tano - ctmi.orgctmi.org/books/download/huduma-tano.pdfmwalimu ametiwa mafuta ili kujenga juu ya...

26
Miki Hardy TANO Huduma Kila kitu kilichoandikwa katika Agano Jipya kuhusu utendaji wa pamoja wa hizi huduma tofauti katika kulijenga Kanisa kitahusika maadamu Kanisa lidumupo duniani.

Upload: others

Post on 05-Feb-2020

12 views

Category:

Documents


0 download

TRANSCRIPT

Miki Hardy

TA NOHuduma Kila kitu kilichoandikwa katika Agano Jipya kuhusu utendaji wa pamoja wa hizi huduma tofauti katika kulijenga Kanisa kitahusika maadamu Kanisa lidumupo duniani.

Huduma Tano

na Miki Hardy

9

10

Hakimiliki © 2013 na Church Team Ministries International (CTMI).

Huduma Tano na Miki Hardy.

Imechapishwa na Church Team Ministries International (CTMI).

Toleo la kwanza: Julai 2017

Jalada limebuniwa na: Idara ya Habari ya CTMI

Haki zote zimehifadhiwa. Hakuna sehemu ya chapisho hili inayoweza kunakiliwa, kusambazwa, au kutolewa kwa namna yo yote ile isipokuwa kwa ruhusa ya mchapishaji.

Vifungu vya Biblia vimetolewa katika Biblia, Swahili – Union Version, 1962. Haki zote zimehifadhiwa.

Machapisho mengi ya Church Team Ministries International yanapatikana kwa gharama nafuu ikiwa yananunuliwa kwa jumla kwa ajili ya matangazo, kuchangisha fedha, kugawa bure, na kwa kuelimishia.

Kwa maelezo zaidi, tuandikie: Media Dept., CTMI, Trianon, Mauritius; au tuma baruapepe kwa: [email protected]

Tembelea tovuti yetu: www.ctmi.org

ISBN 978-99949-0-300-9

Yaliyomo

I. Huduma Tano 4

II. Mtume 9

III. Upako wa Kinabii 12

IV. Mwinjilisti 15

V. Mwalimu 18

VI. Mchungaji 21

.............................................................................

.......................................................................................

......................................................................

..................................................................................

.....................................................................................

.................................................................................

3

4

Sura ya I

Huduma Tano

“Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii, na wengine kuwa wainjilisti na wengine wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapofikia umoja wa imani na kumfahamu sana mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.” Waefeso 4:11-13.

Kama umetumia muda kiasi kuisoma Biblia utaafiki kwamba Mtume Paulo, ambaye ndiye mwandishi wa maneno haya, alifanyika mfuasi wa Yesu Kristo kwa namna isiyokuwa ya kawaida alipokuwa akielekea Dameski. Anaandika katika Wagalatia 1:11-12 ya kwamba Injili aliyoihubiri si kitu ambacho mwanadamu alikibuni, au kitu alichopokea kutoka kwa mwanadamu, au kufundishwa. Ila, aliipokea moja kwa moja kutoka kwa Yesu Kristo kwa njia ya ufunuo. Hata hivyo, ujumbe wake haukuwa tofauti na ule uliohubiriwa na mitume wengine - ujumbe wa Kristo, Kristo aliyesulubiwa. Anaelezea katika nyaraka zake ya kwamba kuhubiriwa kwa msalaba, ambao ni nguvu ya Mungu, kunaweza kumkamilisha kila mtu katika Kristo ikiwa tu kutafanyika kupitia vipawa vilivyomo kwenye Huduma Tano.

Kanisa la MwanzoInasikitisha kwamba Wakristo wengi siku hizi wanakubali tu uwepo wa Huduma Tano pasipo kuona umuhimu wake au hata kuelewa utendaji kazi wake katika Kanisa. Wengine wanaonekana kutishwa na athari zake katika huduma zao binafsi na hivyo wanachagua kupuuza huu utumishi wa Huduma Tano. Pasipo kujali imani ya mtu, hakuna Mkristo mkweli juu ya nafsi yake anayeweza kuhitimisha kwamba huduma na vipawa anavyotoa Yesu kwa watu kuongoza na kulijenga Kanisa lake vilikuwa ni kwa ajili ya kanisa la mwanzo tu. Utendaji wa hizi huduma tano kama tunavyouona kwenye Agano Jipya, zikifanya kazi kwa pamoja katika kulijenga Kanisa, utakuwepo muda wote Kanisa litakapokuwepo duniani. Roho yule yule aliyekuwepo Kanisa lilipoanza, yu kazini hata leo. Yesu hajabadilika. Yu ngali anatoa huduma zile zile leo kama alivyotoa hapo mwanzo - kwa lengo lile lile - ili kwamba Mwili wake upate kujengwa na

watu wake wakamilishwe ndani yake. Katika nyakati za giza za Kanisa huduma hizi zilitoweka kwa muda kutokana na udunia na udini kuutawala Ukristo. Lakini leo, Mungu anazirejesha na kuwarejesha watu wake tena kwenye msingi wa kweli, ili kwamba wafanyike watu wazima rohoni na kuufikia umoja wa imani. Hii ndio sababu hizi huduma, ambazo zinaweza kuunganishwa tu kupitia injili ya msalaba, ni muhimu sana kwa Kanisa.

Pako TofautiKila huduma katika hizi tano, huwakilishwa na upako maalum, na kila upako ni tofauti. Kazi inayofanywa na kila huduma hutegemea sana upako wake. Hii ndio maana ni hatari sana kujaribu kutafsiri huduma hizi kwa namna tunayoamini ‘zinapaswa’ kutenda kazi, kwani kwa njia hii watu hujipachika vyeo na kuwaigiza wengine. Yesu alikuwa na huduma hizi zote tano na yeye huzigawa kama aonavyo vema, ili kwamba asili yake iweze kuwemo Kanisani kupitia wanadamu ambao kwao amewekeza upako wake. Kwa hivyo, huduma hizi humwakilisha Yesu Kanisani. Pindi zinapofanya kazi katika umoja, Kristo hudhihirishwa. Huduma Tano pamoja na wazee wengine wa kanisa la mahali pamoja huiwakilisha mamlaka ya Kanisa. Wote hawa hufanya kazi kwa pamoja katika kuyatimiza mapenzi ya Mungu. Kwa hivyo, basi, mtu mmoja peke yake anaweza kuwakilisha sehemu moja tu ya mamlaka ya Kristo ndani ya Kanisa la mahali pamoja.

Kufanya kazi pamojaHii inaelezea ni kwa nini Wakristo katika makanisa mengi wanashindwa kukua zaidi ya pale walipofikia. Kwa kawaida, chakula pekee cha kiroho wanachopata hutoka katika upako mmoja, ambao ni wa mchungaji. Mambo yote humhusu yeye, na kila kitu huanzia na kuishia kwake. Kuna maelfu ya makanisa ya jinsi hii ambayo hayana kabisa mahusiano na huduma nyingine wala makanisa mengine, na yanaishi katika hali ya kujitenga kabisa. Lakini, katika Agano Jipya, hatuoni huduma huria au makanisa yaliyojitenga. Kinyume chake, tunaona makanisa mengi sana ya mahali pamoja yaliyotapakaa katika himaya nzima ya Kirumi, yote yakiwa yameunganishwa na Huduma Tano, na yakitumika na kufanya kazi katika umoja. Hii ndio sababu watu wa Mungu waliweza kukua na kufikia utu uzima rohoni. Hapakuwepo na mipaka ya kikabila, rangi, lugha, utaifa, au cheo!

Vivyo hivyo, huduma zinazojumuisha Huduma Tano hazina uhuru binafsi. Mtu mmoja peke yake hawezi kuikamilisha kazi ya Mungu. Huduma zote tano ni muhimu sana kwa Kanisa zifanyapo kazi pamoja. Kuna uelewa fulani leo hii Kanisani kwamba, kama wewe ni mwalimu basi una huduma yako binafsi, kama ni mwinjilisti, una huduma yako binafsi, na ikiwa wewe

5

ni nabii, una huduma yako binafsi. Cha kusikitisha ni kwamba, mara nyingi huduma hizi hazikuungwa na kanisa la mahali pamoja, wala moja na nyingine. Nyingi zinajiendea katika uhuru binafsi kabisa, haziwajibiki kwa mtu yeyote. Wenye nazo wanahubiri wanachotaka, wanafanya wanachotaka na wanakwenda wanakotaka. Sioni uthibitisho wowote wa mambo kama haya katika Agano Jipya. Hakika, ninaona kinyume chake kabisa. Ninaona hizi huduma tofauti zikifanya kazi kwa kushirikiana moja na nyingine pamoja na watu waliotumwa na kanisa la mahali pamoja katika kuyaendea makanisa mengine kwa lengo la kuchangia katika kuwaanda Wakristo na kuujenga Mwili wa Kristo. Na kote kote, ninaona ya kwamba wote hawa walijinyenyekeza mmoja kwa mwingine. Utendaji wa kazi wa jinsi hii ni matunda ya Injili; ni nguvu ya msalaba inayofanya kazi katika maisha ya watu wa Mungu.

Mapenzi ya Mungu kwa KanisaJambo lingine la muhimu sana tunalopaswa kuelewa ni kwamba hizi huduma daima hutumwa. Tunaona katika Kitabu cha Matendo ya Mitume na katika nyaraka za Mtume Paulo kwamba yeye alitumwa na kanisa lake la mahali pamoja, na aliporudi alitoa hesabu kwa wale waliokuwa wamemtuma. Unapokuwa hujatumwa huwajibiki kutoa hesabu kwa mtu yeyote. Uko huru na unaweza kuingia na kutoka upendavyo. Hata hivyo, tunaona kwenye Maandiko Matakatifu ya kwamba huduma hizi na Wakristo kwa pamoja walitumwa na mtume au jumuiya za wazee kutoka katika makanisa yao. Mtume Paulo alikuwa ni sehemu ya baraza la wazee wa Kanisa lililokuwako Antiokia. Aliondoka kwenda katika safari zake za kimisionari na kurudi. Alipokuwa akisafiri, alijenga mahusiano ya kudumu na watenda kazi wenzake, pamoja na watumishi wengine katika makanisa ya mahali pamoja. Zaidi ya hapo, aliendelea kufanya kazi katika umoja nao katika kuieneza Injili na kuliimarisha Kanisa.

Kuna mifano mingi sana katika kitabu cha Matendo ya Mitume na katika nyaraka za Agano Jipya inayothibitisha jinsi Huduma Tano zilivyofanya kazi katika umoja ili kuwaandaa Wakristo kwa kazi ya huduma na kulileta Kanisa katika utu uzima rohoni. Tunawaona Mitume wakifanya kazi kwa kushirikiana na huduma nyingine zote, kwamba ni manabii, wainjilisti, wachungaji au walimu. Hakuna hata mmoja aliyetenda kwa uhuru wake binafsi na kila mmoja alitambua nafasi na umuhimu wa mwenzake, na hili lilileta umoja wa imani na kuliwekea Kanisa msingi imara. Kanisa linazihitaji hizi huduma zote kwa sababu kila upako ni tofauti na ni muhimu katika kulijenga Kanisa. Kwa jinsi hiyo Wakristo wanawezeshwa kukua katika kumfahamu sana Mwana wa Mungu na kufanyika watu wazima rohoni, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo. Hayo ndiyo mapenzi ya Mungu kwa Kanisa lake.

6

Kujenga huduma zenye matundaMwishoni mwa miaka ya 1980, Mungu aliingilia kati maisha yangu kwa namna ya kimuujiza ambapo maisha yangu na huduma yangu vilibadilika. Wakati huo, mimi nilikuwa ‘ndiye mwenye mamlaka’ kanisani lakini sikuwajibika kwa njia yoyote kwa wazee wenzangu. Tulikuwa kundi la wachungaji tuliokuwa tukifanya kazi katika makanisa tofauti kisiwani Mauritius, na kila mmoja alikuwa na mpango wake wa kujenga himaya yake mwenyewe. Hapakuwepo na umoja halisi miongoni mwetu bali matengano na mashindano. Nilitumika katika uhuru wangu binafsi lakini nilikuwa nikimenyana na hisia za kukata tamaa na kushindwa. Nilivunjika moyo kwa sababu watu ambao Mungu aliniaminia niwatunze waliendelea kufungwa na minyororo ya dhambi na walionekana kutokukua kiroho. Pamoja na hayo, nilikuwa na matatizo nyumbani mwangu katika uhusiano wangu na mke wangu. Nilikaribia kukata tamaa kabisa. Lakini Mungu, kwa neema yake, aliniongoza kwenye kitabu cha Matendo ya Mitume na nyaraka za Mtume Paulo na nikaanza kuona Kanisa lilivyopaswa liwe. Ujumbe wa msalaba ukanifumbua macho na nikaiona hali yangu. Nikagundua tatizo lilikuwa kwangu na nikatubu mbele za Bwana. Mara tu nilipokubali kuyapoteza maisha yangu, kuuchukua msalaba wangu na kumruhusu Bwana anivunje na kunifinyanga - si kitu rahisi kukubali - nilianza kushuhudia ushindi mkubwa katika maisha yangu, ndoa yangu, mahusiano yangu na wazee wangu wa kanisa, na katika utumishi wangu. Watu wa Mungu wakahisi mabadiliko ndani yangu nao wakaitikia kwa nia ile ile ya moyo. Jambo la muhimu ni kwamba hii kazi ni sharti ianzie kwa mtumishi wa Mungu.

Leo, tuna mahusiano ya karibu na huduma mbalimbali duniani kote, kwa kadri tunapofanya kazi pamoja nao katika kulijenga Kanisa. Nimeshuhudia Huduma Tano zikifanya kazi na kuzaa matunda katika kanisa la mahali pamoja, Wakristo wakijengwa na kufikishwa katika utu uzima rohoni katika Kristo. Ninaamini hii ndio njia pekee kwa Kanisa kuinuka kutoka lilikojificha na kuiangaza nuru ya Kristo Yesu duniani kote.

Jukumu la kila hudumaKwa kadiri ya uongozi wa neema ya Mungu, kila upako katika Huduma Tano hubeba mamlaka tofauti. Kwa mfano, mtume na nabii hubeba mamlaka iliyo kuu zaidi kuliko huduma nyingine.

Mtume huweka msingi; humdhihirisha Kristo na moyo wake kwa Kanisa. Kwa maana nyingine, kila Mkristo anayeupokea ujumbe wa kitume hufahamu kuanzia saa aliyoamini ya kuwa ameyapoteza maisha yake na ya kwamba si yake tena. Mtume ni baba wa makanisa, viongozi na

7

Wakristo wengi, kwani kutokana na upako ulio juu ya maisha yake yeye hutoa uangalizi, mwongozo na ulinzi kwa Kanisa. Kwa msingi huo, ni rahisi kuelewa ya kwamba huduma na upako wake huleta umoja miongoni mwa makanisa mbalimbali. Mtume pia ni mlinzi wa mafundisho ya uzima ya Kristo.

Nabii ana jukumu la kipekee la kuwa kinywa cha Mungu kilichovuviwa na Roho Mtakatifu. Yohana Mbatizaji ndiye mfano bora wa huduma hii katika Agano Jipya. Aliponena habari za Yesu alisema: “Ambaye pepeto lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake, na kuikusanya ngano yake ghalani, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.” Ni huduma yenye mamlaka, inayohubiri toba, utakaso na kutengwa na dunia, kulikoambatana na hofu ya Mungu.

Shauku ya Mwinjilisti ni kutangaza Habari Njema za Yesu Kristo kwa ajili ya wokovu wa roho za watu, na yuko tayari kuutoa uhai wake kwa ajili ya hili. Ujumbe wake ni rahisi lakini wenye nguvu na huambatana na miujiza na uponyaji. Uwepo wa mwinjilisti katika makanisa ya mahali pamoja ni muhimu sana kwa sababu upako alionao huwahamasisha Wakristo na kuwatia moyo kuishiriki Habari Njema ya Yesu Kristo.

Kama mchungaji anayejali kondoo zake, Mchungaji huwachunga, huwalisha na kuwalinda watu wa Mungu. Upako wake humpa mamlaka ndani ya kanisa la mahali pamoja, lakini kamwe haitumii hii mamlaka kuwakandamiza wazee wenzake au Wakristo walio chini yake.

Mwalimu ametiwa mafuta ili kujenga juu ya msingi uliowekwa na mitume na manabii kwa kuwasilisha fundisho la ki-Biblia la Kristo kwa uwazi na usahihi. Hufurahia kuyapekua Maandiko kwa kina, na upako alionao humwezesha kuiwasilisha kweli ya Mungu Kanisani.

Huduma Tano kamwe hazifungamani na huduma huria. Wanaotumika katika Huduma Tano wote ni sehemu ya uongozi wa kanisa la mahali pamoja na wote hufanya kazi pamoja katika umoja ili watakatifu wanufaike na pako zote tofauti na waandaliwe kwa kazi ya huduma.

8

Sura ya II

Mtume

Huduma ya Utume ni miongoni mwa huduma tano zilizotajwa katika Waefeso 4 zinazolikamilisha Kanisa, na ni huduma muhimu mno katika Mwili wa Kristo. Neno ‘Mtume’ tafsiri yake ni ‘aliyetumwa’, ikimaanisha Mtume ni mjumbe au balozi wa Yesu Kristo.

Mtume si mtu anayetumika katika uhuru wake mwenyewe, bali kama ilivyo kwa Mchungaji, Mwinjilisti, Nabii na Mwalimu, yeye ni sehemu ya baraza la wazee wa kanisa la mahali pamoja. Yeye hutumwa na kanisa hilo kwa kazi maalum, na mara arudipo hutoa hesabu ya kazi aliyofanya. Hivyo basi, Mtume huunda sehemu ya timu ya utumishi ya kanisa la mahali pamoja; hujitiisha chini ya baraza la wazee na hufanya kazi kwa kushirikiana na zile huduma nyingine nne. Kwa kadiri ya uongozi wa neema ya Mungu, kila upako wa kila huduma katika Huduma Tano hubeba mamlaka tofauti. Kwa mujibu wa Biblia, ni wazi kwamba Mtume hubeba mamlaka ya rohoni iliyo kuu zaidi kuliko huduma hizo nyingine, kutokana na ukweli kwamba hiyo ni sehemu ya upako alioupokea.

Mteule wa MunguHatuna mfano mzuri zaidi wa Huduma ya Kitume na upako unaoambatana nayo katika Kanisa la Agano Jipya, kuliko Paulo mwenyewe. Tunapoyachunguza maisha yake na huduma yake, tunaiona mamlaka ambayo Mungu mwenyewe alimpa kwa ajili ya kulijenga Kanisa. Huu upako ulishuhudiwa na kukubalika kila mahali alipoihubiri Injili ya Yesu Kristo. Lakini, pamoja na mamlaka aliyokuwa nayo, hakuwa dikteta, bali alijenga mahusiano. Ni lazima ieleweke ya kwamba upako wa Kitume ni lazima utambuliwe kwanza na baraza la wazee, lakini pia na watu wa Mungu kwa ujumla. Si kitu kinachoweza kubuniwa; na wala hauwezi kuwa juu ya mtu anayetafuta hicho cheo kwa matakwa yake binafsi.

Ujumbe wa KitumeHuu upako hudhihirishwa kwanza kabisa na ufunuo wa Injili aliyoipokea Mtume. Huduma ya Kitume haiwezi kutenganishwa na Injili ambayo Kristo aliwafunulia Paulo na Mitume wengine. Katika Wagalatia 1:11-12, Paulo anasema ya kuwa ufunuo wa Injili aliyoihubiri ulitoka moja kwa moja

9

kwa Yesu Kristo. Si kitu alichopokea kutoka kwa mwanadamu, na wala hakufundishwa. Na katika Waefeso 3, ananena juu ya ufahamu wake katika siri ya Injili ambayo ilifichwa tokea mwanzo, bali sasa imefunuliwa na Roho kwa Mitume na Manabii.

Ni nini alichohubiri Paulo? Ni ufunuo upi aliopokea kutoka kwa Bwana? Katika 1 Wakorintho 2:2, anasema: “Maana naliazimu nisijue neno lolote kwenu ila Yesu Kristo, naye amesulibiwa.” Katika 1 Wakorintho 3:10, anaandika kwamba kwa neema aliyopewa na Mungu, ameweka msingi kama mjenzi mkuu. Msingi wa kweli wa maisha ya Ukristo si imani yetu kwa Kristo tu, bali pia ni kujifananisha naye katika mateso yake, kifo chake na kufufuka kwake. Hiki ndicho kiini cha Ukristo... Injili ya Kitume, ujumbe wa msalaba, ambao Paulo aliuelezea kuwa ni “nguvu ya Mungu!” Kwa hivyo, si kile tu tunachoamini kilicho cha muhimu, bali ni pamoja na maisha tunayoishi. Ilikuwa dhahiri kwa makanisa yote kwamba Paulo aliishi kile alichokihubiri. Hakuna neno alilosema au kuandika lililopingana na namna alivyoenenda yeye mwenyewe.

Ufunuo wa Injili hii ni ishara madhubuti ya Huduma ya Kitume, kwa sababu ndio msingi wa mpango mkamilifu na pekee wa Mungu kwa Kanisa lake, na kwa huo mitume wanalijenga Kanisa. Hii ndio maana msingi unapowekwa kanisani na Mtume, Wakristo hupata uelewa wa kile Mungu alichowaitia maishani mwao; kwa sababu mwito huo unakuwa dhahiri na wanakuwa na mfano wanaoweza kuuiga.

Mitume wa siku za leo ni lazima wapokee na kuuhubiri ufunuo ule ule kama Paulo. Bwana mwenyewe atawaangazia nuru wale aliowaitwa kwenye huduma hii na kuwafunulia ile siri ya Injili ya utukufu wa Yesu Kristo.

Baba wa KanisaUthibitisho mwingine muhimu wa Huduma ya Kitume ni uhusiano wa kiroho kati ya mtume na uongozi wa kanisa anapotumika, pamoja na watu wa Mungu. Hili linadhihirika katika kitabu cha Matendo ya Mitume na katika nyaraka za Paulo. Katika 1 Wakorintho 4:15, Paulo anaandika: “Ijapokuwa mna waalimu kumi elfu katika Kristo, walakini hamna baba wengi. Maana mimi ndimi niliyewazaa katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili.” Anawaambia wazi wazi kwamba ijapokuwa wengine wengi wanaweza kuwa wamekuja kuwashuhudia habari za Yesu, yeye ndiye aliyewazaa katika Injili. Hazungumzii kule kuzaliwa upya na Roho, ila anazungumzia msingi aliouweka maishani mwao kupitia ufunuo wa Injili. Tunamwona Paulo akinena kwa ujasiri katika 1 Wakorintho 16:1 kwamba kanisa la Korintho lilipaswa kufanya kile alichoyaagiza makanisa ya Wagalatia kufanya kuhusu changizo kwa ajili ya watu wa Mungu. Yeye hakuwa

10

mchungaji wa lile kanisa, lakini alikuwa na uhuru wa kuwaambia kuhusu suala hilo kwa sababu ya uhusiano aliokuwa nao katika Roho. Walijitiisha chini ya upako wa Kitume uliokuwa juu ya maisha ya Paulo, na huu upako ndio uliompa mamlaka ya kuwatangazia mapenzi yote ya Mungu. Mfano mwingine wa hili ni katika uhusiano wa Paulo na Wakristo wa Makedonia. Hili linatuthibitishia kwamba Mtume ni baba kwa makanisa anayofanya nayo kazi.

Utii na mamlakaTunaona utii ule ule kwa mamlaka ya Kitume katika mioyo ya watumishi wa Mungu, ambao walitambua upako uliokuwa juu ya maisha ya Paulo na wakajenga mahusiano imara na ya kudumu naye katika Roho. Katika 1 Wakorintho 4:17, Paulo anaandika: “Kwa sababu hii nimemtuma Timotheo kwenu, aliye mwanangu mpendwa, mwaminifu katika Bwana, atakayewakumbusha njia zangu zilizo katika Kristo, kama vile nifundishavyo kila mahali katika kila kanisa.” Paulo anamwita Timotheo mwanaye kwa sababu alimzaa katika Injili. Alikuwa na uhuru na ujasiri wa kumtuma Timotheo popote alipohitaji kumtuma, wakati wowote ule, kutokana na uhusiano wa kina uliokuwepo kati yao katika Roho. Katika Matendo 20, tunasoma pia juu ya uhusiano wa rohoni uliokuwepo kati ya Paulo na wazee wa kanisa la Efeso. Tunaweza kuhisi ya kuwa utii wao ulitokana na mahusiano yao ya rohoni. Upako wa Kitume ndicho chombo kilichoyaunganisha makanisa ya Agano Jipya.

Mlinzi wa fundishoMtume pia ni mlinzi wa fundisho. Tunamuona Mtume Paulo mara nyingi akiitetea Injili aliyoipokea na kuiishi. Pia, aliyaonya makanisa mara kwa mara dhidi ya mafundisho ya uongo yaliyokuwa yakiwakabili. Kukosekana kwa Mitume wa kweli siku hizi kumesababisha mafundisho mengi ya uongo na ghiliba za misisimko kuweza kuingia na kuota mizizi Kanisani. Ufunuo anaouleta Mtume, upako ulioambatana na huduma yake, pamoja na kielelezo cha maisha yake, vyote huleta ulinzi na uimara katika maisha ya watu wa Mungu. Mtume hubeba moyo mnyenyekevu kwa kuwa amejifananisha na mateso na kifo cha Kristo. Hivyo, Paulo aliweza kusema, “Nifuateni mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo”.

11

Sura ya III

Upako wa Kinabii

Upako wa Kinabii ni mojawapo ya huduma tano zinazolikamilisha Kanisa Mungu alizowapa wanadamu ili kuwafikisha Wakristo katika utu uzima rohoni. Tafsiri rahisi kabisa ya nabii ni kwamba yeye ni msemaji kwa niaba ya Mungu. Kwa kuvuviwa na Roho Mtakatifu, anatoa mwongozo wa kiroho kwa Kanisa, pamoja na kulirudi pale inapolazimu.

Utofauti kati ya karama ya unabii na Huduma ya KinabiiWakristo siku hizi wamekuwa mara nyingi wakiielewa Huduma ya Kinabii kwa nija isiyo sahihi. Wamekuwa wakizingatia eneo moja tu: madhihirisho ya karama za Roho, kama vile unabii, neno la hekima, na neno la maarifa. Lakini, tunahitajika kuwa na picha ya wazi zaidi juu ya maana ya Huduma ya Kinabii na umuhimu wake kwa watu wa Mungu.

Mtume Paulo anatuhimiza sote tuzitamani karama za rohoni hususan karama ya kuhutubu au kutabiri, ingawa ni dhahiri kwamba si kila Mkristo anayetabiri ni nabii. Ni muhimu sana tulielewe hili, kwa sababu kuna watu wengi leo hii wanaojitangaza wenyewe kuwa ni manabii kwa sababu tu walishawahi kutabiri. Wale mabinti wanne wa Filipo mwinjilisti hawakuwa Manabii, ijapokuwa walikuwa wakitabiri (Matendo 21:8-9). Nabii hutumika katika karama za rohoni pia, lakini kutokana na upako na mamlaka aliyopewa na Mungu, yeye hufunua mambo kwa uwazi zaidina huleta ufahamu mkuu zaidi wa rohoni, ambao Mungu huutumia katika kulijenga na kuliimarisha Kanisa.

Upako wa kinabii kwenye Agano la KaleKatika Agano la Kale, mojawapo ya mambo makuu katika huduma ya kinabii ilikuwa ni kuigeuza mioyo ya watu wa Mungu ili wamrudie kwa njia ya toba. Katika 2 Samuel 12, tunasoma jinsi Mungu alivyomchagua nabii Nathani amkabili Mfalme Daudi juu ya dhambi yake. Neno la unabii kutoka kwa Nathani halikumhukumu Daudi; badala yake lilizaa moyoni mwake hali ya huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu na toba ya kweli. Hii sura ya mamlaka ya Mungu hudhihirika zaidi kupitia upako wa Kinabii.

12

Nabii wa Agano la Kale aliwaonya watu wa Mungu kusudi waweze kuepuka hukumu ya Mungu. Neno la unabii lilikuja moja kwa moja na kwa njia ya wazi, na liliwadhihirishia hali za mioyo yao. Mungu aliwatia mafuta manabii mbalimbali ili wafikishe ujumbe usiokuwa na majadiliano, ambao ulikuja kwa uthibitisho mkubwa pamoja na hofu ya Mungu. Nabii ‘alipopiga panda’, watu walijua kwamba Mungu alikuwa amemaanisha katika kile alichotaka kusema. Kwa bahati mbaya, hata nyakati zile, mara nyingi watu waliifanya mioyo yao kuwa migumu dhidi ya Neno la Mungu.

Upako wa Kinabii katika Agano JipyaTunahitajika tuelewe ya kwamba Nabii wa kweli hatabiri tu mambo mazuri. Upako wa Kinabii unapaswa ulete hofu ya Mungu Kanisani, kwa sababu unaifunua dhambi na kuitangaza njia ya utakatifu na utakaso.

Katika Agano Jipya hatuna mfano bora zaidi wa huduma ya Kinabii kuliko ule wa Yesu mwenyewe. Katika Mathayo 3:12, Yohana Mbatizaji anatamka: “Ambaye pepeto lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake; na kuikusanya ngano yake ghalani, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.” Yesu alikuja akihubiri ujumbe wa toba, utakaso, kutengwa na hukumu, lakini daima alifanya hivyo kwa moyo uliojaa neema na upendo.

Katika Mathayo 21:12-13, tunamwona Yesu akiudhihirisha tena upako wa Kinabii pale alipowakuta watu wakiuza na kununua hekaluni. Hasira yake takatifu iliwaka na akachukua kikoto na kuwatoa nje wafanyabiashara hao. Hapa kuna eneo la huduma ya Kinabii ambalo mara nyingi halieleweki vizuri. Ijapokuwa alijidhihirisha kwa njia hii, Bwana bado alikuwa akienenda katika neema na upendo, kwani ilikuwa ni lazima kuwakabili na kuwakemea wale waliokuwa wakiitumia nyumba ya Mungu kama soko. Mungu huchagua kunena kwa njia tofauti, lakini kamwe moyo wake haubadiliki. Yeye ni Mungu wa upendo na rehema, lakini pia ni Mungu wa haki na kweli, ambaye sifa za utakatifu wake zinadhihirishwa hapa kupitia upako wa Kinabii.

Nabii ameitwa kufanya kazi maalum sana ya utakaso Kanisani katika siku hizi za mwisho, kwa sababu hakuna huduma nyingine inayoweza kulitekeleza hilo. Palipo na dhambi, Nabii wa kweli ataitangaza pasipo woga wowote; lakini kamwe hatafanya hivyo katika mamlaka ya kimwili. Kwa maana hiyo, Kanisa halitajihisi kuhukumiwa adhabu, bali litauhisi moyo wa Bwana ukiwaongoza kutubu. Wakati unakuja ambapo Manabii wataleta mwanga palipo na giza na kuyafunua makusudi ya moyo yaliyofichika, kwa sababu upako wa Kinabii huleta hali ya utakaso na kutengwa na dunia katika mioyo ya Wakristo.

13

Mtume na NabiiKatika Agano Jipya, twaweza kuona eneo lingine muhimu linalohusu upako wa Kinabii katika Waefeso 2:20. Kupitia maisha ya Paulo na Barnaba tunaona wazi wazi kwamba Nabii hufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu sana na Mtume katika kuuweka msingi wa Kanisa. Huduma hizi mbili hubeba mamlaka kuu zaidi katika roho kuliko huduma zile nyingine tatu. Mtume hupokea na kuuleta ufunuo wa Kristo, naye Nabii huhakikisha ya kwamba Kanisa linasimama katika kweli na linaenenda katika fundisho la uzima.

Nabii ni Mjumbe wa baraza la Wazee Wanadamu wanaweza kujitwalia utukufu mwingi pindi Mungu anaponena na kutenda kupitia wao. Hii ndio sababu kujitiisha na kuwajibika chini ya baraza la wazee katika kanisa la mahali pamoja ni ulinzi madhubuti dhidi ya matumizi mabaya ya upako wa Kinabii. Tofauti na tulivyozoea kuona Kanisani katika siku za leo, manabii wanapaswa wawe sehemu ya uongozi wa Kanisa la mahali pamoja na watumwe kutoka hapo kama ilivyo kwa huduma nyingine. Katika Matendo 15, tunasoma jinsi Manabii, Yuda na Sila, walivyotumwa kutoka katika Kanisa la Yerusalemu kuongozana na Paulo na Barnaba walipokuwa wakirudi Antiokia. Ikiwa mtu hajaungwa na timu, ila ana huduma yake yenye uhuru binafsi, anaweza kujificha nyuma ya wito wake na kutenda mambo katika mamlaka yake mwenyewe. Anaweza kusema lolote atakalo, na hatakuwa na mtu wa kumsemea maishani mwake. Lakini Nabii anapokuwa ni sehemu ya timu, anawajibika kwa kile anachosema na katika namna anavyoenenda. Atakubali kukemewa na kukabiliwa katika kweli na neema. Maisha yake yatakuwa ni kitabu kilicho wazi kwa wazee wa kanisa na kwa watu wa Mungu.

Nabii wa kweli au wa uongo?Biblia inatuonya waziwazi ya kwamba siku za mwisho kutakuwepo na manabii wengi wa uongo watakaowapotosha watu kwa kuzisisimua tamaa zao za dhambi. Lakini Mungu pia anainua Manabii wa kweli watakaokuwa vielelezo kwa Kanisa; na upako ulioko juu yao utaleta ulinzi madhubuti kwenye maisha ya Wakristo. Hawa hawatajawa na kiburi na majivuno kwa kuutegemea uwezo wao wenyewe. Badala yake watakuwa wanyenyekevu, wenye roho zilizovunjika na mioyo iliyopondeka, huku wakiwa tayari kujikana nafsi zao, kuuchukua msalaba wao na kumfuata Yesu. Watatambulikana kutokana na kujifananisha kwao na mateso na kifo cha Kristo, na watabeba manukato ya maarifa ya Kristo. Wakati wa huduma zenye uhuru binafsi umekwisha, kwani katika siku hizi za mwisho Mungu anarejesha utaratibu katika Kanisa lake kupitia upako wa Kinabii.

14

Sura ya IV

Mwinjilisti

Mwinjilisti anafahamika kama sehemu ya Huduma Tano, na amewekwa Kanisani kwa kusudi maalum sana. Hata hivyo, hatuna budi kutofautisha kati ya uinjilisti, ambao ni jukumu la Kanisa lote (Matendo 11:19), na huduma ya Mwinjilisti, ambaye ametiwa mafuta na Mungu ili atangaze kile Yesu alichokamilisha msalabani kwa kusudi la kuwafikisha watu kwenye toba na wokovu.

Zaidi ya hayo, panaonekana kukosekana ufahamu, au ufunuo, juu ya huduma ya Mwinjilisti Kanisani leo, na dhana iliyopo ni kwamba Mwinjilisti ni mtu anayetembea huku na huko akiwaleta watu kwa Kristo. Hii ni dhana potofu inayohitajika kurekebishwa, kwani wainjilisti wengi wanaozungukazunguka huku na huko wanaishia kutokuwajibika kwa mtu yeyote, huku huduma zao zenye uhuru binafsi mara nyingi zikiwafanya wajihisi kufarakana na Wakristo wengine, wapweke na waliovunjika moyo.

Hata hivyo, mambo matatu yako dhahiri katika Maandiko; kwanza kabisa, Mwinjilisti huunda sehemu ya baraza la wazee wa kanisa la mahali pamoja; pili, daima yeye hutumwa kutoka katika kanisa hilo kwenda kutendea kazi kipawa chake nje ya Kanisa, kwa wasiookoka; na mwisho, analo jukumu la kuwakamilisha watakatifu katika kanisa hilo la mahali pamoja. Kwa maana hivyo tunaelewa ni kwa nini upako wa Mwinjilisti ni muhimu katika kuwajenga Wakristo katika kanisa la mahali pamoja.

Huduma inayotenda kazi kama sehemu ya timuIjapokuwa Mwinjilisti hatajwi mara nyingi katika kitabu cha Matendo ya Mitume, mifano tuliyonayo inaonyesha kwamba aina ya huduma huru zilizoko siku za leo, hazikuwepo enzi hizo. Filipo alikuwa Mwinjilisti maarufu aliyetajwa katika Matendo 21:8. Tunaiona huduma yake ikitenda kazi katika Matendo 8:5 alipokuwa akihubiri Habari Njema za Kristo. Tunachokiona wazi katika Matendo 8:14 ni namna Mwinjilisti anavyofanya kazi kwa kushirikiana na huduma nyingine. Petro na Yohana waliposikia kile kilichotokea baada ya Filipo kuhubiri katika Samaria, walijisikia huru kwenda kumuunga mkono.

15

Filipo, ambaye alitokea katika kanisa la Yerusalemu, aliukubali kwa furaha, mchango wa rohoni ulioletwa na Mitume hawa, ambao walikuwa wazee katika Kanisa lile lile ambalo naye alikuwa mzee. Kulikuwepo na umoja wa dhati kati ya hizi huduma tofauti zilipofanya kazi pamoja kwa manufaa ya Ufalme wa Mungu. Filipo hakuwa na nia ya kuanzisha kanisa jipya la watu aliowahubiri. Kinyume chake, alibaki kuwajibika kwa timu iliyomtuma. Alikuwa huru kumtii Roho Mtakatifu, na wakati huo huo akiwa amejitiisha chini ya baraza la wazee, jambo lililokuwa ni usalama mkubwa kwake. Alifahamu ya kuwa alikuwa ni sehemu ya timu ambamo kila mmoja alikuwa tayari kuutoa uhai wake kwa ajili ya wenzake.

Kuishiriki neema ya Mungu kwa waliopoteaKama ilivyo na huduma nyingine zote katika Huduma Tano, zilizotolewa na Yesu ili kuwakamilisha watu wake, Yesu mwenyewe ndiye mfano wetu bora. Tunasoma katika Isaya kwamba alitumwa “kuwahubiri maskini Habari Njema”. Huu ndio mfano wa juu wa upako unaobebwa na Mwinjilisti. Unampa shauku inayowaka ya kutaka kuwafikia waliopotea na kuwahubiri Habari Njema za Kristo, ili kwamba wengi iwezekanavyo wapate kuokolewa. Anapohubiri hana haja ya kuzama katika maelezo ya kitheolojia au mafundisho yenye elimu, bali huhubiri juu ya mateso, kifo na kufufuka kwake Kristo kwa madhihirisho ya nguvu za Roho Mtakatifu, ambapo watu huchomwa mioyo, hutubu na kumgeukia Yesu. Kupitia upako alio nao, watu watahisi upendo na neema ya Mungu kwao. Kamwe, hawatahisi kuhukumiwa, kushutumiwa au kulaghaiwa. Hii ndio sababu ujumbe wa msalaba ni muhimu sana kwa Mwinjilisti, kwa sababu msalaba wa Bwana wetu Yesu ndio unaodhihirisha wingi wa upendo wa Mungu kwetu sisi.

Kuleta tobaMwinjilisti wa kweli pia anafahamu kwamba kutakaswa ili mtu aokolewe na kutakaswa kutokana na dhambi zake, toba ni ya muhimu; si mwitikio wa juu juu tu wa kumkaribisha Yesu moyoni. Katika Matendo 2, Petro alihubiri ujumbe rahisi wa Msalaba wa Kristo. Wayahudi waliposikia maneno yake walichomwa mioyo yao, wakalia, “Tutendeje, ndugu zetu?” Petro hakuwaambia, ‘Mwalikeni Yesu mioyoni mwenu’. Hapana! Alisema, “Tubuni...” Kupitia upako huu na ujumbe unaohubiriwa, Roho Mtakatifu anaweza kuwaleta na kuwafikisha watu kwenye toba.

Kuwaandaa WakristoZaidi ya hayo, kwa mujibu wa Waefeso 4:11-13, Mwinjilisti ana nafasi muhimu sana katika kuwakamilisha watakatifu. Kama tulivyoona hapo

16

juu, ana wajibu katika kanisa la mahali pamoja, na pia anao wajibu kwa ulimwengu. Kwa maana hiyo, dhana waliyo nayo Wakristo wengi kwamba yeye ni wakala huru wa Bwana ambaye kazi yake ni kurandaranda huku na huko si sahihi, kwani atakuwa na manufaa gani kwa kanisa la mahali pamoja ikiwa kamwe hakai hapo? Anapaswa kuwa na uwezo wa kuwavuvia watu wa Mungu shauku ya kuleta roho za watu kwa Yesu na kuwaonyesha umuhimu wa kushiriki upendo wa Bwana na wengine. Kumshuhudia Yesu kwa watu ni ishara mojawapo ya ukomavu wetu rohoni, na katika hili, Mwinjilisti huchangia katika ukuaji wa kila Mkristo. Tunapaswa tuutambue umuhimu wa huduma hii katika Kanisa, kama ilivyo kwa huduma nyingine zilizoko katika Huduma Tano.

Hutumwa na kanisa kuuendea ulimwenguNi wazi, bila shaka, kwamba Mwinjilisti wa kweli anapaswa kutoka, aende nje! Yeye yuko huru kwenda popote Bwana amuongozapo, kutokana na mahusiano, utii na hali ya kuaminiana vilivyopo kati yake na wazee wenzake. Kwa kuwa hutumwa na kanisa la mahali pamoja, anajua ya kwamba wazee pamoja na kanisa wako nyuma yake, na mara anaporudi, hutoa hesabu ya utumishi aliouendea.

Huambatana na miujizaIshara madhubuti ya Mwinjilisti wa kweli ni kwamba ujumbe wake utaambatana na miujiza na uponyaji kama udhihirisho wa nguvu za Mungu. Watu wanapoona nguvu za Roho Mtakatifu zikidhihirishwa kupitia miujiza, imani huzaliwa mioyoni mwao na wengi huamini kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu na Mwokozi wao. Kwa maana hiyo, kutokana na wajibu alionao, ni muhimu kwamba maisha ya Mwinjilisti yawe kielelezo cha mtu aliyejitoa kwa Kristo kwa ajili ya Kanisa.

17

Sura ya V

Mwalimu

Miongoni mwa huduma tano ziwakamilishao watakatifu zilizotajwa katika Waefeso 4:11, Mwalimu ametiwa mafuta na Mungu ili awasilishe kweli za Neno la Mungu zenye kina na za kudumu kwa watu wa Mungu. Jukumu lake sio kujaza fahamu za Wakristo ujuzi wa ki-akili, bali katika kufundisha kwake, anamruhusu Roho Mtakatifu aandike Neno la Mungu katika vibao vya mioyo yao.

Kuna wachungaji wengi wenye shahada, na shahada za uzamili katika theolojia, ambao wamekuwa wakifundisha theolojia kwa miaka mingi, lakini hawana cha kujivunia kwa taabu yao. Kwa bahati mbaya sana, wengi wao leo hii wamefikia ukingoni, kwa sababu maarifa yao yote hayakuwa na nguvu ya kubadilisha utumishi wao kwa Mungu, wala maisha yao, wala ya waumini wao. Baadhi yao hata wanatafuta kuikimbia huduma.

Ufundishwaji wa Neno ni sehemu ya agizo Yesu alilowapa wanafunzi wake katika Mathayo 28:19-20: “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Lengo la kufundisha sio tu kuwapa Wakristo ujuzi wa Biblia bali, zaidi ya yote, ni kuwafikisha katika utu uzima rohoni.

Kuungwa na huduma nyingineMwalimu kamwe hapaswi kusahau onyo la Mtume Yakobo (3:1) kwamba atahukumiwa kwa hukumu kuu zaidi kuliko wengine. Kuna idadi isiyohesabika ya ‘walimu’ siku hizi Kanisani, watu waliojiteua wenyewe, mahuru - wakiandika vitabu, wakirusha vipindi katika televisheni, wakitangaza mafundisho yao kwenye DVD na CD, wakiandika makala kwenye mitandao, na wakitumia kila njia iwezekanayo kuufikia umma wa Wakristo. Hawajapata kuwepo walimu wengi kama ilivyo leo. Hata hivyo, muundo tunaouona katika Biblia ni kwamba Walimu huunda sehemu ya baraza la wazee wa kanisa la mahali pamoja (Matendo 13:1). Na kama ilivyo kwa huduma zile nyingine nne, si lazima kabisa kabisa mwalimu awepo katika kila kanisa la mahali pamoja, lakini kila kanisa linapaswa kuwa sehemu ya mtandao wa makanisa ambamo huduma hizi zote tano

18

zinawakilishwa. Mwalimu anapokuwa sehemu ya uongozi wa kanisa la mahali pamoja, atatumwa kwa makanisa mengine wanaofanya nayo kazi pamoja, na hivyo atafanyika baraka kwa kila moja. Kwa njia hii, anapotumika, anakuwa si mgeni mwalikwa anayetegemea sifa zake na kutoa taarifa mbalimbali za Biblia kwa kanisa, huku akiwa hana uhusiano wa kweli na watu. Kinyume chake, kupitia injili ya kitume, Mwalimu huungwa na huduma nyingine, hubeba moyo ule ule kwa watu wa Mungu, na anafahamu umuhimu wa kujenga mahusiano.

Kufundisha mafundisho yenye uzimaMara mtume anapoweka msingi Kanisani kwa kuyahubiri mafundisho yenye uzima ya Kristo, mwalimu aliyetiwa mafuta anaweza kujenga juu yake (1 Wakorintho 3:10) kwa kuwa yeye anawasilisha Neno kwa ufafanuzi wenye kina kuliko huduma zile nyingine. Mwalimu anapokuwa amejitiisha chini ya baraza la wazee la kanisa la mahali pamoja, watu wa Mungu hulindwa dhidi ya mafundisho ya uongo.

Huuwasilisha moyo wa MunguTuna mfano ulio mkamilifu wa huduma hii katika utumishi wa Yesu Kristo. Kabla ya Yeye kuja, Mafarisayo walikuwa ndio walimu wa Sheria. Mafundisho yao hayakuwa na upako, na kwa hivyo hayakuweza kuleta mabadiliko katika mioyo ya watu. Lakini wote waliomsikiliza Yesu walishangazwa na mamlaka aliyofundisha nayo, na walikusanyika kwa wingi kumsikiliza. Mafarisayo waliwasukumizia watu mbali, kwa kuwa walitafuta tu kuyakosoa maisha ya watu, lakini Yesu aliudhihirisha moyo wa Baba yake, na maneno yake yaliwavuta watu. Ingawa alichofundisha kiliwapa changamoto na kuwakabili wasikilizaji wake, hata hivyo walitambua ya kwamba alizungumza maneno yenye uzima (Mathayo 7:28-29).

Kuwaongoza Wakristo katika kuuchuka msalaba waoUpako ulio juu ya Mwalimu humsababisha kuchimbua Maandiko kwa kina, ili kuifichua hazina iliyofichwa humo. Yeye mwenyewe hutamani sana aangaziwe, makusudi aweze kuwapa watu wa Mungu mafundisho yenye uzima. Maisha ya mwalimu na mafundisho yake ni lazima yajengwe juu ya msingi wa ujumbe wa msalaba, ambao ni nguvu ya Mungu kwa wale wanaoamini. Kwa maana hiyo, atatambulikana kwa uwezo wake wa kuwaimarisha Wakristo juu ya msingi huo. Inapofanyika katika roho sahihi, huduma ya Ualimu huwaongoza watu wa Mungu moja kwa moja katika kujikana nafsi zao, kuuchukua msalaba wao na kumfuata Yesu.

19

Kuyaacha mafundisho ya uongoMojawapo ya hatari kubwa katika huduma ya mwalimu ni kwamba kiu yake ya kutafuta hazina iliyofichika katika Neno la Mungu inaweza kumuondoa katika njia ya kweli na kumwingiza katika ukengeufu. Hivyo ndivyo mafundisho ya uongo yanavyoingia Kanisani. Biblia mara nyingi inataja juu ya walimu wa uongo na kuwaonya watu wa Mungu dhidi yao. Tito 1:10-11 inatahadharisha dhidi ya watu wenye maneno matupu na waongo, wanaofundisha mambo wasiyopaswa kufundisha kwa ajili ya mapato ya aibu. Watu wa jinsi hiyo huwadanganya watu wa Mungu. Baadhi yao, kutokana na mambo fulani fulani waliyoyapitia maishani mwao, hujenga mafundisho ya uongo, ambayo si kitu kingine isipokuwa ni imani potofu ziletazo uharibifu.

Wengine mistari michache ya Maandiko na hivyo huunda fundisho kutokana na hilo. Lakini hatuwezi kuchukua jambo fulani ambalo Mungu ametupitisha, na kulifanya kuwa fundisho la Kristo, na wala hatuwezi kujenga kitu juu ya mstari mmoja wa Biblia. Lakini tumeshuhudia haya mambo yakifanyika kwa wingi zaidi katika miaka ya hivi karibuni. Kwa upande mwingine, msalaba unapokuwa ndio msingi wa fundisho husika, watu wa Mungu wanakuwa salama, na hawatadanganyika!

Huduma zote tano zinapofanya kazi kwa pamoja, utumishi kamili wa Kristo kwa Kanisa lake unafunuliwa. Mahusiano ya rohoni kati ya hizi huduma huleta usalama kwa watu wa Mungu, kwa kuwa huzuia kila upepo wa mafundisho yatokanayo na hekima za wanadamu kujipenyeza Kanisani. Kanisa linahitaji huduma hizi zote tano ili liweze kuufikia utu uzima rohoni, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo, ambalo linapaswa kuwa ndilo lengo lake. Ni kwa manufaa ya watu wa Mungu wafahamu ni neema ya ajabu kiasi gani inayowakilishwa Kanisani na hizi huduma zinapofanya kazi katika umoja!

20

Sura ya VI

Mchungaji

Tumeiacha hadi mwisho huduma inayofahamika kuliko zote kati ya huduma tano zinazolikamilisha Kanisa - Mchungaji. Neno ‘Mchungaji’ linatokana na maneno ya Kiyunani ‘episkopos’ na ‘episkopeo’ ambayo yanazungumzia kuchunga, kulinda, kutunza, kuongoza, na kulisha. Kwa maneno mengine, Mchungaji pia angeweza, na mara nyingi huitwa, ‘Mchungaji wa kondoo’.

Moyo wa mchungajiManabii mbalimbali wa Agano la Kale - Isaya, Yeremia, Ezekieli na Amosi mara kwa mara walinena kwa niaba ya Mungu, tena kwa ukali, kuhusu wachungaji. Lakini tunauona mfano mkamilifu wa Mchungaji Mwema katika Yesu Kristo, ambaye alisema kwamba mchungaji wa kweli huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.

Haiwezekani kuzungumzia mwito, upako na wajibu wa Mchungaji pasipo kutumia mifano ya kundi, kondoo na mchungaji. Ndani ya wito wa Mchungaji kuna moyo unaojali ‘kundi’, yaani, Wakristo walioko chini ya uangalizi wake. Katika maongezi yake na Petro (Yohana 21:15), tunaona ya kwamba, kabla hajapaa kwenda mbinguni, Yesu alitaka kuhakikisha ya kwamba Kanisa la Agano Jipya lingebaki mikononi mwa watu waliojua na kuufahamu mwito wao, na waliokuwa na moyo kwa ajili ya kundi. Alitafuta, si tu watu ambao wangefanya kazi kwa ajili ya ufalme wa Mungu katika kuhubiri na kufundisha, bali alitafuta watu ambao wangewapenda watu wake na kuwalisha. Kulisha kondoo kunahusikana na kuwatakia kilicho bora zaidi, kuwachunga, kuwapenda, kuwaonya, na kuwaongoza kwa moyo wa Yesu.

Huduma inayounda sehemu ya uongozi wa kanisa la mahali pamojaMchungaji ni mojawapo ya huduma tano ambazo daima huunda sehemu ya baraza la wazee wa kanisa katika la mahali pamoja. Anaheshimika kutokana na mamlaka wito wake unaobeba rohoni; huduma yake si huduma huria. Ijapokuwa wachungaji wote ni wazee wa kanisa, wazee wote si wachungaji, wala hawajaitwa wote katika utumishi wa Huduma Tano.

21

Kwa sababu hiyo, wazee wenzake hawana sababu ya kumhusudu; kinyume chake, wataikubali nafasi au wajibu Mchungaji alio nao katika kanisa husika kwa kuwa wanauhisi huu wito na upako wa Mungu ulio juu ya maisha yake. Hata hivyo, ni muhimu sana kwamba asiwakandamize wazee wengine na kuwafanya vibaraka wa kuitikia ‘Ndiyo’ kwa kila kitu bila kuhoji. Hana mamlaka rohoni ya kufanya hivyo. Hii ndio maana siku zote atatafuta kushirikiana na wazee wenzake katika kufanya maamuzi na atahakikisha yanapata idhini yao. Kwa maana iyo hiyo, kwa ajili ya usalama wake mwenyewe, na wa kanisa analolichunga, atapaswa kuwa tayari kuonywa na kukemewa na hao wazee, pale inapohitajika. Shauku ya moyo wake, makusudi ya nia yake, na maono yake sikuzote ni kuhakikisha kwamba yeye na wazee wanashirikiana katika kuutoa uhai wao kwa ajili ya watu wa Mungu. Mchungaji ana jukumu maalum katika hili: kwa maana ya kwamba yeye ndiye mwenye kuwatia moyo wazee wenzake katika hilo; ndiye mwenye kulinda na kumkumbusha kila mmoja juu ya maono hayo, muda wote. Kanisa zima huutambua na kuukubali mwito wa Mungu juu ya maisha ya Mchungaji. Maisha ya mchungaji yanapaswa kufahamika na watu, na wao wanapaswa wamruhusu ayafahamu yao. Tunapomuangalia Mchungaji tunapaswa tumwone mtu anayemtumikia Mungu na watu wake, sio mtu aliyebeba cheo tu.

Huduma iliyojitiisha chini ya MtumeEndapo kuna Mtume ndani ya baraza la wazee wa kanisa la mahali pamoja, ni wazi kwamba atakuwa na mamlaka kuu kuliko ya Mchungaji, vile vile Mchungaji naye alivyo na mamlaka kuu zaidi ya wazee wengine wa kanisa. Mchungaji anapaswa ajitiishe si tu chini ya baraza lote la wazee, bali pia chini ya Mtume, bila kujali kama huyo Mtume ni sehemu ya uongozi wa kanisa analohudumia Mchungaji huyo au anatoka katika kanisa lingine lililoko kwenye mtandao wa makanisa hayo, kama tunavyoona katika kitabu cha Matendo 20:17-36 na katika nyaraka za Paulo kwa ujumla.

Hatari ya mtu anayetumika peke yakeUpako ulioko juu ya Mchungaji ni tofauti na ule wa Mtume, Nabii, Mwinjilisti, au Mwalimu kwa kuwa umelilenga zaidi kanisa la mahali pamoja. Wakati huo huo, upako huu una mipaka yake, na hapa ndipo huja hatari kwa Wakristo. Makanisa mengi madogo madogo siku hizi yanaongozwa na mtu mwenye shauku ya kuwaongoza na kuwalea watu wa Mungu, lakini ambaye hana kabisa wito au upako wa Mchungaji; na mwingine anao wito lakini anatumika peke yake. Hajitiishi chini ya baraza la wazee alio nao, ama kwa sababu hajihesabu kuwa anapaswa kuwajibika kwa baraza lake la wazee; au kwa sababu yeye ndiye mzee wa kanisa pekee na kwa hiyo hulichunga kanisa lake mwenyewe. Wakati huo huo, hana kabisa uhusiano

22

23

na huduma nyingine zilizopo nje ya kanisa lake. Lakini tunapolikuta neno ‘wazee’ katika Agano Jipya, kila wakati ni katika wingi! (Matendo 14:23 & 20:17, Tito 1:5). Jambo la kusikitisha ni kwamba makanisa mengi leo hii yanaongozwa na wachungaji wanaoamini ya kwamba wana uwezo wao wenyewe wa kuwalisha watu wa Mungu chakula chote cha rohoni wanachohitaji. Hii ni hatari sana!

Inashangaza kuona kwamba katika Agano Jipya, kamwe hatuoni kanisa hata moja ambamo mwenye mamlaka pekee alikuwa ni mchungaji! Kinyume chake , tunaona humo kielelezo cha mahusiano yanayopaswa kuwepo ndani ya kanisa la mahali pamoja, na kati ya kanisa na kanisa. Hata kama kuna Mchungaji katika kanisa la mahali pamoja, hilo kanisa halipaswi kuwa peke yake na lenye uhuru binafsi. Vinginevyo, Wakristo wake watabakia kuwa watoto wachanga, kwa sababu chakula pekee wanachopata ni kutoka kwa mchungaji tu. Wametengwa kabisa na hawana ulinzi wowote, na hawawezi kunufaika na pako tofauti zilizomo ndani ya Huduma Tano. Makanisa yote ya Agano Jipya yalikuwa sehemu ya jamii moja; yote yalipokea mchango wa huduma zote tano, jambo lililowawezesha watu wa Mungu kukua, na kuandaliwa na kukamilishwa kiroho (Waefeso 4:11-13).

Ikiwa ufunuo wa injili na muundo wa Kanisa la Agano Jipya haviwasilishwi kwa njia ya waziwazi Kanisani, itakuwa vigumu kwa huduma za Kikristo kufanya kazi pamoja katika umoja wa Roho. Wachungaji wengi watabakia katika uhuru wao binafsi kwa kuhisi kutishiwa na huduma nyingine, na hawatajihisi salama. Lakini, kama ilivyo kwa huduma nyingine, siku moja Mchungaji naye atatoa hesabu ya jinsi alivyolichunga kundi la Mungu.

24

Contact us:

Botswana +267 74 52 57 50Kenya +254 719 370 389

Malawi +265 999 94 02 06 Mauritius +230 403 4500

Nigeria +234 802 798 4825South Africa +27 814 273 292

Tanzania +255 763 187 898Uganda +256 752 569 474Zimbabwe +263 92 87 693

HEAD OFFICETrianon, Mauritius

+230 403 4500 | [email protected]

Huduma Tano

Inasikitisha kuona Wakristo wengi wanaokiri uwepo wa Huduma Tano wakishindwa kuuona umuhimu wake au hata kuelewa namna hizi huduma zinavyopaswa kulihudumia Kanisa. Wengine wanapatwa na wasiwasi juu ya athari zake kwa huduma zao binafsi na wanaamua kuzifumbia macho. Lakini, pasipo kujali Imani ya mtu mmoja mmoja, ni wazi hakuna Mkristo mkweli atakayesema ya kwamba vipawa ambavyo Yesu anatoa kwa wanadamu katika kuliongoza na kuliandaa Kanisa lake vilikuwa ni kwa ajili ya Kanisa la Mwanzo tu. Kila kitu kilichoandikwa kwenye Agano Jipya kuhusu utendaji wa hizi huduma tofauti katika kulijenga Kanisa litahusika maadamu Kanisa lidumupo duniani. Roho yule yule aliyekuwepo wakati Kanisa linaanza, bado yuko kazini hata leo. Yesu hajabadilika.

Kristo angali anatoa huduma zile zile kama alivyofanya mwanzo, kwa kusudi lile lile: ili kwamba Mwili wa Kristo ujengwe na watu wake wakamilishwe katika Yeye. Enzi za Giza za Kanisa, hizi huduma zilipotea kwa muda kutokana na udunia na udini kulifunika Kanisa. Ila leo, Mungu anazirejesha hizi huduma na kuwarudisha watu wake kwenye msingi wa kweli, makusudi waufikie utu uzima rohoni na umoja wa Imani. Ndiyo maana hizi huduma, ambazo zinaweza kuunganishwa tu na ujumbe wa Msalaba, ni za kipaumbele kwa Kanisa.

9 789994 903009

ISBN 978-99949-0-300-9

Church Team Ministries International | Trianon, Mauritius(230) 403 4500 | [email protected] | www.ctmi.org

CTMI ni mtandao wa Kikristo usio rasmi ulioanzishwa mwaka 2001 na timu ya viongozi kutoka nchi mbalimbali barani Afrika waliounganishwa pamoja na ujumbe wa msalaba na kazi ya Mungu maishani mwao.

SWAHILI