ripoti ya kamati ya kuchunguza na kudhibiti · pdf fileubadhirifu wa fedha za serikali na...
TRANSCRIPT
1
RIPOTI YA KAMATI YA KUCHUNGUZA NA KUDHIBITI HESABU ZA SERIKALI
NA MASHIRIKA (P.A.C) YA BARAZA LA WAWAKILISHI, ZANZIBAR, 2012/2013.
SEHEMU YA KWANZA:
1.0 UTANGULIZI:
Katika Historia ya Kamati za Baraza la Wawakilishi tokea kuanzishwa kwake mwaka 1980,
Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za Serikali (P.A.C) imeanza kuwepo tokea mwaka
huo (1980), na katika kufanya kazi zake, pamoja na kuwa na majukumu mengi, jukumu maarufu
linalotarajiwa kuwanyiwa kazi kila mwaka ni kuchunguza na kutoa ripoti yake juu ya hesabu za
mwaka na matumizi ya fedha za Serikali na Mashirika yake na hesabu nyengine zozote
zitakazowasilishwa mbele ya Baraza kupitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali.
Kwa kawaida, ripoti hiyo ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu huwa ni moja kwa kila
mwaka, na imetokezea mwaka 2009/2010, Kamati ilifanyia kazi Ripoti tatu za Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa wakati mmoja, lakini mwaka huu, Kamati imefanyia
kazi Ripoti tano (Mbili za Ukaguzi wa Hesabu, na 3 za Thamani halisi ya fedha (value for
money) kwa pamoja.
Katika kuzifanyia kazi Ripoti hizo, Kamati imegundua namna Wizara na Taasisi mbali mbali za
Serikali zinavyotekeleza majukumu yao kwa mnasaba wa hoja mbali mbali zilizoripotiwa na
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu. Aidha, kuna hoja mbali mbali zimepata majibu, na
nyingi hazijapata majibu ya kuridhisha. Kibaya zaidi, Kamati imegundua kuwepo kwa
ubadhirifu wa fedha za Serikali na ubadhirifu na ufujaji wa mali za Taasisi hizo, huku Sheria ya
Fedha na Kanuni zake za mwaka 2005 pamoja na Sheria ya Manunuzi na Ugavi wa Mali za
Serikali na Kanuni zake, zinaendelea kuvunjwa. Hali hii inaisikitisha sana Kamati, ambayo kwa
muda mrefu sasa inaendelea kusisitiza haja ya kufuatwa kwa Sheria hizo ipasavyo.
1.1 MAJUKUMU YA KAMATI:
Kamati inatekeleza majukumu yake kwa mnasaba wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Sheria
Namba 4 ya mwaka 2007, Sheria Namba 12 na Sheria Namba 9 za mwaka 2005 (pamoja na
kanuni zao), na Kanuni za Baraza la Wawakilihi, Zanzibar. Kwa upande wa toleo la mwaka
2012, Kamati inatekeleza majukumu yake zaidi kupitia kanuni ya 118(2) ya Kanuni za Baraza,
ambayo hapa chini tunainukuu:
(a) Kuchunguza na kutoa taarifa juu ya hesabu za mwaka za matumizi ya fedha za Serikali na Mashirika yake na hesabu nyengine zozote zitakazowasilishwa mbele ya
Baraza kupitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
(b) Kuchambua na kutafakari ripoti yeyote ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu pale ambapo Rais aliagiza ukaguzi huo ufanywe.
2
(c) Kuchunguza kwa njia yeyote inayofaa mambo yote yanayohusu hesabu za Serikali na asasi zake.
(d) Kutoa Ripoti yake baada ya kufanya uchunguzi kuhusiana na matumizi ya ziada ya fedha iliyotolewa kwa mwaka wa fedha unaohusika.
(e) Kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Kamati yaliyotolewa kwenye Ripoti ya Kamati ya mwaka uliotangulia.
(3) Katika kufanya kazi zake Kamati ya PAC itakuwa na wajibu wa kuchunguza kama:
a. Fedha zilizooneshwa katika makadirio ya Matumizi ya Serikali na
Mashirika yake zimetumika kama iliyvokubaliwa;
b. Matumizi yalikuwa chini ya mamlaka iliyohusika; na
c. Matumizi yaliyofanywa yalizingatia thamani halisi ya fedha.
1.2 WAJUMBE WA KAMATI:
Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za Serikali na Mashirika kwa mwaka 2012/2013,
inaundwa na Wajumbe 8 na Makatibu 2. Wajumbe wa Kamati ni hawa wafuatao:
1. Mhe. Omar Ali Shehe Mwenyekiti 2. Mhe. Fatma Mbarouk Said Makamo Mwenyekiti 3. Mhe. Abdalla Juma Abdalla Mjumbe 4. Mhe. Farida Amour Mohammed Mjumbe 5. Mhe. Mbarouk Wadi Mussa (Mtando) Mjumbe 6. Mhe. Mohammed Mbwana Hamad Mjumbe 7. Mhe. Shadya Mohd Suleiman Mjumbe 8. Mhe. Shamsi Vuai Nahodha Mjumbe.
Aidha, kwa upande wa Makatibu (ambao ndio Sekretarieti ya Kamati), kazi zote za uratibu wa
Kamati, zimeratibiwa na Watendaji wafuatao:
1. Ndg. Amour Mohd Amour Katibu. 2. Ndg. Othman Ali Haji Katibu
1.3 REJEA ZA KAZI:
Katika kutekeleza jukumu lake lililoainishwa na Kanuni ya 118(2)(a) ya Kanuni za Baraza la
Wawakilishi, toleo la 2012, Kamati imefuatilia Ripoti tano za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali. Ripoti hizo ni hizi zifuatazo:
1) Ripoti ya Ukaguzi Yakinifu wa Miradi ya Maendeleo ya Wananchi na Miradi ya TASAF, kwa mwaka wa fedha 2009/2010.
3
2) Ripoti ya Ukaguzi Yakinifu wa Udhibiti na Uhifadhi wa Mali za Kudumu za Serikali, kwa mwaka wa fedha 2009/2010.
3) Ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu kwa Mawizara, Mashirika na Taasisi za Serikali, kwa mwaka wa fedha 2009/2010.
4) Ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu kwa Mawizara, Mashirika na Taasisi za Serikali, kwa mwaka wa fedha 2010/2011.
5) Ripoti ya Ukaguzi Yakinifu kwa Miradi ya Taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa mwaka wa fedha 2010/2011.
Mbali na Ufuatiliaji huo wa Ripoti hizo, Kamati kwa kutumia kanuni ya 118(2)(c) ya Kanuni za
Baraza la Wawakilishi, Kamati pia ilifuatilia uchambuzi wa Mapato na Matumizi kwa Baadhi ya
Taasisi na Mashirika ya Serikali kwa mwaka 2010/2011, ili kuangalia kwa namna gani Taasisi
hizo zinakusanya na zinatumia fedha za umma kwa mujibu wa taratibu za Sheria zilizowekwa.
1.4 UHUSIANO ULIOPO BAINA YA KAMATI YA PAC NA AFISI YA MDHIBITI
NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZANZIBAR.
Kwa kawaida, baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, kuwasilisha Ripoti
yake ya ukaguzi katika Baraza la Wawakilishi, kazi inayofuata ni Ripoti hiyo kuwasilishwa na
kukabidhiwa kwa Kamati ya Kuchunguza Hesabu za Serikali na Mashirika (P.A.C), kwa lengo la
kuifanyia kazi, na baada ya kazi hiyo, Kamati nayo hutakiwa kuwasilisha ripoti yake Barazani.
Hali hii kwa namna yoyote ile, inazifanya Taasisi hizi mbili kuwa na mashirikiano ya karibu
mno kila wakati.
Aidha, Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu inashirikiana na Kamati ya P.A.C katika
ufuatiliaji na utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewea na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu katika ripoti yake. Na takriban Afisi ya Mdhibiti na Kamati ya P.A.C zinasimamia kwa
pamoja dhana nzima ya matumizi ya fedha za umma kwa mujibu wa Sheria na taratibu
zilizowekwa. Kwa namna moja ama nyengine, Afisi hii ya Mdhibiti na Kamati hii ya P.A.C, ni
vigumu kuzitenganisha. Katika hali kama hii, ni wazi kwamba, kazi ya kukagua, kuchunguza na
kudhibiti fedha za Serikali ni ngumu mno na inahitaji moyo wa kizalendo. Lakini ni muhimu
mno kwa Serikali, na Serikali inayojali maslahi na ustawi wa wananchi wake, kama ilivyo kwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hufanya kila njia kuwepesisha utekelezaji wa majukumu ya
Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, pamoja na Kamati ya Kuchunguza
na Kudhibiti Hesabu za Serikali.
Ili kuunganisha spirit ya uzalendo na kusimamia ipasavyo majukumu haya mazito, lazima
changamoto zinazoikabili Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu, ziondolewe mara
moja, ili kuweka wepesi na kujenga ujasiri wa watumishi wa Afisi hii, wa kudhibiti hesabu za
Serikali. Hili katika utekelezaji wake, litaanza kwa kupiga kelele juu ya maslahi madogo ya
4
watendaji wa Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu. Kamati imezoea kulipigia kelele
suala hili zaidi ya miaka mitano iliyopita, na itaendelea kufanya hivyo, kwa kuamini kwamba,
iwapo tutajenga imani na ukinaifu kwa wakaguzi wa fedha za Umma, tutakuwa tumeshajenga
ngome ya kufichuliwa kwa wabadhirifu wa mali za umma.
Aidha, katika kuzipa uwezo Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu pamoja na Kamati
ya P.A.C, ni kuzipa wepesi katika kutekeleza Sheria zinazohusiana na utekelezaji mzima wa
majukumu yao. Kwa mfano kwa kuwa kuna mapungufu mengi ya kiutendaji katika sheria yake
namba 11 ya 2003 ya Uanzishwaji Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu, na kwa
kuwa Sheria Namba 12 ya mwaka 2005 na Namba 9 ya mwaka 2005 tayari zinahitaji
kurekebishwa kutokana na ama kuwemo kwa baadhi ya vifungu vya sheria hizo vinavyopingana
na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984; ama sheria za kimataifa za ukaguzi au hata kupitwa na
wakati, basi ni wazi kwamba, kufanyiwa marekebisho ya haraka kwa Sheria hizo, ni kuzisaidia
sana Afisi ya Mdhibiti na Kamati ya P.A.C, kuweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi
mkubwa.
La mwisho ambalo pia ni muhimu, ni uhusiano wa kitaaluma unaohitajika uwepo baina ya Afisi
ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu na Kamati ya P.A.C. Hii ina maana, Ripoti yoyote ya
ukaguzi inayotelewa na Afisi ya Mdhibiti ni ya kitaalamu. Na kwa bahati njema, Wajumbe wa
Kamati sio wote wataalamu wa Ukaguzi, lakini wanalazimika kufanya kazi za ukaguzi
(uchunguzi wa fedha na matumizi yake). Katika hali hii, kama Wajumbe hawa wa Kamati,
hawasomeshwa vizuri masuala ya fedha na wakayafahamu, kazi tunayowapa ya kudhibiti fedha
za Serikali haitafanyika kabisa ama haitatekelezwa kwa ufanisi. Hili linahitaji kwanza kuijengea
uwezo wa kifedha na kitaalamu Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu, ili nayo iweze
kuiwezesha Kamati ya P.A.C kutekeleza majukumu yake, kitaaluma na kitaalamu.
Hili na lifanyike pia kwa kuongeza utaalamu kwa Sekretarieti ya Kamati, ambayo ndio roho,
macho na masikio ya Kamati, lakini pia kwa kuongeza bajeti ya Afisi ya Mdhibiti, ili fursa zaidi
za masomo kwa Wajumbe, Sekretarieti ya Kamati pamoja na Watendaji wote wa Afisi ya
Mdhibiti ziweze kuongezeka.