dodoma
6. Bw. Alfred Malugu 26/06/2020 Jijini Dodoma
7. Bw. Henry Mapunda 17/07/2020 Chuo Kikuu cha Dodoma
8. Bw. Selestin Msigala 09/06/2020 Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam