· web viewmila huimarishwa na kurekebishwa na desturi za jamii ambazo kwa ufupi ni mazoea ya...

Download  · Web viewMila huimarishwa na kurekebishwa na desturi za jamii ambazo kwa ufupi ni mazoea ya jamii katika muhula maalum wa historia. Tofauti kati ya mila na desturi ni kwamba, mila

If you can't read please download the document

Upload: hoangthu

Post on 04-May-2018

653 views

Category:

Documents


81 download

TRANSCRIPT

WIZARA YA UTAMADUNI WA TAIFANA VIJANA

UTAMADUNI CHOMBO

CHA

MAENDELEO

WASHIRIKI

Maofisa wafuatao, ambao ni wataalamu wa fani mbali mbali za shughuli za maendeleo ya utamaduni na vijana walishiriki kikamilifu katika kutoa maandishi haya.

Ndugu A.O. Anacleti;

Ndugu Albert Kanuya;

Ndugu L.J. Kawala;

Ndugu J.S. Magille;

Ndugu R. Masimbi;

Ndugu R.D. Mollel;

Ndugu Kemal Mustafa;

Ndugu A.A. Mturi;

Ndugu J.S. Mwenge;

Ndugu D.K. Ndagala;

YALIYOMO

Msamiati..(v)

Dibaji(vii)

Kazi Kama Kiini na Msingi wa Utamaduni wetu 1

Sanaa katika Maendeleo ya Utamaduni ..20

Lugha ya Kiswahili katika Kudumisha na Kuendeleza

Utamaduni wa Taifa 30

Michezo kama Sehemu ya Burudani katika Kuandaa Umma

Na Kutangaza Utamaduni 37

Malezi na Maendeleo ya Jamii 44

Uhifadhi wa Urithi wa Utamaduni katika Maendeleo .49

Mipango ya Maendeleo ya Utamaduni 62

MSAMIATI

Dhana: Wazo maana na picha, hasa inayopatikana katika fikra za

Mtu/watu kuhusu jambo; kitu au tendo Fulani;

Kidhi: Kutosheleza haja;

Aidha: Zaidi ya hayo (Yaliyokwishatajwa);

SURA YA KWANZA:

Utashi: Hali ya kuhitaji/kutaka kitu kwa moyo wote;

Maadili: Haki, sawa, tabia nzuri, mambo mema na manyoofu;

Usanifu: Ustadi, umahiri, ustadi wa utunzi;

Vigano: Hadithi za fasihi simulizi;

Hisia: Maono, fikira za moyoni;

Athari: (1) Dosari (2) Mpato wa kitu/wazo/jambo juu ya kitu kingine;

Itikadi: Msimamo wa kisiasa, imani;

Msamiati: Neno, maneno ya lugha, orodha ya maneno, orodha ya maneno na maana yake;

Samani: Chombo, kitu cha kutumia kufanyia kitendo, kitu/vitu vya nyumbani k.m. viti, meza, vitanda, rafu na kadhalika;

Hamasa: Ari, shauku, moto, hisia ya kutenda/kufanya kitu.

Kaya: Familia, jamaa, hasa katika kijiji wanaoishi pamoja.

Mali ghafi: Vitu/bidhaa/mazao ambayo bado hayajapitishwa kiwandani. Vitu/bidhaa/mazao vinavyotumika katika kutengeneza/kuundia vitu/bidhaa/nyingine.

Dhalilisha: Dunisha, ondoa thamani, tia unyonge.

SURA YA PILI:

Tamthiliya: Michezo ya kuigiza/maigizo, hasa ya jukwaani.

Motisho: Kitu kinachompa ari, kumtia moyo mtu atende/afanye jambo.

Riwaya: Hadithi ndefu iliyoandikwa katika kitabu. Kwa kawaida si chini ya maneno 45,000.

SURA YA TATU:

Tohoa: Badili umbo la kitu/neno kwa madhumuni au hitilafu maalum.

Nyambua: Badili umbo la Kitu/neno ili kupata sura/hali nyingine inayotukia au kukusudiwa;

Lahaja: Vilugha vya lugha moja na tofauti zao kufuatana na jinsi zinavyosemwa katika sehemu mbali mbali tofauti;

Amali: Tendo linalotendwa, shughuli ya kila siku;

Weledi: Hali ya kuelewa, kujua na kadhalika, ustadi, umahiri;

Giligili: Kitu kilichoko katika hali iliyo kati ya umaji maji na ugumu.

SURA YA NNE:

Uchwara: Kitu cha onyo, kisichokuwa kamili wala stadi.

SURA YA SITA:

Tathmini: Kuchunguza/kupima thamani au matunda ya kitu/kazi iliyokwishafanywa na hali ilivyo.

Nyanja: Fani;

Udarisi: Hali ya kusoma kitabu barabara, kukutana darasani kwa

funzo, kuhudhuria shule, kusomesha/kufundisha;

DIBAJI

Alipoitoa hotuba yake ya kwanza katika Bunge mnamo tarehe 10 Desemba, 1962 mara tu baada ya kuchaguliwa kuwa Rais, Ndugu Mwalimu Julius K. Nyerere alitangaza kuundwa kwa Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana. Akielezea baadhi ya sababu zake za kufanya hivyo alisema aliunda Wizara hiyo mpya kwa vile aliamini kuwa Utamaduni ni kiini na roho ya Taifa. Alisendelea kusema kuwa katika makosa yote ya ukoloni hakuna lililo baya kupita lile la jaribio la kutufanya tuamini kuwa hatutakuwa na Utamaduni wetu; au kuwa Utamaduni tuliiokuwa nao haukuwa na thamani yeyote jambo ambalo ingelifaa tulionee haya badala ya kuwa ni kitovu cha majivuno juu ya Utamaduni wetu.

Maneno haya ya busara aliyoyasema Baba wa Taifa letu yalirudiwa tena kwa njia nyingine na Chama mnamo mwaka wa 1970, wakti kielelezo cha Uhai na Utashi wa Taifa. Kwa hiyo ni sawa kabisa kusema kuwa Mtukufu Rais, Mwalimu Julius K. Nyerere ndiye aliyeweka msingi wa juhudi mpya za kufufua Utamaduni wa Taifa letu baada ya Uhuru. Kutokana na msingi huo, wale waliopewa jukumu la kutekeleza wajibu huo kwa upande wa Wizara, wamejitahidi kujenga juu ya msingi huo. Msingi huo pamoja na tamko la Chama vimekuwa ndiyo dira ya kuiongoza Wizara katika utekelezaji wa kazi yake iliyo ngumu, lakini pia ya muhimu sana.

Wizara imewateua wataalamu waka kadhaa waandike kitabu hiki ambacho kinaitwa UTAMADUNI CHOMBO CHA MAENDELEO. Madhumuni makubwa ya kitabu hiki ni kuupa umma wa Tanzania fursa ya kutafakari katika kitabu kimoja, dhana na juhudi za utekelezaji way ale mambo muhimu ambayo kwa pamoja yanaunda Utamaduni wa Taifa. Kuna sababu nyingi za kuutambua Utamaduni kuwa ni chombo cha maendeleo. Moja ni kuwa vipengele na fani mbali mbali za Utamaduni ndizo zilizoko katika kiini cha Umoja wa jamii. Utamaduni ni sehemu ya siasa ya Taifa letu lenye msingi na shabaha ya Umoja wa kweli. Uhuru wetu uliletwa na Umoja. Maendeleo hayapatikani bila ya Uhuru na Umoja. Hivyo Utamaduni kama nguzo ya Umoja, ni chombo cha maendeleo.

Kadhalika maendeleo hayapatikani bila kazoo. Kwa hiyo kazi ni sehemu ya Utamaduni. Sina shaka wote tunakubaliana kuwa maendeleo yasiyo na amani, uhuru na umoja siyo maendeleo ya kweli na ya kudumu. Hatuwezi kufurahia mabadiliko ambayo yanaleta kuvurugika au kuvunjika kwa familia na jamii. Ni kosa kuyachukulia mabadiliko yenye matokeo mabaya kama hayo kuwa ni maendeleo. Kitabu hiki

kinaonyesha wazi kuwa popote ambapoUtamaduni umepuuzwa au kupigwa vita, matokeo yake ni vurugu katika maisha ya familia na jamii. Wakoloni waliupiga vita Utamaduni wetu. Msomaji akikaa na kutafakari, vizuri, atakubali kuwa madhara ya vita hivyo dhidi ya Utamaduni, tunayaona mpaka leo.

Kutokana na ukosefu wa malezi bora na yaliyokamila yenye kusisitiza wajibu wa kila mmoja kwa jamii na miiko ya jamii, matatizo mengi yametokea duniani. Kwa mfano, ndoa zinazidi kuvunjika; ulevi, uvivu na uzururaji vimeongezeka; heshima, adabu na nidhamu vimepungua. Njia kubwa ya kuyakabili matatizo ya maisha ni kukubali kwa dhati kuwa UTAMADUNI NI CHOMBO CHA MAENDELEO. Mtu ni utu, na Utamaduni unao mchango mkubwa sana katika kujenga utu. Binadamu asiye na utu hana tofauti kubwa sana na mnyama. Msimamo wa Taifa letu ni maendeleo ya watu yenye kuletwa na watu. Pamoja na hayo yote, kitabu hiki kinadhihirisha kuwa fani za Utamaduni zenyewe zinaweza kuzalisha mali na hivyo kutoa mchango mwingine katika maendeleo ya Taifa kwa upande huo wa mendeleo ya vitu.

Wizara inatazamia kuwa baada ya umma kujisomea wenyewe mambo muhimu ambayo yanaunda Utamaduni wetu, kutatokea msisimko mpya wa kuupenda, kuuendeleza na kuudumisha Utamaduni katika Taifa letu. Kuudumisha Utamaduni katika Taifa letu. Kuudumisha Utamaduni ni kuurithisha kwa vizazi vijavyo. Hivyo uhusiano wa kudumu kati ya UTAMADUNI na VIJANA ni suala mojawapo la msingi katika jitihada zote zinazohusu Utamaduni. Vijana ndio walioko msitari wa mbele katika kujenga na kulinda Taifa. Malezi ya vijana na suala la msingi katika maendeleo ya Taifa. Utamaduni ukithaminiwa kwa dhati, utajitokeza sana kwa vijana. Vijana ndio wanaoleta maendeleo makubw na kwa hiyo, ni muhimu utamaduni uende bega kwa bega na Vijana, wenyewe wakiwa ni chombo cha maendeleo.

Waandishi wa kitabu hiki wanaonyesha jinsi wahenga wetu walivyothamini utamaduni na kuufanya kuwa ni chombo muhimu katika maendeleo yao. Utamaduni ulishika nafasi muhimu katika kuzifanya familia kuwa katika hali ya umoja, utulivu na nidhamu zaidi. Waandishi wameonyesha pia jinsi ambavyo Taifa letu limekubali kuyakaribisha mazuri kutokana na utamaduni wa mataifa mengine, ili mradi yasivuruge msingi imara wa utamaduni wetu wenyewe. Msimamo huu unazingatia siasa yetu ya kuwachukulia binadamu wote kuwa ni sawa na ni ndugu. Aidha kitabu hiki kinasaidia kuipunguza ile kasumba ya kuamini kuwa mambo mengi mazuri tuliyonayo yameletwa na wageni kutoka ngambo. Ukweli ni kuwa mababu zetu waliweka misingi ya mengi katika shughuli za maendeleo.

Mwisho natoa shukrani zangu za dhati kwa wataalamu wa Wizara kwa juhudi walioifanya katika kutekeleza wajibu wa kuandika kitabu hiki. Kitabu chochote kuhusu Utamaduni hakiwezi kukamilika maana suala hili ni kubwa sana na linagusa kiini cha uhai na maendeleo yetu. Hivyo Wizara inaomba radhi kuhusu zile sehemu ambazo huenda zitaonekana kuwa zinao upungufu mkubwa. Nawaomba wasomaji wakikamilishe kwa kutuletea maoni yao na kutusahihisha kwa nia ya kujenga. Ninawaomba viongozi wa ngazi zote na hasa wale wa Vijiji, Wilaya na Mikoa wazidi kuzingatia siku hata siku umuhimu wa miradi ya Utamaduni inashikilia nafasi inayostahilik, kwa kuzingatia kwamba ni kuelewa utamaduni wa watu ndipo tunaweza kupanga kukidhi mahitaji yao kikamilifu. Juu ya yote nawaomba wananchi ambao ndio kitovu na shabaha ya Utamaduni, wakisome kitabu hiki chenye lengo la kutufanya tutambue zaidi jukumu la Utamaduni katika maendeleo ya Taifa, na kuwa maendeleo ya kweli ni yale yanayokubali kuwa Utamaduni ni chombo cha maendeleo.

C.Y. MGONJA, BUNGE

WAZIRI WA UTAMADUNI WA TAIFA NA VIJANA

Februari, 1979

SURA YA KWANZA

KAZI KAMA KIINI NA MSINGI WA UTAMADUNI WETU

Mwaka 1970 Mkutano Mkuu wa 15 wa TANU uliutambua utamaduni kuwa ni kielelezo cha utashi na uhai wa Taifa. Tangu hapo jitihada imefanywa kuzingatia maana hii katika utekelezaji. Lakini kuna haja ya kusema kwamba wengi wameelekea kuliona tamko hilo kuwa ni azimio la busara la Chama bila kuingilia undani wa Azimio lenyewe.

Ili kuzingatia jambo hili kuna haja ya kuelewa utashi na uhai hasa wa Taifa unaloelezwa na vielelezo mbalimbali vya utamaduni. Ili Taifa lolote liwepo halina budi kwanza kabisa liwe na watu na ni lazima watu hawa wawe na ardhi katika mazingira maalum wanamoishi. Na ni muhimu kwamba watu hao wawe na mbinu maalum za kutawala mazingira hayo kwa manufaa yao. Lakini mwanadama hawezi kutawala mazingira yake bila kufanya kazi. Ni kwa kazi ndiyo mwanadamu anajieleza na pia kueleza mahitaji na utashi wake wa asili. Ndiyo kusema kwamba utashi wa Taifa ni kufanya kazi na ni kwa hivyo tu Taifa linakuwa hai.

Kimsingi, tunaweza tukasema kwamba uhai wa Taifa unaoelezwa na utamaduni ni msingi wa uchumi na maendeleo ya Taifa hilo. Msingi wa uchumi hapa kwetu Tanzania unategemea masharti manne ya maendeleo ambayo ni watuk, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Hivyo, utamaduni wetu ni kielelezo cha watu wetu, ardhi yetu, siasa yetu na uongozi wetu. Tukikubaliana hivyo basi, tunaweza tukachanganusw kazi kama kiini halisi na msingi wa utamaduni wetu.

Utamaduni wa watu hutokana na mambo haya manne tuliyotaja hapo juu na wakati huo huo hathiri ambo haya manne. Ni katika kufanya kazi ndipo watu wanapounda utamaduni wao na kuutumia utamaduni huo kufanikisha kazi zao. Katika kufanya kazi na jinsi kazi yenyewe inavyofanywa ndiyo hali ambayo huonyesha tofauti baina ya Taifa moja na jingine. Tunalosema hapa ni kwamba uhai wa jamii na hata wa Taifa hutokana na kazi na ni kwa kazi ndio jamii mbali mbali hutofautiana na jamii nyingine. Kusema kweli, jinsi sura ya mtu binafsi inavyomtofautisha na wengine wengine ndiyo pia jinsi kazi na mtindo wake vinavyotofautisha matfifa mbalimbali.

Hivyo tabia ya kazi ndicho kitambulisho kikuu cha jamii mbali mbali. Na ni tabia hii ya kazi ndiyo tunayoiita Utamaduni.

kwa hiyo ni tabia ya kazi kwa jamii nzima. Tabia hii hudhihirishwa na kiwango kilichofikiwa na jamii katika uzalishaji mali. Kiwango cha Utamaduni hutegemea sana kiwango cha ufundi wa kisayansi na ujuzi uliofikiwa na jamii katika muhula maalum wa historia yake. Kiwango hiki hudhihirika katika vipengele sita muhimu.

VIPENGELE VYA UTAMADUNI

Kipengele cha kwanza ni mila ambayo ni hali ya kudumu ya maisha ya kila siku ya watu ambayo inahusu sana asili ya watu na hivyo hupokezwa kutoka kizazi hadi kizazi na huthaminiwa sana na watu kama dira ya maisha yote ya kijamii. Mila hizi hujumuisha mambo muhimu katika jamii kama vile malezi toka utoto hadi uzeeni katika maadili ya jamii. Mila huonekana katika miiko, mapokeo, historia, matibabu, matambiko, heshima, adabu na sheria zihusuzo taratibu za jamii kama vile ndoa, uzazi, urithi na vifo. Mila za watu huwa ni tunu kubwa kwa jamii yoyote ile na huwa wako tayari kuzitetea kwa hili yoyote ile. Na hii huwa hivyo kwa vile mila husaidia pia kueleza uhusiano uliopo kati ya jamii na mazingira yao. Mila, kwa namna Fulani ni katiba ya jamii. Lakini tofauti na katiba zingine, yenyewe hutokana na uzoefu wa watu wenyewe katika jitihada yao ya kutaka kuendelea katika jamii.

Mila huimarishwa na kurekebishwa na desturi za jamii ambazo kwa ufupi ni mazoea ya jamii katika muhula maalum wa historia. Tofauti kati ya mila na desturi ni kwamba, mila ni uzoefu uliothibitisha na hivyo una tabia ya kudumu, ambapo desturi ni mazoea ya matendo ambayo yanweza yakabatilishwa au baadaye kupokelewa kama mila ya jamii. Desturi za watu hujumuisha vitu kama vile namna zao za mavazi, ujenzi, salamu, na namna zao za kula. Mambo haya yote hubadilika haraka sana jinsi watu wanavyobadilisha mbinu zao za uzalishaji mali. Desturi pia hubadilika haraka haraka wakati watu wanapopanua upeo wao wa mawasiliano na jamii nyingine. Watu wa jamii wanavyokutana na wageni ndivyo wanavyopokea desturi mpya na kuziambatanisha na desturi zao. Hivyo desturi ndiyo kielelezo cha kiwango cha jamii cha kupokea mawazo mapya na kuyasanifu kwa mahitaji yao ya kijamii. Mapokezi haya vile vile yatategemea sana kiwango kilichofikiwa katika ufundi na ujuzi wa kisayansi pamoja na msimamo wa kisiasa.

Kipengele kingine muhimu ambacho ni kielelezo cha tabia ya kazi ni lugha. Lugha ni chombo muhimu sana katika utamaduni wa watu. Lugha siyo tu kwamba inawezesha watu kuwasiliana katika kazi zao za kawaida, ila pia ni matokeo ya kazi au ari ya binadamu katika kushirikiana na wenzake. Undani wa suala hili utaelezwa katika sura

inayohusu lugha ya Taifa. Hapa yatosha kusema kwamba lugha ni mojawapo ya vitambulisho vya Utamaduni na pia ni chombo mahsusi cha kueneza Utamaduni wa watu na kuupatia sura kwa njia ya hadithi, methali na msamiati.

Kipengele kinachojulikana zaidi kama sehemu muhimu ya Utamaduni ni sanaa. Sanaa ni kipengele cha utamaduni ambacho kinaiwezesha jamii kueleza kiwango cha mafanikio yao kihisia. Sanaa yoyote ile yenye msingi katika juhudi ya watu kila mara hufanya mambo haya matatu makubwa. Kwanza, hueleza juhudi iliyofanywa na jamii ya watu; pili, hueleza matatizo ambayo jamii ilibidi ipambane nayo ikiwa matatizo hayo ni ya kijamii, kisiasa ama kiuchumi; na mwisho, sanaa ndicho chombo ambacho jamii zisizokuwa na jadi ya kusoma na kuandika inatumia katika kuhifadhi na kuwasilisha kumbukumbu za mambo muhimu katika maisha yao. Kumbukumbu kama hizi zinaweza tu zikawasilishwa na kukumbukwa zikiwasilishwa kwa njia ya kisanii inayofurahisha kuburudisha. Kwa njia hizi zote sanaa hueleza na kusifia mafanikio ya jamii kwa jumla na kuweka kumbukumbu ya mafanikio hayo.

Kitu kimoja cha lazima katika mfumo wote wa kazi ni ukweli kwamba kazi haiwezi kuendelea bila mapumziko. Hii ni kwa vile kazi hufanywa kwa nguvu na akili za mtu. Akili hizi zina mipaka na hivyo inabidi kwaba kila baada ya muda Fulani binadamu apumzike. Katika kupumzika hurudisha nguvu zake zilizotumika. Hii inawezekana tu kama akipata burudani ya kufaa. Burudani ya kufaa ni ile inayopanua uwezo wa mtu na jamii kwa jumla, wa kuzalisha mali zaidi na kwa maarifa zaidi. Hivyo burudani ni sehemu muhimu ya utamduni. Burudani inajumuisha kazi za hiari, michezo, shesrehe, na hata vinywaji, hasa vile vinavyotumiwa kama kichocheo cha majadiliano kuhusu namna ya kuendeleza zaidi mbinu na uywezo wa kuzalisha mali. Matumizi ya namna hii ya vinwaji ndiyo yaliyokuwapo katika jamii nyingi kabla pombe haijafanywa bidhaa ya biashara.

Kipengele cha mwisho ni itikadi, ambayo ni pamoja na imani ya watu. Kipengele hiki ndicho huweka hatua za kufuatwa na jamii nzima. Itikadi ndiyo mwelekeo wa vipengele vingine vya utamaduni na kama ilivyo na vipengele vingine, kipengele hiki hutegemea sana mbinu za uzalishaji mali zainazotumika katika jamii na kiwango kilichofikiwa na jamii. Mbinu hizi za uzalishaji mali ndizo zitakazoeleza uhusiano uliopo katika uzalishaji mali na hivyo uhusiano wa kijamii. Kutokana na ukweli kwamba itikadi ya kijamii hutokana na kutegemea uhusiano uliopo katika uzalishaji mali, inayumkinika kwamba aina ya itikadi iliyopo katika jamii itakuwa ni kielelezo halisi cha aina ya mfumo wa maisha ya kijamii kwa jumla. Kwa mfano, mahali ambapo uhusiano wa uzalishaji mali si wa kibinafsi, imani ya watu katika jamii kama hiyo ni ya kutosheleza mahitaji yote ya kila mtu. Na mahali ambapo jamii ni ya kitabaka na imegawanyika katika tabaka la wafanyakazi na wafanyiwa kazi, imani ya watu katika jamii ya namna hiyo huwa ni ya kimwinyi na kibwanyenye.

UHUSIANO WA UTAMADUNI NA MSINGI WA UCHUMI

Tumekwishasema kwamba, kiini na msingi wa utamaduni ni kazi. Kwa hiyo utamaduni na mfumo was kuzalisha mali vinategemeana na hatuwezi kuvitenganisha. Kwa vile uzalishaji mali ndio msingi mkubwa wa uchumi, ni lazima watu wafanye kazi ili waweze kuishi, na wanaishi kufuatana na utamaduni wao. Hiyo ndiyo sababu katika siasa yetu imesisitizwa kwamba kazi ni uhai. Ili kukabiliana na mazingira yao barabara, watu hawawezi kufanya kazi kiholela, jamii lazima iwe na utaratibu na nidhamu ya kuzalisha malai. Utaratibu huo husimamiwa na taasisi mbali mbali kama zile za kiuchumi, kisiasa na kiitikadi na hufuatana na utaratibu wa mfumo wa uzalishaji mali wa jamii na maendeleo yake kihistoria.

Nchi yoyote ina mchanganyiko wa watu ambao hufanya kazi za aina mbali mbali. Hapa Tanzania tunao, kwa mfano, wakulima, wafugaji, wavuvi, wawindaji, wafanyakazi viwandani na ofisini, wanajeshi, wafanya biashara na viongozi wa Chama na Serikali. Kila aina ya kazi ina historia yake na hufuatana na uzoefu mbali mbali kutokana na kukabiliana na mazingira yanayoathiri kazi. Muhimu sana katika kila aina ya kazi ni mfumo wa uzalishaji mali na uhusiano wake na maisha ya jamii. Mfumo wa uzalishaji mali unazingatia jinsi watu wananvyoshirikiana katika kufanya kazi na kugawa mapato au ziada inayopatikana kutokana na kazi zao.

UTAMADUNI KATIKA JAMII ZA ASILI

Tukiangalia historia ya nchi yetu tutaona kwamba kabla ya kuingia mfumo wa uzalishaji mali wa kibepari, tulikuwa na jamii zetu zilizohusiana sana katika kuzalisha mali kukidhi mahitaji yao ya lazima kwa kujitegemea au kwa kutegemeana kwa njia ya biashara. Wakulima walibadilishana mazao yao na wafugaji, wavuvi na wawindaji. Kila kikundi cha watu kilifuata utaratibu wa kazi kulingana na mazingira yake. Na taasisi zao za kijamii zilitofautiana kufuatana na utaratibu wa kazi. Kwa mfano, taasisi za wakulima zilisisitiza sana kumheshimu mkuu wa ukoo ambaye alikuwa anatunza ardhi kwa niaba ya ukoo mzima. Kwa hiyo, tukiviangalia vielelezo mbali mbali vya kiuchumi, kisiasa, kidini, kisheria na kiitikadi vya wakulima, tutaona kwamba vyote vilihusiana sana na umuhimu wa kuhakikisha kwamba nyenzo ya kimsingi kabisa ya kuzalisha mali kwao, yaani ardhi, intunzwa barabara kwa uongozi bora.

Kulingana na utaratibu wao wa kazi, baadhi ya wafugaji hawakuweka umuhimu sana kwenye mambo ya kiukoo: kwa mfano Wamasai, walisisitiza zaidi utaratibu wa kirika. Tofauti kama hizi zilisababishwa na mahitaji mbali mbali kuwashirikisha watu kikazi na lazima wawe na ushirikiano wa kijamii ambao ni mpana zaidi kuliko ule wa kiukoo kwa sababu wanatumia eneo kubwa zaidi kuliko wakulima wanaopanda mazao na kukaa karibu na mashamba yao. Pia wafugaji wanahamahama zaidi kufuatana na mahitaji katika mbinu zao za kuzalisha mali na kupambana na mazingira yao.

MISINGI YA MILA NA DESTURI

Hivyo, tofauti za mila na desturi kati ya watu wa sehemu mbali mbali zinatokana zaidi na tofauti za kazi na mifumo ya jamii zao. Kwa mfano, baadhi ya jamii za wafugaji hazikupenda kula nyama na maziwa wakati huo huo mmoja. Ilibidi muda Fulani upite ambao uliaminiwa kuwa kimojawapo katika vyakula hivi kimekwisha tumboni ndipo kingine kiliwe. Ilisadikiwa kwamba kutokufanya hivyo kungeleta madhara kwa mifugo. Desturi hii ilisimamia mgawanyo wa chakula katika jamii hasa kati ya watoto na watu wazima na pia kuhakikisha kuwa chakula hakikutumika ovyo ovyo. Kuna haja ya kuzingatia desturi kama hizi, kwa mfano, tunapohimiza ulaji wa chakula bora.

MAZINGIRA

Mazingira yanaathiri sana maisha ya watu na mbinu zao za kuzalisha mali. Kwa hiyo wafugaji, kwa mfano, hupaswa kuwa na ujuzi wa kutosha wa mazingira yao. Milima, mito na vijito, majani na wanyama wa porini huathiri sana ufugaji kwa njia mbalimbali. Majina yanayotumika hueleza kikamilifu tofauti zilizopo kati ya kitu kimoja na kingine ili matumizi yake yawe rahisi wakati wa uzalishaji mali. Milima, kwa mfano, huelezwa ina rangi gani, inatumiwa vipi, na ina hali ya hewa ya namna gani kwa njia ya majina inyopewa. Majina ya majani huonyesha kama majani hayo ni matamu au machungu, kama yananenepesha ngombe au yanaongeza maziwa au kama ni dawa. Kwa vile jamii hizi hutegemea mifugo, kila kijisehemu cha mifugo huwa na jina lake kamili. Hivyo lugha huathiriwa sana na mazingira na hii inadhihirisha kuwa lugha inahusiana sana na hali halisi ya kazi na uzalishaji mali katika mazingira maalum. Kwa hiyo, lugha ikiwa chombo cha mawasiliano, lazima iwe na maneno ya kutosha kupambana na kufafanua haya yote. Ni kwa hivi tu ndipo lugha inaweza kuwa chombo kikubwa cha kuendeleza elimu na kuirithisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Hivyo hivyo mavazi ambayo ni mojawapo ya mahitaji ya lazima, inabidi yalingane na mazingira ya mvaaji. Kwa mfano, vazi lolote ambalo linafanya utendaji wa kazi kuwa mgumu sio zuri au la heshima hata ikiwa ni ghali kiasi gani. Baadhi ya jamii za wawindaji zilikuwa haziruhusu kuoga mara kwa mara wala kuvaa mavazi ya aina Fulani. Hii ni kwa kuwa zana za kuwindia za jamii hizi zilikuwa duni ilibidi wawindaji wamfikie mnyama karibu bila kumshtua. Mavazi ya rangi rangi na harufu ya sabuni au vitu vingine vinavyoambatana na kuoga, huwafanya wanyama kushtuka na kukimbia kabla wawindaji hawajapata nafasi nzuri ya kuwaua. Hivyo mavazi na kuoga vilikuwa ni vikwazo katika kujitafutia uhai. Hii ni sawa sawa na jinsi tai na koti vinavyoweza kuwa vikwazo katika kulima, au kanzu kuwa kikwazo katika kuchunga ngombe. Hivyo basi, pamoja na matatizo mengine ya mavazi ya asili, kila jamii ilihakikisha kuwa mavazi yake hayakuwa kipingamizi cha uzalishaji mali, jambo ambalo tunapaswa kukumbuka tunapohimiza mavazi bora.

MISINGI YA UFUNDI WA KIASILI

Pamoja na kuyafahamu mazingira, jamii hujitahidi kuyashinda kwa kujitengenezea zana za kufanyia kazi. Wavuvi, kwa mfano, wanapaswa waelewe ni wakati gani ulio salama kwenda kuvua. Vile vile ni lazima wavuvi wawe na ufundi wa kutengeneza ngalawa na vifaa vingine vya kuvulia, pamoja na ujuzi wa kusafiri kwenye maji. Kwa hiyo, ufundi wa asili na viwanda vidogo vilistawi kulingana na aina za kazi ambazo, kama tulivyokwishaeleza, ziliathiriwa na mazingira.

Sehemu nyingine wakulima walitengeneza mifereji ya kumwagilia mashamba kama vile Sonjo, Pare na Kilimanjaro. Taratibu za mgawanyo na matumizi ya maji huko Sonjo, kwa mfano, zilikuwa imara kabira. Viongozi wa mifereji walikuwa na hadhi kubwa kwa sababu walikuwa na madaraka juu ya kitu muhimu cha uzalishaji mali, yaani maji. Zana zao za kulimia zilikuwa miti ambayo ilikuwa na uhusiano na hali ya ardhi na kiwango cha ufundi wa umwagiliaji maji. Huu ni mfano mmoja tu wa jinsi wakulima ambao kwa sasa wanasemekana na baadhi ya wataalamu kwamba wako nyuma, walivyoweza kumudu kuongoza mazingira yao kwa kubuni ufundi uliolingana na mahitaji yao. Pia ni uthibitisho kwamba hapa Tanzania tulikuwa tunaendelea kiufundi na kiteknolojia hata kabla ya ukoloni.

Ukweli huu umethibitishwa na utafiti wa kimapokeo na akiolojia uliofanyika huko Bukoba kuwa, baadhi ya ufundi wetu wa asili ulikuwa umekwisha fikia kiwango cha juu sana miaka mingi kabla ya mataifa ya Ulaya kufanya hivyo. Imeonekana, kwa mfano, kuwa wahunzi wa Bukoba walikwishafanikiwa kutengeneza chuma cha pua yapata kama miaka elfu mbili iliyopita. Hivyo, katika kujaribu kufufua na kuimarisha ufundi kulingana na siasa yetu ya Ujamaa na Kujitegemea yafaa kuzingatia uwezekano wa kuwashirikisha mafundi chuma wetu na mafundi wengine katika viwanda vyetu nchini, ili kuendeleza msingi wetu wa kiteknolojia kwa jumla.

Watu wenye ujuzi zaidi walipewa hadhi maalum katika jamii zao. Wengine kutokana na ujuzi wao, waliheshimiwa zaidi na hata kuwa viongozi wa dini au siasa kama vile waganga wa mvua, watabiri na viongozi wa vita. Lakini katika sehemu zingine watu walikuwa na desturi ya kuwabagua baadhi ya mafundi muhimu katika jamii. Kwa mfano, huko Sonjo wahunzi hawakuruhusiwa kulima wala kuwaoa mabinti wa wahunzi. Mifano ya aina hii ilikuwako pia katika sehemu za Wilaya ya Mara Kaskazini, Serengeti na Umasaini. Wahunzi walifanywa waonekane kama watu duni sana ingawa kazi yao ilikuwa ya muhimu kwani ilithaminiwa sana. Kudharauliwa huku kwa wahunzi kulikuwa ni mbinu za kuhakikisha kwamba wahunzi hawa hawakutumia nyenzo hii muhimu kwa manufaa yao kinyume cha mahitaji ya jamii nzima. Ilibainika wazi kwa jamii kwamba ufuaji wa chuma na ufinyanzi wa vyungu ni shughuli zilizohusiana nazo zilikuwa ni njia kuu za uzalishaji mali ambazo zilibidi ziwe mikononi mwa jamii nzima.

Jamii nyingine zilizoendelea zaidi katika kiwango cha mbinu za kuzalisha mali zilistawisha utawala wa kifalme au kitemi. Katika jamii hizi kulizuka mgawanyo wa kazi na wa ziada iliyopatikana, mpaka kukatokea matabaka katika jamii kulingana na mgawanyo huo. Matabaka haya yalisababishwa na maendeleo ya mgongano kati ya mbinu za kuzalisha mali na uhusiano wake wa kijamii.

MISINGI YA BIASHARA

Jamii zetu zilibadilishana mazao ili kujipatia mahitaji ya lazima. Biashara hii ilisaidia kuwafanya watu wa jamii mbali mbali kufahamiana humu humu nchini na hata nchi za nje. Ilikuwepo biashara, kwa mfano, kati ya baadhi ya jamii za nchi yetu na jamii za nchi nyingine kama vile India na Uchina kwa muda mrefu sana. Wataalamu wa akiolojia wamepata samani za biashara kama vile sahani na sarafu zilizoletwa nchi hii kiasi cha zaidi ya miaka elfu moja iliyopita. Biashara hii ilileta uhusiano kati ya jamii zetu na jamii za nchi nyingine. Vile vile biashara hii iliwapatia watawala vitu vya anasa na pia vifaa vya kuimarisha ulinzi wao. Hali hii iliwawezesha kuanzisha biashara ya nje na ndani ambayo hatimaye, ilileta kuzuka kwa kundi la wafanya biashara.

Ingawaje biashara ni mojawapo ya vyombo muhimu vya uhusiano na ushirikiano baina ya jamii na jamii au nchi na nchi, kundi la wafanya biashara halizalishi mali ila hununua bidhaa kwa kutumia mtaji wa biashara ili ziuzwe tena kwa faida mara nyingi bila ya kujishughulisha na utengenezaji wake. Hata hivyo kupanuka kwa biashara kumechochea utengenezaji wa vyombo vya usafiri kama vile majahazi na meli.. Pia biashara ya nje imewawezesha watu kufahamu mahali pa kuuza na kununua bidhaa mbali mbali.

Biashara kati ya Pwani na Bara iliendelea kustawi na kuwanufaisha sana Waarabu. Kadhalika biashara iliziimarisha baadhi ya tawala za jadi. Mtemi Mirambo wa Tabora, kwa mfano, aliunda na kuimarisha jeshi lake la Waluga luga na kulitumia kushika sehemu ya biashara hii baada ya kuona faida na kutata isiendelee kusimamiwa na Waarabu.

Kutokana na mababadiliko ya mfumo wa uzalishaji kuanza kuwa wa kibepari katika nchi za Ulaya, palitokea haja kubwa ya watu wa kufanya kazi huko Amerika, Mashariki ya Kati na sehemu nyingine kwa gharama ndogo. Katika jitihada za kukidhi haja hii, biashara ya watumwa ilianzishwa katika Bara la Afrika.

Wakati huo huo pamoja na biashara ya watumwa kulikuwa na biashara ya pembe za ndovu ili kukidhi mahitaji ya anasa huko nchi za nje. Biashara hizi ziliznzisha misafara kati ya Pwani na Bara. Tokeo mojawapo la biashara hii ilikuwa ni kustawi kwa utani kati ya jamii zilizoshiriki kwenye misafara na zile ilimopita misafara hiyo. Utao huo uliwawezesha wahusika kupata misaada walopokuwa mbali na kwao maana wasingeweza kujitegemea kikamilifu kabla ya kupata nyenzo za kuzalisha mali. Iliwezekana mtu kupata nyenzo za kuzalishia mali kutoka kwa watani kwa njia ya kuoana ama kutaniana. Kwa hiyo, utani kati ya Wanyamwezi na Wazaramo ni mojawapo ya mifano ya uhusiano wa kijamii yenye msingi wa uchumi.

Uhusiano wa kiutani pia ni mojawapo ya desturi zilizobuniwa na wananchi ili kuziba pengo lililokuwepo kati ya jamii na jamii kuhusu uhusiano wa jamii. Utani uliwawezesha watu ambao hawakuwa na mawasiliano kuwasiliana bila tatizo lolote. Hivi sasa utani unasaidia na unaweza ukasaidia watu wanaofanya kazi mahali pamoja kuhusiana Vizuri, mradi tu desturi hii inazingatiwa na kauratibiwa vizuri. Utani unaweza ukatufaa katika kuvunja mipango ya ubinafsi na ukabila ambayo kwa hakika ni vikwazo vya maendeleo ya Ujamaa tuliyonuia.

MISINGI YA KUZUIA BIASHARA YA WATUMWA

Ingawa ni kweli kwamba biashara hii ilikuwa ya uchungu na ya aibu,Wazungu wenyewe walikuwa wameendesha biashara hii kwa miaka mia tatu. Sababu yao halisi ya kuzuia biashara ya watumwa ilitokana hasa na mabadiliko katika hali ya uzalishaji mali huko Ulaya na Amerika. Kiwango cha teknololjia na ufundi kwa wakati huo, kufuatana na maendeleo ya mgongano kati ya mbinu za kuzalisha mali na uhusiano wake wa kijamii, kilifikia mahali ambapo kazi nyingi zingeweza kufanywa na mashine kwa kutumia wafanyakazi wachache zaidi. Wakati huo mabepari wengi walishindana katika jitihada zao za kutumia vibarua waliopatikana kwa wingi na kwa urahisi ili kutumia mtaji wao na kueneza masoko yao. Pamoja na kutumia mashine ili kuongeza faida kwa kutolipa mishahara mingi, mabepari pia walikuwa na haja ya kuuza mashine zao na kueneza masiko yao kwa kuongeza idadi ya watu wenye uwezo wa kununua bidhaa zao. Kwa hiyo hapakuwepo tena na haja ya kutumia watumwa. Mfano huu ni uthibitisho kwamba maadili ya wanyonyaji na wanyanyasaji hayategemei zaidi utu, ila hutegemea zaidi faida wanayoweza kupata na maendeleo ya maslahi yao ambayo hayaheshimu utamaduni wa watu wengine hata kidogo. Ni Ujamaa peke yake ndiyo wenye maadili yanayothamini utu.

MISINGI YA NGOMA

Taifa letu lina utajiri mkubwa wa ngoma. Ngoma hizi kiasilia zina shabaha maalum ya kudumisha na kustawisha jamii. Ngoma za wavulana zina madhumuni ya kuwafanya wavulana waonyeshe utayari wao katika ushupavu na ujasiri katika suala la ulinzi.Zile za wasichana huonyesha zaidi utayari ea wakina mama katika kudumisha shughuli za nyumbani na uzazi. Ingawa ngoma zinatofautiana kutoka jamii moja hadi jamii nyingine, zote zimo katika makundi makubwa matatu.

Kundi la kwanza ni la ngoma ambazo shabaha yake ni kuwatayarisha au kuwakabidhi watu jukumu katika kuendeleza na kuzilinda jamii zao. Ngoma za namna hii ni kama vile ngoma za jando na unyago ambazo huwapa vijana jukumu jipya baada ya mafunzo maalum. Kundi la pili ni ngoma zinazochochea hamasa za kufanya kazi kulingana na taratibu za uzalishaji mali katika mazingira ya jamii. Bugobogobo kwa mfano, ni ngoma maarufu ya kuhimiza kilimo na kazi nyingine katika mazingira ya Usukuma. Kundi la tatu ni la ngoma zinazohusiana na dini kama vile matambiko, sherehe za mavuno na mazindiko ya mashamba na kaya.

Kuhusu ulinzi, ngoma huambatana na utenzi juu ya matukio mbali mbali na kuwasifu mashujaa wa vita. Jamii zinazoshambuliwa huiona vita kama kipingamizi cha kuzalisha mali. Ngoma na nyimbo katika sehemu za wafugaji husifu watu walioua samba au wanyama wengine wakalai. Hii ni kwa sababu ufugaji kama msingi wa maisha, unategemea ustawi wa mifugo. Wanyama wakali huwa ni kipingamizi cha uzalishaji mali. Ikitokea kuuwawa kwa wanyama wakali wanaotishia maisha na mifugo, jamii hufurahi na vielelezo vya furaha hiyo huwa ni pamoja na ngoma zenye kuipongeza jamii na kuwasifu mashujaa wa matukio hayo.

Watu wanaojitoa muhanga kuondoa vikwazo hivi hupata nafasi maalum katika jamii.

Kazi ya uwindaji ni ngumu nay a kubahatisha. Hivyo mawindo yakipatikana na watu wakishashiba, huwepo furaha. Ngoma huchezwa kama kielelezo cha mafanikio ya kazi yenyewe ya kuwinda. Wakulima mara nyingi hucheza ngoma na michezo yao mingine wakati wa kiangazi ambapo hapakuwa na uwezekana wa kulima. Ni wakati huo ndipo walipofanya shughuli mbali mbali za kustawisha jamii, kama vile ndoa na sherehe za jando na unyago. Na kama mvua zikichelewa kunyesha ngoma au nyimbo za furaha huahirishwa, na badala yake hufanywa matambiko. Nyakati za mvua zikiwadia, shughuli za ngoma na sherehe huachwa na watu hujishughulisha na kupanda mazao ili kuhakikisha uhai hapo baadaye.

Mifano yote iliyotolewa inaonyesha kuwa, kiasili, michezo na sanaa za maonyesho kama vile ngoma havikukwamisha kazi, bali vilikuwa na wajibu maalum katika kuimarisha na kustawisha jamii. Jamii zetu hazikuwa na taratibu za kuwa na ngoma ambayo madhumuni yake ni starehe tu. Kila ngoma ilikuwa na kazi yake maalum katika shughuli nzima za kijamii. Hii ndiyo maana kiasili wacheza ngoma hawakulewa pombe kwanza ndipo wakacheza, kwani walitambua kwamba kucheza ni sehemu ya kazi na siyo mzaha. Katika shughuli nyingi za utamaduni wetu, pombe ilitumika, lakini ulevi ulikuwa ni mwiko kwa vile wakati wote watu walitambua kuwa wako katika kazi ya kujenga na kulinda jamii yao.

MABADILIKO YA UTAMADUNI BAADA YA KUVAMIWA NA WAGENI

Wageni waliokuja nchini kwetu tangu karne ya 11 walikuwa hasa wa aina mbili wenye nia zilizofanana. Wageni hao walikuwa ni Waarabu na Wazungu. Nia yao kubwa ilikuwa ni kujenga msingi wa biashara kati yetu na kwao, biashara ambayo kulingana na matashi yao, ingefaidi nchi yao zaidi. Ujenzi wa msingi huu ulifanywa kwa namna tatu. Njia hizo ni kueneza dini yao ikiwa ni pamoja na mila na itikadi zao. Kuanzisha biashara katika maeneo yaliyokuwa na faida zaidi na tatu kutaka kutawala sehemu ya nchi yetu. Mafanikio yao katika malengo haya yalitofautiana kutoka sehemu moja hadi nyingine. Athari za Kiarabu zilistawi zaidi mahali ambapo Waarabu walikaa zaidi, na athari za Kizungu zilistawi zaidi pale ambapo Wazungu walikaa zaidi. Imani, michezo na taratibu nyingine katika jamii zetu zilivurugika kiasi Fulani, wananchi walifundishwa kufuata mambo ya kigeni na kufanywa waamini kuwa mambo yao yalikuwa ya kishenzi. Mavazi kama vile kanzu, baibui, suti na tai yalianza kuthaminiwa bila ya kujali uhusiano wake na uzalishaji mali ambao tumekwishauelezea. Lakini kuingiliwa huku kwa mavazi kwa mfano, kunaeleweka maana biashara ya nguo ndiyo iliyokuwa nguzo mojawapo kubwa ya uchumi wa kibepari siku hizo.

Mashindano na uhasama baina ya makundi hayo mawili ya wageni viliendelea na hatimaye kuenea kwa wafuasi wa makundi hayo, hivyo kuvuruga umoja wa kijamii, ambao ni sharti moja la lazima kwa ustawi wa Utamaduni. Kila kundi lilijitahidi kuimarisha upande wake kwa kuwatafuta watu wa kufanya kazi kwa niaba yake. Hivyo, shule za dini zilianzishwa ili kuwapata walimu wa dini. Mbali na kusoma wanafunzi walifundishwa kuyakataa mambo ya dini nyingine na pia kuyakataa mambo yao ya asili. Zaidi ya hayo, wafuasi wa dini moja walikatazwa kuwaoa wafuasi wa dini nyingine hata kama kimila hawakuwa na kipingamizi cho chote. Hivyo kinyume cha matarajio, dini ikawa ni chombo cha kuwatenga watu na kupandikiza chuki kati yao, badala ya kuwa chombo cha umoja, amani na upendo kama ilivyokuwa hapo awali.

Taratibu za urithi nazo ziliingiliwa na mgawanyiko wa dini. Watoto walinyimwa urithi na wazazi wao kwa sababu ya kufuata dini tofauti na wazazi wao. Dini na athari nyingine zilizoambatana nazo zilileta aina mpya ya mgawanyiko katika uzalishaji mali, licha ya kwamba dini mpya ziliweza kuunganisha watu katika makundi makubwa chini ya imani moja, bila ya kujali kabila, rangi au maumbile.

Kufuatana na siasa ya ubeberu, mabepari wan chi za Ulaya waligawana Afrika katika sehemu na kila nchi kuleta wafanyabiashara wake pamoja na wanajeshi wa kulinda maslahi yake. Nchi yetu iliangukia mikononi mwa Wajerumani, ambao walianzisha unyonyaji wao wa kikoloni kwa kutumia kampuni yao ya biashara. Hii ilitokea baada ya Karl Peters kufanya mikataba na viongozi wa jadi ili kupata ardhi na kuandaa ueneaji wa utawala wa Kijerumani katika nchi nzima. Kwa hiyo, Wajerumani walianza kushika shughuli za uchumi na biashara badala ya Waarabu. Pale ambapo vishawishi vyao vilikataliwa walitumia nguvu, jambo ambalo lilisababisha mapambano kati yao na Waarabu. Mapigano kati ya Bushiri na Wajerumani ni mojawapo ya migongano ya namna hiyo. Waafrika walitambua mapema sana kuwa kutawaliwa na wageni kungeharibu kabisa mfumo wa maisha yao ikiwa ni pamoja na kuangamiza utamaduni wa Mwafrika. Mkwawa ni mfano mzuri wa viongozi wa wananchi waliokataa kabisa kutawaliwa na wageni na akapigana nao mpaka kuwa kwake.

Pamoja na kushika biashara badala ya Waarabu, utawala wa Kijerumani ulichukua ardhi nzuri ya nchi ili kuwawezesha baadhi ya Wajerumani kuishi hapa na kuanzisha mashamba makubwa ya kutoa malighafi kama vile pamba, katani na kahawa kwa ajili ya viwanda vya Ujerumani. Kwa sababu mabepari wa Kijerumani walitumia mtaji wa kuzalisha mali, kulizuka haja ya kuwa na vibarua. Mifumo ya uzalishaji mali ya asili ilizuia uwezekana wa kuwepo vibarua, maana iliwalazimisha watu kujitegemea. Kwa kuwa mashamba yalihitaji vibarua wengi na vibarua hawakuwepo, utawala wa Kijerumani ulitumia mbinu mbal imbali za kuwakamata watu kwa nguvu huko vijijini na kuwasafirisha hadi kwenye mashamba. Mtindo huu wa manamba uliende. Kwa hiyo, Wajerumani walivuruga sharti lingine la maendeleo ya utamaduni ambalo ni lile la watu kuzalisha mali chini ya mipango yao wenyewe na kwa manufaa ya jamii yao. Wananchi walilazimishwa kupanda mazao ya biashara kwa ajili ya viwanda na masoko ya Ulaya na kuwawezesha kununua bidhaa kutoka kwenye viwanda hivi. Ujira waliolipwa vibarua hawa ulikuwa wa chini sana.

Pamoja na kulazimishwa kupanda mazao ya biashara, wananchi walilazimisha kulipa kodi ambayo viwango vyake vilipangwa kiwilaya na wala sio kulingana na uwezo wa mlipaji. Wananchi wengi walioshindwa kulipa kodi walilazimishwa na serikali ya kikoloni kufanya kazi kwa muda maalumu badala ya kodi. Kazi walizofanya zilikuwa ni kubwa zaidi kuliko kiwango cha kodi waliyodaiwa. Madhumuni ya kuwalazimisha wananchi kulipa kodi na kutafuta pesa kwa kuanya kazi kama vibarua au kwa kupanda mazao ya biashara, ilikuwa kuanzisha mfumo wa uzalishaji mali wa ubepari wa kikoloni hapa nchini. Mfumo huu uliambatana kama pete na kidole na utamaduni wa kibepari. Katika kufanya hivyo utawala wa kikoloni ulikuwa chombo cha mabepari. Hiyo ndiyo sababu mojawapo iliyowafanya watawala wa Kijerumani wawe wakatili mno.

KUTENGULIWA KWA MISINGI YA MALEZO NA UONGOZI

Shule zilijengwa ili kuongeza watu wenye uwezo wa kufanya baadhi ya kazi kwa niaba ya Wakoloni. Walitakiwa makarani kukusanya kodi, walimu wa dini, karani wa mashamba na kadhalika. Kama tulivyokwishaeleza, mafunzo yote yaliyotolewa yalitukuza ubora wa mambo ya wageni na ubaya wa mambo yetu ya asili. Mafunzo na vishawishi vingine yaliambatana na sheria kali kuhakikisha kwamba masharti ya wakoloni yanafuatwa.

Sehemu ambazo viongozi wa jadi hawakutambuliwa au walikataa kushirikiana na utawala wa kikoloni, waliwekewa maakida. Kazi ya maakida ilikuwa ni kuhakikisha kwamba amri za Wakoloni zinafuatwa. Wao walikuwa ni wawakilishi wa watawala na hawakujali Utamaduni wa wananchi ukijumlisha matakwa na matatizo ya wananchi na sehemu zao za kazi. Kazi ya maakida ilizidi kuwa ngumu kwa sababu mara nyingi hawakuelewa utamaduni wa watu. Hii iliwafanya wadharauliwe na kuwafanya wategemee zaidi mabavu na amri katika kulinda maslahi ya Wakoloni. Kuwachapa watu viboko kwa mfano, likawa ni jambo la kawaida.

Mfumo wa uzalishaji mali wa kibepari ulioanzishwa na kusisitizwa na Wakoloni ndio uliokuwa mwanzo wa vijana kuviacha vijiji vyao kwenda kutafuta kazi sehemu nyingine. Baadhi ya vijiji vilibakiwa na wazee, kina mama na watoto. Hii ilisababishwa na njia mbali mbali zilizotumiwa kuwapata vibarua ambazo zimekwishaelezwa. Utaratibu huu ulivifanya vijiji kupungukiwa na watu wenye uwezo wa kufanya kazi, jambo ambalo lilipunguza uwezo wa kuzalisha mali, maana vijana ndio sehemu muhimu yenye nguvu katika jamii na katika mbinu za kuzalisha mali. Wazee hawakuwa tena na watu wa kuwahudumia katika mahitaji yao mbali mbali. Vijana nao hawakuwa na watu wa kuwategemea huko walikokwenda kwa upande wa mashauri na misaada wakati wa shida. Huu pia ndio ulikuwa mwanzo wa kupotea kwa mapokeo yetu. Hiki ndicho chanzo cha vijana kutaka kuiga ovyo ovlyo mambo ya wageni kwa vile walikosa maelekezo ya jadi yao kutoka kwa wazee.

Maisha ya ndoa nayo yaliathiriwa, maana wanaume waliwaacha wake zao vijijini kwa muda mrefu, jambo ambalo lilikuwa geni. Watoto wadogo waliyakosa malezi ya baba zao kwa muda mrefu. Baadhi ya wanaume walirudi na wake wengine au waliwakuta wake zao wameshazaa nje ya ndoa. Kwa njia hizi zote mfumo huu wa uzalishaji mali uliathiri malezi ya asili na kuleta mfarakano katika maisha ya ndoa, pamoja na kuanzisha tabia ya uvivu, ulevi, uzururaji, uhalifu na maovu mengine mengi kama hayo.

UTAMADUNI NA UTAWALA WA KIINGEREZA

Utawala wa vitisho wa Wajerumani uliwachukiza wananchi na hata ukasababisha vita vya Maji Maji. Vidta vya Maji Maji vilikuwa ndiyo ushindi mkubwa wa utamaduni hapa nchini. Katika vita hivi babu zertu walisahau vikwazo na vitofauti vidogo vidogo na badala yake kujumuika pamoja kupinga uvamizi. Walitumia imani yhao katika dawa kama kiungo cha umoja wao. Na pia walijumuisha silaha zote walizokuwa nazo katika kumkabili adui. Ingwa Wajerumani walifanikiwa kuwashinda wapiganaji wa vita vya Maji Maji, matokeo ya vita hivi yaliwalazimisha Wajerumani kutumia mbinu tofauti katika kuendeleza utawala wao wa kikoloni. Tangu hapo walisisitiza zaidi maendeleo ya kiuchumi ya wakulima kwa kuwavutia zaidi katika mfumo wa uzalishaji wa mazao ya biashara kama vile pamba, ufuta na mibuni badala ya kuwashurutisha sana kufanya kazi katika mashamba ya walowezi.

Haikuwepo tofauti kubwa baina ya utawala wa Kiingereza na ule wa Kijerumani. Madhumuni yao yalibaki kuwa yale yale, yaani kuhudumia mahitaji na kukuza utamaduni wa mabepari wa kwao. Jambo jipya ni kuwa mambo ya Kiingereza yalisisitiza na mambo ya Kijerumani yalisahauliwa. Mila na desturi za Kiingereza zilianza kuenezwa na hasa lugha ya Kiingereza.

Waingereza walitumia mbinu za kijanja ili kuonekana kwamba wai walikuwa wapole zaidi kuliko Wajerumani. Walijitahidi kujificha nyuma ya watu wengine. Katika kutawala kwa mfano, walianzisha Tawala za wenyeji na katika uchumi, biashara ndogo ndogo zilishikwa na wageni walioingia hasa kutoka Asia. Waingereza wenyewe waliendesha kazi ya biashara ya nje pamoja na kazi ya kutoa malighafi kwa niaba ya mabepari wa huko Uingereza. Walitumia mbinu hizi kusisitiza unyonge wa Wazalendo. Kwa kusisitiza unyonge huu, walitambua kuwa wananchi watapoteza ile hali ya kujiamini na kujithamini. Baada ya hapo ingekuwa rahisi sana kuwadhalilisha na kuuzima utamaduni wao. Msingi wa ubaguzi wa rangi ulitokana na mfumo huu wa ubepari na ukoloni.

KUVURUGIKA KWA MISINGI YA UCHUMI YA WAINGEREZA

Waingereza waliona ya kuwa njia mojawapo ya kuimarisha na kudumisha ubaguzi wa kikabila ni ile ya kutukuza sana utawala bandia wa makabila. Walijaribu kutumia vibaya hali ya kuweko kwa makabila kwa kueneza sumu ya gawanya utawale. Kadhalika walijaribu kuvika watu vilemba vya ukoka kwa kuwafanya waamini walikuwa na serikali zao za kikabila zilizoshirikiana na utawala wa kikoloni. Ukweli ni kuwa utawala hasa ulikuwa ni mmoja tu, nao ni wa kikoloni na vingine vyote vilikuwa ni vyombo tu vya utawala wao.

Upungufu wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi vijijini na upungufu wa ardhi nzuri ya kustawisha mazao ya chakula, ulipunguza sana uwezo wa wananchi kujitosheleza kwa chakula. Watu walipaswa kutumia fedha kupata mahitaji yao ya lazima badala ya kuyalima wao wenyewe, maana uwezo wao wa kufanya hivyo ulikuwa umeshavurugwa kufuatana na mabadiliko yaliyoletwa na mfumo wa ubepari na ukoloni. Pia msukumo huu wa kuzalisha mali kwa ajili ya biashara uliwafanya watu waanze kuthamini fedha kuwa ni msingi wa maendeleo yao. Hii ndiyo maana tunakuta baadhi ya watu walianza kukwepa kazi za mikono na hasa kilimo na badala yake wakatafuta kazi za kuajiriwa au biashara ndogo ndogo ambazo hata hazikidhi haja zao za lazima. Lakini kazi za kuajiriwa na biashara ndogo ndogo wakati huo zilikuwa zinaleta tama ya kufanana fanana na mabwana wanyonyaji.

Ulimaji wa mazao ya biashara ulibadilisha taratibu za umilikaji wa ardhi. Katika sehemu nyingine, kwa mfano, badala ya ardhi kuendela kuwa nyenzo maalumu ya uzalishaji mali ambayo ilimilikiwa kwa pamoja, ardhi ilianza kumilikuwa kibinafsi na hata kuuzwa kama bidhaa nyingine. Mabadiliko haya yaliwafanya wenye fedha nyingi kununua na kujilimbikizia ardhi kwa matumizi yao, au kwa kukodisha au kama dalili ya utajiri. Mambo hayo yote yalisababisha kuzuka kwa matabaka miongoni mwa wananchi.

Kuingizwa kwa bidhaa kutoka nchi za nje kulifanya ufundi wetu wa asili na viwanda vidogo vidogo kufifia. Bidhaa hizi zililetwa kwa wingi sana na kuzifanya bidhaa zilizotengenezwa katika viwanda vyetu vidogo zisithaminiwe. Jambo hili liliwafanya mafundi wa asili kama vile wahunzi, wafinyanzi, wachongaji na wasukaji kupoteza ujuzi na umuhimu wao katika jamii. Wananchi walishawishiwa na kuamini kuwa kila kitu walicholeta wakoloni, hasa nchi iliyokuwa inatawala kwa wakati huo, kilikuwa bora. Wakati wa kutawaliwa na Wajerumani, kwa mfano, bidhaa zilizotengenezwa Ujerumani ziliaminiwa kuwa ni bora sana. Baada ya kuwa chini ya Waingereza imani hii ilibadilika na badala yake bidhaa toka Uingereza zikaaminiwa kuwa ni bora zaidi. Kila kitu kizuri kilisemekana kuwa ni cha Kizungu na kitu kibaya kilisemekana kuwa ni cha Kiafrika. Mpambanuo huu, ambao masalia yake bado yapo, haukuwa na uhusiano wowote na hali halisi ya uzalishaji mali au vitu vyenyewe vilivyopambanuliwa, bali ulitokana na itikadi ya kibepari ambayo ilienezwa na kusisitizwa na taasisi zote za kikoloni.

Upo ushahidi kuonyesha kwamba baadhi ya vyombo vilivyotengenezwa na mafundi wetu wa asili vilikuwa bora zaidi kuliko tulivyouziwa na mabepari, kwa mfano, majembe ya mkono. Ufundi huu haukuendelezwa na badala yake ulidhalilishwa na kupigwa vita. Matokeo yake ni kwamba ujuzi wa ufundi wa kijadi ulianza kutokomezwa, na hivyo kuua kabisa msingi wa kiteknolojia wa Kitanzania ambao ungewezesha ugunduzi wa vyombo na mashine nyingi.

Wakoloni walitufundisha kuheshimu bendera na nyimbo za mataifa yao, kuwaabudu viongozi wao, na kupenda kutumia lugha zao. Pesa na stampu tulizotumia wakati huo zilikuwa na picha na maandisha ya watawala wa kikoloni. Vielelezo vyote vya fwakati wa ukoloni vilisisitiza ubora wa wageni waliotutawala. Ili mradi vyote hivyo vilisaidia uzalishaji mali wa kibepari. Njia zote za usafiri zilizojengwa wakati huo ziliunganisha bandari na vitovu vya uzalishaji mali za mabepari kama vile mashamba na migodi. Sehemu ambazo hazikuwa na shughuli za uzalishaji mali za kutosheleza kuleta faida kwa mabepari hazikushughulikiwa kimawasiliano. Pia huduma nyinginezo ziliwekwa katika sehemu ambazo zilitarajiwa kuwapatia mabepari faida. Kwa njia na viwango mbali mbali, matukio haya na mengine mengi yaliingilia na kuathiri sana maendeleo ya utamaduni pamoja nay ale ya aina nyingine.

UTAMADUNI TANGU UHURU

Kupatikana kwa Uhuru kulileta matumaini mapya miongoni mwa wananchi. Kwa mara ya kwanza tuliunganishwa na serikali moja ambayo ilitetea maslahi ya wananchi kwa jumla na ambayo ilitokana na jitihada zetu za pamoja chini ya TANU kupingta ukoloni. Badala ya watawala wa kikoloni tulikuwa na viongozi wananchi, badala ya kuimba wimbo wa Taifa la Kiingereza tulitunga wimbo wetu wa Taifa, na badala ya kupandisha bendera ya Kiingereza tulipandisha bendera ya Taifa letu.

Hatua hii ilikuwa ya maana sana kwetu, maana tuliweza kutumia vielelezo tunavyovielewa na ambavyo vina umuhimu wa misingi katika maisha na jadi yetu kama Taifa. Wimbo wetu wa Taifa ni sala kwa Afrika na Tanzania ambamo tunaombea baraka Bara letu na nchi yetu, na kwetu sisi na viongozi wetu, na ni sala inayosisitiza umoja wetu na ule wa Bara la Afrika. Bendera yetu ya Taifa ilitengenezwa kwa rangi zenye maana maalumu kwa Taifa letu. Rangi nyeusi inamaanisha sisi Watanzania, rangi ya Manjano inamaanisha ardhi, kijani inamaanisha mazao yetu na abluu inamaanisha bahari inayotuunganisha.

Mara tu baada ya kupata uhuru, kupepea kwa bendera ya Taifa na kuimbwa kwa wimbo wa Taifa havikubadilisha utaratibu na hali ya maisha wakati huo. Tuliendelea kuwa na hali ambayo ilitokea kufuatana na mgongano kati ya mbinu za kuzalisha mali na uhusiano wake wa kijamii. Yaani tuliendelea kukabiliwa na uchaguzi kati ya utamaduni ulio na misingi katika mfumo wa uchumi wa asili na utamaduni wa kupandikiza wenye misingi ya kibepari.

HATUA ZA KUFUFUA UTAMADUNI WETU

Ili kubadilisha utamaduni wetu ni lazima kwanza tubadilishe mbinu zetu za kuzalisha mali. Hii ni kwa vile uhusiano wa kijamii huelezwa hasa na uhusiano uliopo kati ya mbinu za kuzalishia mali na wazalisha mali, na uhusiano uliopo kati ya wazalisha mali katika jamii. Wakoloni kwa kumiliki na kuongoza mbinu za kuzalisha mali kulingana na shabaha zao, waliweza kutufanya tusijiamini sisi wenyewe na kutuon- dolea utu wetu. Ni kwa kumiliki ardhi na mali nyingine za asili ndiko kulikowawezesha kututawala na kutunyonya. Kwa kupotosha mbinu za umilikaji wa mali, ili zisilingane na utaratibu wa jamii zetu waliweza kutufilisi Utamaduni wetu na kutugeuza tuwe kama vivuli vyao na kuiga mila na desturi zao. Hivyo hatua ya kwanza ya Serikali yetu katika kuimarisha uhuru na kukuza utamaduni wetu, ilibidi iwe kutaifisha ardhi yote ili wananchi waweze kupata ardhi ya kujilimia mazao yao na kuzalisha mali bila vipingamizi. Tukitambua ardhi kama chimbuko la uzalishaji mali na maendeleo ya binadamu, itaonekana kuwa kutaifisha ardhi ilikuwa pia ni hatua ya kimapinduzi ya kujikomboa kiutamaduni. Hatua nyingine kama vile kurekebisha mfumo wa uchifu, kuondoa kodi ya kichwa na kufuta ada katika shule na hospitali ya serikali, zilipanua uwanja wa kutuwezesha kufufua utamaduni wetu katika misingi ya umoja na usawa.

Makovu na maradhi yaliyoachwa na wakoloni dhidi ya utamaduni wetu yatachukua muda mrefu kupotea. Pamoja na jitihada zote zilizofanywa, bado zilikuwepo kasoro nyingi, na baadhi yake zilikuwa zinaendelea na kupanuka. Kwa mfano, uzururaji mijini ulikuwa unaongezeka kwa sababu ya kishawishi cha kukimbilia mijini ili kutafuta kazi za mishahara au biashara ndogo ndogo. Ongezeko katika bei ha mazao ya kilimo liliwafanya wakulima matajiri na makabaila kupanuka zaidi na wale maskini liliwafanya kuwa maskini zaidi. Mikopo ya kufanyia shughuli mbali mbali iliendelea kutolewa kwa makabaila na watu wenye madaraka na mishahara mikubwa, kufuatana na mfumo wa uzalishaji mali wa kibepari.

Makundi ya kitabaka yaliendelea kuonekana, lugha kama chombo cha mawasiliano ya umma, ilipata maneno mapya ya kuyatambulisha makundi haya. Watu wenye madaraka na kipato kikubwa waliitwa manaizi na wenye kipato kidogo waliitwa kabwela. Manaizi walikaa Uzunguni, yaani sehemu zilizokaliwa na Wazungu kabla ya kupata uhuru. Kwa kifupi, mfumo wa jamii ulikuwa bado ni wa kibepari kwa kila hali, ingawa mabadiliko yalikuwa yameanza kuonekana.

Kutangazwa kwa Azimio la Arusha mwaka 1967 ulikuwa ni mwanzo wa hatua za kubadilisha mfumo wa uzalishaji mali wa kibepari hapa nchini. Njia kuu za kuzalisha mali kama vile mabenki na viwanda zilitaifishwa. Viongozi waliwekewa miiko ili wasitumie nafasi zao kujilimbikizia mali. Azimio pia lilisisitiza kujitegemea badala ya kutegemea misaada kutoka nchi za nje. Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ilianza kuwa msingi wa shughuli zote za Taifa. Mwaka huo huo Mwalimu Nyerere alitoa msimamo juu ya Elimu ya Kujitegemea na juu ya Ujamaa na Maendeleo vijijini. Hivyo kutangazwa kwa Azimio kulikuwa ni mwanzo wa Mapinduzi halisi ya Utamaduni wa Mtanzania.

Uanzishaji wa vijiji umekuwa ni hatua ya kuunda viungo maalumu vya kuzalisha, kumiliki na kutumia mali badala ya familia za asili ambazo zilikuwa viungo vidogo, mbali na kwamba zilivurugwa na utawala wa kikoloni na mfumo wa uzalishaji mali wa kibepari. Jambo kubwa ambalo limesisitizwa katika vijiji ni demokrasi, yaani uhuru wa wananchi kuamua mambo yao wenyewe. Hii inawapa moyo wa kujiamini, kujithamini na kutumia uwezo wao katika kuleta mapinduzi ya kijamaa hapa nchini, chini ya Chama cha Mapinduzi. Ili kuwasaidia wananchi katika kazi hii, taasisi mbali mbali zimeundwa kitaifa kusimamia utekelezaji wa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea nchini. Na ingawa taasisi hivi zinajitahidi kutekeleza wajibu wake, baado kuna mambo kadhaa ya msingi ambayo yanahitaji kuzingatia katika kuongeza ufanisi wa utekelezaji, kufuatana na jinsi taasisi hizi zinavyoendelea kujikomboa kutokana na kusumbua za ubepari zikiwa ni pamoja na uzembe, ulaji wa rushwa na magendo.

Sisi Watanzania tumekubaliana kwamba maendeleo yetu ni lazima yawe ni maendeleo ya watu. Yakubalika pia kwamba ili watu waweze kuendelea kidhati ni lazima waheshimu kazi na wawe na ufundi. Kusema kweli kila utamaduni una ufundi au teknolojia ya aina Fulani. Lakini teknolojia inaweza kuwa ya manufaa kwa watu kama itakuwa inampunguzia mwanadamu mzigo mzito alio nao kutokana na uwezo wake mdogo wa kuyakabili mazingira yake na hivyo kuimarisha uhusiano mzuri na wa amani na majirani zake, ambao kwa pamoja ndio wanaunda utamaduni wa jamii.

Kwetu sisi kutokana na hali ya hivi sasa ya uchumi wa dunia unaoongozwa zaid ina mahitaji na utashi wanchi za kibeberu, inatulazimu kuwa katika mstari wa mbele kwa kutumia utamaduni wetu kama chombo cha ukombozi dhidi ya hila za kibeberu. Wakoloni walijaribu kuuangamiza utamaduni wetu ili watutawale. Sisi hatuna budi kuutumia utamaduni katika kuzingatia maendeleo ya kijamaa na hivyo kukamilisha ukombozi wetu. Ili kutumia utamaduni kwa njia hii utamaduni lazima uwe wa watu. Jambo hili ni lazima lizingatiwe na wafanyakazi wote. Ni lazima hawa waelewe kwamba wana jukumu la kuwatumikia watu kwa ari kubwa na moyo, na muhimu zaidi ni lazima wauelewe utashi na misingi ya uhai wa jamii na kujiunga na umma katika kuendeleza utashi huo; na kudumisha vile vilivyo na tunu mioyoni mwao, kama kielelezo halisi cha hali ya maisha yao na uhusiano wao wa kuzalisha mali, na uhusiano wa kimazingira. Kazi yoyote inayofanyiwa umma ni budi itokane na mahitaji ya umma na siyo matashi ya watekelezaji.

Tukizingatia umuhimu wa Utamaduni katika upeo huu mpana, ndipo tunaweza tukatumia vipengele vya utamaduni kuwa ni vielelezo halisi vya msingi wa uchumi, na kuwa kwa wakati huo huo, ni vyombo mahsusi vya kuubadilisha msingi huo. Kwani ukweli ni kwamba vipengele kama hivyo ndivyo vielelezo vya misingi ya ujuzi wa Kisayansi uliopo katika jamii.

Hivyo njia pekee ya kutekeleza mapinduzi ya kweli ni kutambua kwa dhati kwamba licha ya utamaduni kuwa ni tunda la maendeleo ya jamii, utamaduni pia ni chombo kikubwa ambacho knaweza kikatumiwa katika kutukwamua kutokana na minyororo ya ujinga, umaskini na maradhi. Lakini jambo hilo linaweza kutokea tu, tukitambua zaidi na zaidi undani wa utamaduni wetu na msingi wake. Ni lazima tutambue kwamba msingi halisi wa Utamaduni ni kazi, na kwamba vipengele vyote vya utamaduni ni vielezo tu vya juhudi zetu katika kutekeleza kazi ambayo ndiyo msingi wa uhai wetu. Na uhai wetu ndio msingi wa uhai wa jamii. Ni katika msingi huu ndio utamaduni unakuwa sio tu kielelezo cha utashi na uhai ta Taifa, lakini pia roho ya Taifa hilo.

SURA YA PILI

JINSI SANAA INAVYOSAIDIA

MAENDELEO YA UTAMADUNI

Sanaa ni fani muhmu ya utamaduni. Kama ilivyoelezwa katika sura iliyopita, utamaduni ni matokeo ya juhudi za mwanadamu kupambana na mazingira ili audumishe uhai wake. Juhudi hizi zimekuwepo tangu mwanadamu alipotokea. Kwa hiyo tunaweza kusema kuwa sannaa zilianza tokea hapo. Wachunguzi wa mambo ya kale, kwa mfano wamegundua zana nyingi zilizotengenezwa na kutumiwa na watu wa kale wa sehemu mbali mbali za Tanzania. Vile vile kuna michoro ya aina mbali mbali iliyotengenezwa na watu wa kale katika mapango kama yale ya Kondoa.

Si rahisi kutoa maelezo ya kitu au dhana yoyote yanayokubalika na watu wote. Kama tungewaomba watu mia moja kutoa maelezo ya maana ya sanaa, inawezekana tungepata aina mia moja tofauti za maelezo. Wengine wanaelewa sanaa kuwa ni michongo ya sura mbal imbali za wanadamu au wanyama. Wengine huchukulia sanaa kuwa na maana ya uchoraji wa namna mbali mbali, ambapo baadhi wanalielewa neno hili kuwa maana ya mashairi au hadithi. Tofauti hizi mara nyingi husababishwa na tofauti za mazoea na mazingira ya watu au jamii. Ni wazi kwamba mtu ambaye amekulia katika jamii ambayo ni wachongaji wa sanamu za wanyaama, ataelewa maana ya sanaa kuwa ni michongo ya wanyama, vivyo hivyo mtu aliyekulia katika jamii iliyo hodari katika ushairi ataelewa sanaa kuwa ni mashairi. Tatizo la pili linatokana na matumizi ya neno Sanaa katika kuwakilisha fani zote zilizo katika kundi hilo moja. Wengi walizitambua fani zinazohusika kwa majina yake mahsusi yaani ngoma, nyimbo, michongo, hadithi, mashairi au sarakasi.

Kwa kifupi, sanaa ni ustadi wa kuweka na kupanga fikra kwa njia ya hisia au zana. Inaweza ikawa ni kitu, utaratibu wa kuchezesha mwili, miondoko, utoaji wa sauti, uzungumzaji au uandishi wenye mpangilio maalum ikiwa na lengo la kutoa ujumbe, kukidhi matumizi ya namana mbali mbali au kupamba. Fundi wa Sanaa msanii ni muumbaji wa namna yake. Yeye huyapanga mambo kama anavyotaka na kwa njia aipendayo, ili mradi tu afikie lengo lake. Katika kufanya hivyo ana uhuru mkubwac sana. Ingawa itambidi ajifunze kutoka kwenye mazingira yake na kuheshimu mipaka aliyowekewa na jamii yake, anaweza kuumba atakavyo. Uhuru huu ni pungufu kidogo kwa upande wa msanii wa zana. Msanii huyu anaongozwa na matumizi ya zana anayotengeneza. Hakuna maana ya kutengeneza mtemba usio na tundu la kuwekea tumbaku au kiti kisichoweza kukaliwa.

Sanaa zinaweza kugawanywa katika makundi matatu kufuatana na matumizi yake. Kundi la kwanza ni sanaa za hisia au kujieleza. Sanaa hizi zina lengo la kutoa ujumbe kwa jamii kama njia mojawapo ya kutoa elimu, kuleta mabadiliko ya namna mbali mbali au kama msukumo wa kazi na ibada kama vile ngoma, tamthiliya, fasihi andishi na fasishi simulizi kama vile mashairi na hadithi, picha za filamu, uchongaji, ufinyanzi na ufuaji wa sanamu na uchoraji wa picha. Kundi la pili ni sanaa za mapambo, ambazo mara nyingi huitwa nakshi. Huu ni ustadi wa kuweka marembo kwenye vitu mbali mbali kama vile vyombo vya nyumbani, nguo na mavazi, nyumba na fanicha. Kundi la mwisho ni sanaa za zana ambazo zinajulikana na wengi kama ufundi wa mikono. Huu ni utengenezaji wa vitu vinavyotumiwa katika maisha ya kila siku. Mifano ni vyungu, vikombe, visu au viti. Mara nyingi sanaa hizi za kundi la tatu huwekewa sanaa za nakshi au za kujieleza. Kwa mfano kuna vikombe vilivyowekewa marembo ya namna mbali mbali, au visu vilivyowekewa sanamu za binadamu au wanyama kwenye mipini.

Katika jamii za kiasili, kabla utamaduni wetu haujaathiriwa na mataifa ya nje, sanaa zote ziliundwa kama sehemu ya kazi na shughuli mbali mbali za jamii. Kulikuwa na ngoma au nyimbo ambazo zilikuwa msukumo wa kazi za kilimo, uchungaji, uwindaji, vita, utwangaji au usagaji, zilikuwepo ngoma, muziki na michongo iliyotumiwa kama sehemu ya ibada au matambiko. Hadithi, nyimbo na masimulizi ya aina mbali mbali yalitumiwa kama mbinu ya kuelimisha watoto na vijana ili kuwatayarisha katika jukumu lao la kuendeleza uhai na maslahi ya jamii zao. Usanii wa zana ulikuwa ni fani muhimu sana ya kuipatia jamii vifaa mbali mbali walivyohitaji katika shughuli zao za majumbani na uzalishaji mali.

Baada ya kuja kwa wageni elimu mpya ilianzishwa na ilikuwa na misingi na utaratibu tofauti na ile ya kijadi. Malengo ya elimu ya kikoloni yalikuwa ni kumjenga Mtanzania ili akidhi maslahi ya watawala hao na kuwa mnyapara wa maslahi ya mabepari. Kwa hiyo sanaa zetu zikawekwa kando na vijana wakaanza kufundishwa sanaa za kigeni. Ili mtu aweze kukubali kama amestaarabika, ilikuwa lazima kwa mfano aonyeshe uwezo wake wa kucheza dansa za kizungu, awe mwendaji wa mara kwa mara kwenye maonyesho ya picha za filamu za Kizungu, awe na uwezo wa kuelewa fasihi ya Kizungu au aweze kuchora picha kwa misingi ya Kizungu. Baadhi ya waliosoma, walifanywa Wazungu weusi. Badala ya kuwa mbele katika kutetea heshima na maendeleo ya sanaa za Waafrika, wakawa askari wa mkoloni katika kuzipiga vita.

Kwa ujumla zipo sababu tatu zilizowafanya Wakoloni waamue kupiga vita sanaa zetu. Sababu ya kwanza ni kwamba walipokuja hawakuelewa maana na madhumuni ya sanaa zetu. Badala ya kujaribu kujifunza zaidi, walijiamulia kuwa hatuna sanaa nzuri na kwamba tulistahili kurithishwa sanaa zao. Sababu ya pili ilitokana na ukweli kwamba utamaduni wa mtu hukamilisha utu wake. Mtu aliyejengekea katika misingi ya utamaduni wake mwenyewe ni mtu anayejiona huru na hujithamini. Hakika hisia kama hizi ni za hatari kwa mtu anayetaka kumtawala mwenzake. Walifahamu kuwa wakituondolea utamaduni wetu ingewawia rahisi kututawala na kutunyonya kwa kuwa sasa hisia za uhuru na fahari zingekuwa zimepotea. Sababu ya mwisho ilikuwa ya kibiashara. Jambo moja muhimu lililosababisha ukoloni ni matashi ya mabepari kupata masoko, ambayo wanaweza kuuzia bidhaa walizotengeneza katika nchi zao, na kununulia mali ghafi kwa ajili ya viwanda vyao. Kwa hiyo ilikuwa muhimu vile vile kujenga moyo wa kupenda bidhaa za Ulaya katika nchi walizotawala. Ni wazi kwamba kama wangewaacha Watanzania katika misingi na maendeleo ya sanaa zao, wasingeweza kuuza bidhaa zao kwa kiwango kikubwa.

SANAA KATIKA MAWASILIANO

Sanaa ni chombo chenye nguvu sana katika kuleta mafanikio au elimu inayotarajiwa. Ni kweli kwamba si sanaa peke yake ambazo zinafanya mambo hayo, lakini nguvu zake ni kubwa kuliko ambazo zinafanya mambo hayo, lakini nguvu zake ni kubwa kuliko hotuba, maandishi au mazungumzo ya kawaida. Sio suala rahis kuleta mabadiliko katika jamii. Watu wengi huamini kuwa hali ilivyo ni sawa tu, haina kasoro. Kwa hiyo tunapotaka kuleta mabadiliko, iwe kwa nia njema au mbaya, inahitaji maelezo ya ushawishi w hali ya juu. Mambo hayo ni rahisi kutekelezwa kwa njia ya sanaa kuliko njia nyingine yoyote. Hii ni kwa kuwa sanaa hutumia kivutio cha uzuri na mifano ya kimatendo badal ya maneno matupu. Kwa sababu ya nguvu hizi, sanaa hutumiwa na mabepari hali kadhalika wajamaa katika kutetea maslahi yao.

Katika mfumo wa kibepari sanaa zinatumiwa kutetea maslahi ya waatawala na wanyonyaji. Kwa hiyo utakuta ujumbe wa sanaa zao huficha ukweli, na kuyaelezea mambo kama ni sawa yalivyo na kwamba hayawezi kubadilishwa. Wasanii wengi hawajihusishi na Umma pamoja na matatizo yake. Badala yake wao huwa ni vibaraka wa watawala na wanyonyaji.

Sanaa katika Ujamaa zimeshikamana na shughuli zote za maisha ya watu. Huambatana na fikra sahihi za watu hao, historia yao na matumaini yao. Nchi yetu inafuata misingi ya Ujamaa na Kujitegemea. Katika mfumo huo msanii ni sehemu ya umma. Yeye ni sehemu ya umma. Msanii ana jukumu la kuburudisha Umma na kuwa mtetezi wake. Jukumu lake ni kutoa ukweli, kuupa mwamko wa kuzalisha mali, ili umma uweze kukabiliana na mazingira yanayohusika. Kwa hiyo sanaa kama kielelezo kama silaha ya mapambano, kama msukumo wa maendeleo ya Taifa, ni lazima zihusishwe kikamilifu katika juhudi zetu za kujikomboa, kujenga Ujamaa na juhudi zetu za kujitegemea. Sanaa za Kitanzania ni lazima zimtetee mkulima na mfanyakazi.

SANAA KAMA KIELELEZO CHA HISTORIA

Sanaa ni kielelezo cha Historia ya maendeleo ya Taifa. Zaidi ya kuwa kielelezo vile vile Sanaa huweza kubadilisha mkondo wa maendeleo hayo. Kama tulivyokwisha kuona huko nyuma, sanaa zinaundwa kutokana na mazingira ya watu. Taifa linavyozidi kupanuka. Historia hiyo inaelezwa na sanaa za watu wake. Kwa kuwa sanaa, hasa nzuri, zinarithishwa kwa vizazi vipya, wakati ule ule hutumika katika kufundisha historia ya Taifa hilo. Historia hii hueleza kushindwa, mafanikio, ushujaa na uzalendo wao. Nyimbo, fasihi simulizi, ngoma na mashairi katika Tanzania vinaonyesha wazi tulikotoka, matendo yetu ya sasa na matarajio ya siku zijazo. Mafanikio ya hivi karibuni ya kuandika au kutafiti historia ya Tanzania yametegemea sana uwanja wa Sanaa. Vitabu kama Mtemi Miramabo havingeweza kuandikwa bila ya kutegemea fasihi simulizi, nyimbo na muziki asilia za Watanzania wa sehemu zinazohusika.

SANAA KATIKA KUSIFU JUHUDI ZA WANANCHI

Kusifu ni jambo ambalo linasaidia sana kujenga moyo na kuongeza juhudi za wananchi na viongozi wao. Binadamu akisifiwa huhakikishiwa usahihi wa matendo na juhudi zake. Jambo hili humpa motisho na kuongeza juhudi na maarifa yake katika kupambana na yanayomngojea.

Msanii akiwa ni mtetezi wa Umma, analo jukumu la kusifu juhudi mbali mbali za wananchi pamoja na viongozi wao. Jukumu hili kiasili lilitekelezwa vizuri sana. Zipo nyimbo au hadithi zinazosimulia uhodari wa watu mbali mbali katika kutetea na kuendeleza maslahi ya jamii. Msanii wa leo anaendelea na juhudi hii. Msimamo wa dhati wa Umma au viongozi wake, nguvu na juhudi zao katika harakati za mapambano na ujenzi wa Taifa vinasifiwa na Wasanii kwa namna mbali mbali nchini pote.

Tunazingatia sana methali isemayo Mgema akisifiwa, tembo hulitia maji. Methali hii inakuwa tu na ukweli mahali ambapo sifa zinazotolewa zimejaa chumvi nyingi, hazina ukweli unaokubaliki. Aghalabu kusifu kwa namna hii humfanya mtu avimbe kichwa na kupunguza juhudi na mor wake. Tunazungumzia kusifu mtu kutokana na matukio halisi yenye ukweli unaokubalika. Vile vile ni lazima kuzingatia ukubwa na umuhimu wa matendo hayo katika maendeleo ya Taifa.

Ukosoaji nao vile vile una mipaka yake. Kimsingi tunapozungumzia kukosoa, tunaongelea kukosoa kwa nia ya kujenga na wala siyo kubomoa. Mtu ambaye ana nia ya kujenga hutumia ukweli katika sanaa yake, ambapo mwenye nia ya kubomoa hulundika lawama nyingi zisizo na msingi au kutia chumvi nyingi katika hoja zake. Hiyo ni hujuma. Sanaa zinazokosoa hutumia uzuri kuonyesha ubaya na kamwe hazikashifu.

SANAA NA ELIMU KWA UMMA

Elimu ni suala la msingi sana kwa Taifa lolote. Pamoja na mbinu nyingine zote zinazotumiwa katika kutoa elimu kwa Umma, Sanaa zinahusika sana katika jambo hili. Kutokana na nguvu ya sanaa kama chombo cha mawasiliano, mafanikio yake huwa ni makubwa zaidi. Kwa kweli watu wanapokwenda kutazama ngoma, tamthiliya au muziki, watu wanapohudhuria maonyesho ya sanaa za kuchonga au kuchora, wanapokwenda dansini au kutazamana sinema, watu wanaposoma vitabu vya hadithi au mashairi, hawafanyi hivyo ili kupoteza wakati, bali wanafanya hivyo wakiwa na lengo si la burudani tu bali pia, kujifunza. Wanataka waelewe zaidi juu ya nchi yao au nchi nyingine, juu ya mazingira yao na juu ya maisha yao kwa ujumla.

Kwa mfano, baada ya Azimio la Arusha kupitishwa mwezi Februari mwaka 1967, jambo la kwanza muhimu lilikuwa ni kuwaelimisha wananchi juu ya Azimio hilo ili walielewa barabara na ndipo utekelezaji wa ujenzi wa Ujamaa na Kujitegemea uanze na kuendelea kwa kasi. Sanaa zilijihusisha kikamilifu katika utoaji wa elimu hiyo. Vikundi vya ngoma, kwaya na muziki vilitunga nyimbo zilizofafanua Azimio. Tamthiliya, ngonjera, mashairi na tenzi vilitungwa na kuonyeshwa hadharani kuchapishwa vitabu. Sanaa za kuchora na kuchonga zilitengenezwa. Hata picha ya filamuFimbo ya Mnyonge ilitengenezwa. Vyote vilikuwa na lengo la kuendeleza ufahamu wa Taifa juu ya Azimiola Arusha.Mfano mwingine ni kwamba ni mapema mwaka 1978 ofisi kuu ya sensa iliwaomba wasanii wa ngoma, kwaya na muziki,

Washiriki katika kutoa elimu kwa Taifa juu ya umuhimu wa hesabu ya watu kwa kutunga nyimbo zenye lengo hilo. Mwaka huo huo mwishoni,

Wasanii wetu walishiriki katika kuwapa moyo askari na wananchi kwa jumla katika kukabiliana na uvamizi wa fisadi Idi Amin Dada wa Uganda.

Zaidi ya kumfundisha mambo mbalimbali, sanaa pia humjenga

mtu kiakili. Aghalabu sanaa humuuliza mtu maswali, maswali ambayo

humfanya aendelee kujiuliza mapka atakapopata jibu. Mfano viten- dawili vinatumiwa sana kama chemsha bongo kwa watoto wadogo Watu wazima nao wanayo misemo ambayo iko katika mafumbo. Kuweza kufumbua mafumbo haya inahitaji kufikiri sana. Methali ni aina moja ya mafumbo ambayo huwakilisha hekima nzito na pana kuliko maneno machache yaliyo katika methali hizo. Katika kufumbua mafumbo kama haya, mtu hupata zoezi kubwa la kufikiri na katika kufanya hivyo, uwezo wa akili yake wa kuelewa na kufafanua majambo hupanuka. Ingawa sanaa si kichocheo pekee cha uwezo huu, zina sehemu kubwa sana.

SANAA KAMA KITAMBULUSHO CHA TAIFA

Tumekwisha kuona kuwa sanaa ni matokeo ya mazingira, mahali na kwa wakati maalum. Hivyo sanaa za mahali tofauti haziwezi kufanana kikamilifu. Sanaa basi huwa kitambulisho cha jamii ya watu.

Kwa mfano Sanaa ya ufinyanzi imeenea sehemu nyingi sana za Afrika na dunia kwa ujumla. Lakini ukifananisha vyungu vya Tanzania na vya nchi nyingine utakuta kuna tofauti hata ikiwa ni ndogo tu. Sanaa ya uchongaji vile vile imeenea kila mahali lakini haifanani kwa nchi zote.

Ingawa msimamo wa Taifa letu ni kwamba tuko tayari kujifunza kutoka kwa mataifa mengine, hii haina maana ya kufutilia mbali sanaa zetu.

Lengo ni kushirikisha ujuzi na ufundi wa wenzetu ili kuzifanya sanaa zetu zipendeze na ziwe imara zaidi, bila ya kuharibu sifa ambazo zinazifanya zionekane tofauti na wengine. Mfano mzuri ni sanaa ya ujenzi. Kiasili tunayo mitindo mingi sana ya ujenzi hapa nchini, mitindo ambayo kama tungeiendeleza katika mazingira mapya ya sayanzi na ufundi, ingekuwa ni kitambulisho kizuri sana cha Taifa letu.

SANAA NA UCHUMI WA TAIFA LETU

Pamoja na uwezo wake wa kusukuma maendeleo ya fani nyingine za maisha, Sanaa zinaweza kusadia maendeleo ya Taifa kiuchumi, hasa kutokana na mauzo. Sanaa za zana ni sehemu muhimu sana katika jambo hili.Mauzo ya vifaa mbalimbali huwaingizia wananchi fedha na hulipatia Taifa fedha za Kigeni, kama itakavyoelezwa katika sura ya mipango.

Kutokana na mazao ya sanaa za zana, Taifa letu linaweza kufikia hatua ya kujitegemea, kuna zana nyingine tunazotumia sasa hivi ambazo zinatengenezwa na wasanii wetu. Vifaa kama vikapu vya taka maofisini, trei za kuwekea majivu ya sigara, vifaa vya nyumbani kama vyungu na miko,ni vitu ambavyo vinatengenezwa na wasanii wetu. Zana nyingi sana zinatengenezwa kwa mitambo ya hali ya juu, tusisahau kuwa ufundi wa mikono mara nyingi hutoa kitu ambacho ni bora zaidi ya kila kilichoundwa kwa mitambo. Pia kuna suala la kujitosheleza. Kutokana na uwezo wetu mdogo kifedha, hatuwezi kununua vitu vingi kutoka nchi za nje ili kukidhi mahitaji yetu kikamilifu. Pia viwanda vyetu vikubwa nchini bado havijakua kufikia hatua ya kuzalisha mahitaji yetu yote. Kwa hiyo ufundi wa mikono bado una manufaa kitaifa.

Sanaa aza maonyesho kama vile muziki, ngoma, tamthiliya, picha za filamu na sarakasi, hingiza fedha. Fedha hii hupatikana kutokana na malipo ya viingilio kwenye maonyesho. Katika nchi ambazo wananchi wake wana uwezo mkubwa kifedha, vikundi na kmapuni nyingi hutegemea mapato ya kutosheleza mahitaji ya wanamuziki bila ya kulazimika kufanya kazi nyingine zaidi. Sanaa hizi vile vile huweza kuwekwa katika sahani za santuri, kanda za kunasia sauti au kanda za picha za filamu. Vitu hivi huuzwa na kuingiza fedha. Pamoja na riwaya, mashairi, utenzi na ngonjera, baadhi ya sanaa hizi huchapishwa katika vitabu. Vitabu hivi huuzwa na kuyaingizia fedha makampuni ya uchapishaji na utoaji vitabu na kuwapatia waandishi wanaohusika mapato kama malipo ya kazi zao.

Njia nyingine ambayo inaweza kusukuma uchumi moja kwa moja ni utalii. Kuna watalii wengi ambao wanakuja nchini ili kuona mambo mbali mbali ikiwa ni pamoja na sanaa. Tamasha za sanaa za Kitaifa au Kimataifa huwa ni kivutio kikubwa sana cha wageni. Wageni hawa iwe ni watalii au washiriki katika tamasha hizo, huingiza fedha za kigeni nchini.

Katika suala hili la biashara ya sanaa, huzuka hali ambayo ama inarudisha nyuma maendeleo ya sanaa, au kupotosha mwelekeo sahihi wa ukuzaji na matumizi. Baadhi ya wasanii huwa na tama ya pesa. Badala ya kusisitiza ubora wa bidhaa na ujumbe wa sanaa zao. Kwa hiyo hulipua lipua tu bila kutumia muda wa kutosha na busara. Ni rahisi sana kwa mtu ambaye anatanguliza pesa kuweza kupotosha mkondo wa mawasiliano katika sanaa.

Kwa mfano hapa Tanzania hatujawa na uwezo wa kutengeneza picha za filamu za kutosha. Kwa sababu fani ya filamu ilikwishastawi nchini kama njia ya elimu ya burudani, inabidi tuendelee kuagiza filamu kutoka nchi za nje. Filamu nyingi kati ya hizo hazina uwiano na mahitaji au madhumuni ya Taifa letu. Mara nyingine mabepari hutengenezesha filamu kwa madhumuni ya kupotosha msimamo thabiti wanchi nyingine. Baadhi ya filamu hizo huweza kupenyeza na kuonyeshwa kwa wananchi kinyume cha matarajio ya utamaduni wa Taifa.

WAJIBU WA TAIFA KWA MSANII

Tumekwisha kuona umuhimu wa sanaa katika Taifa. Sanaa si kitu kinachozuka bila kutengenezwa. Sanaa ni matokeo ya juhudi za baadhi ya watu miongoni mwetu wasanii. Katika mazingira ya kiasili, msanii alipewa moyo kwa heshima aliyopata kutoka kwa jamii. Kimsingi hakukuwa na malipo rasmi kwa kazi zake isipokuwa labda kwa msanii wa zana. Kazi zake alizihesabu kama mchango wake kwa jamii, na heshima aliyopewa ilitosha kuwa malipo. Katika mazingira ya sasa suala hili la kuwatunza wasanii wetu ni la kimsingi. Katika historia yetu ya harakati za ukombozi na ujenzi wa Ujamaa na Kujitegemea, wapo wasanii ambao wametoa mchango mkubwa sana. Inawezekana kabisa kuwa wengi wetu hatawafahamu. Kwa mfano mwimbaji hodari Makongoro Kingombe, alitoa mchango mkubwa sana kwa njia ya sanaa yake wakati wa kupigania uhuru. Nyimbo zake alizoziimba wakati wa mikutano ya TANU enzi hizo, zilisaidia sana katika kuwaelimisha wananchi juu ya maana na umuhimu wa mapambano yetu na Wakoloni na kusaidia kushawishi wananchi kukiunga mkono Chama cha TANU katika mapambano hayo. Msanii kama huyu akipewa moyo, ataongeza juhudi zake kwa manufaa ya Taifa.

Ni wajibu wa jamii kuhakikisha kuwa wasanii wana uhuru wa kuendesha shughuli zao. Kwa mfano, wengi wetu tunafahamu picha za hadithi za akina Chakubanga, ambazo hutolerwa kila siku katika magazeti ya Chama ya Uhuru na AMzalendo. Kazi anyoifanya msanii huyo, Chris Gregory ni ya kuelimisha, kukumbusha na kukosoa. Ni wazi kwamba mafanikio yake yanatokana na kiujiamini kwake pamoja na uhuru alionao. Bila hivyo asingeweza kuyawasilisha mambo kama anavyofanya kwa undani na ushupavu wa hali ya juu. Lakini msanii nae anao wajibu katika jambo hili. Uhuru anaopewa ni kwa ajili ya maslahi ya umma. Uhuru huo akiutumia kwa kuuhujumu umma ule ule uliompa uhuru, ni wazi kwamba umma utamnyanganya uhuru huo. Msanii anawajibika kuheshimu mipaka ya uhuru wake. Hakuna mtu ambaye anaweza kuishi katika kundi la watu na akaruhusiwa kupuuza miiko ya kundi hilo.

Raia wa Taifa lolote wanatarajiwa kulipenda na kulitumikia Taifa lao. Msanii pia lazima awe mbele katika jambo hili. Upendo huo hauwezi kuwepo kikamilifu ikiwa msanii huyu halielewi Taifa lake kwa mapana. Ni lazima aelewe ipasavyo historia, matarajio na itikadi na siasa ya nchi yake. Ingawa msanii anao wajibu wa kufanya jitihada za kuyaelewa mambo hayo, Taifa lina jukumnu la kuhakikisha na kumsaidia kufikia lengo hilo. Ikiwa tunamtaka msanii kuieleza siasa ya Chama cha Mapinduzi, ni wajibu msanii mwenyewe apewe nafasi na msaada wa kuilewa, ndipo atakapoweza kuitangaza barabara. Wale ambao tumepata kumsikia Mwinamila akiimba nyimbo za kisiasa, bila shaka tunavutiwa sana na nyimbo zake. Hii siyo kwa sababu ya maadili yake na jinsi anavyopanga. Mafanikio haya ameyapata kwa sababu ya kiwango chake kikubwa cha kuielewa Siasa ya Chama.

Suala la kuonekana au kusikika ni suala la msingi kwa msanii yeyote. Kazi yake ni kazi ya kuwasiliana na watu. Ni wakati sanaa yake inapowafikia anaowakusudia, ndipo huona kuwa lengo lake linatekelezeka. Kwa hiyo ni muhimu kuandaa mipango ambayo itaziwezesha sanaa kufika zilikokusudiwa. Vyombo vya habari na vya usambazaji wa vitu vinala jukumu kubwa sana katika suala hili.

Pamoja na vikwazo kutokana na kutawaliwa kwetu, shughuli za sanaa ziliendelea katika mazingira ya kiasili hasa katika miji midogo na vijijini. Si sahihi kusema kuwa Sanaa zetu zilikufa kabisa. Baada ya nchi yetu kupata uhuru mwaka 1961, juhudi zetu zililenga katika kufufua na kukuza sanaa zetu, kazi ambayo kwa kweli mpaka sasa bado inaendelea. Juhudi za kufufua sanaa zinalengo katika kupambana na kufuta kabisa mfumo mbaya tulioachiwa na Wakoloni na wakati ule ule, kuongeza hazina ya sanaa kiulimwengu.

Katika vikao vya miaka ya karibuni vya Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), maazimio yamelenga katika kuzihimiza nchi za Kiafrika kufufua na kukuza utamaduni wao ili uwe kwa upande mmoja kitambulisho chao kama Taifa, na kwa upande mwingine, mchango wao kwenye hazina ya sanaa ya ulimwengu.

Jukumu la pili linalolikabili Taifa letu ni kuzikuza sanaa hizo asilia ili zilingane na kutumia mazingira yetu ya sasa. Kuna mabadiliko makubwa ambayo yametokea na kuyafanya maisha yetu, ya sasa, yawe tofauti nay ale ya kiasili au ya enzi za Ukoloni. Ikiwa ukuzaji haukuzingatiwa, sanaa hizi zitakufa. Kwa hiyo ikiwa tunataka sanaa hizo zieleweke na kupendwa na Watanzania, ni lazima zifuatane na mazinginra ya leo. Kutokana na uvumbuzi wa kisayansi na kufundi, ni wazi pia kuwa maendeleo ya sanaa zetu yanaweza kuwa makubwa na mazuri zaidi ikiwa tutatumia uvumbuzi huo. Kwa mfano, lazima zitafutwe mbinu bora za kutengeneza ala zetu za muziki ili zidumu zaidi, bila ya kuharibu umbo lake.

SURA YA TATU

NAMNA KISWAHILI KINAVYODUMISHA

NA KUENDELEZA UTAMADUNI WA TAIFA

Kipengele kingine muhimu cha utamaduni ni lugha. Wasanifu wa lugha hufafanua maana ya lugha kwa namna mbali mbali. Ketu Watanzania lugha ni chombo cha mawasiliano kati ya mtu na mtu katika jamii ili kuweza kuelewana. Lugha ina kanuni zake zilizokubalika na jamii kisarufi. Kanuni hizo ni pamoja na wakati, sifa, msamiati. Mtu hupata wazo ambalo huliweka katika hali ya Ki-matamshi, ambayo ipo katika misingi iliyokubalika kimsamiati na kisarufi, na kuweza kutoa ujumbe aliokusudia; na kwa mawimbi ya sauti ujumbe humfikia msikilizaji. Lugha ni chombo muhimu sana katika jamii yoyote ile kwani huleta uelewano katika kufanya shughuli za kila siku.

HISTORIA YA KISWAHILI

Kama lugha nyingine zote duniani, Kiswahili kina historia yake. Asili ya neno Swahili kama inavyhoeleza kamusi ya Kiswahili Kiingereza iliyotayarishwa mwaka 1903 na mwandishi aliyeitwa Madan, inatokana na neno la Kiarabu Sawahil ambalo maana yake ni pwani. Hii inathibitisha kwamba Waarabu, wakiwa ndio wageni wa kwanza kufika katika pwani ya Afrika ya Mashariki, walikuta Kiswahili kikiongewa na wenyeji wa pwani hii.

Licha ya kutazama asili ya jina lake, Kiswahili ni lugha ya Kibantu ambayo ina utajiri mkubwa wa historia ya majilio ya wageni mbali mbali waliofika katika pwani yetu; vile vile historia kuhusu kuhama kwa makabila mbali mbali ya Afrika ya Mashariki. Kutokana na hali hiyo basi, Kiswahili kama lugha zote duniani kimetohoa maneno na kuongeza msamiati wake. Maneno hayo ni kutoka kwenye lugha za Kiarabu, Kireno, Kijerumani na Kiingereza. Kutohoa huko kumefanyika kufuatana na jinsi wageni wenye lugha hizi walivyokuja na kuishi Afrika ya Mashariki.

Kiarabu ndio lugha ya Kigeni ambayo ina athari kubwa katika Kiswahili kuliko lugha nyingine zote ambazo si za Kibantu, kwani maneno kadhaa ya Kiarabu yamekopwa na lugha hii. Hata hivyo sababu zilizofanywa hili hii ikatokea zitaelezwa baadaye.

Utaratibu wa kuunda maneno ya Kiswahili unafanana sana na wa lugha nyingine za Kibantu zilizopo Mashariki ya Afrika. Kufanana huku ni katika uundaji wa neno. Katika muundo wa maneno ya lugha za Kibantu, uundaji wa maneno hutokana na Kiini tendo. Kwa mfano kiini tendo cha neno -piga ni -pig-. Unaweza kunyambulisha kiini tendo hicho na kupata maneno kama vile: kupigwa, anapigwa, pigika, pigana na kadhalika.

UENEAJI WA KISWAHILI

Tangu zama za zama, Kiswahili kimetumiwa katika kukidhi haja mbali mbali. Kiswahili kama inavyoonyesha historia kimepitia enzi ngumu na ova za utumwa. Hii inadhihirishwa na biashara iliyokuwa ikifanywa baina ya Waarabu na makabila yaliyokuwa yakiishi katika pwani ya Afrika ya Mashariki. Hivyo ilibidi Waarabu wajifunze lugha ya Kiswahili kama lugha ya mawasiliano, ili kuwarahisishia mawasiliano na kufanikisha biashara yao. Hivyo basi lugha hii ilienea kufuatana na jinsi biashara ilivyoenea toka pwani hadi bara.

Baadaye Waarabu waliamua kuishi katika pwani ya Afrika ya Mashariki. Kuishi kwa Waarabu katika pwani hiyo kuliiathiri lugha ya Kiswahili pamoja na Utamaduni wa jamii za sehemu hiyo kwa jumla Lugha ya Kiswahili, kama ilivyokwisha elezwa, ilitohoa maneno mbali mbali ya lugha ya Kiarabu kwa mfano: Kitab Kitabu, Khutba Hotuba, Swalaa Sala, Sitta Sita.

Wareno nao walifika katika pwani yetu kwa madhumuni ya kutawala. Ingawa katika kuishi kwao katika pwani yetu hawakuathiri sana utamaduni wa wakaazi wa hapo, baadhi ya maneno kutoka kwenye lugha yao yalitoholewa na kuongezea msamiati wa lugha ya Kiswahili. Maneno hayo ni kama vile: Mesa Meza, Vihno Mvinyo. Maneno haya yote tunayatumia hadi hii leo.

Wakati wa enzi ya Wakoloni wa Kijerumani, Kiswahili kilianza kufuata mwelekeo mwingine. Watawala hawa walikuja na mtindo mpya wa kutawala, vile vile walikuwa na lengo tofauti kidogo na watawala waliopita wakiwa na nia yao ilikuwa kulowea kabisa hivyo walitumia mbinu za kujifunza barabara lugha ya Kiswahili, nap engine kujaribu kuiendeleza, ili waweze kutawala vyema pia kuwaelewa vyema watawaliwa. Kiswahili ilibidi kitumike katika shughuli zote za kiutawala yaani katika ofisi za serikali, kuhubiri dini, kufunzia masomo mashuleni, pia shughuli nyingine zote zilizohusu mtawala na mtawaliwa. Walichagua lugha hii kwani kutokana na tulivyokwishaona, Kiswahili kilishaenea hadi bara.

Athari ya kuwepo kwa utawala huu katika ueneaji wa Kiswahili, ni kwamba Kiswahili kilipata mwelekeo mwingine kwani ulikuwepo msukumo ambao ulisababishwa na Wakoloni wa Kijerumani wakiwa na nia na lengo maalum. Kiswahili kilitohoa maneno ya Kijerumani kama vile Heller ambalo kwa Kiswahili ni hela. Schule ambalo ni shule.

Baada ya Wajerumani kushindwa na Waingereza na kuwaachia koloni, lugha ya Kiswahili nayo ilibidi ifuate mwelekeo wa watawala wapya waliokuja. Kwa vile lugha ni chombo kilicho na mizizi katika umma, kadri Waingereza walivyoiyumbisha na kuikandamiza jamii yetu, lugha ya Kiswahili nayo ilifuata kuyumba huko au pengine ilifuta mwelekeo mpya. Waingereza waliendelea kuifanya lugha ya Kiswahili chombo cha kuwarahisishia shughuli zao za kiutawala. Vile vile walisisitiza ifundishwe mashuleni ili uwepo urahisi wa kuwapata makarani na wafanyakazi watakaosaidia katika shughuli ndogo ndogo za kiutawala kwa manufaa yao.

Wakati wa ukoloni wa Kiingereza kuliundwa Kamati ya Lugha ya Kiswahili ya Afrika ya Mashariki, mnamo mwaka wa 1930. Kazi kubwa iliyofanywa na Kamati hii nbi kuziandika upya Kamusi ya Kiswahili Kiingereza na Kiingereza Kiswahili. Kamati hii ilikipa Kiswahili mwelekeo mpya. Iliamuliwa kuwa Kiunguja ambacho ni mojawapo ya lahaja za Kiswahili, kiwe ndicho Kiswahili sanifu kwani kilikuwa kinatumika sana katika shughuli mbali mbali; vile vile kilishaandikwa sana katika makala na vitabu mbali mbali. Mwelekeo huu ulikuwa mzuri na tena wa kimsingi kwani tunaushikilia hadi hii leo na umerahisisha ukuzaji wa Kiswahili.

Elimu mashuleni ilifundishwa kwa Kiswahili, yaani kuanzia shule za msingi mpaka shule za kati. Madarasa ya juu yalifundishwa kwa Kiingereza. Kutokana na hali hii basi, wasomi walianza kujitokeza katika mambo mbali mbali, mojawapo ikiwa ni sanaa ya uandishi. Hii ilikuwa hatua nyingine ya maana sana katika kuikuza lugha ya Kiswahili, kwani uandishi ni chombo muhimu sana cha kuleta mapinduzi na mwamko wa siasa nchini.

Uandishi huo ulikuwa wa hadithi mbali mbali na mashairi. Mwandishi mashuhuri ambaye alijitokeza katika enzi hii alikuwa ni hayati Shaaban Robert. Hayati Shaaban Robert alijulikana sana kwa ajili ya Mashairi yake pamoja na riwaya zake za Kiswahili. Maandishi yake yana mafunzo na maelezo mbali mbali yenye falsafa ya siri ya jamii yetu.

Magazeti na vyombo vingine vya kuenezea habari vilianza kutumika wakati huu. Vyombo hivyo ni kama vile radio na senema. Kwa mfano Idhaa ya Dar es Salaam (hivi sasa ni Redio Tanzania) ambayo ilian-zishwa mwaka 1953, ilikuwa ikitoa matangazo yake kwa Kiswahili na ilisaidia sana katika uenezaji wa Kiswahili ndani na nje ya mipaka ya nchi.

Kiswahili kilitohoa maneno ya Kiingereza. Baadhi ya maneno hayo ni kama vile shirt ambalo kwa Kiswahili ni shati, man of war manoari, driver dereva.

Kiswahili nil ugh iliyo hai. Hii inathibitishwa wazi na jinsi lugha hii inavyoweza kuyatohoa maneno ya lugha hizi na kuyaweka katika muundo wa lugha ya Kiswahili. Kwa mfano, neno la Kiingereza Bicyle katika muundo wa Kiswahili ni Baiskeli au Motorcar katika muundo wa Kiswahili ni Baiskeli au Motorcar katika muundo wa Kiswahili ni Motokaa, engine ni injini na kadhalika. Mtindo huu si kwa maneno ya lugha Kiingereza tu bali hata Kiarabu, Kijerumani, Kireno na kadhalika. Ni lugha chache tu kubwa zenye uwezo huu.

KISWAHILI KAMA CHOMBO CHA UKOMBOZI

Licha ya kuwa chombo cha Utamaduni, lugha huweza kuwa chombo cha ukombozi; kwa mfano, wakati Mwalimu Nyerere alipoanzisha harakati za kupigania Uhuru; ndipo Kiswahili kilipogeuka na kuwa silaha ya kuwapiga vita Wakoloni. Kwa vile Kiswahili kilishaenea sehemu karibu zote za nchi yetu, ilikuwa rahisi kwa Mwalimu na Chama kuendeleza kampeni ya uhuru katika sehemu mbali mbali za Tanzania.

Tulipopata uhuru, lugha ya Kiswahili ilifuata mwelekeo wa Kimapinduzi ambao sasa ni wa manufaa kwa jamii yetu. Juhudi zinazofanywa kuimarisha Kiswahili ni tofauti na zile za Wakoloni. Lengo la juhudi hizo ni kuimarisha kuendeleza jamii yetu katika misingi ya utamaduni wetu na kuturudishia asili na hadhi yetu, ambayo ilikuwa imepuuzwa.

Lugha ya Kiswahili imetumika kumzindua na kumfanya kila Mtanzania ajione ni sehemu ya Taifa. Kwa mfano, neno ndugu limekuwa ni ishara kubwa ya usawa na udugu. Hapo awali neno ndugu halikuwa na maana pana kama hivi sasa kwani lilikuwa na maana ya mtu wa kuzaliwa naye au mwenye uhusiano wa jamii. Kutokana na mwamko huu basi, imekuwa rahisi kwa wananchi wa Tanzania, kuweza kufanya kazi pamoja na kuishi pamoja bila kubaguana. Kwa hiyo imekuwa rahisi kwa Watanzania kupokea maelekezo ya Chama na Serikali kutekeleza Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Kiswahili ni kiungo kikubwa cha wananchi chini ya uongozi wa Chama. Kiswahili ni lugha ya umma.

Lakini baadhi ya wasomi wa zamani walidharua lugha ya Kiswahili na kuichukulia kuwa ni lugha ya watu wasioelewa, lugha ambayo haitaweza kamwe kuelezea taaluma mbali mbali za juu. Hii ilikuwa kasumba mbaya ambayo chimbuko lake ni historia kama inavyoonekana. Wasomi hao wakizungumza Kiswahili hata na watu wasiojua Kiingereza, wanachanganya maneno ya Kiingereza katika mazungumzo.

Tabia hii ni ya kuwatenga wasomi wawe mbali na jamii. Zamani. Wasomi walizungumza zaidi na wasomi wenzao tu, na walipohusishwa watu ambao si wasomi, basi mambo kama haya yalitokea. Kwa vile lugha ni sehemu ya utamaduni wowote ule, baadhi ya wasomi walidharau mila na desturi zao za asili, kama walivyodharau lugha yenyewe. Waliiga Uzungu, nap engine walipozungumza Kiswahili, athari kubwa ya lafudhi ya lugha ya Kiingereza ilijitokeza.

Hali hii ilikuwepo hata katika utoaji wa huduma mbali mbali kwa jamii. Ofisi zote za Serikali ziliendesha shughuli kwa lugha ya